Ngara: Ukosefu wa maji wasababisha wanafunzi kukosa masomo

WANAFUNZI wa shule za sekondari Wilaya ya Ngara, Kagera wanakosa masomo kwa kuwa “wanapoteza” muda mwingi wakisaka maji kwa ajili  ya matumizi.

Hali hiyo inatokana na kutokuwepo mwa maji maeneo jirani na shule zao. FikraPevu imeshuhudia adha hiyo kwa wanafunzi na walimu wa shule hizo na hapa inaeleza zaidi.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Lukole ambayo inao wanafunzi 507 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, hulazimika kutembea kilomita 10 kwenda na kurudi kuchota maji mtoni.

Wanafunzi wakitoka kuchota maji kisimani.

Maji hayo, pamoja na kupatikana mbali, bado hayako salama kwa matumizi ya binadamu.

Uongozi wa shule wakiri

Mkuu wa shule hiyo, Aaron  Dishon Sekazoya ameiambia FikraPevu kwamba tatizo la maji katika shule hiyo ni kubwa ambapo kwa mwezi zinatumika Sh.720,000 za kukodi gari la mzabuni kuchota maji mtoni  kupikia chakula cha wanafunzi.

Anasema hizo ni fedha nyingi ambazo haziwezi kuwepo kila mwezi, hivyo wanafunzi wenyewe wanaenda kuchota maji kwa ajili ya kupikia, kusafisha madarasa, vyoo, mabweni na huduma zingine zinazohitaji maji.

“Watoto wetu wanapoteza muda wao wa darasani kwa kufuata maji kwa umbali wa zaidi ya kilomita 10, wangepaswa kuwa darasani, lakini hawafanyi hivyo kwa kuwa maji nayo ni muhimu kwa maisha ya shule,” anasema mwalimu huyo.

Wanafunzi hao hutumia muda usiopungua saa sita njiani kila wanapofuata maji.

Sekazoya anaiambia FikraPevu kwamba ukosefu wa maji safi na salama, umekuwa chanzo kikubwa cha kuwepo kwa magonjwa ya matumbo, hali inayoendelea kutshia afya za wanafunzi, walimu na watumishi wengine wa shule.

Shule ya Sekondari Lukole ilianza mwaka 2009 baada ya majengo yanayotumiwa na shule hiyo sasa kuachwa na wakimbizi- raia wa Burundi mwaka 2006 na kukabidhiwa wilaya ya Ngara.

Uongozi wa wilaya hiyo uliamua kuanzisha shule ya sekondari na kuyakabishi majengo kwa ajili ya madarasa na nyumba za walimu.

Wanyama, wanafunzi watumia maji pamoja

FikraPevu imeshuhudia maji wanayofuata huko mtoni, hukutumiwa na wanyama; ng’ombe, mbuzi na kondoo wanaofugwa jirani na mto huo.

Mbali na wanafunzi wa Lukole, pia wanafunzi wa Shule ya Sekondari Baramba, wanakabiliwa na changamoto hiyohiyo ya kukosa muda wa masomo darasani kwa kuwa wanafuata maji.

Shule nyingine yakumbwa

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Baramba, Irene Sara Matovu akizungumza na FikraPevu shuleni hapo alisema shule hiyo inatumia lita 12,000 za maji kila siku kwa ajili ya kupika, kusafisha vyoo na mabweni.

Anasema shule hutumia Sh. 150, 000 kila siku kwa ajili ya kulipa wanaoleta maji shuleni hapo, ambapo kwa mwezi zinatumika Sh.4.5milioni. Shule hiyo ina wanafunzi 600.

Matovu anasema changamoto ya uhaba wa maji  inatokana na  mashine inayosukuma maji ya K9 kuharibika mara kwa mara na kutotengenezwa kwa muda.

Anasema tatizo hilo limeathiri maendeleo ya  taaluma kwa wanafunzi shule wa shule yake kwa kiasi kikubwa.

Halmashauri yazungumzia maji

 

Kibao cha kutunza chanzo cha maji.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Aidan Bahama ameiambia FikraPevu kwamba wanafahamu kuwepo kwa tatizo la maji kwa shule hizo na wananchi wa maeneo hayo.

Anasema halmashauri yake  imeandaa mikakati ya kukarabati mtambo wa kusukuma maji eneo la K9 na kwamba tayari ndani ya bajeti ya mwaka 2017/18, zimeombwa fedha, kiasi cha Sh.40 milioni kwa ajli hiyo.

Bahama anasema katika shule ya wasichana Baramba, ameahidi Sh. 2 milioni kusaidia kulipia gharama za kununua mafuta ya gari la shule ili liweze kuchota maji kwenye Mto Kabaheshi.

“Bajeti yetu  inategemea mapato ya ndani na mahitaji  ya halmashauri kulingana na  changamoto zilizopo mapato yanayopatikana hayatoshelezi, hivyo tunakwama kumaliza kero zote kwa wakati, hili la maji linasumbua sana, ” anasema Bahama.

Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Wilbard Bambara anasema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 halmashauri imeomba serikali kupatiwa Sh.100 milioni kwa ajili ya kukamilisha mradi wa K9 Kijiji cha Kasharazi.

Anasema mradi huo ukikamilika kwa kununua mitambo mipya na kurekebisha baadhi ya miundombinu katika kijiji hicho, shida ya maji itakwisha.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ngara, Vedastus Tibaijuka  amewasilisha Sh. 500, 000 kwa shule ya Baramba zilizotolewa na mkuu wa wilaya hiyo, Luteni Kanali Michael Mtenjele kupunguza baadhi ya changamoto hasa kulipia maji yanayohitajika katika shule hiyo ya serikali.

Mbunge wa Jimbo la Ngara, Alex Ghashaza ameahidi kushughulikia tatizo la maji katika shule za Lukole na Baramba na Kijiji cha Kasharazi, chenye wanakijiji wanaofikia 1,500.

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Udumavu, utapiamlo wawatesa viongozi wa Afrika, wahaha kuokoa maisha ya watoto wanaokufa kila mwaka

Viongozi wa Afrika wamekubaliana kuondoa vikwazo vya lishe vinavyowazuia watoto na jamii kutambua na ...

Girls’ education affected by water availability

We world population – close to 6.6 billion, lives in the driest half of ...

Mtwara: Viongozi wa vijiji watengwa katika usimamizi wa elimu

VIONGOZI wa ngazi za mitaa na vijiji mkoani Mtwara wamedai kutengwa na kutoshirikishwa katika ...