Connect with us

Jamii

‘Teni pasenti’ kuwaponza watumishi wa Tanroads Kilimanjaro

Published

on

ASILIMIA 10 ya malipo ya rushwa na upendeleo, huenda “ikawatokea puani” watumishi wawili wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), mkoani Kilimanjaro.

Inadaiwa kuwa watumishi hao wamekuwa maarufu kwa kupokea asilimia hiyo, maarufu kama –teni pasenti- bila woga.

Watumishi hao tayari wameanza kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambanana Rushwa (Takukuru) baada ya Ikulu kuagiza kufanyika kwa uchunguzi huo.

Ikiwa uchunguzi utakamilika, wanaweza kushitakiwa mahakamani kwa matumizi mabaya ya madaraka na hata rushwa.

FikraPevu imepewa taarifa kutoka serikalini kwamba baada ya Ikulu kupokea barua ya malalamiko kutoka kwa makandarasi wa Kilimanjaro, iliagiza Takukuru kuanza uchunguzi “mara moja.”

Kuanza kwa uchunguzi huo kunafuatia barua iliyoandikwa na makandarasi wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa Rais Dkt. John Magufuli, baada ya kudai kwamba “wameshindwa kusaidiwa na ngazi zingine,” hivyo kuomba kusaidiwa na ofisi namba moja, Ikulu.

FikraPevu imeiona barua iliyoandikwa kwa Rais Magufuli na makandarasi hao wakitaka kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua kwa watendaji hao wa Tanroads.

Barua hiyo ya malalamiko inaonesha kuandikwa Februari 28, 2017 na kwamba ilifikishwa Ikulu, Dar es Salaam baada ya siku nane, yaani Machi 6, 2017.

Takukuru wazungumza

Ofisa mmoja kutoka Takukuru, Makao Makuu Dar es Salaam, ameiambia FikraPevu kwamba kweli uchunguzi umeanza na unafanywa na watendaji ambao hawako Kilimanjaro.

“Sina haja kukueleza wanafanya nini na kina nani wanachunguzwa, lakini elewa timu yetu ipo makini huko na kazi zinaendelea,” alisema, huku akisisitiza “usiweke jina langu popote.”

Taarifa zilizopatikana kwa FikraPevu zinadai kuwa watumishi hao wa Tanroads wamekuwa wakitumia nafasi zao, hasa “kuwaminya” makandarasi kwa kuomba rushwa ndipo wapate zabuni.

Malalamiko ya makandarasi wa Kilimanjaro kwa baadhi ya watendaji wa Tanroads, Kilimanjaro yamekuwa yakipazwa mara kwa mara na makandarasi, huku wakieleza kuwepo kwa kampuni mbili tu zinazopewa upendeleo.

FikraPevu haitataja majina ya kampuni hizo kwa sasa kwa kuwa hazikufikiwa mapema. Kazi inaendelea kuzifikia.

Uongozi Tanroads wazungumza

Meneja wa Tanroads Kilimanjaro, Ntije Nkolante, amekiri kuwepo kwa malalamiko hayo, lakini akadai kuwa makandarasi hao siyo wakweli kwani uamuzi wa nani apewe kazi, haufanywi na mtu mmoja wala wawili, ni jopo la wataalam.

“Zipo bodi nne zinazohusika hadi kupatikana kwa mzabuni ambaye anapewa kazi, hivyo siyo rahisi kuchakachua kwa namna yoyote ile,” anaiambia FikraPevu.

Ntije anasema kuna timu ya tathmini, kitengo cha ununuzi, menejimenti na meneja mwenyewe, hivyo siyo rahisi kwa watu wawili kushawishi wengine ili kupendelewa kwa kampuni moja au mbili.

Katika malalamiko ya makandarasi hao, wanaitaja kampuni moja iliyopewa zabuni ya kujenga madaraja eneo la KIA, lakini ilishindwa kutekeleza mradi huo kwa madai ya kutokuwa na uwezo.

Meneja huyo wa mkoa amekiri kampuni hiyo kupewa kandarasi na kushindwa

kutekeleza mradi huo, lakini akaitetea kwamba mradi ambao kampuni hiyo imeshindwa ni mdogo ikilinganishwa na miradi mikubwa iliyotekeleza wilayani Same, Kilimanjaro.

