Connect with us

Biashara/Uchumi

Soko la Hisa la Dar: Fursa ya kipekee kwa wajasiriamali wazalendo Tanzania

Published

on

Soko letu limekuwa likiwanufaisha zaidi wageni na wananchi wa nchi jirani ambao hulitumia kikamilifu kujinufaisha na wazalendo wengi kutoelewa nini kinachoendelea. Kwa wale waliokwisha jitosa, huwezi amaini jinsi wanavonufaika na kuwekeza zaidi na zaidi.

Leo kidogo tutupe jicho kwenye hii sekta ya hisa… Si sekta ngeni sana ila kwa hapa nchini wananchi wengi hawajaigundua na kushiriki kikamilifu kama nchi jirani na Tanzania. Wenzetu Kenya wamejitahidi kwenye ushiriki wa soko lao la Hisa la Nairobi (Nairobi Stock Exchange). Na kwa Afrika Mashariki, hili Soko la Hisa la Nairobi ndilo soko kubwa kuliko yote.

Soko letu la hisa la Dar es Salaam (DSE) japo kila siku limekumbatia usemi ni soko geni nchini, lina zaidi ya miaka  15 tangu lianze kufanya biashara mwaka 1998 mwezi  wa Aprili. Kwa muda wote huu wa miaka 15 soko limekuwa halina ukuaji  wa  kuridhisha  wala kuvutia. Mpaka leo 2013 kampuni zilizojisajili ni 17 tu, (Soma hapa zaidi http://www.dse.co.tz/main/index.php?page=5)  Idadi ya wananci wanaoshiriki kuuza na kununua hisa bado ni ndogo sana na uelewa wa jamii juu ya hili soko ni mdogo sana!

Pamoja na changamoto zake, hili soko lina faida kubwa kwa wale walioligundua na wanaoendelea kulitumia. Kuna mjasiriamali mmoja, yeye alinunua hisa za Twiga mwishoni mwa miaka ya 90 au mwanzoni mwa miaka ya 2000 zikiwa zinauzwa kati ya 200-300 kwa kipande. Leo hii kipande hicho hicho cha Twiga Cement kinauzwa kati ya 2500-2006 kiasi cha miaka 13 tu mbele.

Mdau huyu wa soko hilo anakiri kama angejua ukuaji ni wa kiasi hiki basi angenunua zaidi ya hizo alizonunuaga. Na ameendelea kuongeza vipande vyake kila awezapo. Anadai yeye hupenda kuwekeza kwenye hisa sababu hakuna usumbufu wa uendeshaji . Ukishanunua hisa unakaa na kungoja zipande ama zishuke ili na wewe uuze za kwako. Anakiri kuwa soko hili limemnufaisha sana na anawashauri wengine wajiunge nalo wapate kunufaika pia.

Wengi wetu wenye mitaji midogo midogo tunaweza kunufaika kwa kujiunga na hili soko la hisa la Dar es Salaam na kununua vipande kwa pesa tuliyonayo. Vipande vingi vimeonesha kupanda thamani yake ikiwemo hisa za makampuni ya bia (TBL na SBL), Saruji (Twiga  na Simba ) na Bank kama NMB. Kama mwekezaji mzalendo, ukijitosa ukanunua hisa zako za 2,000,000 leo, baada ya miaka 4 unaweza kuziuza hata kwa faida kubwa tu bila kuteseka na usumbufu wa uendeshaji kama zilivyo biashara nyingine.

Upande wa pili soko hili la hisa pia lina magumu yake kama kupotea kwa mtaji wako kutokana na kushuka kwa thamani ya vipande. Hili kwa mfano, limewaathiri wawekezaji walionunua hisa za CRDB na TOL ambazo zimekuwa zikikumbwa na kushuka kwa thamani mara kwa mara. Muhimu ni kuwa makini tu kwa kuchagua vyema ni hisa zipi ununue na kampuni ipi uwekeze.

