KWA Monica Ibrahim, kahaba anayefanya shughuli zake pale Mbeya Carnival Night Club, mapenzi ni furaha iliyopotea kitambo kwa kuwa inamletea majeraha mengi maishani mwake, kiasi cha kumlazimu kuendesha maisha ya ukahaba ambayo awali aliyachukia mno.

Mara ya kwanza alipobakwa na kijana mmoja kijijini kwake Sungwi, Kisarawe, Pwani wakati wa likizo akiwa anasoma sekondari alijua kwamba ni ajali tu kwa sababu alimpenda pia kijana huyo ingawa hakuwa tayari kwa wakati huo na hakuthubutu kuripoti tukio hilo popote, lakini wakati mapenzi ya kweli yalipoibuka, mambo yakageuka kuwa mabaya zaidi.

“Niliolewa na mwanamume ambaye nilimpenda. Alikuwa kama mfalme kwangu kwa sababu alionesha mapenzi ya dhati na kunijali. Tulibahatika kupata watoto wawili kwenye ndoa yetu – kwa kiume na wa kike.

“Lakini ghafla, mambo yakabadilika. Mume wangu akaanza kunipigia bila sababu za msingi, anachelewa kurudi na akija amelewa chakari, wakati mwingine harudi kabisa nyumbani hata kwa siku tatu akisingizia alikuwa na shift kazini,” Monica alimweleza mwandishi wa FikraPevu akielezea masahibu ambayo baadhi ya wanawake wanakumbana nayo katika ulimwengu wa mapenzi.

Anasema alilazimika kuikimbia nyumba yake jijini Dar es Salaam, maeneo ya Kunduchi, asubuhi moja wakati mumewe, akiwa hajarudi kwa siku mbili, aliporejea ‘kutoka kazini’ (alikuwa mhudumu wa hoteli moja katikati ya Jiji la Dar es Salaam) akiwa amelewa chakari kama kawaida yake, akajitupa kitandani bila kuvua nguo na kumlazimu yeye kumvua nguo kama ilivyokuwa ada.

Ilikuwa ni wakati akimvua nguo hizo ndipo alipogundua kwamba mumewe alikuwa bado amevaa kondomu iliyotumika!

“Kosa kubwa nililolifanya ni kumuuliza. Pombe zilimtoka na akanipiga vibaya, kipigo ambacho sitaweza kukisahau maishani. Yule mwanamume nusura aniue. Nashukuru majirani walitokea kwa wakati na kuninusuru na wakanipeleka hospitali ya Mwananyamala ambako nililazwa kwa wiki mbili.

“Naambiwa hata uso wangu ulikuwa hautamaniki, achilia mbali viungo vingine kiasi cha kushindwa hata kunyanyua mikono. Yeye hakuwahi kuja kunitazama hata mara moja na nilipopona na kuruhusiwa kutoka tu nikaamua kuja Mbeya kwa shoga yangu ambaye naye kazi yake ni kama yangu sasa.

“Kwangu mimi wanaume ni kama wanyama ambao wanatakiwa kuchunwa tu na haijalishi unawachuna kwa namna gani. Ninapenda kuwaona wakiwa wameumia na hiyo inanipa faraja. Natafuta mwanamume mwenye pochi iliyonona, hasa walevi. Nikimpata, ninapendelea tunywee pombe chumbani kwenye faragha. Wenyewe wanadhani ninawapenda, lakini hapana. Ninachowafanyia huko ndani huwaacha wakipiga kelele kwa miezi, au hata miaka,” anasema bila kupepesa macho.

“Tazama hii!” Anamuonesha mwandishi wa FikraPevu vidonge vya valium ambavyo ni vya usingizi na mara kadhaa hupewa wagonjwa wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji.

“Mara tunapokuwa chumbani, nikishaona mwanamume amelewa, ninachanganya kwa hila na pombe yake na kumshawishi kimahaba aendelee kunywa na baada ya dakika chache tu anakuwa hajitambui. Hapo ndipo ninapompukutisha kila kitu na kutokomea.”

Monica ni miongoni mwa wanawake na wasichana wengi wanaofanya biashara ya ukahaba katika eneo la Mbeya Carnival, klabu pekee na maarufu jijini humo iliyoko pembeni mwa barabara kuu ya kwenda Zambia katika eneo la Mafiati, ambayo mara nyingi hufurika watu kuanzia Ijumaa hadi Jumapili huku bendi mbili za jijini humo – Itumba na Baby TOT – zikiwa zinatumbuiza.

