Connect with us

ELIMU

Uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi madarasa ya awali bado ni kitendawili

Published

on

Imeelezwa kuwa  uhaba wa walimu na mlundikano wa wanafunzi katika madarasa ya awali  ni kikwazo kwa Tanzania kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030 yanayohimiza utolewaji wa elimu bora na yenye usawa.

Uchambuzi  wa takwimu uliofanywa na FikraPevu kuhusu elimu ya awali umebaini kuwa miaka miwili mfufulizo tangu mwaka 2016, uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi katika madarasa ya awali umekuwa sio wa kuridhisha.

Hali hiyo imesababishwa na upungufu wa walimu katika madarasa ya awali ambapo mzigo wa walimu kufundisha watoto wengi umeongezeka, jambo linalotishia mstakabali wa elimu ya watoto wanaoandaliwa kuingia katika shule za msingi.

Kwa mujibu taarifa ya mapendekezo ya bajeti ya elimu ya Shirika la HakiElimu (2018) yaliyotolewa hivi karibuni yanaonesha kuwa uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi kwa mwaka 2017 ulikuwa mwalimu 1 kwa wanafunzi 159 (1:159) ukilinganisha na uwiano wa mwaka 2016 ambapo ulikuwa 1:135.

Hiyo ni sawa na kusema wanafunzi katika madarasa ya awali waliongezeka zaidi kwa mwaka 2017 lakini idadi ya walimu haikuongezeka au ilipungua kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa sera elimu bila malipo.

Kimsingi mzigo wa walimu kufundisha umeongezeka  ukilinganisha na mwaka 2016. Kwa mfano kama darasa la moja la awali lilikuwa na wanafunzi 135 ina maana mwaka uliofuata (2017) waliongezeka wanafunzi  wengine 29.

Mtaala wa Elimu ya Awali Tanzania toleo la 2013 na vigezo vya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), unapendekeza uwiano sahihi katika madarasa ya awali ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 25 (1:25).

Ukilinganisha na uwiano uliopo katika madarasa mbalimbali ya awali nchini, bado haukidhi matakwa ya TAMISEMI na uwezekano wa wanafunzi kukosa maarifa ya msingi kuwaandaa kuingia elimu ya msingi ni mkubwa.

Pia  takwimu za TAMISEMI na kuchapishwa kwenye kitabu cha Takwimu za Mwaka 2016 (Tanzania in Figures 2016) ambazo zimetolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) zinaeleza kuwa mwaka 2016 pekee madarasa ya awali nchi nzima yalikuwa na walimu 14,958 lakini waliokuwa na sifa za kufundisha ni 11,920 sawa na asilimia 79.7.

Zinaeleza zaidi kuwa uwiano wa mwalimu (kwa walimu wenye sifa)  kwa wanafunzi kwa mwaka huo ulikuwa 1:131 ambapo ni mara 5 zaidi ya uwiano unaotakiwa wa 1:25.

 

Maoni ya Wadau

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la HakiElimu, Dk. John Kallage wakati akitoa mapendekezo ya shirika kuhusu bajeti ya elimu ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 alisema serikali inapaswa kuweka kipaombele katika utatuzi wa matatizo sugu katika sekta ya elimu ikiwemo suala la ajira za walimu katika madarasa ya awali.

“Kutenga na kuongeza bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu na hasa fedha zinazokwenda TAMISEMI kwa ajili ya elimu msingi. Kutenga bajeti yenye uhalisia wa kutatua changamoto sugu na muda mrefu za miundombinu mashuleni na kuweka kipaumbele katika suala la ajira za walimu,” alisema Dk. Kallage.

Serikali imeshauriwa kuanzisha mpango wa kutoa ruzuku kwa wanafunzi wa madarasa ya awali kama ilivyo kwa shule za msingi na sekondari ili kuboresha ustawi wa elimu ya watoto nchini.

Kwa upande wake, Mwandishi wa Vitabu na Mwanaharakati wa masuala ya Watoto, Richard Mabala amesema licha ya kuongeza idadi ya walimu katika madarasa ya awali, wanafunzi wapewe ulinzi na elimu bora itakayowakomboa fikra na maisha yao.

