Connect with us

Sayansi na Teknolojia

Mitandao ya Kijamii inavyowanyima usingizi viongozi Afrika Mashariki

Published

on

Licha matumizi ya intaneti kuongezeka katika ukanda wa Afrika Mashariki, watumiaji wa mitandao ya kijamii hawatafaidika na huduma hiyo kutokana vikwazo vya kisheria vilivyowekwa na serikali za nchi zao.

Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya mpaka Desemba 2017 imeonesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti imeongezeka kufikia watu milioni 23 ambayo ni sawa na asilimia 45 ya Watanzania wote. Kwa upande wa Uganda matumizi hayo yamefikia asilimia 22.

Hivi karibuni marais wa nchi za Uganda, Yoweri Museveni na Tanzania, John Magufuli wamenukuliwa wakitoa kauli ambazo zinaashiria kuminya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni unaofanywa na watumiaji wa majukwaa na mitandao ya kijamii.

Kwa nyakati tofauti marais hao wawili ambao ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekuwa wakidai kuwa uhuru wa watu umevuka mipaka na kuna haja ya kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuhakikisha usalama wa mataifa yao.

Lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema udhibiti huo wa mitandao ni kuwanyamazisha wananchi ambao wamekuwa na muamko wa kuhoji, kukosoa mwenendo wa viongozi wa serikali ambao wanapaswa kuwajibika kwa wapiga kura kwa kutoa huduma bora za kijamii.

Rais Yoweri Museveni (kushoto)  akiwa na rais John Magufuli (kulia) katika moja ya shughuli za kiserikali jijini Arusha

 

Nini kinaendelea Uganda…

Serikali ya Uganda imesema kuanzia Julai mwaka huu itawatoza kodi ya sh. 200 za Uganda wateja wa kampuni za simu wanaotumia mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Viber, Twitter na Skype ili kukabiliana na ‘umbea’ unaoendelea katika mitandao hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya rais Yoweri Mseveni kuiandikia barua ofisi ya Hazina, Machi, 2018 akielezea jinsi mijadala isiyo na tija kama ‘umbea’ inavyolikosesha taifa lake mapato na muda wa uzalishaji mali.

Ikiwa ni sehemu ya kodi mpya, makampuni ya simu yanayotoa huduma ya vifurushi vya intaneti yatawajibika kuwa na takwimu za wateja wao  wanaotumia intaneti ili kuhakikisha kila mtumiaji analipa  kodi ya ongezeko la thamani.

Waziri wa Fedha wa nchi hiyo, Matia Kasaija tayari ameanza mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Kodi ya mwaka 2014 na mswada umepelekwa bungeni kwa mapitio baada ya kupitishwa na Baraza la Mawaziri.

Akihojiwa na wanahabari, Waziri Kasaija alisema kodi itakayotozwa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii itasaidia kuimarisha usalama wa taifa na kuongeza uzalishaji wa umeme. “Kodi hii itasaidia kuimarisha usalama wa nchi na kuongeza umeme ambao nyinyi watu mtatumia kufurahia zaidi mitandao ya kijamii.”

Kawaida, watumiaji wa mitandao ya kijamii hununua vifurushi vya intaneti kupitia simu lakini bado haijafahamika wazi jinsi serikali itakavyokata kodi hiyo kwa watumiaji hao au namna watakavyoweza kujua watu walioingia kwenye mitandao kama Facebook na Twitter. Kimsingi kila mtu mwenye simu ya mkononi inayotumia intaneti atatozwa kodi.

Mabadiliko hayo yamewashangaza watu wengi hasa watumiaji wa teknolojia ya mawasiliano ikizingatiwa kuwa  upatikanaji wa intaneti nchini humo ni wa asilimia 22 na ziko juhudi mbalimbali za kukuza teknolojia ya mawasiliano.

Wengine wakihitimisha kuwa ni mkakati wa kuwanyamazisha wakosoaji wa rais Museveni ambaye anakusudia kufanya mabadiliko ya sheria ili kumruhusu kugombea tena nafasi ya urais baada ya muda wake wa kukaa madarakani kumalizika.

