Lindi: Mpango wa usafi wa mazingira washindwa kutekelezwa

MNAMO Agosti 8, 2016 viwanja vya maonesho Sikukuu ya Wakulima– maarufu; Nane Nane katika eneo la Ngongo, mjini Lindi vilikuwa vimependeza kutokana na kuwepo kwa mabanda yaliyosheheni bidhaa mbalimbali za kilimo wakati wa kilele cha.

Lakini ukiyaangalia mandhari ya viwanja hivyo leo hii, takriban miezi nane baadaye, huwezi kuamini kama eneo hilo liko katika halmashauri ya Manispaa ya Lindi na linatumika kwa shughuli za kijamii ama limegeuka kuwa jalala kutokana na milundikano ya taka ngumu na laini utadhani halijawahi kufanyiwa usafi katika kipindi cha miaka miwili.

FikraPevu inatambua mikakati ya serikali ya kuifanya Tanzania iwe na muonekano safi kupitia mipango mikakati ya usafi ya kila mwezi kama ilivyoasisiwa na Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, lakini yapo baadhi ya maeneo ambayo yameshindwa kutekeleza kwa vitendo mpango huo wa usafi, hali inayosababisha maeneo hayo kubakia na uchafu wa kudumu.

Lindi na uchafu, kama mapacha

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, katika maeneo ya Mkoa wa Lindi, hususan Manispaa, mwitikio wa wananchi katika suala la usafi ni mdogo mno huku wengi wao wakibeza mpango huo na kuuita ni mpango wa 'nguvu ya soda'.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, katika kuhakikisha kampeni ya usafi wa mazingira kuwa ni ya kitaifa na endelevu, mwaka 2015 na 2016 Rais Magufuli alilazimika kufuta baadhi ya sherehe za kitaifa na kuzifanya kuwa siku za usafi kitaifa pamoja na kuelekeza fedha kwenye upanuzi wa miundombinu.

Wakati alipofuta sherehe za Uhuru wa Tanganyika mwaka 2015, rais Magufuli alielekeza fedha hizo kwenye upanuzi wa barabara ya Morocco-Mwenge na alipositisha sherehe za Muungano 2016 akaelekeza fedha hizo kwenye upanuzi wa  barabara ya kuelekea Uwanja wa Ndege Mwanza.

Dhana kubwa ya kufanya jitihada hizo zote ni kuipa nguvu kampeni hiyo ya usafi na kumfanya kila mwananchi aone umuhimu na kuwajibika kutunza mazingira.

FikraPevu inafahamu kwamba, zipo baadhi ya halmashauri zilizopokea vyema hatua hiyo ya serikali kwa kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya usafi ambapo kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi wananchi wake wamekuwa wakishiriki kwa pamoja kusafisha maeneo yao.

Usafi kila Jumamosi

Mkoa wa Dar es Salaam na Manispaa ya Tabora zenyewe ziliamua kwamba kila Jumamosi wananchi wote lazima washiriki usafi hadi saa nne kabla ya kuendelea na majukumu mengine ya maendeleo, ambapo kwa kawaida hata biashara zote huwa hazifunguliwi mpaka usafi umefanyika.

Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea ni miongoni mwa baadhi ya halmashauri mkoani Lindi zilizoitikia wito wa Rais licha ya changamoto nyingi zinazoikabili wilaya hiyo.

Hata hivyo, FikraPevu imebaini kwamba, bado suala la usafi wilayani humo liko nyuma ingawa mwitikio wa mwamanchi mmoja mmoja unaridhisha.

Uchafu wadumu

Baadhi ya wananchi wilayani humo wameieleza FikraPevu kwamba, changamoto kubwa ni uchafu wa kudumu kwenye maeneo ya upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile kwenye viwanja vya mikutano ya hadhara na michezo ukiwemo Uwanja wa Sokoine, eneo la Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea pamoja na machinjio ya wanyama.

Hayo ni baadhi tu ya maeneo ambayo usafi wa mazingira haufanyiki kama inavyotakiwa.

FikraPevu ilitembelea maeneo hayo na kujionea mlundikano wa taka usio na mpangilio pamoja na majani na nyasi zinazozingira maeneo hayo huku mamlaka zinazohusika zikiwa hazifanyi jitihada zozote.

“Kwa kweli hali ya usafi katika maeneo haya ni mbaya kama unavyoona ikizingatiwa maeneo hayo yanahusu na utoaji wa huduma kwa wananchi kila siku. Kampeni ya usafi imeonyesha kutozaa matunda, licha ya kuwa katikati ya mji lakini wahusika ambao ni Halmashauri ya Mji Mdogo wa Nachingwea bado wapo kimya,” wananchi wa maeneo hayo waliiambia FikraPevu.