“Mimi naamini suala kubwa elimu bure, pili ulinzi kwasababu mimi kama mzazi nikijua shuleni wasichana wanatongozwa, wanatishiwa kubakwa na njiani hakuna ulinzi. Kwahiyo kuwe na ulinzi wa kutosha kuhakikisha watoto wako salama,” amesema.

 

Msimamo wa Serikali

Serikali kupitia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako imesema inaendelea na jitihada za kuboresha elimu ya awali kwa kujenga madarasa, kuajiri walimu na kuhakikisha vifaa vya kujifunzia na kufundishia vinakuwepo mashuleni.

Akisoma bajeti ya elimu jana, Prof. Ndalichako alisema, “Katika kusimamia Elimu ya Msingi na Sekondari, katika mwaka 2018/19 Wizara itatekeleza yafuatayo:  itaandaa Mwongozo wa Kitaifa wa uendeshaji wa Elimu ya Awali unaozingatia viwango. Lengo la Mwongozo huo ni kufafanua viwango vya Elimu ya Awali kwani kwa sasa kuna mifumo mingi ambayo inahitaji uratibu wa karibu kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi hao kusoma katika mazingira tulivu na salama yenye kusaidia kuinua ubora wa elimu na mafunzo.”

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ELIMU

Njia 4 ambazo waliofanikiwa huzitumia kutojali kile wanachofikiria watu wengine

Published

on

Kwa namna moja au nyingine, wote kwa namna fulani tumewahi kujutia kujali sana kile ambacho watu wengine wanakifikiria au watakifikiria. Tunasita kuwa wabunifu, wavumbuzi au kusema kwa uwazi kile tunachokiwaza kwa kuogopa kuonekana kwamba tuna mawazo mabaya au mipango yetu ni mibovu.

Piia tunaweza kujifanyia hivi sisi wenyewe, kwa kukataa changamoto fulani au kuuza mawazo yetu kwa kuhofia kwamba hayatafanikiwa. Mwandishi maarufu Seth Godin anasema siyo “hofu ya kushindwa” inayoturudisha nyuma na kufanya tusiendelee bali “hofu ya kukosolewa”.

 

Je, unawezaje kupuuzia wanachofikiria watu wengine?
Jambo la kwanza unalotakiwa kufahamu ni kwamba, kama watu wengi wamewahi kukumbwa na hali hii na wakafanikiwa kufanya mambo makubwa, waliikabili hofu yao ya kushindwa na kukosolewa na wakafanikiwa. Watu wanaothubutu kwenye mafanikio hufanikiwa kuzuia hali ya kukosolewa kuwakwamisha.

Kama unataka kubadilika kutoka kuwa mtu ambaye ni muoga kuongea mbele za watu na kuwa mzungumzaji mwenye ujasiri, basi jifunze kupitia mbinu hizi zilizotumiwa na watu 4 waliofanikiwa.

 

1. Jiulize wewe mwenyewe: “Nini kitatokea nisipofanya chochote?”
Marie Forleo, mtangazaji wa kituo cha runinga cha Marie anasema, inapotokea nafasi ya kufanya kitu kipya au nje ya uzoefu wako, kitu kinachoweza kukusaidia ni kufikiria hali mbaya kabisa.

Kwa maneno mengine ni kwamba, kabla hujajizuia kufanya jambo kwasababu tu kuna uwezekano wa kushindwa, jiulize kwanza “ Ni jambo gani baya linaloweza kutokea ukifanya…” Je, kuna uwezekano wa wewe kuanguka na kuumia usoni kwa kufanya kitu fulani kipya na chenye changamoto? Na je, ni vipi kama utakaa kimya?

Orodhesha vitu vyote vibaya ambavyo unadhani vitatokea endapo utaikubali fursa hiyo. Andika makosoleo yote unayoweza kuyapata kutokana na uamuzi huo. Na kwa kuongezea hapo orodhesha pia mambo yote ambayo yatatokea kama utaamua kukaa kimya na kuficha mawazo yako na mipango yako kwa ulimwengu. Oanisha orodha yako na fanya maamuzi ya kipi ukifuate baada ya hapo.

