MARY PETRO: Mlemavu anayelala chali kwa miaka 51 sasa!

1_mary

Kwa muda mrefu kumekuwepo na taarifa za ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu; tumesikia walemavu wa ngozi (Albino) kwa namna walivyofanyiwa na wanavyoendelea kufanyiwa ukatili kisa eti Imani za kishirikina. Pamoja na yote uliyosikia lakini hebu fuatilia kisa hiki, ambapo mlemavu asiyejiweza kabisa anavamiwa, anabakwa, anapewa Mimba, mwisho wa siku anajifungua, lakini baada miaka kadhaa mwanaye aliyemzaa akiwa mzima naye ghafla anakuwa mlemavu.

Tangu nchi yetu ipate Uhuru waka 1961 Serikali kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii imekuwa inatoa huduma kwa watu wenye ulemavu bila kuwa na sera timilifu.

Kuwapo kwa Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ni matokeo ya miaka mingi ya majadiliano baina ya Serikali na wadau. Pamoja na kutokuwapo kwa sera, Tanzania imekuwa inajihusisha na mipango mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa inayohusu masuala ya ulemavu.

Kimataifa Tanzania imesaini mikataba mbalimbali kuhusu watu wenye ulemavu hususan mikataba ya Haki kwa watu wenye Ulemavu (1975), Haki za Mtoto (1989) na Haki na Fursa sawa kwa Watu wenye Ulemavu (1993).

Barani Afrika, Tanzania ni miongoni mwa nchi waasisi wa Mpango wa utekelezaji wa muongo wa Watu wenye Ulemavu na mwanachama wa Taasisi ya Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu (African Rehabilitation Institute – ARI).

Hapa nchini serikali imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kampeni za chanjo ya kuzuia ulemavu utotoni (kwa mfano polio), kutunga sheria zinazolinda maslahi na kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu, kuwapo kwa swali kuhusu ulemavu katika sensa ya Taifa ya watu na makazi (2002) na ile ya mwaka jana (2012)  na mandalizi ya kuridhia mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki na Fursa Sawa kwa Watu wenye Ulemavu.

Sera inatoa mwongozo na inaweka vigezo vya utoaji huduma. Sera imejengwa kwa kuzingatia utamaduni wetu na inalenga katika kuleta maendeleo, haki na heshima kwa Watanzania wenye ulemavu.

Changamoto iliyopo ni kutafsiri kwa vitendo matumaini yaliyomo kwenye Sera hiyo na kilichopo tu ni kwamba kundi hili limekuwa likikumbukwa pale tu linapotokea janga au unyanyasaji fulani na baada ya hapo hakuna tena atakayejali na kulitilia maanani,kwani kukosa kwao huduma mbalimbali za jamii, kunawafanya walemavu waathirike kisaikolojia na wengi wao kukata tamaa ya maisha.

Pamoja na jitihada hizo za serikali lakini bado kuna ukweli usiopingika kwamba kuna baadhi ya walemavu ambao serikali haijawafikia mahali walipo, lakini kibaya zaidi hata jamii yenyewe inayowazunguka haijaona umuhimu wa kuwatolea taarifa mahali husika.

Miongoni mwa watu wenye ulemavu ambaye anaonekana wazi kwamba yuko katika hali ngumu huku serikali ikiwa haijui taarifa zake lakini kibaya zaidi jamii nayo ikionekana kumtenga na kutomjali ni Mwanamke Mary Petro (51) mkazi wa kitongoji cha Sima kijiji na kata ya Bupandwa wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.

Mlemavu huyo ambaye hana uwezo wa kutembea,huku akiwa ni mtu mwenye kubebwa na watu wawili wakati wowote anapotaka kufanya jambo lolote ikiwa ni pamoja na kwenda kujisaidia haja kubwa ama ndogo,kula chakula mwenyewe kwa kutumia mikono yake miwili hilo ni jambo ambalo halijawahi kumtokea tangu azaliwe miaka 51 iliyopita.

