Connect with us

DATA

Ucheleweshaji wa miradi ya maji unavyowagharimu wananchi vijijini

Published

on

Baadhi ya wananchi wa vijijini nchini huenda wakasubiri kwa muda kupata maji ya uhakika baada ya Serikali kushindwa kufanikisha ujenzi wa zaidi ya nusu ya vituo vya huduma hiyo muhimu katika maisha ya mwanadamu.

Takwimu zilizopo katika ripoti ya maendeleo ya sekta ya maji mwaka 2016, zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2010/11 na mwaka 2015/16, Serikali ilipanga kujenga jumla ya vituo vya maji 99,515 lakini ilishia kujenga vituo 42,718 pekee.

Vituo hivyo vilivyojengwa ni asilimia 43 tu ya malengo jambo ambalo linaloonyesha kuwa idadi kubwa ya wananchi waliotakiwa kupata huduma hiyo wameshindwa kupata kwa wakati.

Hali hiyo siyo bahati mbaya. Ripoti hiyo iliyotolewa Oktoba mwaka jana inaeleza kuwa theluthi ya miradi hiyo ya maji haikutekelezwa ndani ya awamu ya kwanza ya mpango wa maendeleo ya sekta ya maji (WSDPI) jambo lilofanya baadhi ya vituo vya maji vichelewe kujengwa.

“Hadi Juni 2016, jumla 1,210 kati ya 1,810 iliyopangwa ilikuwa imetekelezwa na kusambaza maji kwa wananchi. Miradi mingine 374 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji katika mwaka huu wa fedha wa 2016/17,” inasomeka sehemu ya ripoti.

Kwa mujibu wa wizara ya maji na umwagiliaji, utekelezaji wa miradi hiyo ilikwama kutokana na sababu mbalimbali yakiwemo masuala ya kifedha.

Wizara hiyo imeeleza kuwa ugawaji wa fedha kwa halmashauri ulizingatia kanuni maalum badala ya mahitaji halisi ya mamlaka zilizotakiwa kuitekeleza na kuzisababishia kushindwa kupata kiwango kinachotakiwa kufanikisha miradi.

Mbali na matatizo katika mgawanyo, pia hakukuwa na fedha za kutosha kugharamia miradi hiyo.

“Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulikuja na miradi ambayo haikuwa na fedha za kuitekeleza,” inasema ripoti hiyo iliyochambuliwa na Fikra Pevu.

Hata wakati kukiwa na matatizo, ripoti hiyo inaeleza kuwa baadhi ya halmashauri hazikuweka miradi ya maji kama kipaumbele huku usimamizi wake ukilegalega.

Pamoja na kutofikiwa kwa malengo hayo, bado vituo hivyo vimekuwa vikiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka Julai 2007 japo si kwa kasi na malengo yaliyotarajiwa.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa vituo vya maji viliongezeka kutoka 2,603 mwaka 2017/08 hadi kufikia 50,995 na kuwanufaisha wananchi milioni 11.6.  

Kwa pamoja, ripoti hiyo inabainisha kuwa hadi mwaka jana,  Serikali imefanikiwa kujenga vituo vya maji  95,733 vinavyowahudumia wananchi 22.79 milioni waishio vijijini Tanzania bara ikiwa ni takriban robo tatu (asilimia 72) ya watu wote wanaoishi katika maeneo hayo kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012.

Kiwango cha wananchi wanaopata maji vijijini kimekuwa mwenendo mseto. Kimekuwa kikipanda na kushuka kutoka mwaka 2005. Kiwango cha juu kufikiwa ni mwaka jana hasa baada ya kuporomoka hadi asilimia 49 mwaka 2013 ikilinganishwa na asilimia 54.7  wakati Rais Jakaya Kikwete anaingia madarakani.

Katibu Mtendaji wa Chama cha Wasambazaji Maji Tanzania (Atawas), Martha Kabuzya anasema mikakati wanayotumia kusambaza maji kwa sasa ni ile iliyopo katika mpango wa maendeleo ya maji.

Anasema kuwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, idadi ya watu wanaopata maji imeongezeka na kwamba wananchi wengi wa mijini wanatumia maji yaliyounganishwa majumbani mwao kuliko kwenye vituo vya umma.

