TANZANIA imejaa watu wengi wanaopenda “ujanjaujanja” katika harakati za kufanikiwa maishani.

Wengi wanapenda kuvuna wasichopanda na kula wasicholima wala huhemea. Wao wanaamini kutumia “njia za mkato” ili waneemeke.

Na katika njia hizo za mkato, hawajali wanamuumiza nani na ana hali gani ya uchumi. Wanachojua wao ni “kula” tu na kupata mali kwa njia ovu.

Miongoni mwa hawa ni baadhi ya maofisa kutoka ofisi zote za serikali, taasisi, mashirika ya umma na binafsi, vyama vya siasa, mashirika ya dini na taasisi zisizokuwa za serikali.

Rais mstaafu Jakaya Kikwete alipotembea Liganga

Kuthibitisha haya ni hatua ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kufuta matokeo ya zoezi la kuthaminisha mali na ardhi lililofanywa na serikali kwa wananchi wa vijiji vya Mundindi na Nkomang’ombe, Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe, ambao wanakalia utajiri mkubwa.

Wakaa miaka 20 ‘burebure’

Wakazi hawa wamekuwa wakiambiwa kujiandaa kuhama maeneo yao, karibu miaka 20 iliyopita, ili kupisha miradi pacha ya makaa ya mawe na chuma cha pua.

FikraPevu ina barua ya kikao cha kwanza cha wananchi wa vijiji vinavyozunguka maeneo ya madini hayo kukutana na kuelezwa kwamba hawaruhusiwi kuendelea na ujenzi au maendeleo yoyote hadi watakapoelezwa. Kikao hicho kiliketi Novemba 24, 1998. Kilijumuisha wawakilishi wa wanavijiji, viongozi wa wilaya na “wakubwa” kutoka NDC makao makuu.

Utajiri unaozungumzwa hapa ni madini. Juu ya ardhi yao; maeneo ya Mundindi lipo eneo la Liganga, kuna madini ya chuma cha pua na Nkomang’ombe, kuna makaa ya mawe. Yote haya ni madini adhimu duniani. Yanahitajika sana kwa ustawi wa viwanda na nguvu ya kuzalisha nishati- umeme.

Mwandishi Simon Mkina akishangaa makaa ya mawe.

Wanavijiji hawa waliamriwa kuyatambua maeneo yao ya makazi, mashamba na mali zilizoko juu ya ardhi – zisizohamishika. Hizi ni pamoja na nyumba, miti na mazao yaliyokuwapo wakati wa zoezi la kuthamini.

Zoezi hili lilifanywa na Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kwa kushirikiana na serikali za vijiji hivyo.

Wajipanga kupiga dili

Katika zoezi hili, imegundulika kuwa baadhi ya wahusika, waliokuwa wakisimamia zoezi hilo, waligeuza mradi wa wao kutajirika kijanjajanja, kwani waliandika majina yao na kuonesha kuwa wanamiliki nyumba, mashamba au miti. Kumbe ni uongo. Rushwa ilitawala kwani wasiokuwepo, viongozi wakubwa waliandikishwa kwa majina ya bandia.

“Hakika hapa watu wengi walikuwa wamejipanga kupiga hela, tena nyingi, hawa wathaminishaji walikuwa wanataka malipo ya bure, kwamba walipwe fidia wakati hawamiliki hata vibanda hapa kijijini kwetu,” anaiambia FikraPevu, Ndimbo Haule (69), mkazi wa Mundindi.

Mzee huyu anaungana na wakazi wa maeneo ya Nkomang’ombe (imezoeleka Mkomang’ombe) na Liganga, ambako Majaliwa alitembelea na kuzungumza na wananchi na kutoa amri ya kuanza upya kwa zoezi la kuthaminisha mali na ardhi.