Ukipita katika eneo hili nyakati hizo, utakuta magari mengi yakiwa yameegeshwa nje, wakati ndani kuna kelele zinazotokana na muziki wa zilipendwa unaoporomoshwa na bendi hizo huku eneo la kuchezea likiwa limesheheni watu.

Baadhi ya wasichana wanacheza bila kupumzika kwani hawawezi kuketi kwa sababu hawana fedha za kununulia vinywaji, ingawa siyo dhambi kupumzika.

Rafiki yangu mmoja ananiambia kwamba wengi kati ya wasichana hao wako kazini, wanawawinda watu wanaohitaji huduma ya ngono kwa malipo.

“Mbeya ni miongoni mwa majiji makubwa Tanzania, nah ii ndiyo klabu pekee ya usiku ambako watu wengi, wakiwemo wale wanaosafiri kwenda nje ya nchi, huamua kuja kupoteza muda wao. Kama ilivyo kwa Dar es Salaam, Mwanza na Arusha, ukahaba umeshamiri jijini Mbeya kama unavyoona. Wengi si wazaliwa wa hapa, wanatoka kila kona ya Tanzania,” rafiki yangu ananieleza.

Mwandishi wetu alijikuta akitikisa kichwa kwa masikitiko akifikiria ni aina gani ya maisha ambayo jamii yetu imeyachagua na vipi kuhusu janga la UKIMWI.

Monica ni mmoja tu kati ya wanawake wengi wanaofanya ukahaba nchini Tanzania, huku wengi wao wakiwa wameingia kwenye biashara hiyo bila kupenda bali wamelazimishwa na sababu mbalimbali za kijamii, ikiwemo ugumu wa maisha, manyanyaso katika familia na hata kubakwa na wanaume wasio na utu – wakiwemo wanandugu.

Kwa mfano, tofauti na sehemu nyingi, makahaba katika maeneo mengi ya Jiji la Mwanza huwa hawajiuzi barabarani, bali hupita kila hoteli na nyumba ya wageni wakigonga milango.

Wakati fulani nikiwa jijini humo niliwahi kugongewa mlango mchana kweupe, nikadhani ni mhudumu, lakini nilipofungua nikakutana na mabinti watatu ambao umri wao haukuwa zaidi ya miaka 18 na walistahili kuwa shule – kama siyo sekondari basi hata chuoni.

Kabla hata sijawakaribisha, wote wakajitoma ndani, wakiwa wamevalia mavazi ambayo walistahili kuvaa usiku.

“Niwasaidie nini?” Nikauliza kwa mshangao.

Badala ya kujibiwa kwa maneno, kila mmoja akaanza kujinadi kwa ama kuonyesha matiti yake au tabasamu.

“Tuangalie, yupi uliyependezwa naye? Au hata ukitaka wote tubaki hapa sawa tu!” ndilo jibu nililoambulia. Wawili tayari walikuwa wamejikaribisha kitandani na mmoja akiwa ameketi kwenye sofa lililopo humo chumbani.

Kwa hasira nilifoka na kuwataka watoke haraka, lakini katika mshangao wangu ndiyo kwanza wakaanza kunicheka.

“Wewe mgeni Mwanza eeh? Sisi tunapita humu kwa sababu tunatambua wapo wanaume wengi wanaogopa kwenye barabarani kutafuta wanawake wa kuwastarehesha, sasa wewe kaka unaonekana mshamba.”

Nilitamani nimzabue kibao, lakini nikasita, na wakati huo huo wawili wakatoka haraka na kumwacha mwenzao aliyeketi kwenye sofa ambaye wala hakuonyesha mshtuko.

“Wewe mbona hutoki?” nikamuuliza kwa ukali.

“Sikiliza kaka yangu, najua unaweza kuwa mgeni, sikulaumu… hata hivyo, sisi hatufanyi hivi kwa kupenda, maisha ni magumu na hatuna pa kwenda,” akanieleza.

Binti huyo, ambaye alijitambulisha kama Bhoke, alisema kwamba alikimbia kijijini kwao huko Tarime baada ya baba yake kumlazimisha aolewe miaka mitatu iliyopita wakati akiwa kidato cha kwanza.

Alipomweleza kwamba hataki kuolewa anataka kusoma, baba yake akaapa kwamba angemuua kwa kuwa tayari alikuwa amepokea ng’ombe saba kwa ajili ya mahari.

