Mazingira ya shule yanavyochochea unyanyasaji wa wanafunzi

 Jamii imetakiwa  kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia unaotokea katika shule za msingi  ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu bora itakayowakomboa kifikra.

 Licha ya serikali kutoa elimu bure na kuongeza idadi ya wanafunzi katika shule, bado wanafunzi wengi wanakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia (Gender Based Violence-GBV) na kuathiri mwenendo wa masomo yao.

Akizungumza katika mafunzo ya siku tano kwa Waandishi wa Habari, Mkurugenzi wa Kituo cha Jinsia Chuo Kikuu Cha Dar es salaam, Dkt. Eugenia Kafanabo anasema mwaka 2015 walifanya utafiti kubaini Ukatili wa Kijinsia katika shule za msingi zilizopo katika Wilaya za Ilala na Temeke ambapo walikutana na ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto ambapo ukatili  unaofanywa watu walio karibu na watoto wakiwemo wazazi, walimu na wafanyakazi wengine wa shule.

“ Ukatili wa kijinsia unatokea hata katika shule za msingi na linaonekana ni mateso ya kisaikolijia yanayofanyika sirini kwa wanafunzi wengi hasa wa kike ambapo huathiri maendeleo ya masomo na wengine hulazimika kuacha shule” anasema Dkt. Kafanabo.

 Ukatili ambao unawakumba wanafunzi hao ni kunyimwa chakula, kupigwa bila sababu, kudhalilishwa kingono, kubakwa na kulawitiwa, kunyimwa pesa ya matumizi, kufanyishwa kazi ngumu na kupewa majina ya kudhalilisha.

“Tuliwahoji  wanafunzi 4000 na kati ya hao wanafunzi 1,268 walisema  hawapewi chakula nyumbani na hata wakifika shuleni hawapati chakula na hukaa na njaa. Lakini wanaopigwa bila sababu walikuwa 663 na ukatili mwingine 553 walidhalilishwa kingono”, anafanunua Dkt. Kafanabo.

Anaeleza kuwa wanafunzi wengi wa shule za msingi nchi hawako salama na wanahitaji uwangalizi wa karibu ili kuwaepusha na matendo hayo ambayo hutendwa na watu wa karibu na wanafunzi, ambapo hukatazwa na wahusika kuwaambia watu wengine kwa yale wanayotendewa.

 Walimu Wakuu, waalimu walezi (patrons), wafanyakazi katika shule na wanafunzi wanatajwa na utafiti huo kuongoza kuwadhalilisha wanafunzi hasa wa kike, jambo linalowaathiri kisaikolojia na kuwalazimu baadhi ya wanafunzi kuacha shule na kujiingiza katika kazi hatarishi.

“ wanafunzi 1343 walisema  Walimu Wakuu katika shule za msingi walidhalilisha  na walimu walezi  (992) wakifuatiwa na wanafunzi wenye umri mkubwa (240). Wanafunzi hawana mahali oa kusema yanayowakuta wanabaki kimya kwa sababu wanatishiwa kuuwawa”, anasema Dkt. Kafanabo.

Kulingana na Utafiti huo, Wasichana wanatajwa kuathirika sana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo wasichana 1,822 walitendea ukatili ikilinganishwa na wavulana 1,513.  

Licha ya wanafunzi hao kunyimwa haki zao shuleni, pia wakirudi nyumbani nako hukutana na ukatili ambao hufanyiwa na madereva wa bodaboda, majirani na ndugu wa karibu wakiwemo wazazi wa kiume.

Ameishauri serikali na wanaharakati kutoa elimu na kutengeneza  mfumo rasmi katika shule utakasaidia wanafunzi kusikilizwa na kubaini changamoto wanazokabiliana nazo, kwa sababu huduma hiyo haipatikani katika shule nyingi. Hata wanaotakiwa kuwalinda wanafunzi ndio vinara wanaowadhalilisha wanafunzi.

“ukatili wa kijinsia ni tatizo ambalo limekita mizizi katika jamii zetu lakini tuendelee kutoa elimu kwa watu ili wabadilike” amesema Dkt. Kafanabo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA), Edda Sanga amesema ukatili wa kijinsia kwa watoto bado ni tatizo kubwa ambalo linafanyika kwa siri, na juhudi za vyombo vya habari zinahitajika ili kuibua matukio hayo na  kutoa elimu kwa jamii kumlinda mtoto na kumuhakikishia haki ya kuishi na kupata elimu.

 

Ukatili wa Kijinsia ni nini?

Ni matendo yote yanayolenga kuvunja haki za binadamu ikiwemo kudhalilisha utu wa mtu. Ukatili huo hutokea kwa wanawake na wanaume lakini wanaoathirika zaidi ni wanawake, hii ni kwa sababu mila na desturi, mifumo ya kisheria na sera inampa sauti na nguvu zaidi mwanaume.

Ukatili wa kijinsia uko wa aina mbalimbali: kutumia nguvu, saikolojia,  kiuchumi, udhalilishaji wa kingono, mauaji na udhalilishaji wa watoto. Vitendo vya ukatili huambatana na vipigo, kuchomwa moto, ubakaji, ukeketaji wanawake, mimba na ndoa za utotoni, mauaji ya wazee, kunyimwa mahitaji na kumiliki mali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya PiepPoint Limited, June Warioba amasema yeye ni mmoja wa waathirika wa vitendo vya ukatili  na anawataka waliotendewa wasikae kimya bali watoe taarifa ili wapate msaada. Anasema ukatili wa kijinsia unaweza kumpata mtu yoyote pasipo kujali hadhi aliyonayo.

 

 

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Udumavu, utapiamlo wawatesa viongozi wa Afrika, wahaha kuokoa maisha ya watoto wanaokufa kila mwaka

Viongozi wa Afrika wamekubaliana kuondoa vikwazo vya lishe vinavyowazuia watoto na jamii kutambua na ...

Kuporomoka majengo Dar: Tumekwama, tumeshindwa!

Sherehe za pasaka ziliingia dosari hususan kwa wakazi wa Dar es Salaam kufuatia kuporomoka ...

Mtuhumiwa wa Madawa ya Kulevya apigwa risasi na kufa akijaribu kutoroka Mahakama ya Kisutu

Mtuhumiwa wa Madawa ya kulevya amepigwa risasi na kufa papo hapo kufuatia kutaka kutoroka ...