DC athibitisha

Kiongozi wa Wilaya ya Ludewa (DC), Andrea Tsere amelieleza gazeti hili kuwa serikali imegundua kuwepo kwa utapeli mkubwa katika mradi wa kufidia wananchi wenye mali na ardhi katika maeneo ya miradi pacha ya Liganga na Mchuchuma.

Wananchi hao wanatakiwa kulipwa fedha hizo baada ya kufanyika tathmini ya mali zao na ardhi ambako mchakato wa kuanza kwa miradi ya maeneo hayo utapita.

Huu ni mwamba wa chuma huko Liganga

Katika maeneo hayo, wananchi wanatakiwa kupisha kuanza kwa miradi hiyo mikubwa inayoendeshwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Sichuan Hongda kutoka China.

Wataendelea kusota

Waziri mkuu, pamoja na kueleza kuwa mchakato bado kuanza kwa miradi hiyo mpaka serikali ijiridhishe, haijulikani lini, alibainisha kuwa gharama za kulipa fidia kwa wenye maeneo hayo ilikuwa kubwa mno, hivyo serikali kutilia shaka juu ya uhalali wake, hivyo kuchukua uamzi huo.

“Kuna baadhi ya watu walijipenyeza na kutaka kuiibia serikali kupitia suala la ulipaji wa fidia. Sasa tumeamua kufanya uthamini upya ili kupata fidia halali ya kutoumiza serikali na mwekezaji,” amesema Majaliwa.

Pamoja na kwamba uamuzi huo unaweza kuwa nafuu kwa wawekezaji, akiwamo serikali yenyewe, ni mwendelezo wa kero kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo ambao wamekuwa wakichoshwa na ahadi za neema kila uchao.

“Sisi tumekuwa hapa miaka mingi sana, leo tumezeeka na hakuna lolote linaloendelea zaidi ya ahadi kwa kila kiongozi anayekuja kututembelea hapa kijiini kwetu,” anaeleza Rhoda Mtewele (57), mkazi wa Nkomang’ombe akizungumza na FikraPevu.

Rhoda, akiwa anatembelea mkongojo kwa umri mkubwa na matatizo ya mgongo, anasema serikali imekuwa ikiwakwamisha mno kupata maendeleo kwa kuwa hawana uhakika ni lini watahamishwa na kupangiwa maeneo mengine.

Zitto Kabwe akitazama mkaa wa mawe huko Mchuchuma wakati akiongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC)

Anasema, “hapa kwa sasa bado siyo salama, kila siku tunaambiwa tutahamishwa kwa ajili ya kupisha mradi wa madini, lakini miaka inaenda na kurudi (anakosea hapa, miaka hairudi), hakuna kinachofanyika.”

Hawa kila mara, kwa miaka mingi sasa, wanaishi kwa wasiwasi wa kuhamishwa, na hata kufukuzwa kutoka katika maeneo yao, kwa kuwa tu wanaishi juu ya utajiri mkubwa. Wamekuwa kama watoto yatima. Hawaelewi kesho yao.

Msomi awasemea

Daktari wa siasa na uchumi, mhadhiri wa vyuo vikuu, Lenny Kasoga ameiambia FikraPevu kwamba wakazi wa maeneo ya Liganga na Mchucuma wanapaswa kuishi kwa wasiwasi huo kwani hakuna wanayemuamini hata sasa.

Anasema tangu anasoma ndani na nje ya nchi, miaka 30 iliyopita, amekuwa akisikia na kusoma kuwepo kwa mipango na mikakati ya kuanza kutumia makaa ya mawe na chuma cha Liganga, lakini anastaafu bila kuona kinachoendelea.

“Hawa lazima waishi kwa wasiwasi, kwani leo wanaambiwa wajiandae kuondoka kwenye maeneo yao na kulipwa fidia, lakini wakijipanga na tathmnini ya mali zao kufanywa,  wahusika hawarejei tena kwa miaka kumi ndipo wanaibuka tena na habari zilezile…Hapo mtu atajengaje, ataendeleza vipi eneo lake na kuweka mazao mengi ya kudumu,” anaongeza Dk. Kasoga kwa kuhoji.