“Ni kweli hiyo kampuni imeshindwa kujenga hayo madaraja kama ilivyoomba na kushinda zabuni, lakini tunashindwa kuelewa ni kwa nini imeshindwa mradi mdogo kama huo, wakati imetekeleza miradi mikubwa wa kujenga karavati kubwa wilayani Same,” Ntije ameiambia FikraPevu.

Tunachokijua

Tanroads Kilimanjaro imekuwa ikilalamikiwa mno kwa madai ya rushwa kwa kazi nyingi za ujenzi wa barabara zinazotolewa kwa kampuni za ndani au nje ya nchi.

Madai haya ya makandarasi yamekuwa yakielezwa “kukomea” ngazi ya mkoa au taifa, bila uchunguzi kufanywa.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Jamii

Manispaa ya Dodoma yapandishwa hadhi na kuwa jiji la 6 Tanzania

Published

on

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli ametangaza kuipandisha hadhi Manispaa ya Mji wa Dodoma kuwa Jiji kuanzia leo Aprili 26, 2018.

Rais Dkt Magufuli ameyasema hayo leo, katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya sherehe za miaka 54 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar mjini humo.

Amesema kwa mamlaka aliyonayo ameona vema Dodoma ipate hadhi ya jiji ikizingatiwa kuwa mikakati ya serikali kuhamia katika jiji hilo inaendelea.

“Nilifanikiwa kuiona Dodoma ilivyokuwa. Imejengwa kila mahali, na Dodoma kweli ni Makao Makuu. Tulizoea Dar es Salam ndiyo yalikuwa makao makuu kwa wakati ule, na paliitwa Jiji. Nikaona niangalie katika nchi yetu tuna Halmashauri ngapi, tuna manispaa ngapi na mimi nina mamlaka gani katika kutengeneza majiji au manispaa au kadhalika,” amesema Rais Magufuli na kuongeza kuwa,

“Nikakuta Arusha ni jiji, Tanga ni jiji, nikaambiwa Dodoma ni Manispaa, nikasema haiwezekani. Kwahivyo kuanzia leo Dodoma linakuwa Jiji,”

Vile vile Rais Magufuli amempandisha hadhi Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kutokana na kupanda hadhi yake.

Hatua hiyo inaifanya idadi ya majiji hapa nchi kufikia sita ambapo Tanzania ina majiji ya Dar es Salaam, Jiji la Tanga, Jiji la Arusha, Jiji la Mwanza, Jiji la Mbeya na Jiji jipya la Dodoma.

Kuna vigezo mbalimbali vinavyotumika ili kuipa manispaa au mji hadhi ya kuitwa jiji. Lakini vigezo hivyo hutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine. Hata hivyo, baadhi ya mambo ambayo ni muhimu ni upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii, miundombinu ya barabara zinazoingia na kutoka katikati ya jiji. Pia uwepo wa huduma za kiutawala ikiwemo ofisi za serikali.

Dodoma ni mji mkuu wa nchi, lakini tangu Tanzania ipate uhuru 1961; serikali haikupeleka shughuli za utawala katika jiji hilo. Alipoingia madarakani 2015, rais John Magufuli alianzisha kampeni ya kuhamia Dodoma.

Taarifa zilizopo ni kwamba wizara zote, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu tayari wako Dodoma na mwishoni mwa mwaka huu, rais atahamishia ofisi yake na ikulu katika jiji hilo jipya.

                              Sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo jijini Dodoma

 

Historia ya Dodoma

Kulingana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jina la Dodoma lilizaliwa hata kabla ya Mji wenyewe. Zipo hadithi nyingi zinazoeleza jinsi jina hilo lilivyopatikana, lakini hadithi inayokubaliwa na wengi ni hii: Tembo alikuja kunywa maji katika Kijito cha Kikuyu na akakwama matopeni. Baadhi ya wenyeji waliomwona walipiga mayowe na kusema “yadodomela” ambayo kwa lugha ya Kigogo maana yake ‘amezama’.

