Mambo ya kuzingatia kukabiliana na ‘TRAUMA’

Makala iliyopita tuliongelea dhana ya Trauma na dalili zake, leo tena tunaendelea kuangalia hali halisi ya trauma, athari na jinsi ya kukabiliana nayo.

Kimsingi tatizo hili ni kubwa na hutokea katika maeneo mbalimbali hata katika nchi zilizopiga hatua ya maendeleo. Mambo mabaya yanatokea kila siku na watu wanayaona. Trauma ni suala ambalo linamzunguka kila mtu katika mazingira yake lakini linatofautiana kutoka kwa mtu mmoja mpaka kwa mwingine.

Kwa Tanzania, vitendo vya ukatili vya mauaji ya wazee na watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), ni miongoni mwa matukio yanayochochea kuongezeka kwa tatizo hili kwasababu linatengeneza mazingira ya hofu kwa wananchi.

Mazingira yasio rafiki huwa ni kichocheo cha trauma.  Maisha ya wazee na watu wenye ulemavu wa ngozi  yako mashakani. Usalama wao ni suala mtambuka kwasababu wanaishi katika hofu na mashaka na wakati mwingine kushindwa kufikia ndoto zao.

Baadhi ya wataalamu wanasema mtu anaweza kuzaliwa na trauma ikiwa mama mjamzito anapitia vipindi vigumu vya ukatili. Hali hiyo humtengenezea mtoto aliyepo tumboni kupatwa na hali hiyo akizaliwa kwasababu anabeba vinasaba (DNA) vyenye hisia za hofu na mashaka.

Meneja wa Usimamizi na Ufuatiliaji wa Miradi wa Chama Cha Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA), John Ambrose ambaye ni Mshauri wa Saikolojia anasema mila na desturi, mtazamo wa jamii una nafasi kubwa kuendeleza trauma kwa  watu.

Anaeleza kuwa trauma inaweza kumpata mtu mwenye matarajio makubwa kuzidi uwezo alionao. Mfano mtu anawaza kuwa na ndege, magari na nyumba za kifahari, na anajua hawezi kuvipata kwasababu ni nadharia/mawazo ambayo hayapo.

Kunia makuu na kutaka kuwafurahisha watu kwa ahadi zisizotekelezeka kunaweza kumuweka mtu katika hatari ya kupata jeraha la kisaikolojia kwasababu tu ameshindwa kufikia matarajio aliyojiwekea.

Trauma inatajwa kujitokeza zaidi kwa wanawake na watoto ambao wanapitia matendo ya ukatili wa kijinsia yanayotokea katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla.

Watoto wako katika hatari ya kupata trauma kama hawatalindwa

Athari za Trauma

Zipo athari nyingi ambazo zinaweza kumpata mtu mwenye trauma ikiwa hajapata tiba kwa wakati. Zifuatazo ni athari zinazoweza kumpata:

 • Kupata ugonjwa wa akili

Ikiwa kidonda cha kisaikolojia kikikaa kwa mtu muda mrefu bila kupata matibabu, anaingia katika hatua ya mwisho ya kukabiliwa na ugonjwa wa akili (Mental Disorder). Akili inavurugika kwasababu ya matatizo mengi yaliyopo kwenye ubongo kutopatiwa ufumbuzi.

Si ajabu kuona idadi ya watu wenye magonjwa ya akili inaongezeka katika maeneo mabalimbali duniani.  Tafiti za Shirika la Afya Duniania (WHO) zinaeleza kuwa asilimia 20 sawa na watoto 2 kati ya 10 wana matatizo ya akili na sababu kubwa kuwa wamepitia katika matukio mabaya ambayo yamewatengenezea trauma.

 • Magonjwa ya moyo

Kutokana na mtu kupata mshtuko na mashaka kwa kuona matukio mabaya mara kwa mara husababisha mapigo ya moyo kwenda kasi isivyo kawaida. Hali hii ikiendelea kwa muda mrefu tatizo la moyo huwa kubwa na mtu anaweza kupata kiharusi na kupoteza maisha.