Umasikini watisha

FikraPevu limetembelea maeneo hayo na kuona umasikini mkubwa wa wakazi wengi wa maeneo hayo, licha ya kuwa katika ardhi yenye utajiri mkubwa wa mali.

Imaculate Isedory, binti wa miaka 14, akiwa amekatizwa shule na wazazi wake, anaeleza namna maisha yalivyokuwa magumu katika kijiji chake cha Liganga.

“Hapa tuna shida sana, nimeacha kwenda shule kwa kuwa mama hana hela ya kunilipia madaftari, viatu na kalamu, nilisaidiwa na padre darasa la kwanza, lakini alipokufa (fariki dunia), nilikosa mtu, nikaacha,” anasimulia kwa FikraPevu binti huyo aliyekuwa peku, ikiwa ni moja ya ishara za umasikini Ludewa.

Licha ya kueleza kuwa mama yake anapembua mpunga na mahindi mashineni, bado maisha kwao ni magumu.

Imaculate anaeleza namna alivyoacha kunywa chai yenye sukari, huku akisema akiamka asubuhi, hustafutahi kwa kunywa bokoboko (uji wa mchele) wenye chumvi.

Inashangaza kwamba serikali imekuwa ikisuasua kuweka wazi ni lini neema ya utajiri kwa wananchi wa Ludewa na Tanzania watafaidika zaidi kwa kuanza kwa miradi pacha ya Liganga na Nchuchuma.

Wachina hawa ni neema au laana?

Hata hivyo, mwanga wa neema ulianza kuchomoza Septemba 21, 2011, wakati Serikali ya Tanzania na kampuni kutoka Beijing, China ya Sichuan Hongda Corporation ilipowekeana saini ya kuanza kuendesha miradi hiyo.

Aliyeshuhudiwa sherehe za kusaini mikataba hiyo alikuwa Makamu wa Rais wa Tanzania,  Dk. Mohamed Gharib Bilal katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam. Katika mkataba huo, ikabainishwa kuwa serikali itakuwa na asilimia 20 ya uwekezaji huo na 80 inayobaki ikamilikiwa na kampuni hiyo ya China.

Kulingana na makubaliano hayo, miradi ya Liganga na Nchuchuma, ingetekelezwa kwa uwekezaji ambao ungegharimu karibu Sh. 5 bilioni (zaidi ya dola bilioni 3 za Marekani).

Wasiwasi wao haujaanza leo wala jana. Haujaletwa na Serikali ya Rais Julius Nyerere, rais wa kwanza wa Tanganyika na baadaye Tanzania. Haujaasisiwa na Rais Ali Hassan Mwinyi, wala kuhuishwa na Rais Benjamin Mkapa. Wala sio Rais Jakaya Kikwete na kamwe hawezi kuwa Rais John Magufuli.

Madini haya yamekuwepo miaka nenda rudi. Wakoloni wameyakuta, hata kama watatamba kwamba wao ndiyo wameyavumbua. Ni waongo. Yamekuwepo jana, leo na yataendelea kuwepo. Labda “yavurugwe” na wenye uchu wa kuifilisi Tanzania na watu wake.

Wasiwasi wa maisha ya wananchi hao umegubikwa na ahadi. Kila awamu ya uongozi wa serikali imekuwa na kauli zinazoweka watu hao katika maisha yasiyokuwa na mwelekeo.

Angalau Mwalimu Nyerere alikuwa na msimamo kwamba madini hayo yasivurugwe, yaachwe hadi Tanzania itakapokuwa na wataalamu wake ndipo yaanze “kufanyiwa kazi.”