Na tangu wakati huo mahala hapo pakawa panajulikana kama Idodomya pale mahali
alipozama yule tembo. Haijulikani kwa uhakika lini jina lilianza kutumiwa. Kwa kukisia huenda  eneo hilo lilianza kutumika tokea mwaka 1860.

Msafiri wa Kizungu H. M. Stanley ambaye alipitia sehemu hiyo mnamo mwaka 1874 aliliita Dodoma. Lakini hakuna kumbukumbu ya kimaandishi ya zamani zaidi kuhusu jina hilo lilivyopatikana.

                               Mji wa Dodoma

Miaka mingi iliyopita, wakati wa kipindi cha wahamiaji wa Kiafrika, wakazi wa Dodoma ambao ni wafugaji waliweka makazi yao katika eneo linalojulikana sasa kama Mkoa wa Dodoma. Katika kulinda mifugo yao, wakazi hawa waliishi kwa kutawanyika na hasa ukizingatia kuwa walikuwa wachache mno kwa Idadi.

Mbali na shughuli za ufugaji, walijishughulisha pia na Kilimo cha kujikimu, kutengeneza ala za muziki na usukaji wa vikapu: waliweza pia kuanzisha usindikaji mdogo wa kutengeneza Chumvi, Nta na Samli.  Pamoja na kufanya kazi hizo, kikwazo kikubwa kwa wakazi hawa kilikuwa ni hali ya hewa.

Mvua zinaponyesha vizuri wanapata chakula cha kutosha lakini mvua zinapokuwa haba, hali ya chakula inakuwa ngumu sana. Mwaka 1890 Utawala wa Kijerumani uliingia mkoani Dodoma.  Na miaka 18 baadaye yaani mwaka 1912, eneo la Dodoma likawa eneo la Utawala wa Wilaya. Mji wa Dodoma ukiwa makazi ya kudumu ulianzishwa mnamo mwaka 1910 kwa

ujio wa reli Kuu ya Kati. Reli Kuu ya Kati ambayo ndiyo hasa ilisababisha kuwepo na kukua kwa Mji wa Dodoma ulitanguliwa na msafara wa Binadamu uliotokana na biashara dhalimu ya Utumwa. Msafara huo ulikuwa kiungo kati ya Bara na Pwani.

Kabla ya Tanganyika kupata Uhuru wake tarehe 09 Desemba 1961, Mkoa wa Dodoma ulikuwa ni sehemu ya Jimbo la Kati (Central Province). Mwaka 1963, Jimbo la kati liligawanywa na kupatikana Mikoa ya Dodoma na Singida. Mkoa wa Dodoma ulianzaishwa kwa Tangazo la Serikali Na.450 la tarehe 27 Septemba,1963.

Continue Reading

Jamii

Utata, nadharia iliyojificha kwenye Hati, kero za Muungano wa Tanzania

Published

on

Leo watanzania kutoka nchi mbili za Zanzibar na Tanzania Bara wanaungano kusherehekea miaka 54 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioasisiwa April 26, 1964 na viongozi wawili wa kitaifa; Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Aman Abeid Karume.

Maadhimisho hayo yanafanyika pale mjini Dodoma, makao makuu ya nchi  na mgeni rasmi ni rais John Magufuli ambapo ataambatana na viongozi mbalimbali waandamizi katika kutathmini mafanikio na changamoto za muungano.

Lakini Muungano bado una kero ambazo hazitafutiwa ufumbuzi licha ya kuwepo mijadala mbalimbali inayonuia kuimarisha Muungano.

Akiwasilisha Mada yake kuhusu Muungano kule Wete- Pemba mwaka 2012, Profesa Abdul Sherrif wa Baraza la Katiba la Zanzibar katika Mjadala wa Katiba Mpya, alizungumza mambo mengi ambayo ndiyo kiini cha kero zisizokwisha za muungano wa nchi hizi mbili.

Jambo mojawapo ni hati ya Muungano ambayo inasimama kama katiba ya muungano ambayo bado inaleta changamoto katika uimarishaji wa Jamhuri.

