Ugonjwa wa ‘presha’ kitanzi kipya kwa wazee, serikali ichukue hatua haraka

UGONJWA wa shinikizo la damu, maarufu kwa jina la 'presha,' unatajwa kuwa kitanzi kipya katika maisha ya wazee Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza.

“Ugonjwa huu unaua!” Wataalamu wa masuala ya afya wanasema, wazee wengi nchini wanakabiliwa na tatizo hilo ukiwamo ugonjwa wa kisukari.

Imebainika kwamba, jamii hiyo ya wazee wilayani Magu inaishi na ugonjwa huo bila wahusika kujitambua.

Hali hiyo inatokana na kutokuwa na uwezo wa kwenda hospitalini kupima afya zao, umasikini na kukosa usaidizi wa kutosha kutoka kwa familia, jamii na serikali kwa ujumla.

Kifaa cha kupima presha.

Zaidi ya wazee 500 kati ya idadi inayotajwa kuwapo 100, 507 Wilaya ya Magu, kati ya wakazi wote 299,759 waishio humo, wamepimwa na kugundulika kuwa na ugonjwa huo wa shinikizo la damu, wengi wao wanatajwa kuwa wanawake.

Halikadhalika, wazee 200 nao wamebainika kuwa ma ugonjwa wa kisukari wilayani humo. Hizi ni takwimu zilizotolewa na idara ya afya wilayani Magu, Februari 2017.

Utafiti unasema asilimia 80 ya idadi yote ya wazee Wilaya ya Magu iliyopo Mashariki mwa Mkoa wa Mwanza, wanaishi vijijini.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) linasema silimia 50 ya watoto yatima Tanzania, wanalelewa na wazee hasa bibi zao, kutokana na kuzaliwa nje ya ndoa.

Miongoni mwa vyanzo vya ugonjwa huo ni pamoja na umasikini, ongezeko la kemikali kwenye figo (renin), kutelekezwa na familia zao, kushindwa kufanyakazi kwa kichocheo kiitwacho Insulin.

Utafiti unasema kwamba, presha ya kawaida huwa ipo 120 – 80, presha inayoelekea kupanda 120-139 80-89.

Presha hatua ya kwanza ni 140-159 90-99, presha hatua ya pili ni 160-179 100-109 na presha hatua ya tatu kiwango chake katika vipimk ni 180-110. Ifahamike kuwa presha inaua.

Kilio cha wazee

Mzee Matondo Joshua (70) mkazi wa Wilaya ya Magu, yeye anaamini wazee ni nguzo muhimu katika maendeleo na amani ya nchi.

Kwamba Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli, itafute ufumbuzi wa haraka dhidi ya maradhi hayo yanayowaandamana zaidi wazee wa kuanzia umri wa miaka 60.

Anasema kuwa, ingawa hafahamu kama ana tatizo la ugonjwa wa shinikizo la damu, lakini muda mwingi mapigo ya moyo wake yanakwenda kasi na kukosa raha.

Mzee huyo aliyekuwa akiongea kwa lugha ya Kisukuma, anasema hana uwezo wa kutembea kutoka umbali mrefu hadi hospitali ya Wilaya ya Magu, kwenda kupima afya yake.

"Naamini hata hospitalini hakuna dawa. Nitakwenda na nini huko Magu? Naomba tusaidiwe vipimo na dawa.

"Mimi nashauri Serikali ianze kuzunguka kutupima sisi wazee, ili ijuwe matatizo yetu ya kiafya halafu ututibu bure. Tulilomba mhola guke," anasema mzee huyo, huku akimalizia kwa kusema katika lugha ya Kisukuma, akimaanisha kwamba, 'wanaomba uzima tu.'

John Katinde (71) yeye anakiri wazee wengi kusumbuliwa na ugonjwa huo wa shinikizo la damu.

Anasema ugonjwa huo unawaandama zaidi wazee kutokana na sababu kuu tano. Mosi, umasikini, pili, kutelekezwa na familia zao.

Tatu, msongo wa mawazo, nne, kukosa huduma bora za afya, tano, dawa kutokuwapo za kutosha hospitalini.

"Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ianzishe kampeni maalumu ya kuwapima bure wazee ugonjwa wa presha (shinikizo la damu). Wazee wasitelekezwe.

"Ikianzishwa kampeni hii kwanza itasaidia Serikali kujua ukubwa wa tatizo la shinikizo la damu kwa wazee, halafu ndiyo inatafuta mbinu ya kukabiliana nao," anasema mzee Katinde.

Haijaripotiwa mzee yeyote kupoteza maisha wilayani Magu, kutokana na ugonjwa huo wa shinikizo la damu, ingawa tatizo hilo linatakiwa kudhibitiwa.

Mzee Katinde ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wilayani Magu (Macsonet), Wizara ya Afya inao wajibu wa kuanzisha maabara za kutembea zitakazotumika kupima afya za wazee vijijini.

