TAMWA yaitaka jamii kumuondolea mtoto wa kike vikwazo ili asome

Jamii imetakiwa kumuondolea mtoto wa kike vikwazo na kumtengenezea mazingira rafiki na salama akiwa shuleni na nyumbani ili afikie ndoto zake za kielimu.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Edda Sanga ambapo amesema jamii na serikali inapaswa kuwekeza rasilimali za kutosha katika elimu ya mtoto kike ili aweze kuwa na mchango katika kuifikisha nchi katika uchumi wa viwanda.

“Jamii na serikali zitafakari na kuwekeza zaidi katika elimu ya watoto wa kike ili kuwajengea uwezo wa kujiendeleza na kuwa na mchango katika familia na taifa letu ambalo tunalenga kufikia uchumi wa viwanda” amesema.

Amesema watoto wa kike wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo ni kikwazo kufikia ndoto zao, hivyo kuna umuhimu wa kuwatengenezea mazingira rafiki wakiwa shuleni na nyumbani.

“ Changamoto nyingine ambazo ni muhimu kuzingatiwa ili kumfanya mtoto wa kike afikie ndoto zake hasa wakati huu wa uchumi wa viwanda ni pamoja na kumtengenezea mazingira rafiki na salama akiwa shuleni na nyumbani”, amesema

Tafiti zinaonyesha kuwa watoto wengi wa kike wamekuwa wakipata ujauzito na kushindwa kuendelea na masomo kutokana na kutembea umbali mrefu kwenda shule au kufanya kazi za familia ikiwemo kuteka maji na kutafuta kuni.

Ripoti ya Utafiti wa Makazi na Afya Tanzania (TDHS-2010) unaonyesha kuwa wasichana 36 kati ya 100 huolewa kabla ya wakati huku wasichana 27 kati ya 100 wakipata ujauzito wakiwa chini ya umri wa miaka 18 kila mwaka.

Ukatili  wa kijinsia unaotokea shuleni nao unatajwa kuwa kikwazo kwa mtoto wa kike kuelimika. Ukosefu wa mazingira rafiki na salama katika shule mbalimbali huendelea hisia za ubaguzi kwa watoto.  Wapo watoto wa kike  wanaokosa fedha za kununulia pedi za kujisitiri, hivyo huishiwa kurubuniwa na kununuliwa na wanaume ambao hufanya nao mapenzi na kuwatelekeza.

                                           Elimu bora itamuhakikishia mtoto  wa kike kufikia ndoto zake

  Mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia anaofanyiwa mtoto wa kike unakiuka haki za mtoto lakini zipo baadhi ya sheria katika nchi yetu ambazo zinachochea ukatili kwa watoto kike. Mabadiliko ya kisera na sheria ni muhimu ili kumtengenezea mtoto kufikia ndoto zake.

“Wadau na asasi mbalimbali za kiraia wamekuwa wakipambana ili kuhakikisha ndoa za utotoni zinatokomezwa lakini kumekuwa na changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni sheria ya ndoa iliyopo ambayo inaruhusu mtoto wa miaka 14 kuolewa kwa idhini ya wazazi/walezi, familia nyingi kuwaoza mabinti wao chini ya umri wa miaka 18 kutokana na hali ya ngumu ya maisha na kwamba wazazi huitumia njia hiyo kujipatia fedha kwa mahari”, anasema Edda Sanga.


"Ni jukumu la wazazi na jamii nzima kutoa elimu ya kijinsia kwa watoto wa kike ili waweze kujitambua na hatimaye kuwezesha kuhimili vishawishi ambavyo huwasababishia kupata mimba katika umri mdogo. Serikali nayo ina wajibu wa kutoa malazi kwa kujenga mabweni karibu na shule ili kuondoa changamoto wanazokumbana nazo njiani wanaporudi nyumbani", Mkurugenzi Mtendaji- TAMWA, Edda Sanga


Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inatamka wajibu wa jamii katika kumlinda na kutunza haki za mtoto ili kuhakikisha analelewa na kuwa ustawi mzuri katika maisha yake.

Kwa upande wake, Meneja wa Usimamizi na Ufuatiliaji wa Miradi wa TAMWA, John Ambrose amesema suala la kumlinda mtoto ni suala mtambuka na linahitaji nguvu ya pamoja ya wadau wote kushirikiana na kuweka mipango endelevu itakayomkomboa msichana na kumhakikishia usalama wake.

Ameeleza kuwa wanaendelea kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili walipoti habari za ukatili wa kijinsia kwa waledi na kusaidia kupunguza tatizo hilo katika jamii.

Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kinaungana na Watanzania wote kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike Duniani kikiamini kuwa nchi inaweza kufikia uchumi wa viwanda endapo vitaondolewa vikwazo vyote vinavyomkabili mtoto wa kike ikiwemo mimba za umri mdogo na kushindwa kutimiza ndoto zake.

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani hufanyika kila mwaka tarehe 11 Oktoba, ambapo mwaka huu yanafanyika kitaifa Tarime mkoani Mara yakiongozwa na kauli mbiu ya “Tokomeza Mimba za Utotoni Tufikie Uchumi wa Viwanda” ambapo linaenda sambamba na lengo la millennia namba tano linalozungumzia kuleta usawa wa kijinsia ili kufikia 50 kwa 50 ifikapo 2030.

 

 

 

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Asilimia 48 ya wananchi wanataka mchakato wa katiba uanze upya

Vuguvugu la kufufua mchakato wa Katiba Mpya limeendelea kujitokeza kwa sura mpya ambapo uchunguzi ...

Uhaba wa maji unavyowatesa wakazi wa mtaa wa Golani

 Saa 5 asubuhi  napita  mtaa wa Golani, kata ya Kimara katika jiji la Dar ...