Prof. Sherrif katika mada yake alieleza kuwa, “katika Hati ya Muungano, kitu kilichofanyika ni kwamba, jina la Serikali ya Tanganyika likabadilishwa na kupewa jina la Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Baadae ikabidilishwa kuwa Tanzania, na kutaka kuufuta kabisa utaifa wa Zanzibar. Wako wanaosema kuwa hiyo haikuwa sawa. Hata Katiba ya Tanganyika ikatumika, baada ya kurekebisha mambo machache tu, kama kubadilisha jina na bendera.

SMZ (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) ikabakia, lakini madaraka 11 ya serikali hiyo yalihamishwa na kupelekwa kwenye Serikali ya Muungano. Sasa, tukiweka serikali 2 hizi katika mizani, zitakuwa hazina usawa tena, kwa sababu Serikali ya Muungano sasa imekusanya madaraka yote ya Tanganyika na mambo 11 ya Zanzibar.

Mambo haya 11 ya Muungano si yote yana sura ya kimataifa, bali yanahusu mambo mengi ya uchumi wa ndani. Biashara ya Nje ni katika mambo hayo ya Muungano, lakini uchumi wetu wakati ule ulikuwa unategemea sana uuzaji wa karafuu nchi za nje. Hali kadhalika, Kodi ya Mapato na Ushuru wa Bidhaa yote haya yamehodhiwa na Serikali ya Muungano, na SMZ inapewa ruzuku ya aslimia nne nukta tano (4.5%) tu.

Vilevile, SMZ inakosa madaraka juu ya biashara na kodi, hivyo inakosa uwezo wa kupanga uchumi wa nchi moja kwa moja. SMZ imeachiwa kazi ya kuendesha serikali bila kupewa nyenzo ya fedha. Kwa hivyo, hata mgawanyo wa madaraka haukuwa wa usawa.

Hati ya Muungano ni mkataba wa kimataifa kama unavyojulikana katika sheria ya kimataifa, na haiwezi kubadilishwa kila mara. Iligawana madaraka kati ya SMZ iliobakia na mambo yote yasiokuwa ya Muungano, na Serikali ya Muungano iliokuwa na madaraka yote ya Tanganyika yasiyo ya Muungano, na Mambo 11 ya Muungano ya Tanganyika na ya Zanzibar.

Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Karume wakiweka saini kwenye hati ya Muungano mwaka 1964. 

Lakini mambo hayakuishia hapo. Kila mwaka au miaka 2, madaraka mengine ya Zanzibar yalikuwa yananyakuliwa na kufanywa Mambo ya Muungano, haya ni pamoja na sarafu (1965), mafuta na gesi (1968)-hili limerudishwa mikononi mwa SMZ, na hata Baraza la Mitihani (1973).

Mpaka sasa, mambo mengine 11 yamehamishwa kutoka katika madaraka ya SMZ na kupelekwa Dodoma – wengine wanasema mambo haya ni 22. Maana yake ni kwamba ile mizani iliyoinama sana baada ya kuundwa Muungano, basi sasa imelala chini kabisa.

Hapa tunapaswa tujiulize swali, je hii ilikuwa ni halali? Hapa hatuna budi kumnukuu Prof. Shivji, mwanasheria aliyebobea katika sheria ya katiba. Huyu sio Mzanzibari lakini ni Mtanganyika; yeye si adui wa Mwalimu Nyerere bali ni mpenzi wa mawazo ya Mw Nyerere.

Mwaka wa 1990 alitoa hotuba yake muhimu sana kama tunataka kufahamu chanzo na sababu za ‘Kero za Muungano’:

Alieleza kwamba sehemu ya Hati ya Muungano inayotaja mambo 11 ya Muungano, ndiyo iliyogawana madaraka kati ya serikali mbili, na kwa hivyo haiwezi kubadilishwa bila kuvuruga muundo mzima wa Muungano.

Na anaendelea kusema kwamba, si Bunge wala Baraza la Wawakilishi, kwa kila mmoja peke yake, hawana madaraka ya kubadilisha sehemu hii ya Hati ya Muungano. Kwa hivyo, Bunge kubadilisha sehemu hii, kama ilivyofanya mara 11, ni kuzidisha madaraka yake, na kuipokonya Zanzibar. Huu ni ‘unyang’anyaji na ubomoaji wa mfumo halisi wa Muungano.’ Mwisho wake SMZ itabakia na kete tupu.