Sofia Maduhu (81) yeye analishukuru Shirika la Maperece linaloshughulika na utetezi wa wazee wilayani Magu, kutoa mashine za kupima shinikizo la damu kwa wazee wilaya hiyo na kuwapatia dawa za kupunguza tatizo hilo.

Holo Nkwabi (68), Juma Bahame (72) na Suzana Samuel, na baadhi yao waliokataa kutaja majina yao wanaiomba Serikalini kuanza kuwalipa wazee pensheni kama wanavyolipwa wenzao wa Zanzibar.

Wazee hao wa wilayani Magu wanasema kulipwa kwao pensheni itawasaidia kupunguza ukali wa maisha, pamoja na kupata uwezo wa kununua dawa na chakula.

Hali ikoje?

Chanzo kikuu cha ugonjwa wa shinikizo la wazee Wilaya ya Magu ni umasikini unaowakabili baadhi yao.

Sababu nyingine ni kutelekezwa na familia zao, kukosa usaidizi wa karibu katika mahitaji yao, unyanyapaa, unywaji wa pombe zikiwamo za kienyeji (gongo) na uvutaji wa sigara.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Dkt. Kudisala Kulwa, anathibitisha wazee 500 waliopimwa hadi kufikia Februari mwaka huu, wana tatizo la ugonjwa huo wa shinikizo la damu.

"Wazee wengine 200 waligundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari. Hili ni tatizo kubwa kwa afya za wazazi wetu hawa," Dkt. Kudisala anaiambia FikraPevu.

Inatajwa hivi sasa idadi hiyo inaweza kuwa imeongezeka hadi kufikia zaidi ya wazee 1,000 wanaosumbuliwa na maradhi hayo wilayani Magu.

Mganga mfawidhi huyo wa Hospitali ya Wilaya ya Magu, anataja mojawapo ya vyanzo vya ugonjwa huo ni pamoja mishipa ya moyo na figo kuchoka kufanyakazi.

"Licha ya mwaka huu Wilaya ya Magu kuongoza kitaifa kutoa huduma bora kwa wazee, sisi tunapoagiza dawa tunahakikisha tunaweka bajeti ya dawa za wazee," anasisitiza Dk. Kudisala.

FikraPevu  Uchunguzi umebaini kwamba, kazi ya upimaji wa ugonjwa huo kwa wazee Serikali imeiacha mikononi mwa Shirika moja la kiraia la Maperece.

Kwa mujibu wa utafiti, zaidi ya sh. Milioni 12 zimetumiwa na Shirika la Maperece kwa ajili ya kutoa vifaa na mashine 60, za kupima ugonjwa huo dhidi ya wazee wilayani humo.

"Uzee haukwepeki. Shirika la Maperece tumetoa mashine hizi kwa wazee wetu hapa wilayani Magu, ili wawe wanazunguka kuwapima pia wazee wenzao ugonjwa wa presha.

“Ugonjwa huu kwa sasa unaonekana kuwa tatizo kwa waze wetu, lazima tupambane nao kuhakikisha tunawasaidia," Julius Mwengela, Mratibu wa Shirika la Maperece anaiambia FikraPevu.

Utafiti uliofanyika mwezi Machi 2013, uliowasilishwa kwenye Mkutano wa Chama cha Wenye Matatizo ya Moyo huko New Orleáns, nchini
Marekani, unasema:

"Matumizi ya chumvi kupita kiasi yalichangia vifo vilivyohusiana na matatizo ya moyo vya watu milioni 2.3 duniani kote."

Asilimia 42 ya watu hao walifariki dunia kutokana na magonjwa ya moyo. Asilimia 41 walifariki kwa ugonjwa wa kiharusi.

Hii ni kwa mujibu wa vifo vilivyorekodiwa mwaka 2010 tu. Hivyo, Tanzania ni vema ikaanzisha kampeni ya utoaji elimu kwa wananchi kujikinga na ugonjwa wa shijikizo la damu.

Kwa mujibu wa utafiti huo, nchi inayoongoza kwa watu wake kula chumvi nyingi kuliko nchi zote duniani ni Kazakhstan iliyopo Asia ya Kati,
jirani na nchi ya Urusi.

Nchi ya Kenya na Malawi zinatajwa kuwa na matumizi madogo zaidi ya chumvi kwa raia wake barani Afrika.

Madaktari bingwa wanasema, wastani wa kiwango cha chumvi unaokubalika kiafya ambao mtu anatakiwa kula kwa siku, ni miligram 2,300 tu. Hii ni Sawa na kijiko kidogo cha chumvi kwa siku moja.

WHO wanasemaje?

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinasema, tayari watu bilioni moja duniani kote wanaathiriwa na shinikizo la juu la damu.

Kwamba maradhi hayo yanasababisha mshtuko wa moyo (Heart Attacks), kupooza na kiharusi (Strokes).

Kwa mujibu wa shirika hilo, takribani watu milioni nane hufariki dunia kila mwaka kwa ugonjwa huo wa kupanda kwa shinikizo la damu.

Kauli ya viongozi

Halmashauri ya Wilaya ya Magu inasema, kazi ya kushughulikia tatizo hilo linatekelezwa na Shirika la Maperece, linaloshughulikia haki za wazee wilaya hiyo.

"Suala hilo la wazee linashughulikiwa na Shirika la Maperece," anasema Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hilari Elisha wakati akizungumza na FikraPevu.

Elisha anasema kwamba, halmashauri inafanyakazi ya kutoa matibabu bure kwa wazee wilayani humo.

Mkuu wa wilaya hiyo, Khadija Nyembo, alipoulizwa namna Serikali wilayani humo inavyoshughulikia kudhibiti ugonjwa huo wa shinikizo la damu kwa wazee, naye alianza kwa kulitupia mpira Shirika hilo la Maperece.

"Maperece wapo wanawasaidia. Wazee wanatibiwa bure, sasa kampeni ya nini?" alihoji kwa njia ya simu mkuu huyo wa Wilaya ya Magu.

Hata hivyo, DC Nyembo akasema tena: "Ukienda pale hospitali ya wilaya (Magu) utaambiwa pisha mzee, pisha mzee atibiwe kwanza. Tunafanya vizuri."

FikraPevu inaamini kuwa viongozi wa idara ya afya na serikali kwa ujumla wilayani humo, bado hawajaona umuhimu wa kupambana na tatizo la ugonjwa huo unaoua!

Jitihada zaidi zinatakiwa kufanyika, ikiwamo kufanyika kampeni ya upimaji wa ugonjwa wa shinikizo la damu kwa wazee waishiyo vijijini.

Kadhalika, maabara na kliniki za kutembea zinatakiwa kupelekwa vijijini kwa ajili ya kazi hiyo, ili Serikali na jumuiya nyinginezo zifahamu ukubwa au udogo wa tatizo hilo kwa jamii ya wazee.

Mratibu wa Mradi wa Kulinda na Kutetea Haki za Wanawake Wazee kutoka Maperece, Gres Rububula, anasema shirika hilo limekuwa likitoa elimu ya umuhimu wa wazee kupima afya zao.

"Jitihada za pamoja baina ya Serikali na mashirika ya kiraia zinatakiwa, ili kuokoa maisha ya wazee wetu," Gres anaiambia FikraPevu na kuongeza;

"Wazee wanaporwa mashamba yao, wananyanyaswa. Tunataka mzee aheshimiwe na athaminiwe mbele ya jamii na kisheria pia."

Mambo ya kuzingatia

Ili kuondoa au kupunguza tatizo la ugonjwa huo, serikali inapaswa kuzingatia mambo makuu matano.

Mosi; ianzishe kampeni maalumu ya upimaji afya hususani ugonjwa wa shinikizo la damu kwa wazee, kwa kutumia maabara na kliniki zinazotembea.

Kwani baadhi ya wazee hawana uwezo wa kusafiri au kutembea, hadi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupima afya zao.

Pili; serikali isambaze vifaa vya kupima maradhi ya shinikizo la damu wilayani Magu na kwingineko nchini, ili kubaini ukubwa wa tatizo kisha kulitafutia ufumbuzi kwa faida ya jamii na taifa kwa ujumla.

Tatu; viongozi wa Serikali na mashirika ya kiraia waelimishe jamii umuhimu wa kupima afya zao, kunguza uzito wa mwili, kupunguza ulaji wa chumvi nyingi, wazee wale vyakula vingi vyenye potasiamu na vyenye vitamini D.

Nne; elimu itolewe kwa jamii kupunguza unywaji wa pombe, kunywa vidonge vyenye kalisi na magnesi, kula vyakula vyenye makapi mengi na kutovuta siga.

Suala la tano na muhimu linalotakiwa kuzingatiwa na Serikali; Ni wazee kulipwa pensheni angalau sh. 100,000 kila mwezi.

Ulipwaji wa pensheni kwa wazee utasaidia watu hao waliopigania uhuru wa nchi, kuendesha miradi yao ya kiuchumi itakayowakwamua umasikini, pamoja na kupata fedha za kununua chakula na dawa.

FikraPevu inafahamu kuwa chocolate zina aina ya kirutubisho kiitwacho flavanols, kinacholainisha mishipa ya damu na kuwezesha damu kutembea vizuri mwilini.

Utafiti unasema asilimia 18 ya wagonjwa wa presha waliokula chokoleti, walionesha kupata ahueni kwa tatizo hilo kushuka.

Hivyo mtu mwenye ugonjwa wa presha anashauriwa kula angalau chokoleti moja kwa siku, iliyotengenezwa kwa cocoa.

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Udumavu, utapiamlo wawatesa viongozi wa Afrika, wahaha kuokoa maisha ya watoto wanaokufa kila mwaka

Viongozi wa Afrika wamekubaliana kuondoa vikwazo vya lishe vinavyowazuia watoto na jamii kutambua na ...

Waendesha bodaboda wanachangia asilimia 13 ya mimba za utotoni nchini

Kuna uhusiano gani kati ya bodaboda na ongezeko la mimba za utotoni kwa wasichana wanaosafiri ...