Soko letu limekuwa likiwanufaisha zaidi wageni na wananchi wa nchi jirani ambao hulitumia kikamilifu kujinufaisha na wazalendo wengi kutoelewa nini kinachoendelea. Kwa wale waliokwisha jitosa, huwezi amaini jinsi wanavonufaika na kuwekeza zaidi na zaidi.

Huu ni wito wangu kwenu wazalendo wenzangu, mkajiunge na soko la hisa la Dar es Salaam na kufaidi matunda yake!

Continue Reading
2 Comments

2 Comments

 1. Mbwana

  02/02/2013 at 10:19 am

  Changamoto yako kwa watanzania kushiriki katika soko la hisa ni nzuri. Ni kweli kabisa ushiriki wao una faida kubwa bila kuvuja jasho jingi la uendeshaji na ufuatiliaji.  Lakini ni wazi kwamba ukiritimba uliojengwa kwenye mfumo wa uendeshaji wa soko hilo, unachangia ushiriki mdogo wa wananchi katika soko hilo.

  Hivi kuna sababu gani mpaka leo hii, miaka 15 toka soko lianzishwe tun- kampuni za madalali tano tu (stockbrokers).  Je madalali hawa, wana mtandao wa kufika nchi nzima? Mtu wa Shinyanga au Katavi, akitaka kununua hisa katika soko hilo analazimika kuwatafuta madalali hao watano tu ambao ofisi zao hazijatapakaa nchi nzima.

  Ushauri wangu, ni bora tuachane na ukiritimba katika uendeshaji wa soko. Zisajiliwe kampuni nyingi zaidi za madalali. Ikibidi yawekwe masharti mahususi kwamba vipaumbele vya usajili wa madalali vitatolewa kwa wale watakao operate kwenye mikoa ambayo haina huduma yao. Tjifunze kwa jirani zetu- Kenya na Uganda…..Mabenki yenye mitandao nchi nzima yamesajiliwa kuuza hisa za soko la hisa….kwanini sisi hatufanyi hivyo? NMB, NBC,CRDB,Postal Bank,Exim Bank zikiruhusiwa kuuza hisa, maeneo mengi ya nchi yetu yatapata huduma hiyo.  Hivi kama leo hii Halmashauri ya Bukoba inatumia mtandao wa benki ya Posta kuuza viwanja vyake, na wanafanikiwa….iweje soko la hisa washindwe kutumia mtandao wa aina hiyo?

  Lakini lingine, soko la hisa wafikirie matumizi ya teknolojia katika kurahisisha kazi zao. Hivi leo hii kama makampuni ya huduma mbalimbali kama umeme, maji nk wanatumia teknolojia ya Mpesa, airtel money na tigo pesa kulipia huduma zao, iweje soko la hisa washindwe kutumia platform hiyo kuwafikia wananchi wengi zaidi? 

  Mimi ninadhani uongozi wa soko la hisa una weakness ya kuwa na innovation ya kuboresha utendaji wao. Waende jirani pale Kenya wala sio Wall Street, wakajifunze.

 2. DORAH MGONDAH

  06/05/2013 at 8:01 am

  Pole na kazi.  Nikiwa mfanyakazi wa kipato cha kawaida, ningependa kupata maelekezo – ni wapi au nimuone nani ambaye atanipa maelezo ya jinsi ya kujiunga na soko la hisa? 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Biashara/Uchumi

Kamari za mtandaoni janga jipya kwa vijana Afrika

Published

on

Ukuaji wa  huduma za miamala ya fedha kwa njia ya mtandao (mobile money) umetenegeneza fursa mpya kwa wafanyabiashara kutangaza na kuuza bidhaa na huduma zao. Moja ya fursa ambayo inavuma kama upepo wa dhoruba nchini ni ukuaji wa sekta ya ubashiri katika mchezo wa mpira wa miguu.