1_mary

MLEMAVU Mary Petro (51) akiwa katika hali yake anavyokaa  kila siku tangu alivyozaliwa.

Mary ambaye hana uwezo wa kutembea kutokana na miguu yake kulemaa ambapo alizaliwa akiwa na hali hiyo, mikono yake ikiwa imekunjamana huku ikiwa imelalia kifuani mwake, hawezi kulala kifudifudi, wala ubavu yeye ni mtu wa kulala chali na anapowekwa ni hapo hapo hadi atakapokuja kuondolewa ama kusogezwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Hakika maisha anayoishi Mary ni magumu huku akikabiliwa na changamoto ya kukosa ulinzi wamaisha yake mara kwa mara,hali inayopelekea wakati mwingine kushinda njaa kwa kukosa chakula kutokana na waangalizi wake kuwa shuleni ama kwenda kwenye mahemezi!.

Ugumu wa maisha ya Mary yamekuja kutokana na wazazi wake wote wawili (Baba na Mama) ambao anawaelezea kuwa walikuwa walinzi na msaada wake wa karibu katika maisha yake tangu alipozaliwa kufariki Dunia.

Hivi karibuni nikiwa nikiwa Katika safari ya Kikazi Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza katika pitapita zangu kwenye moja ya mitaa ya mji wa Sengerema napita katika moja ya vijiwe ambapo kuna watu wengi wanajadili masuala ya kisiasa na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Hata hivyo katika mjadala huo mmoja wa wadau hao anaingiza hoja nyingine kuhusiana na matatizo yanayowakabili walemavu katika wilaya hiyo na namna ambavyo wamesahaulika si kwa serikali na wanasiasa pekee, bali hata jamii yenyewe inayowazunguka.

Mdau huyo anakwenda mbaali zaidi na kutolea mfano wa Mlemavu Mary anayeishi katika kata ya Bupandwa, namna ambavyo anateseka katika maisha yake ya kila siku,lakini kilichonistua ni taarifa yake kwamba pamoja na mateso hayo alibakwa na kujikuta akipata ujauzito!.

Ni simulizi inayotisha kidogo na kama si mvumilivu huwezi kuisikiliza, maneno ya mdau huyo yananigusa na baada ya kutoka kwenye mada hiyo naamua kumvuta pembeni na kumuomba anielekeze mahali alipo mlemavu huyo, naye bila ajizi ananielekeza vizuri hadi katika kitongoji anachoishi.

Kwa sababu ilikuwa majira ya jioni na kutokana na umbali wa eneo husika naamua kulala na kujipanga kwa safari ya asubuhi ili kwenda kumshuhudia Mlemavu huyo,nadamka asubuhi na mapema na kuanza safari ya kwenda katika kijiji hicho, usafiri ni wa shida ndani ya gari tumebanana kupita kiasi,barabara ni ya vumbi na haina ubora!.

Baada ya safari umbali wa kilomita zipatazo 100 nawasili katika kijiji hicho na kwenda moja kwa moja katika ofisi za kata hiyo,ndani ya ofisi hiyo nawakuta viongozi mbalimbali wa serikali, pamoja na Diwani wa kata hiyo Masumbuko Bupamba.

Najitambulisha mbele yao na kueleza nia yangu ya kutaka kuonana na Mlemavu Mary,viongozi hao kwa pamoja na wakiongozwa na Diwani wanaonekana kupata furaha na kuonesha matumaini makubwa. 

Safari ya kwenda katika kitongoji hicho inaanza ni kitongoji kilichopo pemebezoni kabisa mwa kijiji hicho umbali wa kama kilomita 3 hivi kutoka katikati ya kijiji, lakini kibaya zaidi kiko pembezoni mwa msitu mkubwa wa Buhindi.

Msitu huu ni mkubwa na maarufu kwa uzalishaji wa mbao katika kanda ya ziwa,na nyumba anayoishi melamvu huyu iko mita kama 15 hivi kutoka msituni!.

