Connect with us

Jamii

Sakata la kutelekeza watoto Dar lachukua sura mpya. Viongozi wa dini, wabunge watajwa

Published

on

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameitaka jamii kuunga mkono kampeni iliyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwasaidia wanawake wenye watoto ‘waliotelekezwa’ na waume zao.

Akizunguma leo wakati wa uzinduzi wa Chanzo ya saratani kwa wasichana katika viwanja vya Mbagala Zakhem, jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais amesema wanaume waliowazalisha wanawake hao kwa kupenda au bahati mbaya wanapaswa kutimiza wajibu wao wa kutoa matunzo kwa watoto wao.

Amesema zoezi lililoanzishwa na Mkuu wa Mkoa ni hatua nzuri ya kisheria kuwasaidia wanawake ambao wanakabiliwa na ukatili wa kijinsia ambapo mikoa mingine iige ili kuhakikisha wanawake na watoto wanapata haki zao za msingi ikiwemo matunzo.

“Mkuu wa mkoa nakupongeza, hatua hii itatupa takwimu zitakazotusaidia kufanya tafiti, pengine na mikoa mingine itafanya. Naomba baada ya hatua hii wakina mama hawa waelekezwe njia ya kufanya”, amesema Makamu wa Rais.

Ameongeza kuwa taasisi ya Ustawi wa Jamii inapaswa kushughulikia kesi zote za wanawake waliotelekezwa na amewataka watu wasibeze juhudi za Makonda kwasababu zinalenga kuondoa tatizo la malezi katika jamii.

“Taasisi nyingine zitoe ushirikiano, tukikosoa hatua hizi za awali tutakuwa hatusaidii jamii, maafisa wa maendeleo ya jamii wapo pale wayabebe yatakayokusanywa, watakaokubaliana yaishe wayamalize lakini yale yatakayopelekwa mahakamani yapelekwe”.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza na wanawake waliotelekezwa jana jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza awali katika viwanja hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameelezea kampeni hiyo sambamba na kutaja orodha ya wanaume waliozaa na wanawake hao ambapo inajumuisha viongozi wa dini na wabunge.

Kwa mujibu wa Makonda, wanawake 480 wanaodai kutelekezwa, waliofika jana katika ofisi yake kupata msaada wa kisheria, kati yao 47 wamesema wametelekezwa na wabunge na 14 wamedai kutelekezwa na viongozi wa dini.

“Wengine wamewataja wafanyabiashara mashuhuri ambao ukiwatazama huwezi kuamini kama wanafanya ukatili huu”, amesema.

Ameongeza kuwa mwaka 2017 pekee walizaliwa watoto 129,347 ambapo kati ya hao asilimia 60 walitelekezwa ambapo wengine wanalelewa katika vituo vya watoto yatima.

Ikumbukwe kuwa jana wanawake hao wanaodai kutelekezwa wakiwa na watoto wao walifika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kupata msaada ambapo tayari wameandikisha taarifa zao za msingi na kuwaandikia barua wanaume waliozaa nao ili wafike katika ofisi hiyo kwaajili ya hatua inayofuata.

 

Sheria inasemaje juu matunzo

Mila na desturi za Tanzania zinamtambua mwanaume kama kiongozi wa familia mwenye jukumu la kutoa matunzo kwa mke na watoto wake na kuhakikisha anatoa matumizi kama chakula, mavazi , matibabu, makazi na mahitaji ya msingi kama ada za shule, vifaa vya shule na kila kitu ambacho ni mahitaji ya msingi kwa makuzi na ustawi wa mtoto.

Kwa hiyo mzazi asiyejihusisha kwa namna yoyote na huduma hizi ambazo zinatambulika kisheria huyo ndiye aliyetelekeza familia au watoto.

Kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu kifungu cha 166 kinasema kuwa mtu yeyote ambaye ni mzazi au mlezi au mtu mwingine mwenye uangalizi halali wa mtoto yeyote mwenye umri usiozidi miaka kumi na nne, hali ana uwezo wa kumuhudumia mtoto, kwa kuamua au kinyume cha sheria au bila ya sababu za msingi akakataa kumhudumia na akamtelekeza mtoto bila msaada, atakuwa ametenda kosa.

Mzazi akikataa kumhudumia na akamtelekeza mtoto bila msaada, atakuwa ametenda kosa.

 

Wadau wanena

Akizungumza na FikraPevu, Violeth Chonya kutoka Kituo Cha Usuluhishi (CRC), Chama Cha Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA), amesema Makonda anapata nguvu ya kuratibu zoezi hilo kwasababu atalazimika kufanya kazi na wanasheria na watu kutoka ustawi wa jamii kuendesha kesi za utelekezaji watoto ili haki itendeke.

“Yeye anafanya kazi na watu wa Ustawi wa Jamii, dawati la jinsia na wanasheria, wote wanahusika na hizo kesi za child protection (kuwalinda watoto)”, amesema Violeth.

Akifafanua kuhusu umri sahihi wa mtoto kupata matunzo ya baba, amesema ni mtoto yeyote ambaye hajaanza kujitegemea na bado yupo kwenye uangalizi wa wazazi. Ameeleza kuwa wajibu wa kumtunza mtoto ni wa wazazi wote wawili na endapo mzazi mmoja hatawajibika anakuwa amefanya kosa kisheria.

“Mtoto ana haki ya kupata matunzo mpaka pale atakapoanza kujitegemea. Hata kama mtoto ana umri wa miaka 18 lakini hana uwezo kujitegemea wazazi wote wawili wanawajibika kumlea mtoto”, amesema na kuongeza kuwa,

“Hapo kuna Sheria ya Ustawi wa Jamii pamoja na Sheria ya Mtoto ya 2009 inafanya kazi kwasababu ukiangalia pia Sheria ya Ndoa inamwamuru kama baba  kutunza familia. Sheria ya mtoto inasema mtoto ana haki ya kupata matunzo ya baba na mama. Sasa pale inapotokea upande mmoja hautekelezi hilo ni kosa kisheria”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Wanawake Katika Jitihada za Kimaendeleo (WAJUKI), Janeth Mawinza amesema utelekezaji wa familia ni  ukatili wa kijinsia kwasababu una mkosesha mtoto matunzo na haki ya kupata malezi ya wazazi wote wawili.

“Kesi nyingi tunazozipokea ni utelekezaji wa familia hili ndio limechukua nafasi kubwa zaidi lakini pia inafuatia na kesi hizo za ubakaji, vipigo na kesi za kisaikolojia”, amesema Janeth.

Amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza familia na kuishi kwa haki na usawa ili kuhakikisha jamii inapata maendeleo endelevu, “Tumefanikiwa kuwapa watu elimu na kuanza kujitambua na kuanza kupambana na ukatili huo wa kunyanyasa watoto”.

Serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amekemea udhalilishwaji wa watoto ‘waliotelekezwa’ na baba zao ambao tangu jana picha zao zimekuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii baada ya kufika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakiwa na mama zao.

Amewataka wanawake hao kufuata mifumo ya kisheria kupata msaada kwasababu jambo hilo ni nyeti na linahitaji uangalifu ili kulinda maslahi ya watoto kama Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inavyoelekeza.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Jamii

Kwanini wanawake hupata msongo wa mawazo kwa kiwango kikubwa kuliko wanaume?

Published

on

Kama ambavyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya vyombo vya habari, wanawake wapo kwenye nafasi ya kupata msongo wa mawazo kwa kiasi kikubwa kuliko wanaume. Pia kiwango chao cha kupata matatizo ya kiafya au kujiua ni kikubwa mara tatu ya kile cha wanaume.