Kwa lugha nyepesi inatambulika kama ‘kubeti’ au ‘sport betting’. Kilichofanya sekta hiyo ikue ni ongezeko la matumizi ya intaneti hasa kwa vijana wengi wa Afrika. Wateja  wa sekta hiyo wanaweza kupata huduma za kubashiri matokeo ya mpira wa miguu kwa njia ya mtandao popote walipo.

Nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Ghana, Nigeria na Congo DRC zinashuhudia ukuaji  mkubwa wa ubashiri katika michezo na aina zingine za kamari zinazochezwa kwa kutumia simu za mkononi za kawaida au zile zenye uwezo wa kupata intaneti.

‘Sport betting’ hufanyika kwa mtu kubashiri matokeo ya mechi ya mpira inayochezwa siku husika, ikiwa atabashiri/ atatabiri na timu fulani ikashinda dhidi ya nyingine hupata kiasi fulani cha fedha.

Ubashiri huo ambao hufanyika hasa kwenye ligi za mpira wa Ulaya na Ligi ya ndani (Vodacom Premier League), imekuwa ni sehemu yenye mzunguko mkubwa wa pesa. Asilimia kubwa ya ubashiri huo hufanyika kwa kutumia simu ambapo tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa majukwaa ya simu yanaibukia kuwa njia ya haraka ya kucheza kamali za mitandaoni.

Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Colorado cha nchini Marekani, Victor Odundo Owuor anaeleza katika moja ya makala zake kuwa ukijumuisha sekta ya kamali ya Kenya, Nigeria na Afrika Kusini inaweza kufikia Dola za Marekani bilioni 37 kwa mwaka 2018 pekee.

Anasema kuwa  Kenya pekee inakadiriwa kuwa watu milioni 2 wanajihusisha moja kwa moja kwenye ubashiri wa matokeo ya mechi za mpira kwa njia ya simu. Wanaoshiriki zaidi ni vijana wasio na ajira ambao wanaamini kuwa ubashiri ni njia ya haraka kupata fedha na kuondokana na umasikini.

Kwa mukta huo, ni rahisi kuwaona vijana wakigombania fursa ya kubashiri matokeo ya ligi za mpira kwasababu sh. 1000 inaweza kuzalisha sh. 5000 na zaidi.

Inaelezwa kuwa nchini Nigeria, watu milioni 60 walio katika umri wa miaka kati ya 18 na 40 hutumia karibu Dola 5 (zaidi ya Tsh.100,00 ) kwenye ubashiri kila siku. Wengi wao hawana ajira na wanaishi kwenye umasikini wa kiwango cha juu. Fedha wanayoipata hutumia kujikimu kwa maisha ya kila siku.

 

Athari za ubashiri wa mpira wa miguu

Utafiti uliofanywa nchini Kenya umeonyesha kuwa watu ambao wanajihusisha zaidi kwenye ubashiri wa matokeo ya mpira wa miguu mtandaoni, wanafanya hivyo licha ya kufahamu kuwa kuna hatari mbele yao.

Hatari mojawapo ni kwamba vijana hao hukopa fedha ili wakabashiri matokeo ya mpira wa ligi. Hali hiyo huwaingiza katika mzunguko mkubwa madeni.  Kadiri deni linapokuwa kubwa humuweka kijana kwenye wakati mgumu na kufanya maamuzi yanayoweza kugharimu uhai wake.

Licha ya kuwepo sheria zinazosimamia michezo ya bahati nasibu, lakini ubashiri umetawala akili za vijana na kuwafanya kuwa walevi (addictive). Wataalamu wa saikolojia wanahofia kuwa siku zijazo ubashiri utakuwa miongoni mwa sababu kubwa za magonjwa ya akili miongoni mwa vijana wengi wa Tanzania.

Mtafiti Owuor, anaeleza kuwa licha ubashiri au kamari kuwa na athari hasi kwa vijana lakini ni miongoni mwa sekta inayochochea ukuaji wa biashara ya fedha za mtandaoni.