Nafika Nyumbani anakoishi Mary nakuta amelela chali hawezi kulala ubavu wala kifudifudi,kwa maisha yake yote ya miaka 51 tangu kuzaliwa kwake ni mtu wa kubebwa kuwekwa sehemu moja kwenda nyingine,ni mtu wa kulishwa,kunyweshwa,Kuvishwa,kuogeshwa na kufanyiwa kila kitu kama mtoto mchanga!.

2_mary

Hivi ndivyo Mary anavyobebwa kupelekwa ndani, kujisaidia, ama kutolewa ndani ya nyumba.

Anaonekana mwenye Tabasabu usoni,naanza mazungumzo naye. Katika simulizi ya maisha yake haoni taabu kuwa Mlemavu lakini kinachomsumbua katika akili yake ni kitendo cha ubakaji alichofanyiwa miaka 16 iliyopita, ubakaji uliopelekea kupata ujauzito na kumzaa mtoto wake pekee wa kiume!.

Anasema kutokana na yeye kuwa mlemavu asiyeweza kufanya jambo lolote ikiwa ni pamoja na hata kunawa uso, siku moja akiwa ameachwa nyumbani na wazazi wake akiwa amelazwa chini ya Mwembe mkubwa wenye kivuli ambao mara zote alikuwa akiachwa na wazazi wakati wakiwa shambani, ghafla alivamiwa na mtu ambaye hakumfahamu na wala hajamfahamu hadi leo hii na kumbaka.

Anasema hakuwahi kufanya tendo la Ndoa katika maisha yake isipokuwa siku hiyo ambapo baada ya mtu huyo kumaliza haja yake alitoweka na kwa bahati mbaya sana hakufanikiwa kumfahamu, na hakuweza kuwaeleza wazazi wake waliporejea, na kukaa kimya kutokana na aibu aliyokuwa nayo.

“Lakini kadri siku zilivyokuwa zikisonga mbele nilikuwa nikisikia mabadiliko katika mwili, na mwisho wa siku ikathibitika kwamba nina ujauzito, na hapo ndipo iliponilazimu kuweka mambo hadharani mbele ya wazazi wangu….’’ Anasimulia Mary.

Anaongeza “Lakini baada ya hapo ushauri uliotolewa ni kwamba niutoe ujauzito kutokana na hali halisi niliyonayo, hakuna aliyeamini kama naweza kujifungua salama, jambo ambalo nililipinga kwa nguvu zangu zote…’’.

“Nilikataa kwa sababu kwanza mimi ni mlemavu ambaye sikuwa na ndoto za kuolewa na hatimaye kuwa na mtoto, lakini jambo kama hilo limenitokea nikasema hapana, ni afadhali nimzae huyo mtoto kuliko kuutoa ujauzito pamoja na kwamba najua sina uwezo wa kumlea ipo siku nitapata wasamaria wema watamlea nashukuru Mungu kwamba mambo yalikwenda vizuri nikajifungua salama tena nyumbani wala si hospitalini……’’anasema.

Anaeleza kuwa baada ya kujifungua wazazi wake waliamua kumlea mtoto huyo ambapo wakati wa kumnyonyesha walikuwa wakimshikilia mtoto na kumpatia titi ili anyonye kwa sababu yeye mikono yake haiwezi kufanya kazi yoyote, na mtoto huyo aliishi kwa amani na upendo kutoka kwa Babu na Bibi yake na hadi sasa yuko hai na anaendelea na maisha ingawa katika hali ngumu.

“Mwanangu yupo hai ingawa yuko katika maisha ya shida, kama unavyoniona mimi ni mlemavu ambaye sijiwezi hata kidogo, nilimzaa akiwa mzima kabisa lakini na yeye kwa sasa  ni mlemavu….’’.

Anasema “Ulemavu huu ameupatia ukubwani katika mazingira ya kutatanisha sana akiwa darasa la Tatu, hakuna namna naishi lakini najua na natambua wazi kwamba wakati wowote mimi nitakuwa marehemu….’’ Anasema Mary huku machozi yakimdondoka.