Utofauti huu kati ya jinsia hizi mbili bado haupo bayana, baadhi ya watu wanaamini takwimu hizi zimeongezwa chumvi kwasababu tu wanaume ni viumbe “dhaifu” hivyo ni rahisi kwa wao kuonesha dalili hizo. Hata hivyo baadhi ya tafiti zinaonesha kwamba madai haya ni ya kweli, kama hizi zifuatazo:

1. Utofauti wa homoni huchukuliwa kama kigezo kikubwa. Ukilinganisha na wanaume, wanawake hukumbana na matatizo mengi katika viwango vya homoni mwilini ambayo huusishwa na dalili za msongo wa mawazo. Mbali na matatizo mbalimbali ya hedhi, asilimia 15 ya wanawake hupata msongo wa mawazo baada ya kujifungua.

Msongo wa mawazo hujitokeza sana katika kipindi ambacho hedhi hukoma, ambapo melancholia ilibainika kuwa moja ya matatizo ya kiakili mpaka kufikia mwaka 1980. Pia wanawake wapo kwenye nafasi kubwa ya kupata matatizo ya upungufu wa homoni ya thyroid (tezi yake ipo kwenye shingo), ambapo mara nyingi huusishwa na msongo wa mawazo.

2. Kutokana na kigezo cha kimaumbile wanawake wapo kwenye nafasi kubwa ya kupata msongo wa mawazo kutokana na tafiti mbalimbali za mapacha wasiofanana, pia kutokana na historia ya familia.

3. Wanawake hujihusisha zaidi kwenye mahusiano binafsi kuliko wanaume na huathirika zaidi pale wanapovurugwa. Wanawake wengi walioolewa na wale ambao ni mama wa nyumbani wamekuwa na majukumu makubwa zaidi na kujikuta wanashindwa kuhimili majukumu ya kazi na familia, kama vile kutunza na kulea ndugu ambao ni wazee.

 

 Wanawake wenye umri kati ya miaka 25 mpaka 40 kiwango chao cha kupata msongo wa mawazo kimeongezeka mara nne zaidi ya wanaume.

Utafiti uliofanyika Ulaya kwenye nchi zaidi ya 30 na kuhusisha watu milioni 514 umebaini kwamba kiwango cha wanawake wenye umri wa kati kupata msongo wa mawazo kimeongezeka ndani ya miaka 40 kutokana na shughuli hizi. Wanawake wenye umri kati ya miaka 25 mpaka 40 kiwango chao cha kupata msongo wa mawazo kimeongezeka mara nne zaidi ya wanaume.

4. Wanawake huishi kwa miaka mingi zaidi kuliko wanaume na hii huusishwa na kukosa matumaini, upweke, hali mbaya ya kiafya na matatizo mengine ambayo husababisha msongo wa mawazo.

5. Wanawake ni wepesi sana kutafuta kuonana na wahudumu wa afya pale wanapojisikia kwamba hawapo vizuri kiafya tofauti na wanaume, hivyo ni rahisi kwa wao kugundulika wanapokuwa na matatizo ya kiafya. Pia kuna ushahidi kutoka kwa madaktari wa kike na wa kiume kuhusu wepesi wa kugundua hali ya msongo wa mawazo kwa wanawake zaidi kuliko wanaume kwa dalili zinazofanana.

6. Dalili za huzuni kwa wanawake ni kubwa mara nne zaidi ya ilivyo kwa wanaume, na matokeo yake huongezeka zaidi kadiri majira na nyakati zinavyobadilika. Mfano, Tromso mji uliopo Norway, huwa na karibu siku 50 kipindi cha baridi ambapo jua huwa halionekani kabisa.

Katika kipindi hiki watu huchoka sana na kiwango cha utendaji kazi hupungua. Pia kuna ongezeko kubwa la msongo wa mawazo hasa kwa wanawake. Ajali na mauzo ya dawa mbalimbali za usingizi huongezeka zaidi katika kipindi hicho.

Hata hivyo wanawake walio kazini na wale wasio na wenzi wapo kwenye nafasi kubwa si tu ya kupata msongo wa mawazo lakini pia magonjwa ya moyo, kansa ya matiti na kansa ya kizazi.