 

2. Kumbuka kwamba kazi yako haikuelezei wewe ni nani
Rohan Gunatillake anasema watu wengi tuna desturi mbaya ya kuruhusu kazi zetu zituelezee, hivyo kushindwa kwenye kazi fulani hutufanya tujisikie vibaya kwenye nafsi zetu.

Katika mazungumzo yake Rohan anaelezea tiba ya “kutenganisha nafsi na kazi” ambapo anatumia kauli fulani fupi ambazo mtu huzichagua na kuzitamka kwa sauti, kujihusisha nazo na baadaye utaona jinsi zinavyokufanya ujisikie kuhusu hili.

Kauli hizo ni kama vile: “ Mimi sio utambulisho wa kwenye ukurasa wangu wa mtandaoni”, “Mimi sio kampuni yangu”, “Mimi sio wasifu wangu” na “Mimi sio kazi yangu”. Husisha kauli hizi na nafsi yako na uone zitakupa hisia gani.

Anasema kwa kufanya hivi itakusaidia kutenganisha nafsi yako na kazi yako, na hatimaye hukuondolea maumivu unayoyapata pale unaposhindwa kazini. Kama “wewe sio kazi yako” basi hata pale unapokosea ukiwa kazini (kitu ambacho wengi wetu hututokea) hutabeba maumivu hayo ndani yako na kujisikia vibaya wakati wote.

Hivyo ni sawa kabisa kuikubali fursa hiyo mpya na ngumu kwasababu hata isipofanikiwa haimaanishi kwamba wewe binafsi umeshindwa. Ukikumbuka kwamba wewe ni zaidi ya kazi yako itakusaidia kuwa mbunifu.

 

3. Usiruhusu watu wakushushe au kukukwamisha
Kuzuia hali ya kujikosoa mwenyewe ni hatua ya kwanza kwasababu unatakiwa kujiandaa kwa kuwa watu wengine watakukosoa pia.

Mwandishi maarufu Brene Brown anasema, “Kutojali kile watu wanafikiria ni namna ya kipekee katika kupambana”. Katika mazungumzo yake ya 99U, aliwashirikisha watu msemo kutoka kwa aliyewahi kuwa rais wa Marekani, Theodore Roosevelt ambao ulibadilisha mtazamo wake kuhusu kukosolewa.

Haijalishi anayekosoa ni nani; siyo yule anayeelezea jinsi mtu jasiri anavyopambana au pale mtenda mema angefanya vizuri zaidi. Sifa zinatakiwa ziende kwa mtu ambaye yuko uringoni, ambaye uso wake hufunikwa kwa vumbi, jasho na damu… yule ambaye katika wakati mzuri anajua mwishoni ni furaha ya mafanikio makubwa, na katika magumu hata akishindwa, anashindwa akiwa amejaribu kwa kiwango kikubwa.

Msemo huu ulibadilisha kabisa mtazamo wake wa zamani. Brown aliamua kujali kukosolewa kulikotoka kwa mtu ambaye naye alikuwa kwenye uringo kama wa kwake, lakini mtu aliyemkosoa kwa kuamua tu kukosoa huyo hakujali alichokisema. Hafanyi hivi ili kumpuuza mtu huyo kabisa bali hujibu kwa kusema, “Nimekuona, nimekusikia, lakini bado nitafanya jambo hili.

Hutakiwi kuwapuuza watu wasiokubaliana nawe kama vile hawapo; unachotakiwa kufanya ni kuamua kwamba utaendelea kufanya kile ulichokipanga, kwa kuwa umeona kwamba kufanya kuna manufaa zaidi kuliko kutofanya, na hata kama hutafanikiwa haitamaanisha kwamba wewe ni wa kushindwa.

 

4. Kubali kukosolewa
Seth Godin, ambaye ameelezwa hapo mwanzo, ni mjasiriamali na mwandishi mashuhuri ambaye ameshauza vitabu 18 ambavyo vimetafririwa kwa lugha 35. Anasema kwamba binadamu ana “machaguo mawili tu” kwenye maisha: Kukosolewa au “kupuuzwa”.

