Shirika la Global Witness limeeleza kuwa watu 197 waliuawa mwaka uliopita kwa kutetea  matumizi mazuri ya ardhi, wanyama pori na rasilimali asilia.

Shirika la Global Witness likishirikiana na Jarida la The Guardian limeendesha kampeni ya kulinda na kuhifadhi mazingira duniani kote ambapo lilikusanya data za watetezi wa mazingira ambao walinyanyaswa, kutishwa na serikali zao na mashirika na hatimaye kuuawa.

Kuuawa kwa watu wanaotetea ardhi au rasilimali asilia  kulishika kasi mwaka 2017 kuliko wakati mwingine wowote uliopita, ambapo kwa mujibu wa utafiti wa Global Witness unaonesha kuwa watu 4 waliuawa kila wiki duniani kote wakipambana dhidi ya udhalimu unaotokea kwenye machimbo ya madini, mashamba, ujangili na miradi ya miundombinu.

“Hali bado ni tete. Jamii zisipohusishwa kwenye maamuzi ya matumzi ya ardhi na rasilimali asilia, wale wanaotetea wataendelea kuteswa, kufungwa jela na kupokea vitisho vya kuuawa”, amesema Ben Leather,  Kiongozi wa Kampeni kutoka Shirika la Global Witness.

Mauaji mengi yalitokea msituni hasa kwenye nchi zinazoendelea ikiwemo Amerika ya Kusini ambako rasilimali nyingi zina mgogoro na mamlaka za kisheria zinazosimamia mazingira.

Sekta ya madini imetajwa kuwa kichocheo kikubwa cha vurugu na vifo vya watu wanaotetea utunzaji wa mazingira katika maeneo ya migodi. Mapigano ya migodini yalichangia vifo 36 ambavyo vilihusishwa na ongezeko la mahitaji ya vifaa vya ujenzi.

Nchini India, ndugu 3 wa familia ya Yadav: Niranjan, Uday  na Vimlesh waliuawa Mei 2017 walipojaribu kuzuia uchimbaji wa mchanga kwenye kingo za mto uliopo karibu na kijiji cha Jatpura.

Uturuki nako kulishuhudia wanandoa Ali na Aysin Büyüknohutçu, walipigwa risasi wakiwa nyumbani kwao baada ya kupata ushindi wa kisheria uliozuia uchimbaji wa mawe ambayo yalikuwa yakitumika katika ujenzi wa hoteli na sanamu ya manispaa. 

Kilimo cha biashara nacho kinatajwa kuwa kichocheo cha mauaji ya watetezi wa mazingira kwasababu ya ongezeko la mahitaji ya soko la mafuta ya michikichi, miwa, soya na nyama. Mashirika na kampuni zimekuwa zikitoa ruzuku ili kujitwalia ardhi kwa ajili ya kilimo cha mazao na wanyama na kuwalazimisha watu kuondoka katika ardhi yao.

Brazil ambayo iko karibu na misitu ya Amazon iliripoti vifo 46 vya watetezi wa mazingira ambapo watu wanaoishi katika misitu hiyo wako hatarini kutokana na uwepo wa baadhi ya watu wanaotaka kutumia vibaya rasilimali hiyo.

Peru nayo ilishuhudia mauaji ya wakulima sita ambao waliuliwa na kundi la wahalifu ambao walitaka wauziwe ardhi kwa bei ndogo kisha wajipatie faida kubwa kwa kuuza ardhi hiyo kwa wafanyabiashara wa zao la michikichi.  Tukio hilo ambalo lilitokea Septemba mwaka jana lilizua taharuki kwa watetezi wa mazingira wa nchi hiyo.

 

Tanzania nayo yatajwa

Wayne Lotter, Mkurugenzi wa taasisi ya kuhifadhi wanyama pori ambaye amekuwa akipokea vitisho mbalimbali aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mwaka jana.

Mhifadhi huyo wa wanyama pori aliuawa eneo la Masaki jijini Dar es Salaam wakati akitoka uwanja wa ndege wa Julius Nyerere akiwa kwenye gari kuelekea kwenye makazi yake. Watu wawili, mmoja akiwa na silaha alifungua kioo cha gari na kumpiga kwa risasi Lotter ambapo kupoteza maisha.

Lotter alikuwa Mkurugenzi na mwanzilishi wa shirika lisilo la kiserikali la PAMS, linalotoa huduma za uhifadhi na msaada wa kupambana na ujangili kwa jamii na serikali za Afrika. Tangu shirika hilo lianzishwe nchini Tanzania mwaka 2009 alikuwa ameshapokea vitisho vingi vya kuuawa kuhusiana na kazi yake. Baadhi ya watu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kudaiwa kuhusika na mauaji hayo.

Shirika la PAMS lilifadhili na kukisaidia kikosi kazi (NTSCIU) kilichoundwa kupambana na ujangili ambapo katika harakati hizo walifanikiwa kumkamata mfanyabiashara mkubwa wa pembe za ndovu, Yang Feng Glan ambaye anajulikana kama “Queen of Ivory”  na majangili wengine ambao walikuwa wakiendesha shughuli zao kwenye mbuga mbalimbali nchini.

Katika mahojiano yake kabla hajafariki, Lotter alisema anaamini kazi yake ilisaidia kupunguza kiwango cha ujangili kwa asilimia 50.

Takwimu za sensa ya Tembo zinaeleza kuwa idadi ya Tembo barani Afrika imepungua kwa 30% kati ya mwaka 2007 na 2014. Tanzania ilikumbwa na anguko kubwa la idadi ya Tembo ambapo inakadiriwa kuwa wamepungua kwa 80%.

Msemaji maalumu wa Umoja wa Mataifa, John Knox amezitaka serikali zote duniani kuwalinda watetezi wa mazingira na vyombo vya habari kuweka wazi vitendo vya uonevu dhidi ya wanaohifadhi maliasili.

“Inawezekana kufuatilia zaidi visababishi na sababu hatarishi ikiwemo kushindwa kwa serikali kuwalinda hawa watetezi dhidi ya vitisho na vurugu. Nafikiri kuna dalili kwa serikali kuanza kuitikia wito wa kimataifa kwa kesi hizi lakini mambo mengi yanatakiwa kufanyika”, amesema  Knox.

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

WAJIBIKA: Sekta ya manunuzi kinara wa rushwa serikalini, sekta binafsi nchini

Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG)aliyestaafu, Ludovic Utouh amesema  mapambano ya rushwa ...

Wakazi Ileje wasubiri barabara ya Shs. 107.6bil. kuwaunganisha na Malawi

WAKAZI wa Wilaya ya Ileje mkoani Songwe wamesema hawataamini ahadi ya serikali ya kujenga ...

Miundombinu: Unataka kwenda Nyasa, unaweza kuogelea tope?

UNAWEZA ukawa mwendo wa saa 3 na dakika 39 tu kwa gari ndogo kutoka ...