“Kwa vijijini vituo vya maji vya umma bado ni muhimu kutokana na mazingira yake lakini watu wengi wa mijini hawavitumii hivyo kwa kuwa wameshaunganishwa na mfumo wa bomba,” anasema Kabuzya ambaye ni mtaalamu wa rasilimali maji.

Atawas  inajumuisha mamlaka za usambazaji maji zote nchini zikiwemo Shirika la Maji Safi na Taka (Dawasco) na mamlaka ya usambazaji safi na taka Morogoro (Moruwasa).

Kuhusu baadhi ya mamlaka za maji kutotosheleza mahitaji, Kabuzya anasema kuwa idadi ya watu imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka ndiyo maana wakati mwingine kiwango cha wanaopata maji kimekuwa kikipanda na kushuka.

Hata hivyo, ucheleweshaji wa fedha za ujenzi ni moja ya changamoto zinazozikabili mamlaka hizo katika jitihada za kuongeza wigo wa usambazaji maji kwa wananchi.

Changamoto nyingine anaitaja kuwa upotevu wa maji ambao unaotokea kutokana na miundombinu kuchakaa au watu wasio waaminifu kuiba maji ili kukwepa kulipia huduma hiyo.

“Kwa sasa fedha za ujenzi wa miradi zinatoka serikali kuu na kazi za mamlaka ni kuendesha mradi na kuufanyia matengenezo. Hii ina maana kadri miradi inavyocheleweshwa ndivyo na sisi tunavyochelewa usambazaji maji kwa wateja wetu ambao ni wananchi,” anasema Kabuzya.

Ukosefu wa maji unazigharimu zaidi familia nyingi hususan akina mama na watoto ambao hulazimika kutembea umbali mrefu kuyasaka hususan maeneo ya vijijini yenye ukame wa maji.

Hellena Longo, mkazi wa Madibira wilayani Mbarali, Mbeya anasema wakati maji ya bomba ya umma iliyowekwa kwenye kitongoji chao cha Tolinyengo yanapokatika hususan wakati wa kiangazi, hulazimika kwenda mtoni kuteka maji. Mto huo uitwao Lyandembela upo takriban kilomita nne kutoka nyumbani kwake.

Hivi karibuni akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Lindi, Rais John Magufuli alikasirishwa na kucheleweshwa kwa mradi wa maji wa Ng’apa baada ya kubaini kuwa umetumia miaka sita kujengwa.

Kutokana na kucheleweshwa huko, Rais alimwagiza Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kumnyang’anya pasi ya kusafiria mkandarasi wa mradi huo hadi hapo atakapoukamilisha.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, mhandisi Mbogo Futakamba anasema kuwa katika awamu ya pili ya mpango wa maendeleo ya sekta ya maji wamejipanga kuondoa mapungufu yaliyojitokeza yakiwemo yakiundeshaji.

Awamu ya kwanza ya mpango huo ilikuwa kati ya mwaka 2006/07 na 2013/2014.

Futakamba ameeleza katika ripoti hiyo iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana kuwa katika awamu hii kuna zaidi ya wakala 300 wa utekelezaji miradi ya maji nchi nzima ili kufanikisha usambazaji wa huduma za maji safi na salama kwa wananchi zaidi milioni 20.

Mipango ya awali ya kutekeleza mpango huo inabainisha kuwa mahitaji ya awali ya kifedha ni Dola za Marekani 3.32 bilioni sawa na Sh7.23 trilioni.

Hadi Oktoba mwaka jana, Futakamba anasema kiwango ambacho kilishakuwa kimeahidiwa kutolewa kilikuwa Dola za Marekani 1.65 bilioni sawa na Sh3.59 trilioni.

“Kuna jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha kuwa fedha zinawafikia watekelezaji wa miradi kurahisi kutoka kwenye chanzo kikuu.  Baadhi ya wadau wa maendeleo wameanzisha mipango ya kifedha ambayo imelenga kuongeza upatikanaji wa maji nchini,” anasema Futakamba.