Wewe ndiye unayechagua. Ila kama unajizuia kufanya kitu fulani kwa kuogopa kukosolewa basi jiulize maswali haya:
Je, nikikosolewa kwa hiki ninachotaka kufanya, nitapata matatizo yoyote makubwa? Je, nitapoteza kazi yangu au nitapoteza marafiki wa muhimu? Kama madhara pekee unayoweza kuyapata kwenye kukosolewa ni kujisikia vibaya kuhusu kukosolewa, basi oanisha hisia hiyo mbaya na faida unakayoipata kwa kufanya kitu chenye thamani.

Kuwa tofauti ni jambo zuri na lenye faida kubwa sana kwa taaluma yako. Kujisikia vibaya hupotea baada ya muda. Baada ya kuoanisha pande hizo mbili na umeshachagua njia ipi ya kuifuata, jibu swali hili.

Nawezaje kutengeneza kitu ambacho wakosoaji watakikosoa?
Utakapoacha kuwachukulia wanaokukosoa kama ishara ya kwamba umefanya kitu kibaya, na kuwaona kama ishara ya kwamba umefanya kitu kinachoonekana kwenye jamii, hofu hiyo hupotea ghafla. Wakati mwingine hii huwa kama alama ya heshima kwamba ulifanya kitu muhimu sana ambacho watu wengine waliona kuna haja ya wao kutoa maoni yao.

Ni jambo la kawaida kutojiamini au kuruhusu maneno ya watu yaongoze ufahamu wako. Lakini ukizitumia mbinu hizi kubadilisha ufahamu wako, utaweza kuikabili hofu ya kushindwa na kufanikiwa katika kile ulichokusudiwa ukifanye.

Continue Reading

Afya

MPANDA:  Shule inayoongoza kwa ufaulu Kyela licha ya changamoto lukuki

Published

on

Wanafunzi wa shule ya msingi Mpanda iliyopo kata ya Ipyana wilayani Kyela wanalazimika kusoma kwa kupokezana kutoka na madarasa ya shule ya kuchakaa na kutokufanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hilder `Kajubili ameiambia Fikra Pevu kuwa  shule yake inakabiliwa na upungufu wa madarasa kutokana  na ukweli kwamba madarasa yaliyokuwepo yalijengwa muda mrefu na tayari yameanguka.

Jitihada za kujenga madarasa mapya ili kuwawekea mazingira mazuri wanafunzi zimekuwa zikisuasua jambo linaloleta changamoto katika ufanisi wa walimu kufundisha darasani.

“Tuna uhaba wa madarasa sana, kwahiyo tuna double sessions (mikondo miwili) umeona madarasa tuliyanayo mengi ni magofu. Kwa hiyo tuna vyumba vya madarasa 6 tu, hao ni wengi sana (wanafunzi)wengine wanaingia mchana, wengine wanaingia asubuhi,” amesema Mwalimu Hilder.

Shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1957 ina wanafunzi 832 ambapo wavulana ni 417 na wasichana 415 ambao hutumia vyumba 6 tu. Hiyo ina maana kuwa kwa wastani kila darasa lina wanafunzi  72 ambapo ni juu  ya uwiano unaohitajika wa darasa 1 kwa wanafunzi 40 (1:40).

Awali kabla ya madarasa kubomoka wanafunzi wote walikuwa wanaingia asubuhi, lakini uchakavu na kuanguka kwa kuta za madarasa kulikosababishwa zaidi na mvua za msimu kumeifanya shule hiyo kuzungukwa na magofu.

Upungufu huo wa madarasa pia umechochewa na mwamko wa wazazi kuwapeleka watoto shuleni baada ya kuanza kwa utekelezaji wa elimu bila malipo lakini imekuwa ni changamoto kwa walimu kuwahudumia wanafunzi wote katika shule hiyo.

              Moja ya darasa liliaharibika katika shule ya msingi Mpanda

Licha ya shule hiyo kukabiliwa na upungufu wa madarasa, pia ina upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo ambapo walimu na wanafunzi wanatumia matundu 4 tu.

“Tulijenga vyoo vya muda kwanza, vyoo vya kawaida lakini ni vichache matundu yako manne; mawili wasichana na mawili wavulana. Ni vile vya kuflashi, unamwaga maji,” amesema Mwalimu Hilder.

