Rais Magufuli anastahili pongezi, na kuungwa mkono

Katika moja ya mambo ambayo huwa najiuliza na nashindwa kupata majibu kuhusu sisi watanzania ni kuwa, kama leo akija mgeni na kutuliza swali, tunataka kiongozi wa aina gani? Inawezekana tukashindwa kujibu swali hilo. Na kama tutajaribu kujibu, basi tunaweza kutoa majibu ya kitoto, ambayo muuliza swali anaweza kuishia kucheka na kutuona wajinga. Nimefikia hatua hii baada ya kujaribu kufuatilia maoni ya watanzania wenzangu kuhusu nchi yetu inavyoendeshwa.

Si muda mrefu sana umepita, tangu kelele na purukushani za uchaguzi mkuu zitawale vichwa na masikio yetu. Kila mahali ilikuwa ni kilio, kilio, kilio. Watanzania tulio wengi tulikuwa tunalalamika kuhusu uholela, ubabaishaji, upigaji dili na vingine kama hivyo ambavyo vilikuwa vimefikia hatua ya kuonekana ndio hali ya kawaida.

Uzuri ni kwamba watawala wenye akili na busara, walisikia kilio hicho na kujua watanzania tunataka nini, na Tanzania inataka nini. Yaani serikali na mtawala anaweza kuondoa hayo. Kwa kabwela kama mimi walau nilipata faraja kuona kuwa, kuna mtu mahali alisikia kilio changu, na alisikia kilio cha Tanzania, na akajitolea kukaa na kufanya kazi ya kutafuta hiyo serikali itakayoondoa kilio changu.

Kinachoonekana kwa wengi sisi makabwela ni kuwa, tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, kumekuwa na kule kujisikia ni mtanzania ambaye utu na heshima yako vimeanza kuonekana. Nina mifano mingi tu ya kutoa ambayo watanzania sasa tunaichukulia kama ni “granted”, lakini kiuhalisia imetokana na kazi.

Ni muda mrefu kulikuwa na malalamiko kuwa ukienda kuomba huduma, iwe ni hospitali, ofisi za serikali, mashirika ya umma na hata ya binafsi, matokeo yalikuwa ni kunyanyaswa, kupuuzwa na kudharauliwa. Lakini leo hata ukienda ukiwa peku na ukiwa na midabwada, unaheshimiwa na kuhudumiwa kama wakubwa. Hii ni u-turn ya karne, ambayo ilikuwa ni stahili ya vigogo tu, lakini leo sisi makabwela tunaonekana watu. Sikitarajia hili kwa muda mfupi namna hii.

Lililokuwa linakera zaidi ni kuwa, tulifika wazo hata sisi wenyewe kusema nchi yetu imekuwa shamba la bibi. Watu wanajipigia “dili” mchana kweupe na kuihujumu serikali bila hofu, na kutamba mitaani na kututukana juu. Tena na kujiita watu ndio wanaume hasa. Maliasili zetu zilikuwa zinawanufaisha wengine na sio kutunufaisha sisi, tukilalamika tulikuwa tunaonekana washamba. Ni juzi tu tumeona kazi iliyofanyika kwenye suala la usafirishaji wa mchanga. Mbali na hilo sasa sasa tunasikia kabisa wezi wanasema Magufuli amebana sama, sio rahisi tena kuwaibia watanzania kama zamani.

Nchi ilikuwa na mwelekeo wa kuwa pepo ya wauza unga na mateja, lakini sasa tunaona walau kuna watu wanafanya kazi ya kupambana na haya. Unga sasa umeanza kuogopwa. Tofauti na zamani kuwa unga ilikuwa ni sifa.

Kuna lingine ambalo sijui kama kweli tunalifuatilia au la. Muundo wa chama unabadilika, chama kinarudi mikononi mwa wananchi, kinarudi kuwa chama cha kuangalia matatizo ya mtanzania toka ngazi ya chini kabisa, na kumhudumia mwananchi. Na sio mwananchi au mwanachama kumhudumia kiongozi wake.

Haya ni machache tu ambayo nayaona na yananigusa moja kwa moja kama mtanzania wa chini, ambayo yananifanya niseme kweli kuna mtu aliyesikia kilio changu, na sasa anakifanya kazi akiniangalia mimi.

Kinachonisikitisha ni kwamba, kauli zinazotoka kwa baadhi ya watanzania wenzangu, zinasikitisha sana. Sauti hizo zimekuwa ni distraction za ajabu sana, ambazo zinawatoa watu kutoka kwenye kushughulikia mambo ya maana, na kuanza kushughulika na distractions. Hili ndio linanifanya niwe na wasiwasi na mtazamo wa baadhi ya watanzania wenzangu. Na najiuliza hivi tunachotaka watanzania ni nini? Lugha tamu za kuwafurahisha watu, wakati nchi yetu inadorora?

Kuwachekea watu wanaoleta distraction, na kukejeli serikali ambayo inaonekana wazi kabisa ina moyo wa dhati kufanya kazi kwa ajili ya Tanzania na watanzania? Sijui kama maswali haya ni magumu sana, au sijui kama neema ya siku mbili ya sisi makabwela japo kuonekana watu, inatufanya tusahau kilio cha muda mrefu.

Kwenye mkutano mkuu wa chama uliofanyika hivi karibuni, Mh Rais John Magufuli alitoa hotuba yenye akili sana. Ni bahati mbaya sana hotuba yake ni kama iligubikwa na kufunikwa na distraction za ajabu zilizokuwa zinaendelea kwenye vyombo vya habari. Mimi binafsi nilipenda sana ile hotuba, ambayo kwa maoni yangu binafsi ilistahili kuwa “state of the union address”, ichambuliwe na kujadiliwa kwa makini, ili na sisi kama watanzania tushiriki kwenye yale yaliyosemwa.

Mbali na mambo ya mageuzi ndani ya chama, Mh Rais alisema tatizo kubwa la Tanzania na mtanzania ni umaskini. Tunaweza kusema mengine yote, na kuweka porojo nyingi au kupiga siasa nyingi, lakini ukweli ambao kila mtanzania anauona ni kwamba, tatizo kubwa la Tanzania ni umaskini. Kama chama, serikali, na viongozi wanatambua, wanataja bila kuogopa kuwa hilo ndio tatizo, basi bila shaka wanajua kazi iko wapi.

Binafsi naona kujipanga kwa dhati kwa chama na serikali, ili kutoa leadership kwa Tanzania ya sasa. Kweli hii nchi bila kazi haiwezi kwenda popote, ni kuongopeana tu. Sioni kama tutakuwa na busara, kama tutawasumbua viongozi wetu kwa mambo ya kitoto, wakati kuna mengi makubwa ya kuhangaika nayo ili tuishi maisha bora na ya staha.  Kuitukana serikali, kumkejeli Rais na serikali yake, na hata kuwatweza viongozi wetu, sidhani kama kunaweza kusaidia kuondoa matatizo yetu.

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Zitto, Mnyika walishangaa Bunge; “Liko ‘out of touch’ na wananchi asema Zitto!

Katika taarifa yake katika mitandao mbalimbali ikiwamo blogu yake, Zitto amesema inasikitisha kwamba Bunge ...

TUCTA: Tutatangaza mgomo nchi nzima kupinga posho za Wabunge

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), limesema lipo tayari kutangaza mgogoro mkubwa na ...

Asilimia 48 ya wananchi wanataka mchakato wa katiba uanze upya

Vuguvugu la kufufua mchakato wa Katiba Mpya limeendelea kujitokeza kwa sura mpya ambapo uchunguzi ...