 • Kupoteza maisha (kifo)

Ikiwa trauma haijapata tiba mapema hutengeneza tatizo lingine la ugonjwa wa akili (kichaa) na likiendelea bila hatua stahiki kumnusuru mgonjwa anaweza kupoteza maisha.

Hatari aliyonayo mtu mwenye Trauma

Licha ya mtu mwenye trauma kupata matatizo ya kiafya yaliyotajwa hapo juu lakini mfumo mzima wa maisha yake huaribika kwasababu akili imevamiwa na anakosa uwezo wa kufanya maamuzi juu ya maisha yake mwenyewe.

Mshauri wa Saikolojia, John Ambrose anasema trauma haimdhuru mtu kiafya pekee lakini inaenda mbali na kuathiri mfumo mzima wa maisha.  

Anaeleza kuwa mtu mwenye trauma yuko katika hatari ya kupoteza mambo 5 yafuatayo:

 1. Tumaini (Hope)

Kila mtu ana matumaini ya kupata jambo fulani katika maisha yake. Trauma ikitokea humjengea mtu hofu na kumuondolea matumaini aliyonayo katika maisha yake. Inaelezwa kuwa kila siku binadamu anatengeneza mawazo 50,000 ambayo ni matokeo ya taarifa mbaya tunazosikia na kusoma. Mawazo hayo yasipofutwa hutengeneza msongo wa mawazo na kuondoa tumaini la kuishi.

 1. Dira

Mwelekeo sahihi humfanya mtu kufika mahali sahihi, lakini ni tofauti kwa mtu mwenye trauma ambaye anakosa njia sahihi ya kufika kwenye matarajio yake.  Hisia za hofu, mashaka na uoga humzuia mtu kuwa na dira sahihi.

 1. Ndoto

Ndoto ni picha ambazo mtu hutengeneza katika akili yake na sio kitu halisi lakini kinaweza kutekelezeka kama kitawekwa katika matendo. Mtu mwenye trauma ni vigumu kutengeneza ndoto nzuri na akatamani kuifikia. Wakati wote anawaza mabaya yaliyotokea au aliyoaona.

 1. Imani

Kutokuwaamini watu wanaomzunguka na hutafuta kujitenga akihofia usalama wake. Mfano watu wenye ulemavu wa ngozi katika nchi yetu wanalazimika kuishi kwa mashaka na tahadhari kwa kuhofia kuuwawa.

 1. Thamani

Thamani ya mtu ni pamoja na kuthaminiwa na kupendwa na watu wa karibu. Trauma humfanya mtu kuona athaminiwi na kupata heshima anayostahili, akitafakari mabaya aliyofanyiwa katika maisha yake.

Mtu mwenye trauma hopoteza thamani, dira, matumaini na imani 

 

Jinsi ya Kukabiliana na Trauma

Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Zainabu Rashidi anasema matibabu ya kisaikolojia kwa mtu aliyepata trauma yanachukua muda mrefu mpaka mtu arejee katika hali ya kawaida.

Njia  zifuatazo zitakusaidia kukabiliana na trauma katika hatua za awali kabla hali haijawa mbaya:

1. Kukubali kuwa tatizo limetokea.

Mtaalamu wa Saikolojia anasema hatua ya kwanza kwa mtu aliyepata trauma ni kukubali kuwa ana kidonda cha kisaikolojia. Watu wengine wana matatizo lakini hawataki kukubali kuwa wana matatizo, katika hali ya namna hiyo mtu huyo hawezi kupata tiba.

“Kubali kuwa wewe una trauma, sisi wenyewe tunaweza kujichunguza. Mwingine hajikubali, ukijikubali utapata dawa sahihi” anashauri.

2. Hatua ya pili ni kujitathmini hali uliyonayo kwa wakati huo.

Angalia mazingira yanayokuzunguka kama yako salama. Usiruhusu matukio yaliyopita kuharibu siku yako kwa kuwekeza muda mwingi kufikiri jambo lililotokea na ambalo haliwezi kutokea tena.

