Rais Magufuli, Lowassa ‘kuvaana’ uchaguzi Kenya. Jubilee waishutumu Tanzania kuiba kura

SASA ni dhahiri kwamba Rais John Magufuli atakuwa katika mikakati ya kuhakikisha swahiba wake, Raila Odinga anashinda urais wa Kenya katika uchaguzi wa nchi hiyo uliopangwa kufanyika Agosti 8, mwaka huu.

Wakati Rais Magufuli yuko katika mradi huo, aliyekuwa akichuana naye kuwania urais wa Tanzania, Edward Lowassa, ametangaza kumuunga mkono Uhuru Kenyatta, rais aliyeko madarakani, akiwania muhula wa pili.

Ni kutokana na kuwa na kambi hizo kuu mbili katika uchaguzi wa Kenya, inatarajiwa kuwa waliokuwa wagombea urais Tanzania mwaka 2015, Dk. Magufuli na Lowassa, watarejea kwenye mchuano, ingawa sasa ni katika siasa za Kenya.

Rais Magufuli akiwa na Raila Odinga

Rais Magufuli na Raila

Uswahiba wa Rais Magufuli na Raila, sio siri. Umekuwepo kwa miaka mingi sasa, ulianza wakati wote wakiwa mawaziri wenye dhamana za ujenzi katika nchi zao.

Uhusiano wa viongozi hao, unaelezwa kuwa umegeuka kuwa “undugu” baina ya familia zao; huku kila familia zikitembeleana.

Mara ya mwisho Raila kumtembelea Rais Magufuli ilikuwa mwaka jana, ambapo alienda kwa helkopta hadi kijijini kwa Rais Magufuli, Chato, Geita na kusherehekea Sikukuu ya Krismas huko.

Raila akiwa jijini Dar es Salaam, aonekana katika mgahawa wa Break Point na mmiliki wa mgahawa huo, Daudi Machumu.

Katika uchaguzi uliopita wa Kenya, Raila akiwa mgombea wa nafasi hiyohiyo, Dkt. Magufuli, wakati huo akiwa waziri kwenye serikali ya Rais Jakaya Kikwete, alikwenda Kenya kusaidia kampeni za Raila Odinga. Hata hivyo, swahiba wake huyo alishindwa na Uhuru.

Akiwa huko, Dk. Magufuli alionekana akiambatana na Raila katika majukwaa ya kuomba kura, tena akiwa amevalia nguo, skafu na kofia za chama cha Raila- Orange Party.

Pamoja na kwamba alishindwa uchaguzi, urafiki wao uliendelea kuimarika na hata Dkt. Magufuli alikuwa mgeni maalum katika msiba wa mtoto wa Raila aitwaye Fidel (akiwa amepewa jina la Rais wa Cuba Fidel Castro). Huyu alifariki mwaka 2015.

Lowassa na Uhuru

Historia ya urafiki wa Rais Uhuru na Lowassa haiko wazi na inaonekana wawili hawa hawajawahi kuwa na ukaribu unaofahamika kwa jamii kama aliokuwa nao Rais Magufuli na Raila.

Hata hivyo zipo taarifa kuwa wanasiasa hao wawili wamekuwa na uhusiano unaodaiwa kuwa wa kibiashara na kwamba umekuwepo kwa muda sasa. Biashara hizo hazijaweza kuwa wazi mpaka sasa, kama zipo.

Edward Lowassa

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya

Hata hivyo, mapema mwezi Mei mwaka huu, Lowassa, ambaye ni waziri mkuu aliyejizulu wa Tanzania, baada ya kudaiwa kuhusishwa na kashfa ya kampuni yenye utata ya kufua umeme ya Richmond ya Marekani, aliieleza dunia kuwa atamsaidia Uhuru ashinde.

Lowassa akiwa anawakaribisha nyumbani kwake Monduli, Arusha, baadhi ya wabunge wa Kenya na viongozi wa chama cha Jubilee, kinachomsimamisha Uhuru kwenye uchaguzi wa mwaka huu, alisema yeye na familia yake wanamuunga mkono Uhuru.

