Connect with us

Jukwaa la Maisha

Kwanini wanawake wanaamua kubaki na waume wanaosaliti mahusiano ya ndoa?

Published

on

“Marriage is a promise. Not just between the couple but to the community at large, to generations past and to those yet to be born”. Heritage.org

“Ndoa ni ahadi. Siyo tu baina ya wanandoa bali hata na jamii yote inayowazunguka, kwa vizazi vilivyopita na vizazi ambavyo havijazaliwa”

Hiyo nukuu hapo juu inaonyesha uzito wa ndoa. Ndoa  siyo utani wala mchezo!

 Kwanini watu huingia kwenye ndoa?

Kuna watu watakuambia “najua kuoa, sijui kuacha”. Wengine watakuambia, ndoa ni taasisi ambayo waliomo wanataka kutoka, walio nje wanataka kuingia”. Ukweli ni upi?

Watu huoana kufuatana na utashi wao na sababu wanazozijua wenyewe. Hata hivyo ni sawa tukisema kwamba watu wengi huingia kwenye  ndoa  kwa lengo la kuishi na yule wampendae kwa kadri inavyowezekana. Kwa wale ambao  viapo vyao vya ndoa vinasema “hadi kifo  kiwatenganishe”, tunaweza kusema kwamba, wanaingia kwenye ndoa kwa maisha ya kudumu pamoja hadi watakapoiaga  dunia. Ndoa inawapatia wanandoa uhalali kiimani, kimila na kisheria wa kuishi kinyumba, kuzaa na kulea watoto, kutunzana, kupendana kwa kiwango cha juu na pia kuhudumiana. Mwanandoa anapata haki zake na kubanwa kutekeleza  wajibu unaompasa kutimiza.Kwa maneno mengine ndoa zina miiko yake na kanuni na taratibu zake ambazo zinapaswa kuzingatiwa ili ndoa isimame.

Pamoja na kwamba lengo la kuoana ni kuishi na kudumu pamoja, hali halisi ni kwamba kuoana na kuachana siku hizi ni jambo la kawaida. Ndoa zinafungwa tena kwa  gharama kubwa. Watu wanasherehekea na kushuhudia viapo vya mke na mume kuishi pamoja maisha yao yote tena kwa mapenzi makubwa katika hali zote. Ni ya kweli hayo au ni mchezo wa kuigiza tu? Baada ya sherehe na cherekochereko wanandoa wanaanza maisha katika hali halisi ya maisha. The party is over. Kufumba na kufumbua unasikia hawapo tena pamoja. Sababu zipo nyingi ikiwemo kukosa uvumilivu na subira.

Mwanzo wa ndoa tunaambiwa ni tamu kama chungwa, katikati ni tamu kama limao au ndimu na mwishowe huweza kuwa chungu kama shubiri! Inapokuwa kwenye utamu wa chungwa, wanandoa huwa kwenye ulimwengu wa kivyaovyao, wa kiparadiso fulani na siyo rahisi kufikiria kuna siku ndoa hiyo itakapogeuka kuwa chungu! Maisha ya ndoa, siyo lelemama, ni safari isiyo na ramani inayoeleweka. Kuna sehemu itakuwa tambarare, mara utakutana na mabonde, milima na wakati mwingine utalazimika kupita juu ya madaraja mabovu ya kuvuka mito yenye mamba na viboko!

Moja ya sababu zinazochangia kuvunja mahusiano ya kindoa ni USALITI. Kwanini usaliti unaingia kwenye ndoa ni mada nyingine tutakaoijadili wakati mwingine. Yatosha kusema kwamba wanawake wamekuwa jasiri sana kusimamia ndoa zao pale zinapokumbwa na dhoruba hii. Wanawake mara nyingi wanapogundua mume ana mahusiano nje ya ndoa hawaachii  ngazi. Katika mazungumzo ya kawaida siyo ajabu ukasikia watu wanasema “huyu mwanamke sijui anangoja nini haondoki”. Swali hili ni pasua kichwa  hasa kwa watu ambao  hawajaonja tamu na chungu ya ndoa

Moja ya mambo ambayo hushtua wanandoa sana ni pale mmoja anapogundua kuwa mwenziwe kumbe siyo muaminifu kama alivyoaamini pale mwanzo! Makala hii itaangalia zaidi upande wa wanawake na jinsi wanavyochukulia kitendo cha kusalitiwa kwenye ndoa. Wakati naandika makala hii, nilijaribu kudodosa baadhi ya wanawake wa hali za maisha tofauti tofauti – kiuchumi, kielimu, kiimani za dini, kiumri pia. Nilichogundua ni kwamba wengi wa wanawake waliokaa kwenye ndoa zaidi ya miaka kumi, walishapitia misukosuko kadhaa ya kusalitiwa na waume zao. Wengine walisalitiwa na wanawake waliokuwa na uhusiano nao kwa namna moja au nyingine. Wapo waliokuwa na uhusiano kikazi – wasaidizi wa ndani, masekretari, wabia kibiashara n.k. Wengine walisalitiwa na wanawake waliokuwa ndugu au marafiki wa karibu sana.Vyovyote ilivyokuwa, tukio au matukio hayo yalileta uchungu mkubwa sana na kuzorotesha mahusiano ya ndoa. Kwa wengine matukio hayo yalileta “neema” kimaisha na hata katika uhusiano.