Anaeleza kuwa miamala inayofanyika mtandaoni ndio njia pekee ya kuzinusuru benki ambazo zinakabiliwa na gharama kubwa za uendeshaji na madeni ya mikopo.

Upande wa pili, michezo ya ubashiri na bahati nasibu zinazofanyika kwa njia ya simu zinaongeza mapato kwa serikali kupitia kodi inayokatwa kwenye miamala ya simu.

Hata hivyo, serikali za Afrika ikiwemo Tanzania zimeshauriwa kutathmini na kuwasaidia vijana ambao hawana ajira ili kuwaepusha na madhara hasi ya ubashiri wa mtandaoni wa mpira wa miguu.

Continue Reading

Biashara/Uchumi

Wakulima wa mahindi kuunganishwa kwenye mnyororo wa thamani

Published

on

Imeelezwa kuwa kukosekana kwa  teknolojia ya kisasa na masoko ya mazao  ni miongoni mwa changamoto zinazokwamisha  ukuaji wa sekta  ya kilimo nchini. Changamoto hizo zinachochewa na  uwekezaji mdogo wa rasilimali watu na fedha  kwenye huduma muhimu za kilimo.

Kwa kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, serikali inawajibika kuwawezesha wakulima nchini kupata pembejeo na teknolojia ya kisasa kuhakikisha wanazalisha mazao yenye ubora yanaweza kushindana kwenye soko la kimataifa.

Kwa kutambua hilo serikali ilianzisha benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuhakikisha wakulima wanapata fedha kutoka taasisi hiyo kuendesha shughuli zao. Lakini tangu kuanzishwa kwake, benki hiyo haijawafikia wakulima wengi, jambo linalowakosesha fursa ya kupata mikopo na ushauri wa kiteknolojia.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amesema  serikali imeitaka benki hiyo kuongeza matawi  ili kuwafikia wakulima wengi ambao wanahitaji mikopo kuongeza tija kwenye kilimo.

Amesema tayari benki hiyo imefika mkoa wa Dodoma na hadi kufikia Juni 30, 2018 itakuwa imefunguliwa ili kuwahudumia wakulima wa kanda ya kati  inajumuisha mikoa ya Dodoma, Singida.

“Baada ya ufunguzi wa ofisi ya Kanda ya Kati kukamilika Benki Itafanya uchambuzi wa fursa zilizopo Kikanda na hivyo kuchukua hatua na taratibu za kufungua ofisi nyingine kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha”, alisema Dkt. Kijaji.

Ameongeza kuwa TADB inatekeleza mpango wa miaka mitano (2017- 2021), wa kusogeza huduma karibu na wateja kwa kuanzisha ofisi za Kikanda katika Kanda ya Kaskazini, Kusini, Kati, Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Zanzibar kwa awamu mbalimbali.

Dkt. Ashatu amesema mikopo itakayotolewa kwa wakulima itatumia mfumo wa makundi; kundi la kwanza litahusisha wakulima wadogo wadogo kwa riba ya asilimia 8- 12, kundi la pili la miradi mikubwa ya kilimo kwa asilimia 12 – 16 kwa mwaka. Kundi la mwisho ni mikopo ya ushirika ambapo riba yake inaendana na hali ya soko la matumizi ya mkopo.

Amebainisha kuwa serikali inafanya majadiliano na wadau wa kilimo ili kupunguza kiwango cha riba ili kuwavutia wakulima wengi kukopa na kufaidika na kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Thomas Samkyi alisema kukosekana kwa masoko ya mazao ya kilimo ni changamoto nyingine inayorudisha nyuma maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Katika kutekeleza majukumu ya Benki hiyo, serikali imeanza kutoa huduma kwa kulenga minyororo michache ya ongezeko la thamani katika kilimo cha mahindi kwa kutoa mikopo ya ununuzi wa pembejeo, vifaa na vifungashio vya kisasa vya kuhifadhia mahindi na teknolojia ya uhifadhi wa mahindi ili kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa.