Anasema tangu alipojifungua hadi sasa hajawahi kumshika mtoto wake kwa mikono yake, na anaamini hataweza kufanya hivyo hadi kifo chake kutokana na ulemavu alionao.

Anasimulia kwamba Baba na Mama yake waliokuwa waangalizi wake wa karibu tangu kuzaliwa kwake wote ni marehemu, mtu pekee aliyekuwa amebaki kama tegemeo lake la kila siku ni dada yake ambaye amefariki Dunia Mwezi tano mwaka jana.

“Ndiyo maana nasema hapa nilipo nasubiri na mimi kuaga Dunia ili nipumzike kwa amani… Siwezi kujiua kwa sababu najua ni dhambi, lakini najua kwa shida na mahangaiko niliyo nayo Mungu atanihurumia ili nizikwe nipumzike’’anaeleza.

Ulemavu ni hali inayotokana na dosari ya kimwili au ya kiakili ya muda mfupi au ya kudumu ambayo inampunguzia mtu uwezo na fursa sawa katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika jamii. Upungufu huo unaweza kuchochewa na mazingira na mtizamo wa jamii kuhusu ulemavu.

Katika jamii yetu na kwingineko duniani hali ya mtu kuwa na ulemavu inaambatana na unyanyapaa unaotokana na mila zilizopitwa na wakati.

Kwa mfano, katika Mkoa wa Geita watoto watatu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) wamelazimika kukimbia makazi yao na kwenda kuishi Umahimishoni huko Jijini Dar es Salaam kwa hofu ya kuuawa.

Wa kwanza kukimbia makazi yao ni watoto wawili wa familia moja Bibiana Mbushi na mdogo wake Tindi Mbushi, Bibiana alinyofolewa mguu wa kulia kuanzia kwenye goti na watu wasiofahamika na kutoweka nao wakati wa wimbi la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Bibiana alikaa hospitalini kwa miezi sita na baada ya kupona aligoma kurejea nyumba kwa hofu ya kuuawa, ambapo baadaye yeye na mdogo wake walichukuliwa na Mbunge wa viti maalum anayewakilisha kundi la walemavu Al Shaymaa Kweigr ambaye anaishi nao hadi sasa.

Mwingine ni Adam Robert (14) ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la Nne naye aligoma kutoka hospitalini kwa ajili ya kurejea nyumbani kwao mwaka juzi 2011 kwa hofu ya kuuawa, baada ya kupona jeraha la mkono aliokatwa na kunyofolewa vidole vitatu.

3_mary

MMOJA wa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) mtoto Adam Robert (14) mkazi wa Nyang’hwale wilayani Geita ambaye amelazimika kukimbia makazi yake na kwenda kuishi uhamishoni Dar s Salaam kwa hofu ya kuuawa, hapa ni wakati amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Geita akiuguza majeraha aliyoyapata baada ya kushambuliwa na watu waliomnyofoa vidole vitatu vya mkono na kutaka kumnyofoa mkono wake wa Kushoto.

Kutokana na hali hii watu wenye ulemavu wanaonekana kuwa hawathminiwi na ni tegemezi wasio na uwezo na wanaostahili kusaidiwa na watu wasio na ulemavu katika kumudu maisha yao.

Mtizamo huu unasababisha kutengwa kwa watu wenye ulemavu katika maisha ya kila siku ya jamii inayowazunguka.ni mtizamo hasi na unakwenda kinyume na haki za kimsingi za binadamu.

Kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza kwamba binadamu wote ni sawa na kwamba wanastahili kupata haki sawa bila kujali rangi, kabila, jinsi na dini, lakini kwa mlemavu Mary hilo halipo tena,jamii inayomzunguka inaonekana kumtenga, hana msaada!.