Pamoja na ushahidi uliotolewa hapo juu, bado tafiti zaidi zinahitajika juu ya nadharia za msongo wa mawazo kwa wanaume na wanawake.

Continue Reading

Biashara/Uchumi

RIPOTI YA CAG: Rais Magufuli asisitiza trilioni 1.5 hazijapotea, aitupia lawama mitandao ya kijamii

Published

on

Rais John Magufuli amesema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) aliyokabidhiwa haionyeshi upotevu wa trilioni 1.5 na kwamba ni upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii una lengo la kuigombanisha Serikali na wananchi.

Kauli ya Rais imekuja ikiwa zimepita siku chache tangu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi kutoa kauli inayofanana na ya Rais kuwa hakuna fedha iliyopotea na kilichopo ni kutokueleweka kwa ripoti ya CAG.

Akizungumza leo muda mfupi baada ya kuwaapisha Majaji wa Mahakama, Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema aliwasiliana na CAG, Prof. Mussa Assad na kwamba alikiri kuwa hakuna upotevu wa trilioni 1.5 zinazosemekana hazijulikani zilipo.

“Nilikuwa ninasoma baadhi ya mambo mengine wanasema Serikali imeiba trilioni 1.5. Siku moja nikampigia Controller and General Auditor General (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali) mbona kwenye ripoti yako uliyonisomea hapa Ikulu hukunieleza huu wizi wa trilioni 1.5.” amesema Rais Magufuli.

Amesema kama kweli upotevu wa fedha huo ungekuwa umetokea angechukua hatua mapema za kuwafukuza kazi watendaji waliohusika na ufisadi huo lakini kinachoonekana ni upotoshaji unaofanywa kwenye mitandao ya kijamii na kuwaaminisha wananchi kuwa fedha zimeibwa na Serikali.

“Kwasababu ungenisomea hapo siku hiyohiyo ningefukuza watu, kama nimefukuza wakurugenzi watatu siku hiyohiyo kwasababu ya hati chafu, hawa trilioni 1.5 uliwaficha wapi? Nimejaribu kusoma kwenye ripoti yako (ripoti ya Ukaguzi ya CAG) sioni mahali palipoandikwa zimepotea trilioni 1.5. Prof. Assad aliniambia hakuna kitu kama hicho, nikamuuliza Katibu Mkuu akasema hakuna kitu kama hicho.” Ameeleza Rais Magufuli.

Hata hivyo, Rais Magufuli hakufafanua trilioni 1.5 zimetumikaje kama kweli hazijapotea, zaidi ya kuwalaumu watumiaji wa mitandao ya kijamii kutumia uhuru wa kutoa maoni kujadili ripoti ya CAG ambayo inaonesha trilioni 1.5 hazijulikani zimetumikaje.

“Kuna ugonjwa tumeupata Tanzania wa kufikiri kila kinachoandikwa kwenye mitandao ni cha ukweli. Sasa sifahamu huu ugonjwa umetoka wapi? Lakini ni kwasababu hii mitandao hatuicontrol (hatuisimamii) sisi, wako huko wenye mitandao yao, wao interest (maslahi) yao ni kutengeneza biashara hawajali madhara mtakayoyapata.” Amesema Rais.

Kauli ya Rais imeungwa mkono na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji akiwa bungeni Dodoma wakati akitoa tamko la Serikali juu kutoonekana kwa matumizi ya trilioni 1.5 kwenye matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017.

“Kutokana na matumizi ya mfumo huu wa viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika sekta ya umma, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba hakuna fedha taslimu ya shilingi trilioni 1.51 iliyopotea au kutumika kwenye matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Bunge. Hivyo basi, madai ya baadhi ya watu wasiolitakia mema Taifa letu na Serikali yetu ya Awamu ya Tano hayana msingi wowote wenye mantiki.” Amesema Naibu Waziri.