Tengeneza sentensi inayofunga mjadala wa taarifa au tukio lililopita ili uendelee kufanya mambo mengine kwasababu matatizo yapo na yataendelea kutokea. Jipe moyo na yaone matatizo kama changamoto za kawaida ambazo zinapita.

“Jitathmini mwenyewe, uko wapi? Unafanya nini? Tukio limetokea muda uliopita na halitatokea” anasisitiza Zainabu Rashidi kwa mtu aliyepatwa na trauma muda mfupi baada ya kuona tukio baya.

3. Ongea na mtu unayemwamini.

Hatua ya tatu ni kujenga mazoea ya kuwashirikisha matatizo yako watu unaowaamini ili wakusaidie kutafuta njia mbadala ya kuepukana na trauma. 

“Unapoona kumbukumbu ya tukio lililopita inakuja ongea na mtu unayemwamini. Tunapoongea tunapunguza baadhi ya vitu Fulani katika akili” anaeleeza.

4. Lala kwa muda muafaka.

Dalili ya mtu mwenye trauma ni kukosa usingizi, mtaalamu wa Saikolojia anaushauri kupanga muda sahihi wa kulala kila siku mfano  saa 4 usiku unaacha kila kitu na kupanda kitandani. Lakini wakati wa kulala usiruhusu akili yako kufikiri mambo mabaya yaliyopita maana yatazuia usingizi.

5. Jipe muda na umakini kwa jambo unalolifanya.

Inashauriwa kutengeneza ratiba ya kila siku ambayo inaainisha mambo unayotakiwa kufanya kila siku ili kutoruhusu mawazo mengine kuingilia ratiba yako. Fanya kila kitu kwa wakati na jiepushe kuanzisha jambo bila kulimaliza kwa wakati.

Njia hii itakusaidia kutatua changamoto ya kukosa umakini kwa mambo unayoyafanya.

6. Usijisikie Mkosaji.

Hakikisha wakati wote akili yako iko vizuri kwasababu matatizo ya kisaikolojia yanashusha kinga za mwili na kukuweka katika hatari ya kukumbwa na magonjwa. Muhimu kubali hali yako usijione mkosaji na tafuta njia ya kuondokana na trauma katika maisha yako.

7. Muone Daktari wa Saikolojia.

Ikiwa umejaribu kufuata hatua zote hapo juu na bado trauma inajitokeza, muone daktari akupe ushauri zaidi. Na wengi wanaofikia hatua hii huanzishiwa matibabu ya kisaikolojia ikiwemo kupewa dawa ambazo hudhamiria kutibu ugonjwa wa akili.

8. Msaidie Mtu mwenye Trauma.

Ikiwa umefahamu dalili na madhara yanayoambatana na mtu mwenye trauma mueleke njia sahihi zilizotajwa hapo juu ili kuokoa maisha yake.

Kumbuka kuwa Trauma ni dhana pana inayosababishwa na mambo mengi na hujitokeza katika namna tofauti. Kwa mantiki hiyo hata tiba yake hutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Muhimu ukipatwa na dalili za trauma zilizoainisha katika makala iliyopita muone mtaalamu wa saikolojia akusaidie.

tushirikishane
 • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

 • name *

 • email *

 • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Mambo 13 yatakayokusaidia kukamilisha furaha katika maisha

Kila mtu anapenda kuwa na furaha, lakini kuna wakati huzuni hutawala na mtu kushindwa ...

UTAFITI: Wanaojipiga ‘Selfie’ hatarini kupata magonjwa ya akili

Imeelezwa kuwa tabia ya kujipiga picha mwenyewe (selfie) na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii ...

Tumbaku: Zao lenye neema ya utajiri, lakini linaua kila baada ya sekunde sita

LICHA ya kutajwa kuwa mkombozi wa kiuchumi, lakini zao la tumbaku bado limeendelea kuwa ...