Hata hivyo, FikraPevu inatambua kuwa Mwalimu Nyerere aliyeng’atuka katika nafasi ya urais mwaka 1985, baada ya kuwatumikia Watanzania- akiwa Ikulu kwa zaidi ya miaka 24, aliondoka na msimamo huo na kumwachia Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi, baada ya kuingia madarakani akawa na mtazamo huo, ingawa ulibadilika na kuamua kukaribisha wawekezaji katika biashara na maeneo yenye madini. Hata hivyo, Liganga na Nchuchuma hayakuguswa sana. Mwinyi alikaa madarakani kwa miaka 10.

Alipoingia madarakani, mwaka 1995, Rais Mkapa alikuja na kasi kubwa ya kukaribisha wawekezaji na wengi walionekana wakija Tanzania na mitaji yao kwa ajili ya kuwekeza.

Kama ilivyokuwa kwa Rais Mwinyi, Mkapa naye “alichangamkia” maeneo mengi ya biashara na uwekezaji katika madini, lakini hakuwa na muda zaidi kwenye makaa ya mawe ya Nchuchuma wala chuma cha pua cha Liganga.

FikraPevu inaelewa kuwa alipoondoka madarakani, baada ya miaka 10, Rais Kikwete aliweka nguvu za ziada kwenye uwekezaji wa madini, alikaribisha matajiri kuweka mitaji yao, kwa maana kwamba watakuja na neema kuu kwa Watanzania.

Kwamba watalipa kodi, watasaidia jamii zinazozunguka maeneo ya madini, kuajiri Watanzania katika kazi wanazoweza kumudu na kubwa zaidi, kuleta ujuzi kwa wazawa ambao watakuwa wakifanya kazi ndani ya miradi ya uchimbaji madini.

Ni katika kipindi cha Rais Kikwete, ndipo Liganga na Mchuchuma “zikawika” zaidi. Zikafahamika mno, ndani na nje ya Ludewa, Njombe, Tanzania na nje ya mipaka ya Afrika.

Kilichofanya kujulikana zaidi ni kuwepo kwa mikataba ya uwekezaji mkubwa wa mabilioni ya shilingi katika migodi ya Liganga na Nchuchuma.   

Sasa imebainika kuwa Kampuni ya Sichuan iliyoaminisha umma wa Tanzania kuwa ni tajiri, kumbe haikuwa na akaunti wala kuweka senti mahali kokote; siyo katika benki za Tanzania wala taasisi za fedha za uwekezaji.

“Inaweza kuwa tajiri na kuwa na uwekezaji mkubwa maeneo mengine, lakini hapa kwetu imekuja bila senti, siasa inaweza kuwa iliibeba na hata kushinda zabuni, lakini haiko makini na haikuwa na fedha,” anasema mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) ambaye hakutaka kutajwa jina lake.

Hata hivyo, hakueleza kwa undani ni siasa gani iliyoibeba kampuni hiyo ya China hata kuibuka na ushindi kati ya kampuni 21 zilizoomba kuingia kwenye uwekezaji wa Liganga – Mchuchuma.

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo amesema kampuni hiyo ya Sichuan, pamoja na tambo zote za kuwa na mtaji mkubwa na kushinda zabuni ya kuwekeza katika migodi ya Liganga na Mchuchuma, haikuwa na fedha.

“Hawa hawakuwa na senti katika akaunti hapa nchini,” alisema Prof Muhongo akieleza “ujanjaujanja” wa kampuni hiyo, huku akishangaa namna ilivyopata ushindi katika zabuni iliyotangazwa ndani na nje ya nchi; magazeti ya kimataifa, likiwamo maarufu la Wall Street Journal la Marekani na kusambazwa na mtandao wa devex wenye kuaminika kwa matangazo ya zabuni kubwa duniani.

NDC wanena

Meneja Uhusiano na Mawasiliano Mwandamizi wa NDC, Abel Ngapemba anasema hakuna harufu yoyote ya rushwa katika mchakato huo wa kumpata mwekezaji makini.