Kibaya zaidi kwa upande wake Mary anaonekana yuko katika ukoo wa ‘Wachawi’ kutokana na hali halisi ya ulemavu alionao, lakini pia tukio lililomkuta la kujifungua mtoto mzima asiyekuwa na kasoro yoyote mwilini lakini anapokuwa mkubwa na kuanza shule ghafla anakuwa mlemavu wa kutembelea mikono na kujivuta.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Faustine Lubinza anasema katika kijiji hicho idadi ya walemavu ni kubwa, lakini wote wenye ulemavu wanaaminika kwamba wanasababishiwa na masuala ya kishirikina!.

Umoja wa Mataifa katika kikao chake cha tarehe 20 Disemba 1948 ulipitisha Azimio Na. 27 (a) (III) ambalo linaeleza kwamba binadamu wote wamezaliwa huru wakiwa sawa katika haki na kustahili heshima.

Kwa kadri ya Azimio hili binadamu ana haki ambazo anastahili kuzipata toka kwa jamii na pia ana wajibu kwa jamii. Haki hizo ni za kuitumia jamii, na rasilimali zake kwa ajili ya maendeleo na usalama wake. Kwa kuwa mtu mwenye ulemavu ni binadamu naye ana haki hizo pia.

Licha ya Azimio hili Umoja wa Mataifa umepitisha maazimio kadhaa kuhusu haki na usawa wa fursa kwa watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali.

Kwake Mary, anasema kwa miaka yote ambayo amekuwa na kujikuta akiwa kijijini hapo, hajawahi kupata msaada wowote kutoka kwa majirani na hata kwa uongozi wa serikali ya kijiji, kata na hata wilaya, bali amekuwa akimuona Diwani mara moja moja ambaye mara kadhaa amekuwa akienda kumjulia hali.

Hata hivyo anasema hali hiyo imemfanya ajione mtu aliyetengwa na wa kipekee asiyependwa na jamii inayomzunguka, na hata viongozi wake kutomjali kwani pamoja na misaada mbalimbali inayoletwa kijijini kama vile mgao wa Neti za mbu amekuwa hapati.

“Najiona kama si binadamu mimi, najisikia vibaya sana ninaposikia kuna watu wanapata misaada, hapa kwetu hakuna TV ya kuangalia matukio mbalimbali ya kidunia, wala hakuna redio, isipokuwa tu huwa naambiwa na hawa walezi wangu kwamba mara kuna walemavu wa mahali Fulani wamepata msaada wa chakula, nguo na vitu vingine vingi tu, mbona huku hawafiki…?!’’ anasema na kuhoji.

Viongozi wa kata hiyo akiwemo Diwani wa Kata wanasema wamekuwa wakijitahidi kutoa misaada pale wanapoweza lakini bado hali imekuwa ikizidi kuwa mbaya kwa familia hiyo na mlemavu huyo, na kwamba familia imekuwa ikishindwa hata kufanya shughuli za uzalishaji mali na hasa kilimo kutokana na kutumia muda mwingi katika kumuangalia mlemavu huyo.

Uongozi wa serikali wilaya hauna Taarifa juu ya kuwepo kwa mlemavu huyo ambaye anaonekana kuwa katika maisha hatarishi na hasa ikizingatiwa kwamba alikwishawahi kufanyiwa kitendo cha kinyama cha Ubakaji na mtu asiyemfahamu, ni miaka mingi ndiyo lakini unyama aliotendewa hauwezi kusahaulika kwake.

4_mary

Huyu ndiye Mary Petro Mlemavu asiyejiweza ambaye anaishi huku akiwa amekata tama,anachosubiri ni kifo ili akapumzike.

Katibu Tawala wa wilaya hiyo Joseph Mfangavo ameahidi ofisi yake kumfuatilia mlemavu huyo na kuona namna ya kumsaidia.

”Ndio kwanza nasikia jambo hili kutoka kwako, sikuwahi kusikia kitu kama hiki kwamba kipo wilayani kwetu…’’.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala huyo kwa sasa wilaya ya Sengerema iko katika mchakato wa kufahamu idadi ya walemavu wote walioko katika wilaya hiyo, na kila mlemavu na aina ya ulemavu wake, kazi ambayo inatarajiwa kufanywa na Idara ya Maendeleo ya jamii wilayani humo.