Amesema wakati CAG akifanya ukaguzi wa mahesabu, Serikali ilikuwa inatekeleza mpango mpya wa kimataifa wa mahesabu katika sekta ya umma (International Public-Sector Accounting Standard IPSAS Accural) na kwamba ndio ulioleta mkanganyiko wa mahesabu.

“Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kuanzia mwaka 2016/17, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianza rasmi kuyatambua mapato kwa mfumo wa Accrual. Hivyo basi, kati ya mapato haya ya shilingi trilioni 25.3, yalikuwemo pia mapato tarajiwa (receivables) kama mapato ya kodi yenye jumla ya shilingi bilioni 687.3 pamoja na mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya jumla ya shilingi bilioni 203.92 (transfer to Zanzibar).” Amesema Naibu Waziri na kuongeza kuwa,

“Katika uandishi wa taarifa ya ukaguzi, CAG alitumia taarifa za hesabu na nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Bajeti (Budget Execution Report) ambapo hadi kufikia tarehe 30 Juni 2017, mapato yalikuwa jumla ya shilingi trilioni 25.3 na matumizi yalikuwa shilingi trilioni 23.79.”

Naibu Waziri amefafanua kuwa Matumizi ya trilioni 23.79 hayakujumuisha bilioni 697.85 zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva. Pia Matumizi hayo yalikuwa hayajafanyiwa uhamisho (re-allocation) wakati ukaguzi unakamilika.

Ameongeza kuwa, baada ya kufanya uhamisho jumla ya matumizi yote kwa kutumia Ridhaa za Matumizi (Exchequer issues) yalikuwa shilingi trilioni 24.4. Amedai kuwa trilioni 1.51 zilizodaiwa kutoonekana kwenye matumizi ya Serikali zilitokana na mchanganuo ufuatao;

Katika ripoti ya CAG aliyoitoa hivi karibuni katika ukurasa wa 34 imeelezea kwa undani kuhusu kutoonekana kwa matumizi ya fedha hizo, ambapo aliwataka wabunge kuihoji Serikali ziliko trilioni 1.5 kwasababu katika ukaguzi wake hakubaini zimetumikaje ingawa hakusema zimepotea.

Tangu kutolewa kwa ripoti ya CAG ya ukaguzi wa hesabu za Serikali na mashirika mbalimbali nchini kwa mwaka wa fedha unaoishia June 2017. Mijadala mbalimbali imeendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mambo mbalimbali yaliyoibuliwa na CAG ikiwemo kutojulikana kwa matumizi ya trilioni 1.5.

Baadhi ya vyama vikiwemo vya CCM, ACT-Wazalendo na CHADEMA vilitoa maoni yao kuhusu ripoti hiyo.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amekuwa alijitokeza kwenye mitandao ya kijamii akisisitiza kuwa ukaguzi wa CAG ulihusisha fedha zilizokusanywa na sio za hati fungani ambazo Serikali imezitolea maelezo.

Continue Reading

Jamii

Kwanini kukaa muda mrefu kunasababisha kuganda kwa damu kuliko ukiwa umelala?

Published

on

Unaweza kuwa umegundua kuwa ukikaa sehemu moja bila kubadilisha mkao hata kwa saa moja, miguu yako itaanza kupatwa na hali isiyo ya kawaida. Wengine wanaweza kuhisi mshtuko fulani wa kutekenywa, maumivu au ganzi, lakini wengine wanafikia hatua ya kutoweza kusogeza miguu kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Na wengine wanapooza miguuni kwa muda mfupi.

Dalili hizi hujidhihirisha kwa mtu ikiwa atakaa sehemu moja muda mrefu kwa muda usiopungua saa moja.

Kwa upande mwingine, tunapolala huwa tunajinyoosha miguu yetu kwenye kitanda kwa saa 6 hadi 7. Lakini hatuhisi hali yoyote ya kutuumiza au dalili kama tulizoziona wakati tumekaa.