Prof Shivji anamalizia kwa kusema kwamba, mabadiliko yote yaliyofanyiwa sehemu hii ya Hati ya Muungano ni ‘haramu na batili.’

Kwa bahati mbaya, Serikali ya Tanzania hawakujali onyo la Profesa Shivji, baada ya miaka miwili tu, waliporejesha mfumo wa vyama vingi, wakaendelea na mtindo wao wa kawaida. Wakachukuwa fursa ya kumnyima Rais wa Zanzibar, anaechaguliwa na watu wa Zanzibar, nafasi yake kama Makamo wa Rais wa Tanzania, iliyotajwa katika Hati ya Muungano.

Yeye alikuwa kiungo muhimu kati ya SMZ na Serikali ya Muungano. Sheria hii ilipitishwa na Bunge bila kuhitaji kura ya Theluthi Mbili (2/3) kwa pande zote mbili. Wabunge wengi wa Zanzibar waliogopa kupinga msimamo wa chama tawala.

Mwalimu Nyerere akichanganya udongo wa Tanzania Bara na Tanganyika kuashiria muungano nchi mbili

Baadaye tu wakazinduka na wakaamua kumuingiza Rais wa Zanzibar kama Waziri bila Kazi Maalum katika Baraza la Mawaziri la Tanzania, ambayo ni kumvunjiya heshima yake. Badala yake, wakaleta mfumo wa Makamo Mwenza anaechaguliwa na Watanzania wote, na anatakiwa awashughulikie Watanzania wote, lakini hana nafasi katika SMZ.

Kwa ufupi, ongezeko la Mambo ya Muungano baada ya 1964, na kumuondosha Rais wa Zanzibar kutoka nafasi yake ya Makamo wa Rais wa Tanzania, yamevuruga kabisa muundo wa Muungano. Vilevile, yamevunja Hati ya Muungano, ambayo ilikuwa mkataba wa kimataifa kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Hati ya Muungano ndio Katiba Mama ya Tanzania. Kwa kiasi kikubwa, mambo yaliofanyika baada 1964 kwa makusudi hayakutaka kuheshimu makubaliano kati ya Marehemu Mzee Karume na Mw. Nyerere, na kuheshimu utaifa wa Zanzibar. Sasa, hata Jaji Mkuu (wa wakati huo) na Waziri Mkuu wanathubutu kusema Zanzibar si nchi.”

Huo ndio ulikuwa mtazamo wa Prof. Sherrif kuhusu hati na kero za Muungano na jinsi unavyoleta changamoto kwa nchi zote mbili.

 

Nini Kifanyike

Wadau mbalimbali wameitaka serikali ya Jamhuri kuzileta nchi zote mbili pamoja na kujadili kwa kina mambo yenye changamoto ili kuhakikisha kunakuwa na usawa katika utekelezaji wa matakwa ya hati ya Muungano na Katiba ya nchi.

Mbunge wa Temeke, Maulid Mtolea, akiwa bungeni hivi karibu alisema, “Nawapongeza wazanzibar kwa umoja wao wa kuipigania Zanzibar yao bila kuzingatia wanatokea upande upi wa kisiasa, ndio maana wenzetu wanafanikiwa. Watu wanahisi Tanzania bara hakuna kero za Muungano lakini ukweli ni kwamba kero za upande huo hazina pa kwenda, hazina wa kuzisemea.’

Alisema ili muungano udumu na kuwa imara kuna umuhimu wa kupunguza manung’uniko kwa kujadiliana na kutafuta ufumbuzi wa kero zilizopo.

“Kuwafurahisha watanzania bara siyo kuwabana wazanzibar, ni kuwaacha watanzania bara nao waseme,” alisema Mtolea.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dkt. Hellen Kijo Bisimba amesema watanzania wakubali kuwa kero zipo na watafute njia mbadala za kuzitatua ili matunda ya muungano yaonekane dhahiri kwa pande zote mbili.

“Huu muungano ni muhimu na inasemekana ni wa tofauti sana na wa aina yake na unahitaji kulindwa lakini hautalindika kama tusipokubali kukaa chini na kuuzungumzia na kuona zile tunaziita kero zinachukuliwa na kufanyiwa ufumbuzi,” ameshauri Dkt. Hellen.

