Mtwara: Viongozi wa vijiji watengwa katika usimamizi wa elimu

VIONGOZI wa ngazi za mitaa na vijiji mkoani Mtwara wamedai kutengwa na kutoshirikishwa katika masuala mbalimbali ya elimu, hali inayodaiwa kusababisha ongezeko la utoro na kuporomoka kwa elimu.

Wakizungumza na FikraPevu hivi karibuni, viongozi hao wamesema mara nyingi wamekuwa wakitafutwa hasa pale kunapokuwa na matukio hasi katika jamii, lakini siyo kushirikishwa kabla ya kutokea kwa jambo husika.

Ally Ndumbe ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mbambakofi ambaye anasema anashangazwa na viongozi wa ngazi za juu kuwadharau na kutowashirikisha katika kusimamia elimu ilhali wao ndio wenye watu wanaowaongoza.

Baadhi ya watoto wa darasa la awali na la kwanza mkoani Mtwara wakisomea nje kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Anasema, walimu na viongozi wengine wamekuwa wakikimbilia kuripoti matatizo ya shule na wanafunzi katika ngazi ya wilaya wakati ufumbuzi wake ungeweza kupatikana ndani ya kijiji.

“Mara nyingi nimekuwa nikisikia kwenye vyombo vya habari kuwa matokeo ni mbaya na sababu ikidaiwa ni utoro kwa wanafunzi, lakini watunga sera wametusahau sisi viongozi wa vijiji na mitaa katika kupanga mikakati ya kuboresha elimu, kukiwa na shida ndipo utaona mtendaji wa kijiji au mwenyekiti anatafutwa,” Lidumbe ameiambia FikraPevu na kuongeza:

“Kwa mfano, tatizo la utoro tungeweza kulimaliza kwa kuitisha mkutano wa kijiji na kuongea na wananchi wote kwa ujumla na kukubaliana mikakati ya pamoja kudhibiti hali hiyo… ajabu baada ya matokeo mabaya ndio nasikia sababu ni utoro.”

Naye Hamis Dadi, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, ameiambia FikraPevu kuwa viongozi wa baadhi ya shule katika maeneo yao wamekuwa wakiwatafuta hasa panapotokea ugomvi wazazi na walimu.

“Kofia ya mwenyekiti wa kijiji katika elimu haitambuliki, lakini ukitokea ugomvi wa mwalimu na mzazi ndipo mwenyekiti natafutwa, hakuna uhusiano wa karibu kati ya viongozi wa kijiji na shule.

“Hata watunga sera hawachanganyi walimu na viongozi wa vijiji lakini cha kushangaza wanapotaka kuongea na jamii ndipo mwenyekiti unaambiwa itisha mkutano, tena unaishia kuwa mtu wa kufungua mikutano na kufunga basi,” anasema Dadi.

Anaongeza: “Baadhi ya shule zetu zina mikorosho wanapovuna korosho hawakushirikishi chochote, lakini ikitokea labda zikaibiwa umuhimu wako ndipo unaonekana.”

Dadi anasema kwamba, wakati mwingine wenye mamlaka wanapotoa semina wanawachukua tu wajumbe wa bodi za shule ambao hawana nguvu ya kuwaita wananchi na kuwashirikisha walichozungumza katika semina.

Uwazi

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mtiniko katika Halmamshauri ya Nanyamba mkoani Mtwara.

Amina Ally, mkazi Kijiji cha Mbambakofi iliko Shule ya Sekondari Mtiniko ambayo ni miongoni mwa shule zilizofanya vibaya, anasema hakuwahi kupokea taarifa zozote zinazohusiana na matokeo zaidi ya kusikia kupitia vyombo vya habari.

Ameiambia FikraPevu kwamba, mara nyingi wanakijiji wanapoitwa katika mikutano hujadiliana mambo mbalimbali, lakini siyo elimu.

“Kuna nini kimejificha? Kwanini hatushirikishwi? Hata hayo matokeo mabaya yanayozungumziwa niliyasikia kupitia redioni, lakini uongozi wa shule ulikuwa na nafasi ya kuongea na serikali ya kijiji ukaitwa mkutano wa pamoja tukajadiliana kwa pamoja,” anasema Ally.

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtiniko, Mwalimu Lwitiko Mwakabende, ameeleza kwamba wamekuwa wakishirikiana vyema na jamii katika suala la elimu, hali inayowafanya hata wanakijiji kushiriki katika ujenzi wa nyumba za walimu.

“Uhusiano wetu na jamii uko tu vizuri kama hivi katika ujenzi wa nyumba za walimu walijitolea nguvukazi mpaka tukafanikiwa kuijenga nyumba pamoja na kisima kwa sababu mazingira ya shule kuna tatizo la uhaba wa maji,” anaeleza Mwakabende.

Makamu Mkuu huyo wa shule ameiambia FikraPevu kuwa, wao wamekuwa wakijitahidi kutekeleza wajibu wao kama inavyotakiwa, lakini kuna wakati baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwapa walimu jukumu la kurudisha nidhamu kwa watoto wao hasa wanapowashindwa katika jamii.

“Mwalimu pekee hawezi kumlea mwanafunzi, lakini wakati mwingine wazazi wanakuja kututupia mizigo ya watoto kwamba wanakataa shule hivyo anaomba msaada, inafikia mahali tunashindwa kwa sababu sisi wajibu kuwasimamia wanafunzi wakiwa shuleni,” anasema.

Kuhusu suala hilo, Mwenyekeiti wa Kijiji, Hamisi Dadi, anasema ni vyema walimu wakajipanga katika masuala ya elimu na wao kama jamii wasimamie mienendo ya wanafunzi pindi wanapokuwa uraiani ili kuboresha elimu.