Anasisitiza, serikali haiwezi kuruhusu kuwepo kwa kampuni isiyokuwa na mtaji kuja kuwekeza kwenye mradi mkubwa namna ile, tena ukiwa unabeba neema ya muda mrefu ya Watanzania.

Kuhusu kampuni hiyo ya China kutokuwa na fedha, Ngapemba, alijibu FikraPevu harakaharaka – “hakuna kitu kama hicho, hiyo ni moja ya kampuni tajiri zaidi duniani zilizowekeza kwenye madini, chuma na biashara  zingine kubwa.”

Akizungumzia dili katika uthamini na endapo NDC ilihusika, Ngapemba anasema  shirika lake halihusiki kwa namna yoyote, na kama kuna kitu cha hovyo kilichofanywa huko, ni halmashauri na maeneo mengine ya utendaji, lakini sio wao.

“Sisi ni wasimamizi sawa, lakini zoezi la uthamini hatukufanya sisi, walifanya wengine, sasa kama zipo tuhuma, zinawahusu waliohusika na kamwe sio sisi,” anasisitiza Ngapemba.

FikraPevu yabaini

Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu umebaini kuwa Kampuni ya Sichuan, baada ya kushinda zabuni, iliingia katika ubia wa fedha za mtaji na Benki ya China Africa Development CADB) na China Africa Development Fund (CADF).

Baada ya kubainika kwa ujanjaujanja wa Kampuni ya Sichuan, Serikali ya Rais Magufuli, kimyakimya, imeamua kuingia ubia na Serikali ya China na kuachana na Sichuan, ambayo pamoja na NDC waliunda Kampuni ya Tanzania China International Mineral Resources Ltd (TCIMRL), kuendesha miradi pacha ya mawe na chuma cha pua.

Bosi mkuu aongea

Hata hivyo, Huang Daxiong, aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sichuan, Tanzania ameiambia FikraPevu kuwa kampuni yake haikupata zabuni kwa rushwa na kwamba haijashindwa kazi.

Huang anasema miradi ya Liganga na Mchuchuma ilikwamishwa na serikali yenyewe, kwamba serikali ilishindwa kutekeleza makubaliano ya awali, ikiwamo kupanua barabara kuu kutoka Njombe hadi Nkomang’ombe ambako ndiko kwenye makaa ya mawe.

“Tulishindwa kupitisha mitambo yetu mikubwa kutoka Dar es Salaam hadi kwenye migodi, sasa hatuwezi kulaumiwa sisi kwa hili,” alisema na kukanusha kwamba kampuni yake haikuwa na senti kuendesha miradi hiyo pacha.

Anakanusha kuwepo kwa mipango ya kuvunjwa kwa mkataba baina ya serikali na kampuni yake, kama ambavyo NDC kupitia kwa Ngapemba imeiambia FikraPevu hivyohivyo.

Ni kutokana na kuwepo kwa mzingira ya danadana, katika kukamilisha na kuanza kazi kwa migodi hiyo pacha, huenda zoezi la kuthaminishwa mali likawa endelevu; kwani kila kiongozi ajaye anaona waliotangulia hawakufanya vyema na kwamba walikuwa wakihitaji kuneemeka kwa rushwa na mbinu zingine ovu – binafsi, huku miaka ikizidi kusonga na wananchi wakiishi kwa wasiwasi na danadana za maisha ya neema zikiendelea kuwaweka roho juu.

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Gesi yamfanya aokoe Sh. 1.5 milioni za mkaa kwa mwaka

“KWA mwezi mmoja nilikuwa natumia Sh. 140,000 kwa ajili ya kununulia magunia mawili ya ...

Asilimia 15 ya Watanzania wanapata nishati ya umeme

ASILIMIA 15 ya Watanzania ndio wanaopata nishati ya umeme, kiwango ambacho hakitoshelezi na hakiendani na ...