Akizungumza kwa niaba ya serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Raisi (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema kero zilizopo hazitaweza kuyumbisha muungano na wataendelea kutafuta mbinu mbalimbali kuhakikisha unadumu daima.

“Hakuna changamoto yoyote inayoweza kutufarakanisha, kutenganisha wala kuturudisha nyuma…kwa watu wote na pande zote za Muungano. Mjadala sio uhalali wa Muungano bali mbinu za uimarishaji,” alibainisha Makamba.

Continue Reading

Jamii

LHRC wafichua mambo 5 yaliyovunja haki za binadamu 2017

Published

on

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema  kukithiri kwa mauaji, utekaji, uteswaji, ukatili, kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni, kukusanyika na kujumuika ni matukio makubwa yaliyovunja zaidi  haki za binadamu nchini kwa mwaka 2017.

Akiwasilisha ripoti ya Haki za binadamu Tanzania (2017), Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt. Hellen Kijo Bisimba amesema  ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mwaka 2017 uliongezeka zaidi ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo hatua muhimu zisipochukuliwa  inaweza kuvuruga amani na demokrasia iliyojengwa kwa muda mrefu na waasisi wa taifa.

“Haki za kiraia na kisiasa zilivunjwa zaidi, hasa haki ya kuishi, haki dhidi ya ukatili, haki ya kuwa huru na usalama wa mtu, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kukusanyika na uhuru wa kujumuika. Kuminywa kwa haki hizi pia kuliathiri haki ya kushiriki katika utawala/serikali hususan haki ndogo ya kushiriki katika muasuala ya siasa.” Amesema Dkt. Hellen

Ripoti hiyo imebainisha kuwa haki iliyovunjwa zaidi ni haki ya kuishi kutokana na kuendelea kwa  mauaji ya kujichukulia sheria mkononi, mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola na mauaji yatokanayo na imani za kishirikina.

“Mpaka kufikia Disemba 2017, idadi ya vifo vilivyotokana na na wananchi kujichukulia sheria mkononi ilifikia 917 ambavyo ni vifo 5 zaidi ya vile vilivyoripotiwa mwaka 2016. Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kwa matukio ya kujichukulia sheria mkononi, ukifuatiwa na Mbeya, Mara, Geita, Tanga na Kigoma.” Imeeleza ripoti hiyo.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa mauaji yaliyotekelezwa na vyombo vya dola ikiwemo  akatili dhidi ya  askari polisi yalikuwa 9 ambayo ni 5 zaidi ya  yale yaliyokusanywa 2016.

Dkt. Hellen amesema haki nyingine iliyovunjwa zaidi 2017 ni kushambuliwa na vitisho kwa wanahabari, kufungiwa kwa vyombo vya habari na kutumika vibaya kwa sheria kuhusu uhuru wa kujieleza  ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya 2016.

Anafafanua zaidi kuwa “ Uvamizi wa ofisi za Clouds Media uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na vitisho na ukamataji kinyume na sheria wa wanahabari 10 kwa amri ya mkuu mmoja wa wilaya mkoani Arusha. Jumla ya magazeti 4 yalifungiwa na kulipishwa faini kwasababu tofauti ikiwemo chini ya sheria kandamizi ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ya mwaka 2016.”

Amebainisha kuwa kutekwa na kupotea kusikojulikana kwa mwandishi wa habari kutoka kampuni ya Mwananchi Novemba 2017, Azory Gwanda kuliitia doa nchi katika kulinda wa haki za binadamu hasa uhuru wa vyombo vya habari.

 

Haki ya kuwa Huru na Usalama wa Mtu

LHRC inaeleza kuwa ilikusanya matukio takribani 38 ya uvunjifu wa haki ya usalama wa raia, ikiwemo watu kutekwa au kupotea katika mazingira ya kutatanisha; miili ya watu ambao inaonekana waliuwawa na kuwekwa kwenye mifuko ya sandarusi ikielea kwenye fukwe za bahari ya Hindi.

