Wajane wa Mkoa wa Kagera na ndoto ya Mwitongo

GraceMahumbuka

KIJIJI cha Butiama Mkoani Mara kinaendelea kuwa eneo muhimu katika historia ya taifa. Kijiji hiki kinabeba historia ya matukio muhimu ambayo hushawishi watu wa rika tofauti kutoka maeneo mbalimbali kuvutiwa na eneo hili.

Eneo la Mwitongo ndipo aliishi na kuzikwa mtemi Nyerere Burito, Baba mzazi wa Mwalimu Julius Nyerere. Mwalimu Nrerere naye alizikwa eno hilo tarehe 23, Oktoba 1999 baada ya kufariki akiwa nchini Uingereza kwa matibabu.

Katika kabila la Wazanaki, tafsiri ya Mwitongo ni eneo walipoishi watu na baadaye kuhama hasa baada ya mkuu wa kaya kufariki. Hata hivyo Mwalimu Nyerere hakupenda ukabila na katika maisha yake hakujisifia yeye na kabila alilotoka.

Nyerere hakuwa tayari kuruhusu mijadala ya ukabila iligawe taifa na aliwakemea waliosifia ubora wa makabila waliyotoka. Alijenga umoja na usawa kama msingi wa taifa ingawa msingi huo ulianza kubomoka baada ya kung’atuka kwenye uongozi na kurejea kijijini Butiama.

Safari ya kuzuru kaburi la marehemu Mwalimu Nyerere inaweza kuwa ni jambo kubwa na muhimu kwa mwananchi yeyoye anayethamini historia ya taifa lake. Ni kuenzi mchango wake mkubwa katika taifa alioutoa enzi za uhai wake.

Baada ya kutoka Mwitongo kwa mwendo wa saa mbili, unaweza kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea hifadhi ya taifa ya Serengeti, ambayo ni moja ya maajabu saba Barani Afrika. Ni eneo lenye mkusanyiko wa makabila tofauti ya wanyama kuwahi kuwepo duniani.

Ndoto ya Mwitongo

Kundi la wanawake wajane wa Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa wananchi wengi wanaotaka kukamilisha ndoto yao kwa kutembelea kijiji cha Butiama. Wanataka kufika Mwitongo kumuenzi Baba wa taifa kwa uongozi wake uliotukuka.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wajane wa Wilaya ya Karagwe na Kyerwa (UWK) ambao ni waasisi wa wazo hilo na waratibu wa safari Grace Mahumbuka anasema pamoja na kutaka kumuenzi Mwalimu Nyerere pia watatumia ziara hiyo kutangaza fursa mbalimbali zilizoko Mkoani Kagera.

GraceMahumbuka

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wajane Wilaya za Karagwe na Kyerwa Bi Grace Mahumbuka

Anasema ubunifu wa vazi asilia la utalii ni miongoni mwa maandalizi yanayofanyika na kuwa ziara hiyo ambayo ilikuwa ifanyike mwishoni mwa mwaka jana imesogezwa mbele mpaka mwaka huu wa 2014 kutokana na sababu za msingi.

Kwamba safari hiyo itakuwa muhimu sana hasa kwa wanawake wajane watakaokwenda Butiama kwani pia watapata fursa ya kubadilishana mawazo na Mama Maria Nyerere ambaye ni mjane wa marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

maria-nyerere

Ujumbe wa wanawake wajane waliokwenda kijijini Butiama kuzungumza  na Mama Maria Nyerere ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ziara yao.

Mwenyekiti huyo anabainisha kuwa Mkoa wa Kagera una vivutio vingi vya utalii zikiwemo fursa za uwekezaji wa kiuchumi zinazoweza kusaidia kuboresha maisha ya wananchi ingawa fursa hizo hazijatangazwa jukumu alilosema watalifanya pia wakati wa ziara yao Kijijini Butiama.

‘’Tutautangaza Mkoa wa Kagera na kuhamaisisha utalii wa ndani kwa kutembelea hifadhi ya taifa ya Serengeti, tukiwa Butiama tutaonyesha ubunifu wa vazi la utalii tunaomba wananchi watuunge mkono’’ anabainisha Grace

Hata hivyo anasema kuwa kipato kidogo miongoni mwa wananchi na elimu duni kuhusu hifadhi za taifa ni miongoni mwa vikwazo vikubwa katika kuutangaza utalii wa ndani, ambao unesaidia kuongeza pato la taifa badala ya kutegemea wingi wa watalii wa nje.

Pia anasema watatumia ziara hiyo kama mabalozi wa kupinga dhuruma dhidi ya mali za wajane na yatima, mifumo kandamizi katika jamii huku wakiendelea kupaza sauti yao kuwa elimu kwa watoto yatima itolewe bure.

