Walimu wazuri wanavyozibeba shule za msingi binafsi

*Lakini zipo baadhi hazina walimu wenye sifa kufundisha watoto

Dar es Salaam. Mwalimu ni mtu muhimu katika kumsaidia mwanafunzi kupata maarifa yaliyokusudiwa akiwa darasani.  Japo mwanafunzi anatakiwa kusoma kwa bidii lakini mwalimu ana nafasi kubwa ya kufanikisha au kuzuia ndoto za mwanafunzi kupata elimu bora.

Mafanikio ya wanafunzi yanategemea ufanisi na uzoefu wa mwalimu anapofundisha darasani.  

Licha ya shule nyingi za binafsi kuaminika kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi na kutoa elimu bora, baadhi ya shule zimekuwa na walimu wachache wenye sifa za kufundisha wanafunzi.

Ili mwalimu atambulike na kuwa na sifa za kufundisha lazima apitie mafunzo ya taaluma ya ualimu katika vyuo vinavyotambulika na serikali.

Uchambuzi wa takwimu za Kituo Huru cha Serikali (Opendata) za hadi Machi 2016 za uwiano wa walimu wenye sifa na wanafunzi katika shule za msingi zisizo za Serikali (QPTR), zilikuwa na walimu 13,643 wenye sifa na wanafunzi 298,207.

Kwa mantinki hiyo, katika shule hizo binafsi mwalimu mmoja mwenye sifa anafundisha wastani wa wanafunzi 22 kiwango ambacho ni bora takriban mara mbili ya uwiano uliowekwa na Serikali.

Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imeweka uwiano sahihi wa mwalimu kwa wanafunzi (PTR) katika shule za msingi kuwa ni mwalimu mmoja kwa watoto 40 (1:40). Ikiwa na maana mwalimu mmoja anatakiwa kufundisha wanafunzi wasiozidi 40 katika darasa moja.

Miongoni mwa shule hizo, kuna shule zenye walimu wachache wenye sifa ambao hufundisha idadi kubwa ya wanafunzi kuliko kiwango kinachapendekezwa na Serikali.

Shule 63 zina walimu wachache wenye sifa ambao ni sawa na asilimia 6 ya shule 1,079 zenye walimu wenye sifa ya kufundisha.  Kutokana na hali hiyo mwalimu mmoja hufundisha kati ya wanafunzi 41 hadi 315.

Miongoni mwa shule hizo ni shule ya msingi Kongwa yenye walimu 8 na wanafunzi 915 ambapo kwa wastani mwalimu mmoja hufundisha wanafunzi 114.

Pia shule 72 zilibainika kutokuwa na mwalimu hata mmoja mwenye sifa kati ya shule 1,079 zilizofanyiwa uchambuzi, ambapo ni sawa na asilimia 7 ya shule zote.

Kwa mfano, takwimu zinaonyesha kuwa shule ya msingi Ebenezer iliyopo mkoani wa Dodoma wakati huo ilikuwa na wanafunzi 90 lakini haikuwa hata na mwalimu mmoja mwenye sifa.

Shule  hizo zisizo na walimu wenye sifa za kufundisha zinapatikana katika mikoa ya Arusha, Dar es salaam, Dodoma, Kagera , Geita , Kigoma , Kilimanjaro , Manyara, Mara, Mtwara, Mwanza, Simiyu , Shinyanga, Ruvuma, Pwani na Singida.

Mkoa wa Arusha unaongoza kwa kuwa na shule 26 zisizo na walimu wenye sifa, huku mikoa ya Kilimanjaro na Singida ikiwa na shule moja moja.

 

Licha ya shule hizo kuwa na walimu wachache wenye sifa bado zimeendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi ukilinganisha na shule za umma. Katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana hakuna shule ya binafsi iliyokuwepo katika shule 10 zilizofanya vibaya.