“ Shambulio la Rais (aliyemaliza muda wake)wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu Mkuu wa Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu; na mauaji ya raia, viongozi na askari wa polisi kule Kibiti na maeneo mengine ya Mkoa wa Pwani ambapo watu wasiopungua 40 wakiwemo askari wa polisi 12 wameuawawa tangu mwaka 2015.” Imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

LHRC pia imegusia haki ya kutokuteswa ambapo ilibaini matukio yasiyopungua 22  na mengi (15) yalikuwa ni hukumu ya kifo- ambayo ni uteswaji kwa mujibu wa Mkataba dhidi ya Uteswaji . Mfano ni tukio la kutekwa na kuteswa kwa msanii Roma Mkatiliki na wenzake mapema mwaka huu.

Amezitaja haki zingine ambazo zilikiukwa ni pamoja na haki ya kukusanyika na kujumuika ambapo vyama vya siasa vimezuia kufanya shughuli zao ikiwemo mikutano ya hadhara, maandamano na hata vikao vya ndani kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wakati wa maendeleo.

Hata hivyo, Dkt. Hellen amesema uvunjaji wa haki 5 zilizobainishwa kwenye ripoti ya LHRC ni kiashiria tosha kuwa usalama wa nchi uko shakani na hatua za makusudi zinahitajika kutetea  na kulinda raia na mali zao ili amani izidi kushamiri kwenye jamii ya watanzania.

Viongozi wa LHRC na washiriki wa hafla ya uzinduzi wa ripoti ya Haki za Binadamu 2017, katika picha ya pamoja leo jijini Dar es Salaam.

 

Wadau watoa maoni yao

Akizungumza baada ya uzinduzi wa ripoti ya LHRC, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume amesema msingi wa amani katika nchi yoyote ile ni kuheshimu na kulinda haki za raia hasa haki ya kuishi na kutoa maoni.

Amesema ikiwa tunataka kuifikisha nchi kwenye uchumi wa kati ni lazima haki za binadamu zipewe kipaombele na watawala kwasababu maendeleo hayawezi kuja kama raia hawapati stahiki zao.

“Huwezi kujenga amani kama unavunja haki. Ni muhimu kulinda haki ya kuongea maana ndiyo msingi wa maendeleo yetu. Kuna uhusiano mkubwa kati ya haki ya kuongea na kukutana,” amesema Fatma na kuongeza kuwa,

“Yale mabadiliko ya fikra ya maendeleo yatapatikana vipi kama hukutani na wenzako kubadilishana mawazo? Msingi wa kuleta maendeleo yote ni haki ya kuongea na kujumuika, ukitoa hizo unabakiwa na mfumo ule ule huwezi kuleta maendeleo.”

Kwa upande wake, Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Richard Mabala amesema ripoti hiyo imetoa mwanga wa hali halisi ya nchi yetu na kuna haja ya kufanya tathmini  ya maeneo yaliyo na changamoto katika kulinda haki za raia.

Ameshauri kuwa serikali inapaswa kuweka mazingira wezeshi kwa raia wote kuwa huru kufanya shughuli zao bila kuwepo vitisho vya kisiasa, maisha  ili kuhakikisha amani iliyopo inadumu daima.

Naye, Mtetezi wa Haki za Wanawake kutoka taasisi ya Equality For Growth (EfG), Jane Magigita amesema ili matukio ya kuvunjwa kwa haki za binadamu yapungue ni lazima jamii ielimishwe juu ya madhara ya ukatili ambao umeota mizizi kwenye ngazi ya familia.

Amesema watu wakifunzwa kupendana na kuheshimu wengine, tutajenga  jamii iliyostaarabika yenye maendeleo endelevu.

Akihitimisha kutoa maoni yake, Wakili na Mtetezi wa Haki za Binadamu kutoka LHRC, Imelda Lulu Urio ameshauri kuwa iundwe tume huru itakayochunguza matukio yote yaliyotokea mwaka 2017 ili kubaini kiini cha tatizo na kutoa suluhisho ambalo litakuwa msingi wa kukomesha matukio ya uvunjaji wa haki za raia kwa siku zijazo. “Kiundwe chombo huru kitakachoangalia matukio yote na kuja na suluhisho”.

Continue Reading

Must Read

Copyright © 2018 FikraPevu.com