Siyo mara ya kwanza kwa viongozi wa Uganda kuweka mikakati ya kisheria inayokusudia kudhibiti uhuru wa kujieleza. Februari, 2016 wakati wa uchaguzi mkuus, serikali ilizima mitandao ya Facebook na Twitter sambamba kuzuia huduma za kifedha kwa njia ya mtandao. Baada ya uchaguzi mitandao iliendelea kufanya kazi kama kawaida.

Miezi michache baadaye serikali ilinunu mtambo kubaini maudhui ya picha za ngono (pornography detecting machine) yenye thamani ya Dola za Marekani 88,000 kwa lengo la kulinda maadili na tunu za taifa.

June mwaka jana, Kituo cha Habari cha Uganda kilitangaza kuwa kimeanzisha kitengo maalum cha kupitia wasifu wa watumiaji wa mitandao ya kijamii ili kubaini mabandiko yenye maudhui ya ukosoaji. Mwezi uliofuata wa Julai, gazeti la Daily Monitor liliripoti kuwa serikali imeomba usaidizi kutoka China katika utekelezaji wa mpango kazi wa usalama mtandaoni ambao unalenga kusimamia na kuzuia matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

 

Tanzania nayo haiko nyuma

Hatua inazochukua Uganda hazitofautiani sana na za Tanzania. Tumesikia matamko na kauli mbalimbali za viongozi wa serikali wakilalamikia uhuru wa uliovuka mipaka wa mitandao ya kijamii.

Aprili 21, mwaka huu, rais John Magufuli alijitokeza kwenye runinga wakati akiwaapisha Majaji 10 wa mahakama, ambapo alisema uhuru wa watumiaji wa mitandao kijamii umevuka mipaka na watu wanatumia uhuru huo kupotosha baadhi ya mambo yanayofanywa na serikali yake.

“Kuna ugonjwa tumeupata Tanzania wa kufikiri kila kinachoandikwa kwenye mitandao ni cha ukweli. Sasa sifahamu huu ugonjwa umetoka wapi? Lakini ni kwasababu hii mitandao hatuicontrol (hatuisimamii) sisi, wako huko wenye mitandao yao, wao interest (maslahi) yao ni kutengeneza biashara hawajali madhara mtakayoyapata.” Alinukuliwa rais Magufuli.

Kauli ya rais imekuja wakati kukiwa na mjadala mpana wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali ya mwaka 2017 ambayo inaonyesha kuwa trilioni 1.5 hazijulikani zimetumikaje.

Licha ya rais kukerwa na uhuru wa kujieleza na kutoa maoni ambao unatambulika na katiba ya nchi na mikataba ya kimataifa, Tanzania ilipitisha Sheria ya Maudhui ya Mtandaoni ya Mwaka 2015 ambayo imewatia hatiani baadhi ya watu kwa makosa mbalimbali ikiwemo ‘uchochezi’.

Ili kuipa nguvu sheria hiyo, mapema mwaka huu serikali imepitisha Kanuni Mpya za Maudhui ya Mtandaoni za mwaka 2018 ambapo katika kifungu cha 4 kinawataka wamiliki wa blogu, tovuti, majukwaa, radio na runinga za mtandaoni kujisajili ili wapate leseni za kuendesha shughuli zao.

Waliopewa mamlaka ya kusimamia maudhui ya mtandaoni ambao ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) watakuwa na uwezo wa kuwalazimisha wamiliki wa blogu au tovuti kuondoa maudhui yanayodhaniwa kuwa hayafai ndani ya saa 12 na kama hawajatimiza maagizo hayo wanaweza kulipa fidia isiyopungua milioni tano  au kifungo kisichopungua mwaka mmoja jela.

Akizungumza Septemba 28, 2016 wakati wa uzinduzi wa ndege mbili aina ya Bombadier Q400 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, rais Magufuli alinukuliwa akisema, “Natamani siku moja malaika washuke waizime hii mitandao yote ili baada ya mwaka mzima itakapokuja kufukunga wakute sisi tumeisha tengeneza Tanzania yetu mpya.”

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Biashara/Uchumi

BAJETI YA VIWANDA 2018/2019: Wabunge wampa waziri Mwijage somo la uwekezaji

Published

on

Hatimaye Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewasilisha bajeti ya Sh143.33 bilioni, ikiwa ni ongezeko la Sh21.1 bilioni ikilinganishwa na bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2017/18 yenye vipaumbele 13, huku sakata la kupanda bei ya sukari  na mafuta ya kula likiendelea kuteka mijadala ya wizara hiyo.

Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma, Mwijage alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 43.3 ni za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 100 ni za matumizi ya maendeleo.

Bajeti hiyo ambayo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu imeainisha vipaumbele 13 vya wizara hiyo kwa kushirikiana na taasisi zake ni kutunisha mtaji wa Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF); kuendeleza miradi ya kielelezo ya Mchuchuma na Liganga kwa kulipia fidia, mradi wa magadi Soda Engaruka na Kiwanda cha Matairi Arusha.

Vipaombele vingine ni uendelezaji wa eneo la Viwanda la TAMCO Kibaha, mradi wa kuunganisha matrekta ya URSUS, uendelezaji wa Mitaa na maeneo ya viwanda vya Shirika la Viwanda vidogo vidogo (SIDO);  Kuendeleza Kanda Kuu za Uchumi (Ruvuma, Tanga, Kigoma na Manyoni).

“Pia kuendeleza mradi wa Bagamoyo SEZ & BMSEZ; Kituo cha ughavi Kurasini na Eneo la Viwanda la Kigamboni; Kuendeleza utafiti kwa ajili ya TIRDO (Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania), CAMARTEC (Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini) na TEMDO (Shirika la Uhandisi na Usanifu wa Mitambo); Dodoma Leather and Dodoma SEZ; na ujenzi wa maeneo maalumu ya viwanda,” alisema Mwijage.

Pamoja na vipaumbele hivyo, wizara itaweka msukumo wa pekee katika kuhamasisha ujenzi wa sekta binafsi ya Kitanzania iliyo imara ili iweze kushiriki na kuchangia ipasavyo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

 

Viwanda vilivyopo nchini

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imelieleza Bunge kuwa, kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), hadi Machi mwaka huu, Tanzania ilikuwa na viwanda 53,876 vikiwemo vikubwa 251 sawa na asilimia 0.46.

Waziri wa Wizara hiyo, Charles Mwijage amesema, hadi wakati huo, kulikuwa na viwanda vya kati 173, vidogo 6,957 na vidogo sana 46,495.

Amesema, tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, hadi Machi mwaka huu vimejengwa viwanda vipya 3,306.

 

Dhana ya Kiwanda

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewaeleza wabunge wa Bunge la Tanzania na wananchi maana ya neno kiwanda, kutokana na kuwepo na mkanganyiko wa dhana halisi ya kiwanda.

Kwa mujibu wa Mwijage, kiwanda ni eneo ambalo malighafi huchakatwa kwa muktadha wa uongezaji thamani. Amesema, shughuli yoyote ndogo au kubwa ya kuongeza thamani kwenye malighafi kwa lengo la kutoa bidhaa ni shughuli ya kiwanda.

Amesema, kwa vigezo vya kimataifa, makundi ya viwanda huzingatia ajira, mtaji na mapato lakini kwa Tanzania vigezo vinavyozingatiwa ni kiwango cha mtaji na ajira zinazotokana na shughuli husika za kuongeza thamani.

 Kiwanda ni eneo ambalo malighafi huchakatwa kwa muktadha wa uongezaji thamani

 

Michango ya Wabunge

Waziri Kivuli wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Anthony Komu amesema sera ya viwanda imeipa kisogo miradi ya Liganga na Mchuchuma jambo linaloilazimu Serikali kuagiza chuma nje ya nchi kwa ajili ya ujenzi wa reli na malighafi za viwanda vya nondo nchini.

Akichangia mjadala wa bajeti ya viwanda, biashara na uwekezaji, Komu amesema licha ya miradi hiyo kuanza kuzungumziwa miaka kadhaa iliyopita, serikali imeendelea kupiga danadana kuitekeleza.

Komu ambaye pia ni Mbunge wa Moshi vijijini (Chadema), amesema mwenendo huo unadhihirisha kuwa uwekezaji unaofanywa kwenye sekta ya viwanda hauwezi kuonesha dalili njema iwapo hakutakuwapo na maji ya kutosha.