Tanzania inakadiriwa kuwa na zaidi ya walemavu milioni 4 wenye ulemavu wa aina mbalimbali,na hii inakuja kutokana na Sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka jana, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani kila kundi la watu ama Taifa Fulani asilimia 10 ya watu wake wana ulemavu wa mwili na akili.

Kabla ya sensa ya mwaka jana sensa ya mwaka 2002 hadi kufikia mwaka 2010 Tanzania ilikuwa na watu wenye ulemavu walikuwa milioni 3.4 kutoka na idadi ya watu milioni 34.4, wakiwa na ulemavu wa aina mbalimbali.

Matokeo ya awali ya Sensa iliyofanyika mwaka juzi inaonesha kwamba Tanzania imefikisha idadi ya watu Milioni 44,926,000,ambapo kwa mujibu wa makadirio ya shirika la afya Duniani ya asilimia 10% ya kila jamii kuwa walemavu, sasa Tanzania inaelezwa kuwa na watu wenye ulemavu Milioni 4.49.

Watu wenye ulemavu wa viungo walikuwa 967,932,Wasioona 933,363, wasiosikia 691,380, Ulemavu wa kiakili 276,552, wenye ulemavu mchanganyiko 138,276, Ulemavu wa aina nyingine (Usiojulikana) 449,397 hizi ni takwimu za hadi mwaka 2010. 

FUATILIA SEHEMU YA PILI YA MAKALA HAYA ILI KUJUA NAMNA AMBAVYO MTOTO WA MARY ALIYEMZAA AKIWA MZIMA WA AFYA LAKINI ALIPOFIKA DARASA LA TATU AKABADILIKA GHAFLA NA KUWA MLEMAVU AMBAYE KWA SASA ANATEMBELEA MIKONO NA KUJIVUTA, MAISHA YAKE KWA UJUMLA YALIVYO ,LAKINI UWEZO WAKE DARASANI!!

Kwa maoni, Ushauri kwa ajili ya Mlemavu Mary Petro, ama kujua namna anavyopatikana;

Piga simu 0782-841114 au tuma EMAIL kwenda azariadavid212@gmail.com

 • David Azaria

  Mwandishi wa FikraPevu - Kanda ya Ziwa | Contacts: Email - azariadavid212@gmail.com Mobile: +255 754 841 172/782 841 114

 • Show Comments (9)

 • Shaban nyangassa

  Na ahidi kumsaidia mlemavu huyo kiac cha m1, kwa kweli 2kio hilo limenigusa mno!

  • alex

   kama serikali ya wilaya haina taarifa za watu wake, mfano huyo mama kwa muda wa miaka 51 hiyo serikali inafanya nini? kwa aina hii ya viongozi bado tuna safari ngumu sana tena sana ndugu zangu

  • kuseka

   aiseee nimeumia sana leo, sasa sijui anamawasiliano gani kwa ajiri ya msaada zaidi. inaumaa

  • Padre Gido Nicholas, cmf

   kwanza kabisa nimeamini kuwa wapo wengi kama dada Mary Petro wasiotendewa haki na wanaonyanyaswa. Kitendo alichofanyiwa Mary ni cha kinyama ndio maana anasimulia analia. Ubinadamu umepotea kabisa. Naumia zaidi kwa maneno yake ya kutoa ile mimba na kuamini kuwa ni dhambi. imenigusa sana. Sina cha kumpa kama ndugu yangu Shaban Nyangasa ila naahidi kumwombea katika sala zangu na ibada nitakazoadhimisha. Mwenyezi Mungu ampe maisha yenye amani na upendo na nguvu ya uvumilivu alionao huyu dada. nitamtembelea nami siku moja nikifika Sengerema Geita, naamini kwa msaada wa Mungu nitafika. Asante sana David Azaria kwa jitihada zako za kuguswa na maisha ya walemavu na haswa wale waliosahaulika. Mungu akubariki sana.