Kwa wanawake ambao ndoa zao zilikuwa changa zenye chini ya miaka mitano,  baadhi walionyesha kutokuamini kuwa waume  zao wanaweza kuwasaliti! Waliona kama ni jambo lisilowezekana kwa vile waliamini wanawatosheleza kwa kila hali.Wengine waliendelea kwa kuelekeza lawama kwa  wanawake wenzao kuwa wanachangia mume kutoka nje kwa sababu mbalimbali ambazo sitazijadili kwenye makala hii. Cha ajabu, wanawake wale ambao walionekana kutokufurahia tena ndoa zao, hawakuonyesha dalili zozote za kutaka kuachana na waume zao. Baadhi ya sababu walizozitoa ni kama zifuatazo:

1.  Hofu ya kuishi peke yao:

Wanawake  walionyesha kuwa na  hofu sana ya maisha ya upweke. “Mwanamke aliyeolewa akiwa na miaka 23, akakaa kwenye ndoa miaka 20 na kuendelea siyo rahisi sana kujikata na kuanzisha maisha ya peke yako”– ndivyo alivyosema mama Doris ( siyo jina lake halisi). Mama Doris aliolewa akiwa na umri wa miaka 23  akiwa bado chuoni. Hakuwahi kuishi peke yake.Aliishi na wazazi kabla ya kuolewa. Amekaa na mume zaidi ya miaka aliyoishi na wazazi wake. Ataanzaje  maisha ya peke yake? Kwake ilimuwia vigumu sana kutoka na kwenda kuanza kuishi peke yake kwa vile hakua na uzoefu. Aidha alizidi kusema kwamba ataanzaje tena kuanza kutafuta mwenza mwingine katika umri ule?

2.   Kuhofu kutokujimudu kifedha:

Kipato nacho huchangia sana kumfanya mwanamke aone vigumu kumwacha mwenza wake kisa amemsaliti kindoa. Mrs Y. alinitonya kwamba, kitendo cha mumewe kutoka nje ya ndoa pamoja na kumuumiza kisaikolojia, bado hakitoshi kumfanya aachane na mumewe. Mumewe ni mtu mkarimu sana kifedha na hicho nacho ni kichocheo cha tabia ya mume kutoka nje. “Wanawake wanajigongagonga sana kwa mumewe kwa sababu ya uchumi mzuri alio nao” alisema Mrs Y. Endapo ataondoka, ni kama kujiadhibu kwa sababu hizo pesa zitaliwa na hao mahawara kiulani zaidi. Pia yeye hana kipato kikubwa japo maisha yake ni ya hali ya juu sana. Haondoki ng’o!

3. Hakuna mwanaume aliye mkamilifu:

Wanawake wengi waliamini kwamba wanaume wote ni sawa utadhani wamezaliwa na baba mmoja mama mmoja! Usemi huu wa jumla na wenye maana nzito ulinifanya niwe mdadisi zaidi kutaka kujua unahusiana vipi na kuachana na mwanaume asiye mwaminifu? Mama “B” hakusita kuhitimisha na kusema “Wote wako sawa ila wanatofautiana viwango tu. Kadiri wanandoa wanavyoishi pamoja ndivyo polepole hugundua kuwa zile ndoto za mwanzo kuwa huyo ni wako peke yako hupungua na hata kutoweka baada ya muda”. Mama B ni mama mwenye watoto watano na wajukuu watatu. Ameolewa kwa miaka 35. Kipindi chote cha ndoa, ameishi na mume mwenye tabia ya kusaliti ndoa. Mumewe amezaa mara mbili nje ya ndoa na mmoja wa aliyezaa naye ni  binti wa rafiki yake! Kasheshe lililotokea baada ya aibu hiyo sitaweza kuliandika hapa kwa sababu hakunipa ruhusa kuliandika. Ila yatosha kusema tu kuwa mama huyu mcheshi, mkarimu na mwenye upendo alimsamehe mumewe na kuendelea kuishi naye.

4.  Kupoteza utambulisho:

Hili la utambulisho limenikumbusha kisa na mkasa wa marehemu  Profesor  Maathai Wangari na visa vya kulazimishwa aache kutumia jina la mumewe baada ya talaka!Hili ni janga kwa wanawake kama alivyosema Mrs L. Mhadhiri wa chuo kimoja maarufu. “Fikiria mwanamke uliyetambulika kama Mrs L maisha yako yote, ukajijengea utambulisho na sifa kwa kutumia jina la mume. Ghafla unatalikiana na mwenza wako na kulazimika kurudia jina lako la zamani, jina ambalo hakuna anayelijua isipokuwa walimu wako wa shule ya msingi na sekondari! Utakubali kupoteza kila kitu?” Siyo wengi wenye ujasiri kama wa marehemu profesa Maathai Wangari kwa kukomaa na kutumia akili ya ziada ya kuongeza herufi moja kwenye jina na kuonyesha kuwa hilo siyo jina la huyo mume anayeringa na jina kusudi tu amkomoe mke. Mwanamke aliyekwisha kujijengea jina kikazi au kibishara kwa kujulikana “Mrs” Fulani, humuwia vigumu kuanza kujenga tena sifa yake upya. Jina la mume hasa kama ni kubwa, ni mtaji mzuri kibiashara au kikazi. Mwanamke wa hivi, hawezi kumuacha mumewe kwa vile kamsaliti katika ndoa.