Kukaa kwa muda mrefu kunaweza kusababisha hali isiyo ya kawaida na wakati mwingine damu kuganda (boold clots) ndani ya mwili. Lakini ukiwa umelala huwezi kuhisi hali hiyo ikitokea kwenye mwili. Kwanini iko hivyo?

 Jinsi damu inavyozunguka

Kama tunavyofahamu, moyo ni kiungo au ogani muhimu inayohusika na mzunguko wa damu mwilini. Damu inaanza safari yake kwenye moyo; baada ya kutoka kwenye moyo, damu inaingia kwenye mshipa mkubwa (aota) na kusambazwa sehemu zingine za mwili kupitia mishipa midogo midogo (arteries).

Baada ya damu kuingia kwenye mishipa midogo midogo, hurudishwa tena kwenye mapafu na moyo kwa kupitia mfumo wa mishipa ya vena (venous system).

Mishipa ya vena ina matundu madogo ambayo yanasaidia damu kutorudi nyuma wakati ikisafiri kuelekea kwenye moyo. Kwa msingi huo inapambana na nguvu ya mvutano ambayo inazuia damu isisambae au kusafiri kutoka kwenye miguu hadi kwenye moyo.

Wakati mtu amekaa sehemu moja kwa muda mrefu, damu haiwezi kusafiri haraka kama inavyotakiwa. Hali hiyo huchochea mgando kwenye mwili ambapo matokeo yake ni kuganda kwa damu.

 

Ukiwa umelala…

Ukiwa umelala kitandani, kwa kiasi fulani miguu yako inakuwa imenyooka ukilinganisha na unapokuwa umekaa, na ni rahisi kuisogeza. Kwasababu hii, damu haitalazimika kufanya kazi kubwa ya kushindana na nguvu ya mvutano ili kufika kwenye mapafu na moyo. Matokeo yake damu inasafiri kwa urahisi.

Wakati umelala kwa kiasi kikubwa viungo vya mwili vinakuwa vimetulia, na hali hiyo haiwezi kusababisha tatizo la mzunguko wa damu kwasababu mwili umenyooka na damu hailazimika kusafiri kwenda juu.

Hata hivyo, haimanishi kuwa ukilala unakuwa salama dhidi ya kuganda kwa damu. Hata ukijilaza, mvutano bado una umuhimu katika mzunguko wa damu. Ukijilaza, nguvu ya mvutano inainuliwa kidogo na kupunguza tatizo la kuganda kwa damu kwa saa 8 hadi 15.

Kwa msingi huo, ukijilaza kitandani  bila kugeuka geuka kwa saa 20 au zaidi, unaweza kupata matatizo. Ndio maana madaktari wanakuwa makini hasa kwa wagonjwa wanaolala muda mrefu, jambo wanalolifanya ni kuwageuza mara kwa mara ili kuhakikisha damu haigandi na kuudhuru mwili.

 

Ukiwa umekaa…

Ukiwa umekaa sehemu moja hasa wakati unasafiri kwenye treni, basi au ndege kwa muda mrefu inasababisha shughuli za misuli ya mwili kupungua.

Kwa mkao huo, miguu pia haisogei na muda mwingi hukaa kwenye mwelekeo mmoja. Wakati huohuo damu inakosa nguvu ya kupambana na nguvu ya mvutano. Kutokana na mchakato fulani wa kibailojia, mzunguko wa damu kwenda juu  unapungua. Hali hii kwa kiasi kikubwa inasababisha kuganda kwa damu kwenye mwili na matokeo yake mtu hujisikia kupata ganzi au namna fulani ya kupooza.

Damu iliyoganda ikisafiri kwenye mishipa na kufika kwenye mapafu, inaweza kuleta madhara mbalimbali ikiwemo matatizo ya mfumo wa upumuaji (Pulmonary Embolism).

Ndio maana inashauriwa kusimama na kutembea mara kwa mara wakati ukiwa safarini hasa kwenye safari ndefu au ukiwa kwenye shughuli zinazokufanya ukae muda mrefu.

Continue Reading

Must Read

Copyright © 2018 FikraPevu.com