Licha ya shule msingi Mpanda kukabiliwa na changamoto ya upungufu wa madarasa na matundu ya vyoo kwa miaka miwili mfululizo, bado walimu wameendelea kufundisha kwa moyo  na kuifanya shule hiyo kuwa miongoni mwa shule zinazofanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba wilayani Kyela.

Mathalani katika matokeo ya mwaka 2016, wakati choo cha wanafunzi kimetitia, shule hiyo ilishika nafasi ya 8 kiwilaya na mwaka uliofuata wa 2017 ilipanda na kushika nafasi ya 3  kati ya shule 42.

Naye mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo, Joyce Mwabwagilo (13) amesema wanashirikiana na walimu wao kuhakikisha mazingira yanayowazunguka ikiwemo usafi wa vyoo yanawasaidia kupata maarifa sahihi. “Masomo tuko vizuri, ufaulu uko vizuri lakini changamoto ni upungufu wa madarasa.”

Kwa upande wake, Mwalimu Douglas Mwalukasa ameiomba serikali na wadau kuguswa na hali iliyopo shuleni hapo na kuchukua hatua ya kuwaboreshea mazingira ya kufundishia ili shule hiyo iendelee kufanya vizuri kitaaluma.

“Tuna upungufu wa madarasa, vyumba kama viwili hivi. Tunaendelea kufanya juhudi kuwasiliana na wadau kuweza kutusaidia kukamilisha vyoo vipya tunavyojenga.

                Darasa lingine ambalo halina madirisha na limepata nyufa

Akizungumza na Fikra Pevu, Mratibu wa Elimu kata ya Kyela, Hezron Mwaikinda amesema wanaendelea na mipango ya kutatua changamoto za elimu katika shule za msingi ikiwemo kujenga madarasa na vyoo katika shule ambazo zina upungufu mkubwa  ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kusomea.

“Tunayo mipango kazi, kuna mambo ambayo unakuwa umepewa kipaombele kwa msimu wa mwaka huu ni kujenga madarasa na vyoo. Jukumu tulilonalo ni kuwaomba wadau mbalimbali watusaidie katika ujenzi,” amesema Hezron

Kwa upande wake, Katibu wa Muungano wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Kyela, Loth Mwangamba amesema wataendelea kushirikiana na Halmashauri ya Kyela kuhakikisha wanatafuta fedha kutoka kwa wafadhili ili kuboresha elimu wilayani humo.

Continue Reading

ELIMU

Wazazi wahoji elimu bila malipo isiyo na viwango vya ubora

Published

on

Utafiti mpya uliotolewa na taasisi ya Twaweza unaonyesha kuwa mtazamo wa wananchi kuhusu utoaji elimu bila malipo umebadilika, wengi wao wangependa kulipa ada ili elimu inayotolewa kwa watoto wao izingatie viwango  vya ubora.

Takwimu za utafiti huo zilikusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,786 katika awamu ya 23 ya kundi la pili la Sauti za Wananchi, ambapo imebainika kuwa  juhudi za serikali kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari zinaridhisha lakini changamoto iliyopo ni kupungua kwa ubora wa elimu.

Wakati sera ya elimu bila malipo ilipoanza kutekelezwa, wananchi wengi waliikubali lakini katika miaka ya hivi karibuni mtazamo wao umebadilika na wanataka kuona mfumo huo unazingatia viwango vya ubora  ili wanafunzi wapate maarifa sahihi kukabiliana na mazingira yanayowazunguka.

“Mitazamo ya wananchi kuhusu elimu bure imebadilika kwa kiasi kikubwa ndani ya miaka 12 iliyopita: mwaka 2005, zaidi ya nusu ya wananchi (56%) walisema kuwa ‘ni bora elimu itolewe bure kwa watoto wetu, hata kama kiwango cha elimu ni cha chini’,” imeeleza ripoti hiyo.

Wananchi hawa wamesema wako tayari kulipa ada ili gharamia mahitaji muhimu ya watoto wao waliopo shuleni  ili kuipunguzia mzigo serikali.