5. Hofu ya kupoteza marafiki:

Mwanamke aliyeolewa mara nyingi anajizolea heshima kwa ndugu, jamaa na marafiki. Kwa msingi huu, atajitahidi sana kuchunga ndoa yake isisambaratike. Anajua kabisa kwamba atakapoanza kutafuta talaka na kuipata, kuna uwezekano mkubwa sana wa  kupoteza marafiki kwa vile hao marafiki watamuona “siyo mwenzetu tena huyu”. Jamii nyingi huhusisha maisha ya upweke bila ndoa, kama maisha ya uhuru usio wa heshima. Hata binti anayeishi peke yake, humuwia vigumu sana kuaminiwa na vijana wa kiume kama binti mwenye wasifu wa kuweza kuoleka. Aghalabu huweza kumtumia tu kwa starehe japo wapo pia wasichana wenye kuishi peke yao wanaoolewa.

6. Familia kukataa kumkubalia atafute talaka:

Kiafrika mke na mume ni sehemu ya familia pana. Pamoja na kuwa na uwezo kisheria kufanya maamuzi yao wenyewe, bado kuna mambo ambayo lazima yapate Baraka ya familia pana ( extended family). Mke na  mume huoana baada ya kupata “baraka” za namna moja ama nyingine kutoka kwa familia. Mchumba hutambulishwa na kukubalika, kisha familia nzima hushiriki kupanga harusi. Hii ina maana mke huyu ni kama “wa ukoo” au wa “familia” na pia mume  naye huingia kuwa mmoja wa wana ndugu wa upande wa mke. Mke akipatikana na tatizo, jamii nyingi hushauri tatizo lipelekwe kwenye familia kupata ufumbuzi. Kwa maana hiyo, mke hawezi kukurupuka tu na kudai talaka bila kupitia ngazi mbalimbali za usuluhishi.Hata Sheria ya Ndoa ya 1971 ya Tanzania inataka wanandoa watafute usuluhisho kwanza kabla ya kupata kibali cha kufungua kesi ya talaka mahakamani.Mila nyingi za kiafrika ni kama haziruhusu talaka na ni kama vile talaka haipo! Kidini kadhalika, kuan madhehebu hairuhusu talaka hadi kifo kiwatenganishe.

7. Kuwekeza sana kwenye Hisia kwa mume:

Kuna wanawake hawawaachi waume zao kwa sababu tofauti sana. Hushindwa kuachana na mume kwa vile amewekeza sana maono ya  moyoni kwa huyo mwanaume kiasi ambacho hushidwa kujikata kama mtoto aliyeshikiliwa na kitovu kwa mama.”Kumpenda mtu kwa moyo wako wote kwa muda mrefu hujenga mnyororo mgumu sana kiasi ambacho kufungua na kutokomea msionane tena ni kitu kigumu mno”. Ndivyo alivyoniambia Bi Sara (siyo jina halisi) Mwanamke kama huyu mara nyingi amejiweka katika hali ya kuishi maisha yake yote na huyo mume, amezaa na watoto ambao wameimarisha ule uhusiano ukawa zaidi ya undugu. Mume amekuwa zaidi ya ndugu zake wa damu.  Kwa vyovyote itamuwia vigumu sana kuachana na mume huyu.

8. Kuwa na agenda ya siri

Wako wanawake ambao hata iweje, hawaachani kamwe na waume zao. Wao wanausoma mchezo mzima unavyokwenda wa kusaliti. Hata mwanaume asaliti mara mia, wao bado wako gado! Mwanamke kama huyu anaona mbali zaidi ya unavyoweza kufikiria. Ana malengo yake ya muda mfupi na mrefu tena yenye manufaa makubwa! Nani anaweza kujiuliza ni kwa vipi Hillary Clinton aliweza kusimama imara wakati wa kashfa ya ngono ya mumewe? Leo Hilary yuko wapi? Je angejikita kutafuta talaka ingemfikisha hapo alipo sasa? Kadhalika miongoni mwa jamii zetu za kitanzania, ni wanawake wangapi wa aina hiyo tunawajua? Huu ni mtihani nakuachia – noa bongo utabaini baadhi ya wanawake kama hawa.

10. Usaliti huweza kuimarisha ndoa.

Ndivyo ilivyoandikwa hujakosea ulichosoma. Wakati mwingine jambo ovu huweza kuzaa jema vilevile. Baada ya kosa la usaliti, Betty (siyo jina halisi) alijikuta akiwa karibu zaidi na mumewe. Waliafanya tathmini ya maisha yao, wakajadili mapungufu yao na kila mmoja akakubali kurekebisha kasoro zile. “Unjaua, kabla ya tukio, mawasiliano ni kama yalikwa yamekatika kwa miaka kadhaa. Kila mmoja alikuwa anaishi kivyake tu. Nilipopata ushahidi wa kilichokua kinaendelea, nilimuuliza. Kwa kweli ulitokea ugomvi mkubwa mno lakini tuliishia kulia pamoja na kuapa kuijenga upya ndoa yetu”. Ndivyo Betty na mumewe walivyofanikiwa kuokoa ndoa yao ya miaka 8.

 

Msomaji mpendwa, una la kuongezea?

Wasiliana name kupitia: lady.viva@fikrapevu.com

Continue Reading
13 Comments

13 Comments

 1. R Kahendi

  01/03/2012 at 9:17 pm

  Wow. Umesema ukweli mtupu. Ninawafahamu wanawake kadha waliotalakiwa, na shida zao ndizo hizo ulizotaja. Baadhi yao wanashindwa kujimudu kifedha. Wengine wamepoteza marafiki yao. Isitoshe, wanaume wote wanaokutana nao wana tabia zile za kusaliti mahusiano ya ndoa.

  • mti mkavu

   25/03/2013 at 6:07 pm

   its true katika ndoa talaka si suruhisho cha msingi nikukaa na mumeo na kujaribu kumuuliza kistaarabu ni nini anakosa kutoka kwako. then jaribu kumfuata atakacho katika mahusiano. ukigundua ni tamaa za mwili basi mhamasishe atumie kondom ilkiasijekuletea janga home ikawa ni kwikwi na shida badala ya raha.

 2. ndetichia

  01/03/2012 at 10:26 pm

  yaani umemaliza kila kitu lady v ngoja nikaisevu ili niwe naisoma daily thanks for lesson madame..

 3. Aidan Chriss

  02/03/2012 at 10:46 am

  This is totaly true….na hasa kipengele cha 10..mara nyingi kama mwanamke hana kosa lolote ila hobbie ya mumewe ni kusaliti….hata siku moja mume hawezi mpa talaka mkewe huyo, na soon mume ataanza kujihisi yeye vibaya na kudhani anaibiwa mkewe that is why mke halalamik kwa upuuzi wake wa kusaliti….this is gr8t staff

 4. david

  02/03/2012 at 11:56 am

  umefanya uchambuzi mzuri mno…na ni kweli kutalikiana sio njia muafaka ya kukimbia matatizo..

  • victor

   12/06/2012 at 12:18 pm

   Talaka si nzuri, ila ukiangalia wenye uvumilivu ni wakuhesabu. Kizazi chenye uvumilivu kinatoweka maana hasa ukikutana na wanawake wasomi wanakuja na mawazo kwamba “sitaki matatizo” wanataka maisha bwerere hawajui kukwama kwenye maisha.
   Wengine wanakuja na mipango ya kuzaa na kubaki na mtoto wake, mwanaume a-chape raba.
   Sasa kwa sura kama hii, matatizo ya kuachana huenda yakaongezeka, maana kila mmoja anataka uhuru, na hawataki shida mara leo kugombana, kusalitiana nk.

 5. Hasani

  04/03/2012 at 7:02 am

  Ni kweli wanawake huvumilia wanapodhulumiwa ndoa zao ila wakati mwingine wao huwa wasababishi

 6. Hasani

  04/03/2012 at 7:10 am

  Pia ikiwa Mme ataamua kumsaliti mke wake kwa uonevu hawezi kupata furaha ya kweli

 7. Hasani

  04/03/2012 at 7:14 am

  Nawatafuta malafiki ninaoweza kujifunza nao kuhusu muumba

 8. MAMBA_1986

  10/07/2012 at 10:55 am

  ulichokiandika niukweli mtupu, wanawake niwavumilivu sana, ila hawa wasasahivi hawawezi kuvumilia kabisaa

 9. Kiloya

  20/01/2013 at 2:31 am

  umenena vyema kiongozi

  lakini pia lazima tukumbuke minyororo iliyofungwa na wanaume kwa viumbe hawa kwa kipindi cha miaka mingi tajwa huko nyuma, tangu maelezo katika vitabu vya dini na hata masimulizi ya mababu na mabibi, elimu iliyokuwa ikitolewa katika jando na unyago na ambayo bado inatolewa katika sherehe hizo kwa sasa.

  Bado haitoshi sana kuelezea hofu walizo nazo kuachana na wasaliti wao, ama kwa kudhani kuwa kamwe hawataweza kujisimamia wenyewe na badala yake tufumbue macho tuone sasa kwa nini wanahofu ya kuweza kusimama wao.

  Hebu anza kutizama minyororo hii kwa kuangalia mienendo ya baba na mama hapo ulipo kisha mtupie jicho mdogo wako wa kiume na wa kike hapo nyumbani kisha fikiri zaidi kwa kuichunguza nadharia inayotumika kuwavika watoto hawa wanawake na wanaume tarajiwa taswira ya namna ya kufikiri kwao na kuhusianisha uwezo wao kiasili na mienendo wanayotakiwa kuiishi.

  mazingira, mitazamo na matarajio ya jamii kwa wanawake yanawafanya wanawake kuendelea kuishi ndani ya hatari na wasaliti wao wakisubiri siku zao za kuishi kumalizika na wakapumzike salama. lakini kiukweli si ushujaa, siujasiri, siupendo, sihuruma na wala uanamke kuvumilia katika hali hiyo hatari.

  hebu tuwatake sasa wanawake waamke na wabadilike kwani naamini wakibadilika nasi twaweza kuanza kubadilika kwa kuacha kuwa wasaliti. Haipendezi na wala haivutii kudumu katika tabu na hasa za kujitakia.

 10. Isidory Matandula

  10/03/2013 at 11:17 pm

  Samahani dada nilikuwa nasoma zile sababu zinazowafanya wanawake waendelee kuishi na wanaume wanaowasaliti, nimefika namba 8 nimegundua namba 9 haipo, ni makosa ya uchapaji, au ndivyo ulikusudia iwe ?

 11. Joy

  30/05/2013 at 2:32 pm

  Kuna mtu aliwahi kusema ukitaka uwe na moyo wa kuvumilia usaliti wa mwanaume nawe saliti. Hiyo itakufanya uwe unareffer kwenye usaliti wako na kujipa moyo, "hakuna kipya hata mimi nafanya" .

   hahahaaaaa, good article. thanks for sharing

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Jamii

Hujavuka miaka 30? Unashauriwa kusafiri sana na kuhifadhi fedha kadiri uwezavyo!

Published

on

Kufikisha miaka 30 maishani yaweza kuwa kipindi cha mabadiliko makubwa kwenye maisha ya mtu na taaluma yake. Ni kipindi ambacho malengo ya wengi kitaaluma huanza kuwa wazi na shauku ya kufika sehemu fulani kimaendeleo huongezeka.

Yalifanyika mazungumzo na baadhi ya Maafisa Watendaji Wakuu wa makampuni mbalimbali kuhusu kipi wangependa wafanyakazi wao wawe wamefanya kabla ya kufikisha miaka 30. Haya ni baadhi ya maoni yao kuanzia kwenye suala la kutembelea sehemu mbalimbali, kuweka akiba ya fedha na hata kuanzisha biashara zao wenyewe:

Aaron Smith (Afisa Mtenda mkuu na mwanzilishi wa kampuni ya KX)

Kitu cha kwanza ninachopenda kuwashauri ni kutembelea sehemu mbalimbali duniani. Hakuna kitu kizuri kinachofungua macho kama kusafiri kwenda sehemu mbalimbali ili kupanua uelewa wako na kuboresha mbinu zako za mawasiliano kutoka kwa watu wengine wa tamaduni tofauti.

Uzoefu wa kidunia hauna gharama. Inakusaidia kufahamu mambo chanya kwenye ulimwengu halisi wa watu. Hadi kufikia umri wa miaka 25 nilikuwa nimeshatembelea nchi zaidi ya 40 na kuishi mbali na nyumbani kwa miaka 5. Kilikuwa kipindi kizuri sana.

Kuwa mbinafsi, jitoe kwa kila kitu na uishi maisha kadiri uwezavyo. Kabla ya kufikisha miaka 30 unakuwa huna majukumu makubwa na pengine huna hata familia ya kuitunza. Jitoe na tumia ulivyonavyo vyote ili upate maendeleo makubwa.

Wewe bado ni kijana mwenye nguvu nyingi, mwenye ushawishi na una muda mwingi wa kufanikiwa zaidi hata pale unaposhindwa unaweza kuanza tena na kufanikiwa maana huna cha kupoteza.

Aaron Smith katika moja ya semina zake

Kadiri umri unavyoongezeka ndivyo sababu za kutokufanya jambo fulani huongezeka na mwisho wa siku utakuja kujuta kwa kutokujaribu mapema. Nilipoteza akiba yangu yote ya fedha kwenye biashara nilipokuwa na umri wa miaka 18 na nikafanikiwa kwenye biashara ya pili nikiwa na umri wa miaka 26. Tambua kwamba utakosea huko mbele.

 

Taichi Hoshino (Afisa mtendaji wa Monetise).

Jenga tabia au maadili mazuri. Kuanzia kwenye matumizi mazuri ya muda, maadili ya kazi, kujiwekea mipaka ya kazi au maisha, mazoezi, kula vizuri au kuwa na nidhamu na fedha zako binafsi, maadili ndiyo msingi wako mkuu.

Pale unapokutana na mazingira yasiyotabirika kwenye maisha, maadili mazuri uliyojijengea kwa muda mrefu ndiyo yatakayokusaidia. Anza nayo mapema nayo yatakuwa nawe maisha yako yote.

Taichi Hoshino

 

Jo Burston (Mwanzilishi na Afisa mtendaji mkuu wa Inspiring Rare Birds).

Jifunze kukabiliana na kupanda na kushuka kimaisha. Watu wengi ninaokutana nao walio kwenye miaka ya 20 na kuendelea wako bize kuhangaika kuwasimamia wenzao wenye ujuzi mdogo, wakati ujuzi halisi ni kusimamia kutoka juu hadi kwa watu wenye ujuzi na uzoefu mkubwa. Ujuzi wa mazungumzo na kuzungumza mbele za watu utakupeleka kokote maishani.

Tambua kile unachokipenda na lenga kuwa bora duniani katika kile unachokifanya kupitia kuwa na kiu ya kujifunza zaidi kwa nadharia na kwa vitendo pia.

Tafuta mwalimu au mtu ambaye amewahi kupita kwenye njia unayotamani kuipita. Kuwa mbunifu, mwaminifu na heshimu muda unaoutumia pamoja naye. Anajifunza kutoka kwako pia.

Weka akiba ya kila pesa unayoipata. Jifunze kuweka akiba na utoke nyumbani kwenda kujitegemea mwenyewe. Hakuna mtu anayekudai hivyo achana na hisia kwamba kuna watu unawajibika kwao. Hilo sio jukumu lako.

Jitahidi uanzishe biashara hata kama ni ndogo. Utakapoweza kujifunza mbinu hizi mapema utajifunza namna ya kupata hasara kwa gharama ndogo. Msingi mzuri wa ujuzi wa biashara na fedha utakusaidia kufanikiwa baadaye.

Tembelea sehemu mbalimbali za ulimwengu itakusaidia kujikubali, kuwa na uvumilivu na kuwa jasiri na pia utaona jinsi dunia yetu ilivyo nzuri.

 

Dean Ramler (Mtendaji Mkuu na mwanzilishi mwenza wa Milan Direct)

Jifunze ubunifu wa kwenda mbali zaidi kwa kufanya zaidi ya kile unachotakiwa kufanya au zaidi ya kile unacholipwa kukifanya. Mfanyakazi wa kawaida hufanya kazi mpaka saa 11 jioni kwasababu huu ndiyo muda ambao muda wa kazi huisha. Kila mtu ana haki ya kufanya hivi.

Lakini kuna watu wachache wanaobaki nyuma kama mimi wenye malengo makubwa ambao wanafahamu thamani ya kwenda zaidi na kufanya zaidi ya kile wanacholipwa kukifanya na hawa mara nyingi huangalia namna ya kuzalisha zaidi kwa ajili ya kampuni.

Kama kiongozi mara nyingi utajikuta unawategemea wafanyakazi wachache wale ambao hufanya zaidi ya kile wanachotakiwa kukifanya, na huwa ni mazoea kuwaita hawa wachache kukusaidia kazi muhimu pale ambapo wengi wanakuwa wameshaondoka.

Na sio jambo la kushangaza kwamba hawa wachache mara nyingi ndiyo huja kuwa viongozi wa wenzao ndani ya kampuni, na ndiyo ambao hupandishwa vyeo na kuongezewa mishahara.

Dean Ramler

 

Philip Weinman ( Afisa Mtendaji Mkuu wa Locomote).

Anzisha biashara yako mwenyewe ukiwa bado unaishi nyumbani kwenu. Ni muda mzuri wa kujaribu mawazo mbalimbali ya kibiashara huku ukiwa huna gharama kubwa kimaisha. Tafuta mwalimu au mtu unayemuamini tofauti na ndugu yako ambaye atakushauri na asiwe na malengo ya kufaidika kifedha kutoka kwako.

Katika kipindi hiki utajifunza zaidi kupitia makosa unayoyafanya na pale itakapotokea ukafanya maamuzi ya kutoka nyumbani tayari utakuwa unajua kipi kinaleta faida na kipi hakileti faida. Pamoja na kupata uzoefu kwenye biashara, pia utajifunza kufanya maamuzi na kuyasimamia.

Philip Weinman

 

Christian Mischler (Afisa Mwendeshaji na mwanzilishi mwenza wa Hoteli ya Quickly).

Tembelea sehemu mbalimbali ulimwenguni! Tembelea maeneo mbalimbali na tamaduni tofauti, husaidia kukujengea hali ya kujitegemea na itakupa uzoefu wenye madhara chanya ambao ni wa muda mrefu maishani mwako mwote.

 

John Winning (Afisa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Winning Group).

Ongeza uzoefu kwa kadiri utakavyoweza – ni jambo la muhimu sana kuwa na uzoefu wa aina nyingi kwenye maisha na kwenye kazi pia. Jitahidi kufanya kazi sehemu mbalimbali ikiwemo viwandani au kwenye shule hata kama ni kazi za muda mfupi au za masaa machache. Mimi niliendesha magari ya mizigo, nilifanya kazi ya kusambaza bidhaa majumbani na pia kwenye maduka ya kuuza bidhaa.

Kuwa na uhakika wa kupata elimu zaidi itakayokuvutia. Sio lazima iwe kutoka chuoni lakini hata kwenye kusoma vitabu maana ni vizuri kuwa na shauku ya kujifunza zaidi, na shauku ni motisha nzuri. Sikwenda kusoma chuoni baada ya kumaliza shule lakini miaka iliyofuata ilitengeneza namna au jinsi ninavyofanya kazi na jinsi biashara yangu inavyokwenda.

Kutoka kwenye biashara ya rejareja, mpaka mafanikio binafsi hadi kupata tuzo ya dunia, kumeimarisha sana fikra zangu na uwezo wa kukabiliana na vikwazo na kukamata fursa nyingi kwenye biashara.

John Winning

 

Zach Johnson (Afisa Mtendaji Mkuu wa atmail.com).

Ishi maisha kwa kiwango kikubwa kwa kadiri unavyoweza na pokea kila uzoefu unaoupata pale unapokuja – Yote na kamili.

 Zach Johnson 

 

Charlie Wood (Meneja Mkuu wa Dropbox)

Nashauri watu wapate uzoefu wa miaka kadhaa kutoka kwenye makampuni makubwa hasa wakiwa kwenye kipindi cha miaka 20. Uzoefu ambao wataupata kutoka kwenye makampuni haya utawajenga katika kufanikiwa hapo baadaye.

Wale ambao ni wafanyabiashara kwa asili ni vizuri watimize ndoto zao na kuyaweka mawazo yao kwenye vitendo kwa kuanzisha biashara zao wenyewe au kwa kushirikiana na watu wachache.

Moja ya jambo muhimu ambalo mtu anatakiwa kulifanya kabla ya kufika miaka 30 ni kusafiri kwenye sehemu mbalimbali ulimwenguni, kukutana na watu tofauti na kutengeneza maisha mapya. Uzoefu huu utapanua uelewa wa mtu na kumsaidia kujipanga kwa ajili ya kipindi cha miaka 30.

 

Bevan Nel (Mkurugenzi Mtendaji wa Helping).

Kuwa na nidhamu katika matumizi yako ya fedha, weka bajeti na uifuate!

Pili, kama unataka kufanya biashara, jitahidi uifanye kabla hujaoa/kuolewa na kuwa na watoto na familia. Utakuwa muoga sana na hutakuwa na uthubutu wa kutosha pale tu utakapoanza kuwa na familia na maendeleo ni ya muhimu sana kuanzia mwanzo wa taaluma yako.

Mwisho kabisa, ni vizuri kuendeleza mawasiliano na wafanyabiashara au wateja wako wa zamani. Tunza mawasiliano yao, fanya vyovyote inavyowezekana ili kutunza mawasiliano yako siku zote. Mawasiliano ni muhimu maana hujui ni wakati gani utahitaji msaada kutoka kwa mtu fulani.

Kwa mtazamo usio wa kibiashara….safiri…safiri…safiri! Hiki ndicho ninachowaambia vijana. Kusafiri ni jambo zuri katika kukujengea ujasiri, kukutana na watu wa kufanya nao biashara na pia ni njia nzur ya kujiburudisha na kuamsha mwili na akili.

Bevan Nel

 

Kevin Lynch (Afisa Kiongozi wa Masoko wa Open Colleges).

1. Jifunze kutoka kwa wenzako: Kadiri tunavyozidi kukua katika taaluma zetu kwenye miaka 20 na kuendelea tunahitaji kujifunza sio tu kwa wale waliotuzidi, bali hata kutoka kwa wale tulionao kwenye ngazi moja. Hii itakuhakikishia ujenzi wa msingi imara kwa ajili ya miaka ya 30.

Najifunza sana kutoka kwa wenzangu, watu ambao wananizunguka. Hawa ndio watu wanaofanya mambo yanaenda, ni waerevu zaidi yangu. Watu wanaotuzunguka ndio wanaofanya tuwe tulivyo.

Tunajitahidi kuhakikisha kwamba tunaendeleza utamaduni uliopo na kuhakikisha panakuwa mahali salama kwa wafanyakazi wetu kutimiza majukumu yao, mahali ambapo watu wanaamini maono ya kampuni katika kubadilisha maisha ya watu kupitia elimu.

           Kevin Lynch

 

Nicholas Smedley (Mkurugenzi Mtendaji wa Steller).

Kwa kuwa tupo kwenye biashara ya kuuza na kupangisha nyumba, vyumba na viwanja nafikiri ni muhimu kwa wafanyakazi wetu kulielewa soko. Hakuna njia nzuri zaidi ya ile ya kuingia kwenye soko sahihi.

Ushauri ni anza kuweka akiba mapema kadiri unavyoweza – haijalishi kama ni kupitia hisa au kufanya uwekezaji wa aina nyingi. Hakuna kitu bora zaidi kuliko riba mchanganyiko. Hii itakuingiza kwenye uwanja wa ufahamu wa kuweka akiba na kukuwezesha kununua rasilimali yako ya kwanza kabla ya kufikisha miaka 30 ambao utakuwa ni mwanzo mzuri.

                 Nicholas Smedley

 

Levi Aron ( Meneja wa Yumtable).

Chukua muda tulivu kuweka malengo mapema kabla ya kuanza, yafuatilie na pambana kuyatimiza. Siku zote kumbuka kujipongeza kila unapofanikiwa kufikia hatua fulani. Ni vizuri kujipongeza wewe binafsi. Fanya kazi kwa bidii kukabiliana na vikwazo lakini usisahau kujipongeza na kupumzika kila inapowezekana.

Kumbuka, pasipo na malengo = hakuna jitihada = maisha ya kawaida/chini, Ni nani anataka maisha ya hivyo?

Continue Reading

Jamii

Siri iliyofichika mauaji ya wanandoa nchini

Published

on

Hivi karibuni tumeshuhudia matukio kadhaa ya vifo kwa wanandoa, aidha mume kumuua mke wake au mke kumuua mume wake.

Ni matukio ya kusikitisha ambayo yameripotiwa sehemu mbalimbali Tanzania ikiwemo Mkuranga, Pwani, Dodoma and Tabora. Mauaji haya yamezua maswali mengi huku kila mmoja akitoa tafsiri yake kwa namna anavyoiona hali.

Nimesikiliza maoni ya watu mbalimbali wakijaribu kudadavua ni kitu gani kimetokea mpaka vifo hivi vimetokea; maoni mengi yamekuwa ni kukosa hofu ya Mungu na wengine wakiamini ni nguvu za kishirikina.

Ningependa kutoa maelezo ya kitaalamu kwa nini matukio haya hutokea na nini kifanyike kuzuia aina hii ya matukio kutokea katika ndoa zetu.

Nianze kwa kusema taaluma yangu ni sayansi ya jamii ambayo nimejikita katika Saikolojia ya Binadamu (Human Psychology) na Ushauri Nasihi (Counseling). Naamini kwa taaluma hii niko sehemu sahihi kueleza tatizo hili.

Mauaji kwa wanandoa sio swala jipya duniani na pia linatokea kwa kiwango kikubwa kila mwaka. Dk. Aaron Ben-Zeeve katika kitabu chake In the Name of Love: Romantic Ideology and its Victims cha mwaka 2008 anaeleza kuwa takriban asilimia 40 ya wanawake huuawa na waume zao na asilimia 6 ya wanaume huuawa na wake zao kila mwaka duniani.