“Nikakimbia kwenda Musoma na baadaye nikaja hapa Mwanza. Usiniulize nilifikaje, lakini mwili wangu huu huu ndio ulionifikisha hapa na ninaishi kwa kuutegemea, ingawa ndoto zangu nilitaka kuwa nesi,” alisema binti huyo kwa masikitiko.

Ukahaba umekuwa mada kubwa kwenye mijadala mingi kuhusiana na janga la ugonjwa wa UKIMWI. Vyombo karibu vyote vya habari vinaandika kuhusu maambukizi ya virusi vya UKIMWI na wanawatazama makahaba kama kundi linalochangia kwa kiwango kikubwa maambukizi hayo.

Serikali na mashirika yanayojihusisha na mapambano dhidi ya UKIMWI yanasema makahaba na ukahaba ndilo eneo linalochangia.

Kiwango kikubwa cha maambukizi ya virusi na watu wanaoishi na virusi kimeonekana kwa watu wanaojihusisha na ukahaba – makahaba wenyewe na wateja wao – na hata pale kiwango cha maambukizi kinapokuwa chini kwenye kundi hilo, mara nyingi kinakuwa juu kuliko kiwango kinachoonekana kwa watu wazima wenye maambukizi.

“Samahani kaka. Unaweza kuninunulia kinywaji?” sauti ya kike inayotokea nyuma yangu inanigutusha kwamba kumbe ningalipo jijini Mbeya. Ninageuka na kuwaona wasichana wawili wakiwa wamesimama mezani kwetu.

Rafiki yangu anajaribu kusema jambo fulani lakini ninamkatisha kwa kuvuta kiti kumkaribisha mmoja wao wakati mwenzake tayari alikwishajikaribisha kwenye kiti kingine. Bia mbili zinaletwa kwa ajili yao kupitia kwenye ‘bill’ yetu.

“Mbona hunywi bia?” msichana wa kwanza ananiuliza baada ya kuona nakunywa soda wakati rafiki yangu akingwa bia. Namweleza kwamba sijisikii vyema kutokana na uchovu wa safari. Hili linaonesha kumkera na anataka kunyanyuka, lakini namsisitiza aketi kwani tungependa tuzungumze.

“Mimi sipendi ‘kampani’ ya mtu asiyekunywa pombe, kila wakati yuko macho tu na hiyo siyo staili yangu ya kufanya kazi. Huwezi kumtoroka ukishamnywea bia zake. Haijalishi, inaonekana wewe ni mgeni, bora rafiki yako huwa namuona hapa. Jina langu ni Halima Mgaya na rafiki yangu hapa anaitwa Joyce Chagula. Asante kwa vinywaji,” anasema.

Wakati muda ukiendelea kusonga pengine kutokana na bia tatu alizokunywa, bila kuulizwa, Halima anaanza kuwalaani wazazi wake, hasa baba yake aliyeoa matala, ambaye hakumpeleka shule ingawa alichaguliwa kuendelea na kidato cha kwanza.

“Ninamchukia, kwa sababu kama asingekuwa yeye, sasa hivi ningekuwa mchumi. Yeye ndiye aliyeababisha niwachukie wanaume kwa sababu hakutimiza wajibu wake kama mzazi. Unaweza kuwa baba halafu huwahudumii watoto?

“Sikuomba nizaliwe, lakini yeye na mama ndio walionileta duniani. Hakuna hata mmoja kati yetu aliyesoma sekondari, sasa nikiwa mtoto wa mwisho kuzaliwa, nilidhani baba angebadili mawazo yake na kunipeleka. Badala yake akaondoka na kutuacha – watoto wote 11 – kijijini na kupotelea anakokujua yeye.

“Nadhani wanaume wote wako sawa tu na ninawachukia,” alisema na kuongeza kwamba ana miaka 19.

Halima anasema anapendelea kulala na wanaume waliooa kwa sababu wanajua jinsi ya kumhudumia mwanamke na humwachi fedha nyingi tofauti na vijana wasiooa.

“Najua hiyo siyo sahihi, lakini inatokea tu kwamba wateja wangu wote ni watu waliooa. Najiuliza pengine wake zao huwa hawawatoshelezi ndiyo maana wanakwenda kutafuta ngono nje hata kwa gharama. Inaniuma kufikiria kwamba huenda hata mama hakuwa akimhudumia vyema baba ndiyo maana akaamua kutafuta  wanawake wengine.