Kwamba wanataka hata Katiba Mpya ijayo itamke haki za msingi za wajane na yatima na kuwa wanapinga uteketezaji wa rasilimali za taifa kama wanyamapori na kusisitiza utunzaji wa mazingira kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo anabainisha kuwa baadhi ya wanasiasa wameanza kuweka vikwazo ili maandalzi ya ziara yasifikiwe na baadhi yao kutuhumiwa kutaka kuitumia kwa malengo ya kisiasa jambo ambalo ni kinyume na malengo ya umoja huo.

GraceMahumbuka2

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wajane wa Wilaya za Karagwe na Kyerwa (UWK) Grace Mahumbuka pamoja na wajane wengine wakiwa katika maandalizi ya mambo ya kitamaduni yanayotarajiwa kuonyeshwa kijijini Butiama

Anatahadhalisha kuwa lazima Mwalimu Julius Nyerere aenziwe kwa kauli na vitendo badala ya porojo za kujikosha huku viongozi wakijificha kwenye kivuli chake wakati huo wakimsaliti hata kwa mambo mema aliyoliachia taifa.

Naye Mwenyekiti wa Uhamasishaji wa ziara hiyo Sabby Rwazo anasema hii ni fursa pkee kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera kutembelea Kijiji alichozali,kukulian na kuzikwa Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema ziara hiyo italeta mwamko mpya miongoni mwa wananchi wa Mkoa wa Kagera katika kutambua michango ya viongozi wao na kuthamini rasmilimali za taifa na umuhimu wa kuenzi mila na tamaduni zetu ili zisimezwe na tamaduni za kigeni.

Anawataka wananchi wa Mkoa wa Kagera kwa rika tofauti kujitokeza kwa wingi kuchangia gharama kidogo za safari hiyo ili kuwaunga mkono wanawake wajane wanaotaka kufikia ndoto yao ya kuzuru kaburi la Baba wa Taifa na kufurahia mambo mbalimbali ya kihistoria na utalii.

Akizungumzia umuhimu wa ziara hiyo Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kagera (CCM) Elizabeth Batenga, anapongeza ubunifu wa wanawake hao na kuomba wazo lao liungwe mkono na wadau mbalimbali.

Anasema wazo la kutembelea Kijiji cha Butiama alipozikwa Baba wa taifa marehemu Mwalimu Nyerere  litaleta heshima kubwa Mkoa wa Kagera na kuwa mambo mengi yenye manufaa  hutokana na mawazo ya watu wachache.

Mbunge huyo ambaye pia ameshiriki hatua mbalimbali za uhamasishaji anawataka wasikate tamaa katika maandalizi ya safari hiyo kuwa wataona mambo mengi hata yale ambayo hawakuyakusudia katika safari yao.

Wajane njia panda

Pamoja na mambo mengine kundi la wanawake wajane linakabiliwa na changamoto nyingi ukiwemo unyanyaswaji na udhalilishaji kutoka kwa ndugu wa marehemu baada ya vifo vya waume zao.

Mara nyingi unyanyaswaji huo huusishwa na tamaa ya ndugu kutaka kumiliki mali za marehemu. Yapo matukio ya wanawake wajane kufukuzwa katika nyumba baada ya mwanaume kufariki bila kufikiria hatima yao.

Kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto (WLAC) mwaka 2011 wajane 544 walifika katika kituo hicho kuomba msaada wa kisheria wakati huo viongozi wanaotakiwa kuwasaidia wajane wakiwa  sehemu ya jamii inayofuata mila kandamizi .Idadi kubwa ya wajane hao walitoka Dar es salaam, Karagwe na Kasulu.

Pia mwaka 2011 Chama cha Wanasheria Wanawake Nchini (TAWLA) kilipokea mashauri ya wajane 148, ambapo takwimu kutoka Musoma Mkoani Mara zilionyesha kuwa jumla ya wajane 55 walinyang’anywa ardhi baada ya wenza wao kufariki.

 • Phinias Bashaya ni Mwandishi wa Fikrapevu anayepatikana Mkoani Kagera

 • Show Comments (2)

 • RWAZO SABBY

  Hello Bashayya ahsante sana kwa kutuweka duniani mungu akubariki-Rwazo

 • shakiru mugula

  mwakolage, mugendelele. iapendeza, kutoa elimu nzr hivohivo.

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

 • name *

 • email *

 • website *

ads

You May Also Like

breakingnews

Abiria 38 wa ndege ya ATCL wanusurika kifo Kigoma

Ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) imepata ajali wakati ikitaka ...

20140715_112616

Ajali ya moto yateketeza maduka matatu Mwananyamala Dar

NYUMBA tatu za biashara na makazi ya watu zilizopo katika eneo la Mwananyamala ‘A’ ...

lindi 2

42 wajeruhiwa katika ajali ya basi Lindi. 21 kati yao hali zao ni mbaya

WATU 42 wamejeruhiwa vibaya na 21 kati yao wakiwa na hali mbaya, baada ya ...