“Kwa sasa tumejikita katika mnyororo mzima wa uongezaji wa thamani kuanzia uandaaji wa shambani hadi kwa upatikanaji wa masoko, ikiwemo mahitaji ya uzalishaji wenye tija kwenye sekta nzima ya kilimo kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa mashamba.

“Kupima ubora wa udongo na virutubisho vinavyohitajika kwenye uzalishaji wa mahindi, upatikanaji wa pembejeo za kilimo zikiwemo mbegu bora, mbolea, madawa na vifaa na teknolojia mbali mbali za umwagiliaji na fedha kwa ajili ya kulipia gharama mbalimbali za uzalishaji wa mahindi,” alisema.

Samky alisema usaidizi na mikopo itakayotolewa itakuwa kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kilimo katika kuimarisha minyororo ya thamani katika kilimo

“Inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji na mitambo ya umwagiliaji, uchimbaji wa visima vya maji ya umwagiliaji, ujenzi wa mabawa ya uvunaji maji ya mvua, ujenzi wa maghala bora ya kuhifadhia mahindi na ujenzi wa miundombinu ya masoko,” alisema.

Continue Reading

Biashara/Uchumi

RIPOTI YA CAG: Rais Magufuli asisitiza trilioni 1.5 hazijapotea, aitupia lawama mitandao ya kijamii

Published

on

Rais John Magufuli amesema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) aliyokabidhiwa haionyeshi upotevu wa trilioni 1.5 na kwamba ni upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii una lengo la kuigombanisha Serikali na wananchi.

Kauli ya Rais imekuja ikiwa zimepita siku chache tangu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi kutoa kauli inayofanana na ya Rais kuwa hakuna fedha iliyopotea na kilichopo ni kutokueleweka kwa ripoti ya CAG.

Akizungumza leo muda mfupi baada ya kuwaapisha Majaji wa Mahakama, Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema aliwasiliana na CAG, Prof. Mussa Assad na kwamba alikiri kuwa hakuna upotevu wa trilioni 1.5 zinazosemekana hazijulikani zilipo.

“Nilikuwa ninasoma baadhi ya mambo mengine wanasema Serikali imeiba trilioni 1.5. Siku moja nikampigia Controller and General Auditor General (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali) mbona kwenye ripoti yako uliyonisomea hapa Ikulu hukunieleza huu wizi wa trilioni 1.5.” amesema Rais Magufuli.

Amesema kama kweli upotevu wa fedha huo ungekuwa umetokea angechukua hatua mapema za kuwafukuza kazi watendaji waliohusika na ufisadi huo lakini kinachoonekana ni upotoshaji unaofanywa kwenye mitandao ya kijamii na kuwaaminisha wananchi kuwa fedha zimeibwa na Serikali.

“Kwasababu ungenisomea hapo siku hiyohiyo ningefukuza watu, kama nimefukuza wakurugenzi watatu siku hiyohiyo kwasababu ya hati chafu, hawa trilioni 1.5 uliwaficha wapi? Nimejaribu kusoma kwenye ripoti yako (ripoti ya Ukaguzi ya CAG) sioni mahali palipoandikwa zimepotea trilioni 1.5. Prof. Assad aliniambia hakuna kitu kama hicho, nikamuuliza Katibu Mkuu akasema hakuna kitu kama hicho.” Ameeleza Rais Magufuli.

Hata hivyo, Rais Magufuli hakufafanua trilioni 1.5 zimetumikaje kama kweli hazijapotea, zaidi ya kuwalaumu watumiaji wa mitandao ya kijamii kutumia uhuru wa kutoa maoni kujadili ripoti ya CAG ambayo inaonesha trilioni 1.5 hazijulikani zimetumikaje.