 • Fredrick Mashauri

  Miaka 51 ya mateso kiasi hicho kwakweli yanaumiza sana. Hebu watanzania tuachane na imani za kishirikina yanapotokea maswala kama haya yanayoigusa jamii. Swala la ulemavu halihusiani kabisa na maswala ya uchawi. Tukumbuke kabla hujafa hujaumbika, yeyote anaweza akawa mlemavu wakati wowote. Tubadilike

 • majidi namgumi

  pole sana ndugu.

 • cyprian

  jaman mbona dunia tunaiharibu kias hiki, huyo mlemavu kakosa nin had anafanyiwa hivo? mbona tunajitafutia laana ambazo si nzuri ktk maisha.eeeee mungu ulie juu mbinguni nakuomba mnyoshee mkono wako huyu mlemavu.

 • alikiongwe

  Hawa wabunge wapite vijijini kujua matatizo ya watu kama hawa ina onesha siye huyutu alieonekana, na waja wahuruma na kuktangaza kunawengi wameficha na wana teseka bila ya kupata msada, wabunge na madiwani na viongozi wa serekali za mitaa ndio wajibu wao kujua wanaongoza watu wangapi? ndani ya vijji na majimbo ilkuja walemavu wangapi na wanao jiweza wangapi

 • lcs

  Pole sana dada Mary Mungu ana mpango mzuri tu na wewe ndio maana hili sasa limewekwa wazi na dunia yote imefahamu tatizo lako.

  Tanzania tangu ipate Uhuru ni karibu miaka 53 na kulingana na takwimu za walemavu zilizoonyeshwa hapo juu inaelekea kuwa asilimia 10 ya watanzania wote ni walemavu

  Lakini kama alivyosema mwandishi kuna ulemavu wa aina tofauti ,wengine wanaweza kujihudumia hata kwa kiasi

  .Lakini ulemavu wako unatia huruma sana lakini nina hakika Mungu atakwenda kukuponya na usianze kuwaza kifo kwani vyote ni kwa utukufu wake.

  Nchi yetu sasa imefika mahali pa  kuwa na mipango madhubuti kuhusu ulemavu kama huu kwani ukiangalia waliokuwa wanampa msaada sasa hawapo baba mama ndugu wote wamekufa.

  Mipango ambayo serikali inatakiwa kufanya ni kujenga vituo aidha kila wilaya au mkoa kwa wale walemavu ambao kabisa hawajiwezi kama Mary vituo hivi vinajulikana kama Nursing homes na kuwepo na wahudumu , ma nes na vyakula na hata misaada inaelekezwa hapo.

  Kwa kujenga vituo hivyo haya yote ya ubakaji yasingemkuta dada Mary na serikali kupitia misaada ya watu wangeweza kumhudumia vizuri dada yetu.

  Natoa wito kwa makanisa na wadau wenye mapenzi mema kuliangalia hilo kwani kila wilaya ikiwa na Nusing Home yenye vitanda 100 inatosha kwa kuanzia na wale walio ughaibuni watachangia maendeleo ya nursing homes hizo aidha kwa kutuma vitanda mashuka , nguo nk

  Aidha kwa vile bunge la katiba lipo katika vikao basi hata hili la Nursing homse liwemo kwenye katiba kwa ajili ya raia wetu wenye ulemavu au wazee wasiokuwa na ndugu

  Mungu ibariki Tanzana na watu wake

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

 • name *

 • email *

 • website *

ads

You May Also Like

Polisi feki na RPC

Matapeli watumia sare za Jeshi la Polisi kujineemesha huko Iringa

JESHI la Polisi mkoani Iringa, linawashikilia matapeli wawili waliokuwa wanatapeli wananchi katika mkoa huo ...

breakingnews

Dhamana kwa watuhumiwa si mwisho wa kesi-Polisi

ZANZIBAR JUMATANO APRILI 11, 2012 Jeshi la Polisi limewataka wananchi kutovunjika moyo na kuacha ...