Awamu ya pili ya mpango wa maendeleo ya maji (WSDP II) ilianza kutekelezwa mwaka 2014/15 na inatarajiwa kukamilika mwaka 2018/19.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

DATA

Maambukizi  ya Ukimwi yanavyoshamirisha yatima shule za msingi Iringa, Mbeya

Published

on

Mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe imetajwa kuongoza kwa idadi kubwa ya wanafunzi yatima wanaondikishwa katika shule za mingi, jambo linaloweza kuongeza gharama za matunzo kwa watoto hao.

Kulingana na uchambuzi wa takwimu za Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) za mwaka 2016 zinaeleza kuwa mkoa wa Iringa ulishika nafasi ya kwanza kitaifa kwa kuwa na wanafunzi  29,062 yatima sawa na asilimia 14.4% ya wanafunzi wote wa shule za msingi kwa mwaka huo.

Iringa ilikuwa na wanafunzi  wa shule za msingi wapatao 202,113 lakini kati ya hao mwanafunzi 1 kati ya 10 alikuwa ni yatima.

Kulingana na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, mtoto anahesabika kuwa ni yatima endapo atafiwa na mzazi mmoja au wote wawili. Kimsingi anakosa matunzo au upendo wa mzazi mmoja au wote wawili ambapo inaweza kuwa ni changamoto kwa ukuaji wake hasa katika upatikanaji wa elimu.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa siyo Iringa pekee ndiyo yenye idadi kubwa ya wanafunzi yatima lakini mikoa yote inayounda kanda ya Nyanda za Juu Kusini iko kwenye nafasi ya juu kabisa miongoni mwa mikoa 5  ya Tanzania bara yenye yatima wengi.

Nafasi ya pili inashikwa na mkoa wa Njombe ambao ulikuwa na wanafunzi  yatima 19,794 sawa na asilimia 12.7, ikifuatiwa na Mbeya (41,956) sawa na 11.3%. Mkoa wa nne ni Pwani (26,545) sawa na 10.4% na nafasi ya tano ni Kagera (45431) sawa na asilimia 9.8.

Mikoa hiyo mitano inaunda jumla ya asilimia 44.2  ya wanafunzi wote  731,536 yatima waliokuwepo katika shule za msingi kwa mwaka wa 2016. Hiyo ni sawa na kusema kuwa watoto 4 wa mikoa hiyo mitano kati ya 10 ya Tanzania bara ni yatima.

Lakini iko mikoa ambayo imefanikiwa kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi  yatima ikiwemo Manyara ambayo ilikuwa na wanafunzi 15,854 sawa na 6.2% ikifuatiwa na Kigoma (6.5%),  Singida na Mtwara ambazo zote kwa pamoja zilikuwa na 6.7 %. Na mkoa wa tano toka chini ni Lindi (6.8%).

Nini kiini cha kuwepo utofauti mkubwa wa kimkoa wa uwepo wa wanafunzi yatima katika shule za msingi za serikali na binafsi nchini?

ASILIMIA ZA WANAFUNZI YATIMA KATIKA SHULE ZA MSINGI KIMKOA- 2016

 

Wadau waelezea dhana hiyo

Wadau wa afya na masuala ya elimu ya jamii wanaeleza kuwa kuna uhusiano mkubwa wa ugonjwa wa UKIMWI na uwepo wa wanafunzi wengi au wachache yatima katika maeneo mbalimbali nchini.

 Kulingana na takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) za mwaka 2017 zinaeleza kuwa mikoa ya Mbeya, Njombe na Iringa ambayo ina wanafunzi wengi yatima ndiyo vinara wa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi nchini.

Kwa muktadha huo idadi ya wazazi wanaofariki kwa maradhi hayo nayo ni kubwa; uwezekano wa watoto wengi kubaki au kuondokewa na wazazi wote wawili ni mkubwa. VVU husambazwa zaidi kwa njia ya ngono (Uasherati na uzinzi), Matumizi ya pombe na dawa za kulevya, kutakasa wajane na baadhi ya mila na desturi. Ugonjwa huo hauna dawa wala kinga.

TACAIDS inaeleza kuwa  mkoa wa kwanza ni Njombe wenye  asilimia 14.8 ikifuatiwa na Iringa kwa asilimia 9.1 na Mkoa wa Mbeya unashika nafasi ya tatu kwa asilimia 9. Lakini imebainika kuwa mikoa yenye wanafunzi yatima wachache katika shule ina viwango vidogo vya maambukizi ya UKIMWI. Mafano  Manyara (1.5%) na Lindi (2.9%).

Msemaji wa Tacaids, Glory Mziray, wakati akiongea na wanahabari alisema maeneo watanzania walioonesha kuwa na ufahamu sahihi wa elimu kuhusu Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi wanafikia asilimia 60 jambo linalosababisha kuwepo mwamko mdogo wa kubadili tabia katika maeneo yenye maambukizi makubwa ya maradhi hayo.

Alibainisha kuwa njia mojawapo ya kupunguza maambukizi ya Ukimwi ni tohara kwa wanaume. Njia hiyo napunguza maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia 60 na kusisitiza kuwa ipo haja ya kutoa elimu zaidi juu ya uelewa wa ugonjwa huo ili watoto wapate matunzo ya wazazi wote wawili.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Vijana ya YOPOCODE, Alfred Mwahalende amesema mila, ushirikina na kugombania mali ni sababu nyingine inayoongeza watoto yatima shuleni.

“Sababu zingine ni masuala ya kishirikina ambayo hayazungumzwi sana. Katika maeneo ambayo tumekutana na wanavijiji wanaseama baba alirogwa kutokana na mali ili ndugu zake warithi. Wengine wanatafuta utajiri kwa kutoa ndugu zao kafara.” Ameeleza Mwahalende.

Amebainisha kuwa elimu itolewe kwa jamii juu ya kuwatunza watoto yatima na jinsi ya kujikinga na maradhi yote yanayosababisha vifo kwa wazazi ambao wanawajibika kuwalea na kuwasomesha watoto.

“Ninachoweza kusema ni elimu  itolewe lakini pia Asasi zinazoshughulika na masuala ya watoto yatima zione njia ya kuweka sawa kuimarisha na kuwapokea watoto wengi kwenye vituo vyao.” Amesema Mwahalende.

Continue Reading

Afya

Bajeti ya afya 2018/2019 bado tegemezi, yafyekwa kwa asilimia 20

Published

on

Imeelezwa kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa watanzania kukosa huduma bora za afya kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kutokana na kupunguzwa kwa bajeti ya  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa asilimia 20.

Hayo yamebainika leo bungeni mjini Dodoma wakati waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ambapo amesema wameomba Serikali iwapatie billion 893.4 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo.

“Mhe. Mwenyekiti jumla ya fedha kuu ambayo ninaomba Bunge lako tukufu lipitishe katika mafungu yote mawili kwa mwaka 2018/2019 sh. Bilioni 893.4,” amesema Waziri Ummy.

Kiasi hicho cha fedha kilichoombwa kimepungua kutoka trilioni 1.1 za mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambapo zimepungua bilioni 171.6  na kufikia bilioni 893.4 mwaka 2018/2019 sawa na asilimia 20.

Waziri Ummy amesema kati ya fedha hizo ambazo wizara yake inaomba, fedha zitakazoelekezwa kwenye matumizi ya miradi ya maendeleo zitakuwa Tsh. bilioni 561.75 sawa na asilimia zaidi 60 ya fedha zote, ambapo matumizi ya kawaida yatagharimu bilioni 304. 47.

“Kwa upande wa matumizi ya kawaida kwa mwaka 2018/2019 wizara ikadiria kutumia kiasi cha sh. Bilioni 304,473,476 (bilioni 304.47) kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo sh. Bilioni 88,465,756 (bilioni 88.46) zitatumika kwajili ya matumizi mengineyo na sh. Bilioni 216,720,000 (bilioni 216.72) zitatumika kwajili ya mishahara ya watumishi,” amesema waziri Ummy na kuongeza kuwa,

“Kwa upande wa miradi ya maendeleo wizara inakadiria kutumia sh. bilioni 4.91 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, sh. Bilioni 1.5 ni fedha za ndani na sh. Bilioni 3.41 ni fedha za nje.” amesema waziri Ummy.

Kwa muktadha huo, bajeti ya afya itategemea fedha za wahisani kwa asilimia 60 kugharimia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, ukarabati wa majengo na ununuzi wa vifaa tiba na dawa. Hata fedha bilioni 4.91  iliyoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo bado ni ndogo.

Changamoto iliyopo ni kwamba fedha za wahisani wakati mwingine huchelewa kufika au zinaweza zisiingie kabisa nchini kutoka na masharti ambayo yanaweza kuathiri utolewaji wa huduma za afya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba amesema  serikali haina nia ya dhati ya kuinua sekta ya afya kwasababu bajeti inayotengwa kila mwaka ni ndogo na haikidhi mahitaji ya wizara ya afya.

“Uchambuzi wa kamati umebaini fedha zilizotengwa kwaajili ya utekelezaji wa shughuli wizara kwa mwaka wa fedha 2017/18, ni kiasi kidogo ambacho hakiridhishi na kinyume na matarajio ya Mpango wa Bajeti ambao Bunge na Serikali tulikubaliana,” alisema Serukamba.

Licha ya bajeti ya afya kupungua kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 kwa asilimia 20, fedha za bajeti iliyopita ya 2017/2018 hazikufika zote kwenye wizara hiyo jambo lilikwamishwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya sekta hiyo.

Serukamba amesema, mpaka kufikia Februari mwaka huu, Serikali ilikuwa imetoa Sh. bilioni 576.52 pekee kati ya Sh. trilioni 1.1 zilizokuwa zimetengwa kwaajili ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2017/18,.

Kutokana na bajeti ndogo ya wizara ya afya, wabunge wameshauriwa kuijadili na kuangalia uwezekano wa kuishawishi Serikali kuongeza fedha kwa wizara hiyo ikizingatiwa ni sekta muhimu kwa ustawi wa wananchi ili kuwahakikishia wananchi afya bora.

Continue Reading

Afya

Mgawanyo usio sawa wa hospitali, zahanati unavyokwamisha huduma za afya kwa wananchi

Published

on

Imeelezwa kuwa watanzania watalazimika kusubiri kwa muda mrefu ili kupata huduma bora za afya kutokana na uchache wa vituo vya kutolea huduma hizo ambavyo haviendani na ongezeko la idadi ya watu nchini.

Hali hiyo ni tofauti na matakwa ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 ambayo inasisitiza kuwa serikali inawajibika  kuinua hali ya afya ya wananchi wote na hasa wale walioko kwenye hatari zaidi, kwa kuweka mfumo wa huduma za Afya utakaokidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza umri wa kuishi wa watanzania.

Lakini watanzania wengi hawafaidiki na tamko la Sera ikizingatiwa kuwa idadi ya watu inaongezeka sana kuliko maboresho na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Vituo hivyo vinajumuisha hospitali, vituo vya afya na zahanati ambazo vinatakiwa kujengwa kwenye vijiji, kata na ngazi ya wilaya na mkoa.

Kwa mujibu wa data za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) za mwaka 2017 zinaonyesha kuwa vituo vya kutolea huduma za afya viliongezeka kutoka 6,321 mwaka 2010 hadi kufikia 7,680 mwaka 2016, ambapo ongezeko hilo ni sawa na vituo 1,359 (14%) tu  kwa miaka saba na wastani wa vituo 194 kila mwaka.

Idadi ya vituo hivyo haiendani na ongezeko kubwa la watu. Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Tanzania ilikuwa na watu milioni 45 na hadi kufikia mwaka 2016 inakadiriwa ilikuwa na watu zaidi milioni 50.

Kwa mtazamo wa kawaida ni kwamba karibu nusu ya wananchi hawapati na huduma bora za afya ikiwemo upatikanaji wa vituo vya kutolea huduma za afya, jambo linaloweza kuwaweka katika hatari ya kupoteza nguvukazi ya taifa na hata maisha.

Hata hivyo, bado ziko juhudi mbalimbali zinazofanyika kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi katika maeneo yao. Takwimu za NBS zinaeleza kuwa hadi mwaka 2016 kulikuwa na zahanati 6,658 ambazo zilikuwa na kliniki 89 za mama na mtoto. Lakini changamoto ni kwamba zahanati nyingi zinakabiliwa na upungufu wa madaktari, dawa, vifaa tiba na uchakavu wa miundombinu.

Kimsingi Sera ya Afya inaelekeza kuwa kila kijiji kinapaswa kuwa na zahanati yake ili kuhakikisha wananchi hawatembei umbali mrefu kufuata huduma kwasababu afya ni huduma muhimu ya kijamii na inapaswa kupewa kipaombele.

Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012, Tanzania ina vijiji 19,200  Ambavyo vinahudumiwa na zahanati 6,658 na hivyo basi kuna upungufu wa zaidi ya zahanati 12,000 ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa vijiji vyote.

Kumekuwa na mabadiliko ya kuongezeka na kupungua kwa zahanati nchini. Mathalani mwaka 2013 kulikuwa zahanati 5,680 na mwaka uliofuata wa 2014 zilipungua hadi kufikia 6,002 na sababu kubwa ni  baadhi ya zahanati ni kutotimiza masharti na matakwa ya mwongozo wa matibabu nchini na hivyo kulazimika kufungwa. Juhudi zilifanyika na idadi ya zahanati ziliongezeka hadi kufikia 6,549 mwaka 2015 na mwaka uliofuta wa 2016 zilifikia 6,658.

Kinachotokea ni kwamba wingi wa vituo vya kutolea huduma za afya  unapungua kutoka ngazi ya kijiji, tarafa, wilaya hadi kitaifa. Hali hii inaweza kusababishwa na uhaba wa rasilimali fedha na watu, ubora wa huduma kwenye hospitali husika.

Mwaka 2016, kulikuwa na vituo vya afya 759 nchini kote ambapo ni sawa na kusema kuwa kila mkoa ulikuwa na vituo takribani 29. Kimsingi huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya zina hadhi ya juu ukilinganisha na zahanati kwasababu vinahudumia watu wengi zaidi na vinatakiwa kuwa na vifaa vya kisasa na huduma kama vile upasuaji na kliniki za mama na mtoto.

Idadi ya zahanati zilizoko nchini ni mara 9 ya vituo vya afya ambavyo vinategemewa kuwasaidia wagonjwa ambao hawajapata matibabu ya uhakika kwenye zahanati. Changamoto inayojitokeza ni kuwa vituo hivyo vinaelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaotoka ngazi ya chini na kwa vyovyote vile baadhi yake vitakuwa havina huduma bora za matibabu.

Pia vituo vya kutolea huduma za afya hupungua zaidi katika ngazi ya mkoa hadi kitaifa. Mwaka 2016 kulikuwa na hospitali 263 za wilaya, mkoa na rufani. Hizi ndio hospitali pekee zinazotegemewa na watanzania zaidi ya milioni 50 nchi nzima kupata matibabu.

Pengo kati ya vituo vya afya na hospitali sio kubwa sana ukilinganisha na zahanati ambazo ni nyingi lakini huduma zake hazilingani na hospitali nyingine za ngazi ya wilaya na mkoa.

Na utaratibu uliopo ni kwamba mgonjwa anatakiwa kutibiwa ngazi ya juu ikiwa tu zahanati na vituo vya fya vimeshindwa kumpatia matibabu yanayotakiwa. Kwa utaratibu huo vituo vya afya na hospitali nyingi huelemewa na wagonjwa kutokana na uwekezaji mdogo na  huduma zisizoridhisha kwenye zahanati.

Kutokana na hali halisi ya upatikanaji wa huduma za afya nchini, serikali na wadau wanapaswa kuongeza juhudi za kuboresha na kujenga vituo na hospitali ili kukidhi ongezeko la watanzania ambao wanatakiwa kuwa na afya bora zitakazosaidia katika ujenzi wa taifa.

Ujenzi na maboresho hayo ni muhimu yakaenda sambamba na tathmini ya huduma zinazotolewa, idadi ya vituo ili kuyasaidia maeneo yenye uhitaji mkubwa wa huduma za afya.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2018 FikraPevu.com