“Mwaka 2017, wananchi 9 kati ya 10 (87%) wanasema ‘ni bora tukaongeza viwango vya elimu, hata kama itatulazimu kulipa ada.’ Wananchi,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Serikali pia inaendelea kuboresha viwango vya elimu ili kuendana na ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi. Juhudi za hivi karibuni zimekusudia kuboresha stadi za msingi za kuhesabu, kusoma na kuandika kwa wanafunzi wa darasa la 2, kuboresha mfumo wa kuhakiki ubora wa elimu, kuwezesha wanafunzi kumaliza shule na kuongeza idadi ya wasichana wanaojiunga na elimu ya sekondari.

Pamoja na malengo mazuri ya sera hii ya elimu bila malipo ya ada iliyoagizwa na waraka wa elimu namba 5 wa mwezi Disemba mwaka 2015, bado kuna changamoto katika upatikanaji na ubora wa elimu nchini Tanzania.

Hata hivyo, dhana ya wananchi kutaka kulipa ada inatokana na dhamira waliyonayo ya kupenda kuona jitihada za serikali zikilenga kuboresha elimu kuliko kupunguza gharama za elimu.

“ Hii inaongeza ushahidi zaidi kwenye wazo kuwa wananchi wanapendelea jitihada ambazo zitaboresha elimu kuliko zile zinazopunguza gharama ya elimu,’ imebainisha ripoti hiyo.

Imani ya wananchi ni kuona ubora wa elimu unaenda sambamba na kuwawezesha na kuwawekea walimu mazingira mazuri ya kufundishia ili wanafunzi wapate maarifa yatakayowakomboa kifikra na kimaisha.

“Walipoulizwa iwapo wangependa mpango wa serikali wa kugawa sare za shule bure kwa watoto wao au mpango wa kutoa mafunzo ya ziada na kuwasaidia walimu, wananchi tisa kati ya kumi (87%) walichagua mpango wa kutoa msaada na mafunzo kwa walimu,” imefafanua zaidi ripoti hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza, Aidan Eyakuze amesema, Mitazamo ya wananchi inaonekana kubadilika kwa kiasi kikubwa katika kipindi fulani, ikiashiria kuwa sasa wanaelewa kilichofanyika na walichopoteza. Utafiti huu unadhihirisha kuwa wananchi wanapaswa kuwa sehemu muhimu ya mjadala wa kitaifa utakaolenga kuboresha matokeo ya elimu yetu.”

Naye Mwandishi wa Vitabu na Mwanaharakati wa Haki za Watoto, Richard Mabala amesema wananchi wasiwanyooshee vidole wanasiasa juu ya mstakabali wa elimu nchini badala yake watafute njia mbadala za kuwasaidia watoto wao.

“Tusipende kuwaandama Wanasiasa kuhusu kuwapeleka watoto wao shule binafsi; watu wengi pia wanasomesha watoto shule binafsi. Tatizo kuu ni kuwepo kwa ‘vote of no confidence’ kwa shule za Serikali na hili linapaswa kumulikwa,” amesema Mabala.

Akitoa maoni yake kuhusu matokeo ya utafiti huo, Dk. Perpetua Kessy Nderakindo kutoka chama cha NCCR Mageuzi amesema wazazi wengi wamepitia kwenye mfumo wa elimu uliopo na wameona madhara yake hivyo wako tayari kufunga mkanda kupigania elimu ya watoto wao.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk. Richard Shuka ameishauri serikali kuboresha mazingira ya kusomea na kujifunzia katika shule za serikali ili watoto wa maskini ambao hawana uwezo wa kulipa ada wafaidike na elimu hiyo.

‘Kumsaidia mtoto wa Masikini sio suala la kuandikisha watoto ni kuweka jitihada za makusudi kuibOresha hii elimu,” ameshauri.

Labda kwa kusikiliza sauti za wazazi na kuwawezesha kujihusisha na masuala ya shule, Tanzania inaweza kupiga hatua kubwa katika kuhakikisha watoto wote wanapokea haki yao ya kupata elimu bora.

Continue Reading

Must Read

Copyright © 2018 FikraPevu.com