“Kama kila mmoja akitambua wajibu wake, basi elimu itakuwa nzuri, walimu wajipange katika masuala ya elimu na sisi jamii tuelimishe watoto nini umuhimu wa elimu, naamini kama tukishirikiana tutanyanyua elimu,” alisema.

Akasisitiza kwamba, madaraka wanapopanga mambo ya elimu wasiwatenge viongozi ambao ndio wenye nguvu kwa jamii.

 

Uongozi Mtwara wajipanga

Kufuatia kufanya vibaya katika matokeo ya kidato cha pili mwaka 2016 na mtihani wa darasa la saba mwaka 2016, uongozi wa Mkoa wa Mtwara umeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wanaboresha elimu.

FikraPevu inafahamu kwamba, katika matokeo ya mtihani wa kidato cha pili, shule tisa kati ya kumi zilizofanya vibaya kitaifa zilitoka mkoani Mtwara hali iliyozua gumzo ndani na nje ya mkoa.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, aliagiza kurudishwa nyumbani wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika hasa baada ya kuanza kupokea wanafunzi wanaorudishwa kutoka shule za vipaji maalum kwa kutojua kusoma na kuandika.

Dendego ameiambia FikraPevu kuwa, mbali na changamoto zilizopo waliwekeana malengo ya kuhakikisha ufaulu katika mkoa lazima uanzie asilimia 80 kwenda juu, lakini hakuna halmashauri hata moja iliyoweza kufikia au kuvuka lengo.

“Inauma, watoto wetu wanapokelewa katika shule za sekondari wanarudishwa hawajui kusoma, hata hapa kwenye shule zetu za Kata kuna watoto wanapokelewa hata kusoma na kuandika hawajui, tunamtengenezea nani hili bomu?

“Pengine tutalaumiwa tumeshuka sana, lakini tuliamua kujitathmini, huu ufaulu wa halali kwa sasa, wacha jamii ikunyooshee vidole leo lakini kesho ukitoka unatoka kwa uhakika,” anasema Dendego.

 

Kuwavua madaraka walimu

FikraPevu imeelezwa kwamba, matokeo hayo mabaya yalisababisha baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi zipatazo 63 kuvuliwa madaraka pamoja na maofisa elimu kuondolewa katika nafasi zao.

“Tusipowapa watoto elimu hakuna kingine tunachoweza kuwapa, kama hatutasimamia watoto wasome na waendelee na elimu ya sekondari hatutawasaidia, namwagiza Katibu Tawala kuna makundi ambayo lazima tufanye uamuzi mgumu.

“Haiwezekani miaka mitatu mfululizo shule inakuwa ya kwanza kimkoa, lakini leo baada ya kuweka vizuri masuala ya usimamizi inakuwa ya 160. Haiwezekani. Kimetokea nini pale? Lazima Katibu Tawala wakuu wote wale wa shule wavuliwe madaraka, mtoto anapelekwa vipaji maalum hata kuandika jina lake hawezi,” anasema Dendego.

Chakula shuleni

Katika kukabiliana na matokeo mabaya ya mitihani, Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, ambayo ni moja ya halmashauri zilizofanya vibaya, imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo utoaji wa chakula shuleni.

Akizungumza na FikraPevu, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Saidi Msomoka, anasema katika Bajeti ya mwaka 2016/2017 wametenga kiasi cha Shs. 480 milioni kuboresha miundombinu pamoja na kiasi cha Shs. 78 milioni kuwezesha watoto kupata uji shuleni.

“Sababu zinazofanya kufanya vibaya ni hamasa duni kwa wanafunzi pamoja na kukosa chakula shuleni, unakuta mtoto pengine nyumbani hajapata chochote akija shule nako hakuna chakula, lazima atakuwa na mahudhurio hafifu, kwahiyo katika bajeti yetu tumetenga Shs. 78 milioni kwa ajili ya uji,” anasema Msomoka.

Aidha, ameiambia FikraPevu kwamba, wametenga Shs. 10 milioni kukipa nguvu kitengo cha elimu kutokana na kupangiwa bajeti kidogo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbambakofi katika Halmashauri ya Nanyamba, Hamisi Dadi, anasema suala la chakula kwa watoto ni muhimu hivyo watawahamasisha wazazi kuchangia ingawa wengi wao walishajiwekea dhana ya elimu bure.

“Suala la chakula ni muhimu kwa sababu kuna watoto wengine wanatoka katika familia duni, unakuta hajapata hata chai, kwahiyo ni vigumu kumwelewa mwalimu pindi anapokuwa darasani,” anasema Dadi.

Matofali milioni moja kila kijiji

FikraPevu imeelezwa kwamba, Mkoa wa Mtwara unakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa zaidi ya elfu mbili pamoja na nyumba za walimu.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Mkuu wa Mkoa huo, Dendego, anasema ili kila kijiji kinatakiwa kuwa na benki ya matofali yapatayo milioni moja ya kuchoma au matofali 300,000 ya saruji.

Amesema, hayo yanaweza kufanikishwa kwa ushirikiano wa pamoja baina ya wananchi na serikali za vijiji, mitaa na kata katika kuwahamaisha watu kuchangia maendeleo.

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Biharamulo: Wananchi wajiandaa kuandamana kwa Mkuu wa Wilaya kudai shule yao

BAADHI ya wananchi wa Kitongoji na Kijiji cha Busiri, Kata ya Nyakahura wilayani Biharamulo mkoani ...

Serikali inapoteza bilioni 793 za walimu ‘watoro’

 Utafiti wa taasisi ya Twaweza unaeleza serikali inapoteza bilioni 793 kila mwaka  za mishahara ...

Elimu ya MEMKWA kupunguza idadi ya watoto wasiojua kusoma na kuandika

Elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto, lakini kutokana na changamoto mbalimbali wapo ...