“Sasa miradi ya gesi asili haijatumika vya kutosha lakini cha ajabu serikali imekimbilia kuwekeza kwenye Stiggler’s Gorge na kuanzisha vita na mataifa mengine duniani, ambayo ni sawa na kuhamisha goli, hapakuwa na ulazima huo hasa ikizingatiwa miradi mikubwa iliyoanzishwa haijatumika ipasavyo wala kutengamaa,” amesema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema wizara ya viwanda inapaswa kuongozwa kidiplomasia na si kama Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Akiwa na maana kuwa waziri wa wizara hiyo anatakiwa kupewa safari za nje ya nchi kutafuta masoko ya bidhaa za viwanda vya ndani.

“Huwezi kuongoza wizara hii kama unaongoza Tamisemi, ni diplomasia,” alisema Zitto.

Kutokana na kauli hiyo, Spika wa bunge Job Ndugai amekiri kuguswa na mchango huo na kusisitiza kuwa ni kweli mawaziri inabidi wasafiri ili kuimarisha mahusiano na nchi za nje katika kukuza uchumi wa viwanda.

“Waziri wa Biashara hawezi kukaa na sisi hapa, lazima ende, tumuombee popote pale kwenye mamlaka lazima asafiri, maana bidhaa zetu tutauza Kongwa, kuna soko huko?

“Waziri wa utalii lazima asafiri ‘apige mawingu’ huko na wengine huko, ndiyo ukweli jamani, sisi wabunge lazima tuwasemee,” amesisitiza Ndugai.

Continue Reading

Sayansi na Teknolojia

Mahakama Kuu yazuia utekelezaji wa kanuni za Maudhui Mtandaoni

Published

on

  • Ni zile zinazowataka wamiliki wa blogu na runinga za mtandaoni kupata leseni toka serikalini
  • Wanaharakati wasema zinakiuka haki za msingi za binadamu

Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara  imetoa  zuio la muda  linalozuia matumizi ya Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni  ampaka kesi  ya msingi iliyofunguliwa na watetezi wa haki za binadamu itakaposikilizwa.

Kimsingi kanuni hizo zilipaswa kuanza kutumika Mei 5 mwaka huu, baadaya ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ilitoa wiki mbili kwa wamiliki wa blogu, majukwaa, redio na runinga za mtandaoni kuwasilisha maombi katika mamlaka hiyo ili kupata leseni ya kuendesha shughuli zao mtandaoni.

Hii inatokea kiwa imebaki siku moja kwa tarehe ya mwisho na iliyowekwa na TCRA kuwasilisha mambi ya leseni, Mahakama Kuu imetoa zuio hilo baada ya taasisi sita kuwasilisha mahakamani maombi ya kuzuia matumizi ya Kanuni hizo April 30, mwaka huu.

Taasisi zilizowasilisha maombi hayo mahakamani ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRD), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jamii Media, Chama Cha Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Katika kesi ya msingi ya mapitio ya kanuni hizo, taasisi tajwa zimewashitaki  Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika maombi ya msingi taasisi hizo zinaiomba Mahakama Kuu kufanya mapitio ya kanuni hizo kwa kigezo kwamba Waziri ametumia nguvu ya kisheria nje ya mamlaka yake ( Ultra vires). Pia kanuni hizo zinakiuka haki ya usawa  katika matumizi ya mitandao ya kijamii bila kuwekewa vikwazo vinavyoathiri kundi fulani la watu.

Maombi hayo pia yamejikita kupitia kanuni hizo kwasababu zinapingana na haki ya kujieleza ( Freedom of exepression) haki ya kusikilizwa( rights to be heard) , na haki ya usiri ( Privacy rights) ambazo zote kwa pamoja zinawahusu moja kwa moja watumiaji wa mitandao ya kijamii.

Baada ya zuio hilo la Mahakama Kuu kanda ya Matwara, imepanga kusikiliza  tena kesi ya msingi Mei, 10 2018.

 

Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni

Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni (Online Content Regulations) zilipitishwa na serikali Februari mwaka huu ili kufanya kazi sambamba na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa kuminya uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.