Matumizi mengine

Uwanja wa Sokoine Nachingwea uliopo katikati ya mji huo mdogo na unatumika kwa shughuli mbalimbali kama vile mikutano ya hadhara, michezo na mashindano mbalimbali lakini pia hutumika kwa maonyesho mbalimbali na shughuli za kitaifa kama vile kulaza Mwenge wa Uhuru, lakini umuhimu wa usafi wa mazingira ndani na nje ya uwanja hauzingatiwi.

Aidha, Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea iliyopo takriban umbali wa meta 700 kutoka uwanja huo pia ina mazingira machafu kinyume na taratibu za afya, hali ambayo inahatarisha afya za wakazi na watumishi na kuwepo uwezekano wa magonjwa ya mlipuko.

FikraPevu ilitembelea hospitali hiyo ya wilaya na kujionea baadhi ya miundombinu kama maji ikiwa ni michafu na mibovu, na mazingira ndani na nje yakiwa machafu.

Rais Magufuli apuuzwa

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Lindi wakifanya usafi Desemba 9, 2015

Uchunguzi wa FikraPevu umebaini kwamba, kutotekelezwa kwa agizo la Rais Magufuli la usafi wa mazingira kunatokana na halmshauri kutohamasika kwenye zoezi hilo, ikiwa ni pamoja na kutowahamasisha wananchi kuchangia gharama za usafi hususan uzoaji wa taka.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea na Mkoa wa Lindi kwa ujumla kuna watumishi walioajiriwa kufanya usafi maeneo mbalimbali ya umma kama vile barabara, hospitali, zahanati, masoko, ofisi za serikali pamoja na kumbi za mikutano.

FikraPevu imeelezwa kwamba, hatua ya serikali kuajiri watumishi hao imetokana na makampuni mbalimbali ya usafi kujitoa kwenye uzabuni kutokana na kutolipwa pesa zao.

Felix Msangawale ni mmiliki wa kampuni ya usafi ya Zyamsanga ambaye alithibitisha na kueleza kuwa kampuni yake imeshindwa kufanya kazi kutokana na halmashauri hizo kutofuata mikataba na ulipaji wa fedha.

Aidha, FikraPevu imebaini pia kwamba, ni miezi mitatu sasa baadhi ya watumishi hao wa usafi wameacha kazi katika kile kilichodaiwa kuwa kutolipwa mishahara yao kwa wakati na katika kiasi wanachostahili kutokana na uzito wa kazi wanazozifanya.

Wafanyakazi waonewa

Imeelezwa pia kwamba, serikali haitoi fidia na bima, na kwa mfanyakazi anayepata udhuru kama vile kuugua ama matatizo ya kijamii ikiwemo misiba na kutofika kazini, hukatwa mshahara wake.

“Natakiwa nilipwe shilingi laki moja (100,000) kila mwezi lakini tukienda kwa Mkurugenzi anatuambia halmashauri haijakaa kikao hivyo subirini au wanatulipa shilingi 70,000 kinyume na makubaliano,” Bibi Aisha Manyanya aliieleza FikraPevu.

Bibi Aisha amesema kwamba, hali hiyo imesababisha wafanyakazi wengi kuacha kazi hali inayosababisha usafi wa mazingira usitekelezwe kwa kiwango kinachotakiwa.

FikraPevu inafahamu kwamba, Wilaya ya Nachingwea na Mkoa wa Lindi kwa ujumla ni baadhi tu ya maeneo nchini ambayo zoezi la usafi wa mazingira limeshindwa kutekelezwa.

Viongozi wakuu wanaoaminika kuwa ndio wangekuwa mstari wa mbele nao wanarudi nyuma na kulikwepa jukumu hilo na hali imekuwa mbaya hasa katika kipindi cha masika ambapo hatari ya kuibuka kwa magonjwa ya milipuko kama kipindupindu ni kubwa.

Kilio kikubwa kinanchoelezwa na watendaji kuhusu kukwama kwa zoezi hilo ni bajeti ndogo ndani ya halmashauri zao, ambapo fungu linalotengwa kwa ajili ya usafi halitoshi.

Ni wakati wa serikali kuu kuzipa mamlaka halmashauri ili zitenge fungu kwenye bajeti zao za ndani kugharamia gharama za usafi wa mazingira.

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Vifo vyashamiri kwa wanaotoa mimba Tanzania. Wazanzibari wafanya ngono wakijitambua

WANAWAKE 390,000, kati ya milioni moja, nchini Tanzania hutoa mimba kila mwaka kwa njia ...

Wananchi wamshinikiza waziri Kituo cha Afya kifanye upasuaji

WAKAZI wa Kata ya Igoma jijini Mwanza, wamemshinikiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, ...

Vitambulisho vitaondoa adha ya matibabu kwa wazee Tanzania

Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ...