Ongezeko la wakimbizi Kigoma laongeza changamoto ya huduma za afya

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotoa hifadhi kwa idadi kubwa ya wakimbizi duniani ikiwa nao zaidi ya 300,000.

Ukarimu huo umeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazopokea idadi kubwa ya wakimbizi waliokimbia machafuko katika nchi zao.

Mpaka mwaka 2015, takwimu zinaonyesha kulikuwa na wakimbizi milioni 60 duniani kote ambao ni sawa na ongezeko la milioni 10 wakilinganishwa na waliokuwepo mwaka 2011.

Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, Mali, Afghanstan, Sudan Kusini, Somalia, Ukraine na Syria ndizo nchi zinazoongoza kwa kutoa idadi kubwa ya wananchi waliyoyakimbia mataifa yao.

Pamoja na utekelezaji wa haki hiyo inayotokana na mkataba wa kimataifa, wakimbizi waliopo nchini kama ilivyo kwingineko duniani, wanakabiliwa na huduma hafifu za afya.

Mkoani Kigoma, kuna makambi matatu; Nyarugusu, Mtendeli na Nduta. ambayo yanaelemewa na zaidi ya wakimbizi 117,000 waliokuwepo hadi

Mashirika ya kimataifa, yakiongozwa na Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR) ndiyo yanayowahudumia wakimbizi huku taifa linalowatunza likitakiwa kutoa ardhi pamoja na kuhakikisha ulinzi na usalama wao.

Shirika la Médecins Sans Frontières (MSF) au maarufu kama Madaktari wasio na Mipaka ndilo pekee linalowahudumia wakimbizi hao nchini katika masuala ya afya huku Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) likihakikisha linakidhi mahitaji ya lishe kwa waathririka hao wa mapigano nchini mwao.

Januari pekee, takwimu zinaonyesha wakimbizi 19,000 waliingia nchini kutoka Burundi ikiwa ni idadi kubwa kuwasili ndani ya kipindi kama hicho tangu Mei mwaka 2015.

Kati ya kambi tatu zinazowahifadhi, Nduta pekee hadi Machi ilikuwa na zaidi ya 117,000, mara mbili zaidi ya uwezo wake. Idadi ya wakimbizi katika kambi hiyo inatarajiwa kuongezeka mpaka 150,000 mwishoni mwa Aprili kutoka nchini Burundi.

“Kila siku idadi inaongezeka. Kuna haja ya kufungua kambi nyingine,” anasema David Nash, mkuu wa MSF nchini.

Katika kambi hiyo, MSF ndilo shirika peke linalotoa huduma za afya na kushuhudia wingi wa wagonjwa ukiongezeka kwa zaidi ya mara nne huku malaria ukiwa ndiyo maradhi yanayoongoza hasa kipindi hiki cha masika.

Mbali na kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa, bado kuna changamoto za malazi kutokana na wingi wao jambo linaloongeza uwezekano wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko. Misaada ya kibinadamu nayo inaelezwa kutokidhi mahitaji yaliyopo.

MSF inasema, kwa Januari pekee, wagonjwa 17,000 wa malaria kutoka kambi za Nduta na Nyarugusu walibainika na kutibiwa. Licha ya ugonjwa huo, maambukizi ya mfumo wa hewa, kuhara na magonjwa ya ngozi yanaelezwa kushamiri kwenye kambi hizo.

“Kutokana na uhaba wa malazi uliopo, watu wanalazimika kujisitiri wakiwa wamerundikana hivyo kuhatarisha afya zao. Ingawa misaada inaongezeka lakini hailingani na idadi ya wahitaji,” anasema Nash.

Huduma za uzazi ni haja nyingine ambayo uhitaji wake umeongezeka zaidi ya mara dufu katika kambi ya Nduta. Wanawake waliojifungua wameongezeka pia hasa ndani ya miezi minne iliyopita.

Takwimu zinaonyesha zaidi ya watoto 400 walizaliwa Januari. Watoto wadogo, wajawazito na waliojifungua punde ni makundi yaliyo hatarini dhidi ya zaidi kwenye makambi mengi nchini.

Tangu Mei mwaka juzi, MSF imekuwa ikitoa huduma za afya kwa wakimbizi hasa kambi za Nyarugusu na Nduta. Nyarugusu ina kitengo cha huduma ya kwanza chenye vitanda 40 na kliniki tatu za malaria huku huduma za kisaikolojia zikitolewa pia.

Katika kambi ya Nduta, MSF ina vitanda 120 vya kulaza wagonjwa kwenye vituo vitano vya afya licha ya huduma za kisaikolojia zinazotolewa na taasisi hiyo.