 Kwa mujibu wa Kanuni hizo ili mtu akubalike kutoa huduma ya blogu, jukwaa, redio na runinga za mtandaoni, muombaji atalazimika kujaza fomu inayoelezea gharama tarajiwa za uwekezaji, idadi ya wakurugenzi na wafanyakazi na wana hisa wa jukwaa/blogu husika . Pia kila mwana hisa anapaswa kuainisha mtaji aliochangia kwenye huduma husika, tarehe ya kuanza kufanya kazi na mipango ya baadaye ya ukuaji wa blogu.

Pia wamiliki wanapaswa kulipa kiasi kisichopungua milioni 2 ili apate leseni, jambo ambalo limepingwa na wadau wa habari nchini wakidai ada hiyo ni kubwa na inalenga kuzuia upatikanaji wa habari kwa wananchi kwasababu wamiliki wengi hawana hicho kiasi.

Licha ya mamlaka husika kutoa kibali au leseni ya kuendesha blogu, pia ina nguvu kisheria kunyang’anya kibali/leseni ikiwa blogu itachapisha maudhui yanayodhaniwa ‘ kusababisha au kuhatarisha amani, kuchochea machafuko au uhalifu’ au ‘yanatishia usalama wa taifa au afya na usalama wa umma’.

                         Watumiaji wa simu janja nao watakasa taarifa

 

Waliopewa mamlaka ya kusimamia maudhui ya mtandaoni ambao ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) watakuwa na uwezo pia wa kuwalazimisha wamiliki wa blogu au tovuti kuondoa maudhui yanayodhaniwa kuwa hayafai ndani ya saa 12 na kama hawajatimiza maagizo hayo wanaweza kulipa fidia isiyopungua milioni tano  au kifungo kisichopungua mwaka mmoja jela.

Tangu zilipopendekezwa mwaka jana, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu ikiwemo Mwanzilishi wa JamiiForums, Maxence Melo walijitokeza na kuhoji baadhi ya vipengele ambavyo vilionekana kukiuka faragha za watu, kuminya uhuru wa wananchi kujieleza na kutoa maoni.

Kanuni hizo zitaithiri JamiiForums kwasababu watumiaji wake watatakiwa kutumia majina halisi na siyo ilivyo sasa ambapo mtu ana uamuzi wa kutumia jina lolote. JamiiForums ilifanya hivyo ili kulinda faragha za watumiaji wake na kuongeza uhuru kujieleza.

Haya yote yanatokea Tanzania, ambako juhudi mbalimbali za kuinua teknolojia ya mawasiliano na habari zinaendelea ili kushindana na nchi jirani za Afrika Mashariki kama Kenya.

“Masharti ya usajili na ada yanaonekana kuwa mzigo mkubwa kwa waanzilishi wa blogu na runinga za mtandaoni, hatimaye itakamwamisha mchakato wa kuinua uhuru wa habari nchini”, alisema, Angela Quintal, Mkurugenzi wa Kamati ya Afrika ya Kuwalinda wanahabari.

Continue Reading

Sayansi na Teknolojia

Jinsi Intaneti inavyofanya kazi kwenye ndege

Published

on

Intaneti iko kila mahali. Inapatikana ofisini, kwenye maduka makubwa, hata vituo vya mabasi utaipata huduma hiyo. Sio tena anasa lakini kiuhalisia ni fahari na haki ya kuzaliwa hasa kwa wakazi wa mijini.

Intaneti inamuwezesha mtumiaji wa simu au kompyuta kuangalia video, kusikiliza na kusuma taarifa akiwa popote na wakati wowote. Lakini umewahi kujiuliza huduma ya intaneti (Wi-Fi) kwenye ndege inapatakanaje na inafanyaje kazi ?

Kimsingi ndege zinatumia intaneti (wireless internet ) ambayo hutolewa na watoa huduma za intaneti (ISP). Huduma hiyo huunganishwa na ndege iliyopo angani na mnara wa simu uliopo ardhini ambao una mawasiliano ya moja kwa moja ya intaneti.

Mnara wa simu unawasiliana na kifaa cha ndege kupitia mawimbi ya radio. Gridi za minara ambazo ziko maeneo mbalimbali hukakikisha ndege iliyopo angani inaunganishwa wakati wote bila kuathiri upatikanaji wa huduma hiyo wakati ikisafiri kutoka eneo moja hadi nyingine.