“Mimi naamini Uhuru Kenyatta anao uwezo mkubwa wa kuwaunganisha vyema wananchi wa Kenya na Watanzania. Naahidi  ukifika muda muafaka tutaungana naye kumsaidia katika kampeni zake,” alisema Lowassa.

Tanzania yashutumiwa kuiba kura za Kenyatta

Mmoja wa viongozi wa kambi ya Rais Kenyatta- kupitia Jubilee, Aden Duale, ameishutumu kambi ya Raila, ikiongozwa na muungano wa vyama vya upinzani (NASA) kwamba imejiandaa kuiba kura.

Amedai kuwa wizi huo unapangwa Dar es Salaam, Tanzania, ambapo wataalamu wa mitandao ya kompyuta – wa Tanzania na nchi moja ya Amerika, wanajipanga kutekeleza azma hiyo kwa lengo la kufanya Raila ashinde uchaguzi.

Pamoja na kwamba FikraPevu imeshindwa kuthibitisha juu ya tuhuma hizi, lakini zipo taarifa za kuwepo Dar es Salaam baadhi ya wasaidizi wa Raila.

FikraPevu – wiki iliyopita, Mei 6, ilimuona Raila Odinga akiwa Dar es Salaam na mchana akionekana ndani ya mgawaha wa Break Point, Kinondoni ambako alisema yuko hapo kula samaki wa kuchoma.

Kiongozi huyo wa upinzani aliyewahi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, hakuwa tayari kuzungumza lolote, hasa siasa baada ya kueleza tu; “nimekuja kula samaki.”

Msomi azungumza

Daktari mbobezi katika masuala ya siasa nchini na mhadhiri wa vyuo vikuu, Lenny Kasoga anaeleza kuwa hakuna ubaya wowote kwa Lowassa kutangaza kumuunga mkono mgombea wa urais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

“Sioni tatizo, Lowassa sio waziri mkuu, wala hana dhamana yoyote kubwa katika Tanzania, hivyo ni uamuzi binafsi usioweza kugusa msimamo wan chi,” anaiambia FikraPevu.

Akizungumzia uswahiba wa Rais Magufuli na Raila endapo unaweza kuleta rabsha katika uhusiano wa Tanzania na Kenya, Dkt. Kasoga anaeleza kuwa ikiwa Rais Magufuli atajingaza hadharani- kwamba anamuunga mkono Raila, hiyo inakuwa na tafsiri isiyokubalika kidiplomasia.

Hata hivyo, msomi huyo anabainisha kuwa kama uhusiano wao hautaingilia uchaguzi mkuu, hilo halina shida na urafiki hauna mipaka; iwe wakati wa uchaguzi au baada.

Inachokijua FikraPevu

Tunaamini kuwa katika mazingira yoyote yale, urafiki wa kweli kama ulivyo wa Rais Magufuli na Raila, hauwezi kuvunjwa kwa kuwepo uchaguzi, hivyo inatarajiwa kwamba urafiki huo utaendelea na huenda maswahiba hawa wakasaidiana kwa njia moja au nyingine ili kufanikisha jambo.

Hata kama Rais Magufuli hajatangaza hadharani, hawezi kuacha Raila akahangaika peke yake; kwani “rafiki ni bora kuliko mwanasesere.”

Lowassa naye, pamoja kwamba hajatangaza msaada anaoweza kuutoa kwa Rais Uhuru ili kuhakikisha anashinda; lazima utakuwa ni ushauri wa mbinu za kushinda, hata kama yeye alishindwa na Dkt. Magufuli, lakini ana uwezo mkubwa wa kupanga mikakati ya ushindi.

Je, misaada ya fedha kwa wote wawili inawezekana? Hilo hatuwezi kulijua kwa sasa. Tusubiri.

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Mabadiliko makubwa yaja CCM, January kupata mrithi

"Mwenyekiti atatoa taarifa kwa wajumbe wa CC mchana huu, kabla ya kikao cha Halmashauri ...

Askofu Kakobe: Sina mradi wa kiuchumi, nina utajiri wa rohoni

Askofu Mkuu  wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe ameijibu Mamlaka ya ...

Elimu bure ya Tanzania yatoa changamoto nchini Morocco

Wakati serikali ya Tanzania ikitekeleza sera ya elimu bure kwa shule za msingi na ...