“Kuna ugonjwa tumeupata Tanzania wa kufikiri kila kinachoandikwa kwenye mitandao ni cha ukweli. Sasa sifahamu huu ugonjwa umetoka wapi? Lakini ni kwasababu hii mitandao hatuicontrol (hatuisimamii) sisi, wako huko wenye mitandao yao, wao interest (maslahi) yao ni kutengeneza biashara hawajali madhara mtakayoyapata.” Amesema Rais.

Kauli ya Rais imeungwa mkono na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji akiwa bungeni Dodoma wakati akitoa tamko la Serikali juu kutoonekana kwa matumizi ya trilioni 1.5 kwenye matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.

“Kutokana na matumizi ya mfumo huu wa viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika sekta ya umma, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba hakuna fedha taslimu ya shilingi trilioni 1.51 iliyopotea au kutumika kwenye matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Bunge. Hivyo basi, madai ya baadhi ya watu wasiolitakia mema Taifa letu na Serikali yetu ya Awamu ya Tano hayana msingi wowote wenye mantiki.” Amesema Naibu Waziri.

Amesema wakati CAG akifanya ukaguzi wa mahesabu, Serikali ilikuwa inatekeleza mpango mpya wa kimataifa wa mahesabu katika sekta ya umma (International Public-Sector Accounting Standard IPSAS Accural) na kwamba ndio ulioleta mkanganyiko wa mahesabu.

“Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kuanzia mwaka 2016/17, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianza rasmi kuyatambua mapato kwa mfumo wa Accrual. Hivyo basi, kati ya mapato haya ya shilingi trilioni 25.3, yalikuwemo pia mapato tarajiwa (receivables) kama mapato ya kodi yenye jumla ya shilingi bilioni 687.3 pamoja na mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya jumla ya shilingi bilioni 203.92 (transfer to Zanzibar).” Amesema Naibu Waziri na kuongeza kuwa,

“Katika uandishi wa taarifa ya ukaguzi, CAG alitumia taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Bajeti (Budget Execution Report) ambapo hadi kufikia tarehe 30 Juni 2017, mapato yalikuwa jumla ya shilingi trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa shilingi trilioni 23.79.”

Naibu Waziri amefafanua kuwa Matumizi ya trilioni 23.79 hayakujumuisha bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva. Pia Matumizi hayo yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika.

Ameongeza kuwa, baada ya kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia Ridhaa za Matumizi (Exchequer issues) yalikuwa shilingi trilioni 24.4. Amedai kuwa trilioni 1.51 zilizodaiwa kutoonekana kwenye matumizi ya Serikali zilitokana na mchanganuo ufuatao;

Katika ripoti ya CAG aliyoitoa hivi karibuni katika ukurasa wa 34 imeelezea kwa undani kuhusu kutoonekana kwa matumizi ya fedha hizo, ambapo aliwataka wabunge kuihoji Serikali ziliko trilioni 1.5 kwasababu katika ukaguzi wake hakubaini zimetumikaje ingawa hakusema zimepotea.

Tangu kutolewa kwa ripoti ya CAG ya ukaguzi wa hesabu za Serikali na mashirika mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha unaoishia June 2017. Mijadala mbalimbali imeendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mambo mbalimbali yaliyoibuliwa na CAG ikiwemo kutojulikana kwa matumizi ya trilioni 1.5.

Baadhi ya vyama vikiwemo vya CCM, ACT-Wazalendo na CHADEMA vilitoa maoni yao kuhusu ripoti hiyo.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amekuwa alijitokeza kwenye mitandao ya kijamii akisisitiza kuwa ukaguzi wa CAG ulihusisha fedha zilizokusanywa na sio za hati fungani ambazo Serikali imezitolea maelezo.

Continue Reading

Must Read

Copyright © 2018 FikraPevu.com