Lakini mwanamke anaposhindwa kutimiza majukumu yake, wacha mwanamke mwingine afanye kwa niaba yake!” anasema.

Makahaba daima wana wapenzi wengi. Hii inamaanisha kwamba, kama watakuwa wameambukizwa virusi vya UKIMWI, basi wanaweza kuviambaza kwa wateja wengine – kwa kujua ama kutokujua – hivyo kuongeza maambukizi katika jamii.

Ingawa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) imeeleza kwamba maambukizi ya Ukimwi yameshuka kwa asilimia 20 kati ya mwaka 2010 na 2015 kufikia asilimia 5.1, lakini hali bado ni mbaya na inatisha, kwani kati yao asilimia 6.2 ni wanawake na asilimia 3.8 ni wanaume.

Maambukizi mapya yameshuka zaidi kwa watoto duniani kote kutoka watoto 290,000 mwaka 2010 hadi kufikia watoto 150,000 mwaka 2015, huku maambukizi kwa watu wazima yakiwa hayajashuka tangu mwaka 2010. Nchini Tanzania, watu milioni 1.4 wanaishi na Virusi vya UKIMWI.

Mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa ndiyo inayoongoza kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi nchini ambayo inaongoza kwa asilimia 14.8, asilimia 9.1 na 9 mtawalia.

Mikoa mingine na asilimia za maambukizi katika mabano ni Ruvuma (7.2), Shinyanga (7.4), Dar es Salaam (6.9) Rukwa (6.2), Katavi (5.9), Pwani (5.9), Tabora (5.1), Kagera (4.8) na Geita (4.7).

Mikoa mingine aliyoitaja ni Mara (4.5), Mwanza (4.2), Mtwara (4.1), Kilimanjaro (3.8), Kigoma (3.4), Simiyu (3.6), Morogoro (3.8), Singida (3.3), Dodoma (2.9), Manyara (1.5), Lindi (2.9), Tanga (2.4), Unguja (1.9) na Pemba (0.3).

Kujikinga na maambukizi ya virusi kwa watu wanaojihusisha na biashara ya ukahaba umekuwa ndio mkakati wan chi nyingi katika mapambano dhidi ya UKIMWI, huku njia ya ngono salama ikisisitizwa.

“Pochi yangu imejaa kondomu – za kike na za kiume. Nikipata mteja namwambia kwamba nataka ngono salama, lakini wengine ni wabishi hawataki kutumia, hivyo ninapaswa kujilinda mwenyewe, ninaamua kuvaa kondomu ya kike bila mwenyewe kujua, na hasa kwa vile wengi wanakuwa tayari wamekwishalewa na hawahitaji mambo yoyote ya utangulizi ambayo hata mimi sina haja nayo. Maisha ni muhimu sana kwangu,” anasema Joyce Chagula.

Neno 'changudoa' au ‘kahaba’ linamaanisha mlolongo mrefu wa watu wanaojihusisha na biashara ya ngono katika mazingira tofauti. Hawa ni pamoja na wanawake, wanaume na wanaopenda kufanya ngono ya jinsia moja (mashoga na wasagaji) ambao wanaweza kufanya kama kazi yao ya kudumu ama ya muda, kwenye madanguro, au baa, au hata barabarani na hata majumbani.

“Ni biashara ya aibu, ndiyo. Lakini tutafanyaje? Maisha siyo rafiki kabisa.” Anasema Monica. “Kama ningesoma, ningetafuta kazi nzuri, lakini sina fedha za kuanzisha biashara rasmi. Unaweza kujiunga na VICOBA lakini mikopo yake haikidhi. Ninachokifanya ama kukipata hapa ni kwa ajjili ya kushibisha tumbo tu, wakati mwingine unampata mteja ambaye hakukupi hata senti, anakwambia bia ulizokunywa zinatosha!”

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Vifo vyashamiri kwa wanaotoa mimba Tanzania. Wazanzibari wafanya ngono wakijitambua

WANAWAKE 390,000, kati ya milioni moja, nchini Tanzania hutoa mimba kila mwaka kwa njia ...

Mazingira: Mirija ya plastiki changamoto nyingine uhifadhi wa vyanzo vya maji

Licha ya juhudi mbalimbali za serikali na wadau wa uhifadhi wa mazingira kuzuia matumizi ...

Bagamoyo: Matumizi ya kondom bado ni kitendawili

Wakati nchi yetu ikiwa katika kampeni ya kuhamasisha  matumizi ya njia za uzazi wa ...