“Kuna hofu, huenda kwa sababu idadi ya watu inazidi kuongezeka na miundombinu iliyopo haitoshi. Upo uwezekano itaelemewa baada ya muda mfupi kutokana kwa jinsi wageni wanavyoendelea kuwasili,” anasema Nash.

Msemaji wa WFP nchini, Max Wohlgemuth anasema shirika lake linahakikisha wakimbizi wote nchini wanapata chakula, ambayo ni haki ya msingi kwa kila binadamu. Kuanzia Aprili mwaka 2015, anasema idadi ya wakimbizi imeongezeka Zaidi ya mara nne na shirika hilo linaendelea kuhamasisha wachangiaji kupata fedha za kutosha kwa chakula cha wakimbizi hao.


“Kasi ya michango haiendani na ongezeko la wakimbizi. Malazi hayatoshi hivyo kusababisha msongamano mkubwa kwenye kambi hizo na kuongeza uwezekano wa kutokea kwa mlipuko wa magonjwa,” Max Wohlgemuth, Msemaji wa WFP Tanzania.


Anasema ili kuimarisha afya, shirika hilo hugawa vyakula vilivyoongezwa virutubisho kwa watoto wenye kati ya miezi sita mpaka 59 kwa lengo la kuwaepsha na udumavu.

Licha ya kundi hilo, anasema WFP inatoa vyakula vyenye virutubisho vya ziada kwa wajawazito, watoto wenye utapiamlo, wanawake wanaonyonyesha na waathirika wa Ukimwi wanaotumia Dawa za Kufubaza Virusi (ARVs) na wagonjwa waliolazwa.

Ipo haja ya wadau kujitokeza zaidi na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wakimbizi hawa ambao hawana namna ya kijtafutia ridhki mahali popote nchini zaidi ya kusubiri wanacholetewa na wafadhili hasa wa kimataifa.

Ili kukabiliana na changamoto kadhaa za kufanikisha mahitaji ya wakimbizi hasa chakula na lishe, mwishoni mwa Januari WFP iliboresha mfumo wa ugawaji na kuchagua kundi la wakimbizi kutoka kambi ya Nyarugusu ambalo lilianza kupokea fedha taslimu badala ya mgao wa chakula kila mwezi.

Katika awamu hiyo ya kwanza, wakimbizi wapatao 10,000 wameanza kupokea fedha taslimu kama sehemu ya mradi wa majaribio wa miezi mitatu unaofadhiliwa na Canada iliyotoa mchango wake wa Dola 500,000 za nchi hiyo ambazo ni sawa zaidi ya Sh770 milioni.

Kwenye utekelezaji wake, WFP itatoa Sh10,000 mara mbili kwa mwezi kwa kila mwanakaya aliye katika mradi wa majaribio. Fedha itatumwa kwa mlengwa kupitia mtandao wa simu za mkononi. Katika kipindi chote cha mradi, wakimbizi wataendelea kupata mgao wa mafuta ya kupikia yalioongezewa virutubisho na mchanganyiko maalumu wa uji na badala ya mahindi, kunde na chumvi wanufaika watapewa fedha taslimu.

Mahitaji ya wakimbizi ni muhimu kwa afya zao kama inavyofanywa kwa wananchi wa kawaida. Ikumbukwe, katikati ya Februari, WFP ilipokea mchango wa Euro9.5 milioni kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU) ambazo ni sehemu ya mradi wenye thamani ya Euro24.5 milioni wa kukabiliana na upungufu wa chakula na lishe kwa watu 40,000 kutoka wilaya za Bahi na Chamwino za Dodoma na, Ikungi na Singida Vijijini za mkoani Singida.

Mpango huo unalenga kukabiliana na udumavu ambao hutokea zaidi kwa watoto. Takwimu zinaonyesha watoto wenye udumavu nchini ni asilimia 34 huku Dodoma ikiongoza kwa kuwa na asilimia 36.5 ikifuatiwa na Singida yenye asilimia 29.2

Akipokea msaada huo, Mwakilishi wa WFP nchini, Michael Dunford alisema: “WFP itasimamia na kuutekeleza mradi huu ili kuboresha lishe ya walengwa hasa siku 1,000 kuanzia kutungwa kwa mimba mpaka anapofikisha miaka miwili. Mradi huu utakuwa wa mfano katika kuboresha afya.”

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Balaa CCM: Basi la wajumbe lapata ajali na kuua dereva

UCHAGUZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), nafasi ya Uenyekiti mkoa wa Mwanza umeingia dosari ...

MV Bukoba ikizama

Ajali ya MV Bukoba tumeshindwa kujifunza!

Ni mfano wa sinema ya kutisha iliyojaa kila aina ya ukatili.Abiria wachache walionusurika katika ...