        Minara ya simu inatuma mawimbi ya redio kwenye ndege kuwezesha intaneti

Wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano ya anga wanaeleza kuwa huduma ya intaneti inafanya kazi kama simu za mkononi ambazo zinategemea minara iliyosimikwa katika maeneo mbalimbali ili kuwezesha mawasiliano na intaneti kwa haraka na rahisi.

Huduma ya intaneti kwenye ndege hutolewa na kampuni kubwa kama Gogo Inc. ambayo inamiliki minara ya simu katika maeneo mbali mbali duniani.

Changamoto ya huduma hiyo ni kwamba hupatikana zaidi kwa ndege zinazoruka ndani ya nchi moja.  Ikiwa ndege itapita eneo ambalo halina minara hiyo kama juu ya bahari, intaneti itakata.

Kwasababu minara haiwezi kuwekwa kila mahali, ndege inapopita, intaneti nayo hutoweka na huimarika zaidi sehemu yenye minara.  Lakini wakati mwingine hali ya hewa inaweza kuathiri mawasiliano ya ndege na minara.

Ku na Ka-band

Mapungufu ya huduma za intaneti yanayotolewa na minara yanaweza kutatuliwa kwa msaada wa setilaiti ambayo huzungukazunguka kwenye uso wa dunia. Setilaiti hizo huwasiliana na ndege kupitia kipande cha mawimbi yajulikanayo kama Ku-band.

Setilaiti inatenda kazi kwa kioo akisi ambacho kinaakisi ishara kutoka kwenye mnara wa simu hadi kwenye ndege. Kinachofanyika ni kwamba Antena hufungwa juu ya ndege ikiwa imefunikwa na kisahani kidogo ili kudaka mawimbi kutoka kwenye setilaiti na kuyaelekeza kwenye kifaa kinachowezesha intaneti ndani ya ndege.

         Picha na Gogo Inc.

Teknolojia hiyo ya setilaiti inaweza kutoa intaneti yenye kasi ya Mbps  30 hadi 40, lakini kwasababu setilaiti huudumia ndege zaidi ya moja kwa wakati mmoja, kasi inaweza kupungua. Lakini pia maeneo yenye bahari yanaathiri upatikanaji wa intaneti japokuwa kasi inabaki ileile wakati ukiperuzi Facebook na Youtube.

Kama utahitaji laivu video italazimika kuhamia kwenye mawimbi ya Ka-band. Teknolojia ya Ka-band inakupa intaneti yenye nguvu ndani ya ndege. Inatumia setilaiti ya ya ViaSat1 ambayo kasi yake ni kubwa kwa Mbps 70 hadi 80 sawa na kasi ambayo mtu anafurahia akiwa anatumia intaneti ya nyumbani au ofisini.

Hata hivyo huduma hii ni ghali, inapatikana tu kwa wenye uwezo wa kuinunua. Hupatikana zaidi kwenye ndege kubwa kama JetBlue, Virgin America na Emirates.

 

Kwanini siyo kila ndege inatoa huduma ya Wi-Fi?

Sababu mojawapo tayari tumeiongelea hapo juu- kwamba huduma hiyo ni ghali. Ndege nyingi hazina huduma ya Ku-band kwasababu antenna inayowekwa juu ya ndege inatatiza au yumbisha mwelekeo.

Wataalamu wa anga wanaeleza kuwa kisahani kinachoshikilia antenna ni kinene na kizito; kwa maana hiyo injini ya ndege inatumia mafuta mengi kuhimili uzito wa ziada. Wamiliki wa ndege watatumia pesa nyingi kuwafurahisha wateja wao watapandisha bei ya tiketi ili kufidia gharama za intaneti.

Bahati nzuri, Wahandisi wanaendelea na mchakato wa kutengeneza antenna nyembamba, nyepesi na yenye gharama ndogo inayoweza kutumia mafuta kidogo.

Ikiwa watafanikiwa, watasaidia kuokoa mafuta na fedha nyingi zinazotumika kutoa huduma hiyo.

Naamini hata kasi ya intaneti itaboreshwa ili wasafiri wa ndege wafurahie ukuaji wa teknolojia kwa kutazama na kuperuzi kwa uhuru mambo wayatakayo wakati wakiwa angani.

Continue Reading

Must Read

Copyright © 2018 FikraPevu.com