Uchambuzi huu ulibaini shule 10  za Tusiime, Atlas, Al-Muntanzily Girls, Yemen, Academic International, Al-Muntanzily Boys, Anazak (Dar es salaam), Messa Eng. Med (Mwanza), Martin Luther (Dodoma) na Mtakatifu Yuda (Arusha) ndizo zenye walimu wengi wenye sifa miongoni mwa shule binafsi nchini.

Licha ya shule hizo 10 kuwa na walimu wenye sifa, zina uwiano mzuri  ambapo mwalimu mmoja hufundisha kati ya wanafunzi 9 hadi 26 katika darasa moja.

Kutokana na shule hizo kuwa na walimu wengi wenye sifa zimeendelea kufanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba mwaka 2016 na kuzipita kwa mbali shule zenye walimu wachache wenye sifa zinazohitajika kwa walimu wa shule za msingi.

Shule za Atlas na Tusiime zilikuwa miongoni mwa shule 10 bora kitaifa  zilizofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba, shule nyingine ni Kwema na Rocken Hill (Shinyanga), Mugini (Mwanza), Fountain of Joy  (Dar es Salaam), Mudio Islamic (Kilimanjaro), St Achileus (Kagera), Giftskillfull (Dar) na Carmel (Morogoro).

Wadau wa Elimu wanasemaje?

Licha ya shule nyingi za binafsi kuwa na uwiano mzuri wa mwalimu bado kuna malalamiko kuwa baadhi ya walimu waliopo katika shule hizo hawana sifa zinazohitajika katika kufundisha wanafunzi.

Zipo shule ambazo zinawatumia wahitimu wa kidato cha nne na sita kufundisha. Na mkazo umewekwa katika kuwawezesha wanafunzi kufaulu mitihani na sio kupata maarifa yaliyokusudiwa.

Mwandishi wa Vitabu na Mwalimu wa Shule ya msingi ya Elite, Erasto Kibiki anasema shule binafsi ziko kwenye ushindani hivyo hufanya kila mbinu kutafuta walimu wenye uzoefu ili kufaulisha wanafunzi wengi zaidi.

“Kila shule ina mfumo wake wa kujiendesha na sababu ya kuajiri walimu wasio na sifa hutegemea bajeti ya shule. Wanawachukua wahitimu waliofaulu vizuri na kuwaendeleza ili kuwajengea uzoefu wa kufundisha” anasema Mwalimu Kibiki.

Anasema shule hizo hulazimika kuwachukua wahitimu wa kidato cha sita waliofaulu vizuri ili kuondokana na kasumba iliyoenea kuwa watu wanaosomea ualimu ni wale waliofeli na hawana uwezo wa kutosha.

“Kila shule inataka wanafunzi wake wafaulu, hutafuta walimu wenye uzoefu na kuwalipa vizuri ili kuendeleza ushindani na kuinua ubora wa elimu.”

Naye Afisa Elimu na Mafunzo wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Kinondoni, Prosper Lubuva anasema kila shule ina utaratibu wake wa kuajiri walimu kulingana na ubora wanaotaka ili kufanikisha malengo yao.

“Kila shule ina utaratibu wake wa kuajiri walimu, lakini yapo malalamiko mengi kwa shule binafsi ambazo zinawatumia walimu wasio na sifa” anasema Lubuva.

Anazishauri mamlaka husika kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha shule zote zinatoa elimu bora na kuajiri walimu wenye sifa.

 

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Tatizo la upofu wa macho linavyoitesa dunia

Jicho ni kiungo kimojawapo cha mwili kinachomsaidia mwanadamu na pia wanyama kuona vitu mbalimbali ...

Uelewa mdogo wa wananchi kudhoofisha harakati za upatikanaji wa katiba mpya

Matamanio ya watanzania wengi ni kuwa na katiba bora itakayoweza kusimamia rasilimali za nchi ...

Vichocheo vya Teknolojia: Njia mbadala kuzuia ukataji miti, matumizi ya mkaa

Utunzaji wa mazingira ni wajibu wa kila mwananchi ili kuhakikisha shughuli za kibinadamu zinaratibiwa ...