Takwimu hizo zinadhihirisha wazi kuwa tatizo kubwa liko kwa wanaume kuliko wanawake. Sababu zifuatazo zinaweza kueleza chanzo cha tatizo hili:

Niweke wazi kwamba, sababu za mauaji kutokea ni mchanganyiko wa mambo mengi kwa wakati mmoja, hivyo sababu nitakazozieleza hapa hazina maana ndiyo hizo tu bali zitatoa mwanga kwanini tatizo hutokea.

Nikianza kwasababu za kijamii, makuzi ya watoto wa kiume na watoto wa kike ni tofauti sana karibu jamii zote duniani. Jamii nyingi duniani humkuza mtoto wa kiume na kumfanya kujua yeye ni shujaa, mlinzi na kuwa yuko juu ya mwanamke.

Wanaume wengi tunajiona wajasiri, wenye nguvu na wanawake wako chini yetu hivyo tunaweza kufanya lolote kwao.

                                    Wanaume wengi tunajiona wajasiri, wenye nguvu na wanawake wako chini yetu

Makuzi haya ya jamii yanakwenda moja kwa moja kushawishi saikolojia ya mwanaume, hata katika ndoa. Mwanaume huonesha nguvu zake kwa mwanamke (Masculinity). Hivyo kunakuwa na mpaka baina ya mwanamke na mwanaume.

Hapa tunashuhudia matukio ya mara kwa mara ya wanaume kupiga wake zao kila kukicha. Hii halitokei bahati mbaya kwani makuzi ya jamii yameshawishi saikolojia ya mwanaume na kumfanya mwenye nguvu na anaweza kusahihisha kosa la mwanamke kwa kutumia nguvu na sio mjadala au mazungumzo.

Mjadala kwa wanaume ni dalili ya udhaifu na hii ni dalili ya kuwa na matatizo ya kisaikolojia.

Nitoe mfano mdogo tu, binti mwenye umri wa miaka 21 akitaka kwenda dukani usiku anaogopa sana, ila akisindikizwa na mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 7 anajisikia amani kabisa na uoga hutoweka.

Saikolojia hii inaruhusu amani kwenye mwili wako kwa kuwa tayari mapokeo ya jamii yamekuaminisha kuwa mwanaume ni mwenye nguvu na mlinzi.

Nikigeukia katika upande wa pili wa saikolojia unaochangia vifo kwa wanandoa. Binadamu wote tumeumbwa na nafsi mbili (personality) ambazo ni nafsi imara (strong personality) na nafsi dhaifu (weak personality).

Mtu mwenye nafsi imara ni yule anayeweza kupata msukosuko katika maisha, akaumia ila asikate tamaa akakubali mabadiliko na kuwa tayari kuishi nayo na kufanya vyema zaidi hapo mbele.

Lakini mtu mwenye nafsi dhaifu ni yule anayepitia msukosuko akaumia, akakata tama, akashindwa kuishi na mabadiliko na kuona hakuna namna ya kuendelea kuishi na mabadiliko hayo.

Wengi wetu tumepita huko na tunazidi kupita katika hizi nafsi mbili. Kwa maelezo hayo wanaume wengi wanaoishia kuwauwa wanawake zao mara nyingi wanakuwa na nafsi dhaifu ambazo huwaonyesha wako katika hali mbaya na hawawezi kutoka hapo walipo.

Wivu wa mapenzi ni sababu ya mauaji ya wanandoa

Nafsi hii hujidhihirisha kwa mapenzi waliyonayo kwa mwanamke husika kwamba ni mazito mno hivyo yanawapelekea wafanye vitu vya hatari.

Tafiti nyingi za saikolojia zinaonesha wale wanaowauwa wake zao husikika wakisema; nilimpenda sana huyu mwanamke kaniumiza, ama yeye ndio alikuwa nuru ya maisha yangu, kaififisha, ama wengine husema ni kwa sababu ya mapenzi ndio maana nimefanya haya.

Japo utetezi wa mapenzi hapo juu haukubaliki kisaikolojia ila tafiti zinaonesha nafsi dhaifu inayoandamwa na msongo wa mawazo wa muda mrefu humfanya mtu kupanga tukio la mauaji kwa kuwa haoni kama kuna njia mbadala zaidi ya kifo.

Kwa ufafanuzi zaidi, msongo wa mawazo (stress) hutokana na hali ya mazingira yanayokuzunguka kutokuendana na matarajio ya ubongo wako. Mfano, ulitegemea mpenzi wako ni mwaminifu (hali ya ubongo wako) ila ukamkuta na mtu mwingine (hali ya mazingira) hapo msongo wa mawazo hutokea kwani hakuna usawa baina ya ubongo na mazingira yako.

Kwa mantiki hii ni kwamba, kuweza kuwa na nafsi imara ni lazima tujifunze namna ya kufanya hivyo kwa kuwaona wataalamu wa saikolojia na ushauri nasahi. Ama wakati mwingine, kuzungumza na watu wenye uzoefu na jambo ambalo unalipitia kama vile wabobezi katika maswala ya ndoa, biashara, elimu na mengineyo.

Mantiki hapa ni kwamba, wakati mwanadamu anapokuwa na tatizo lazima apate suluhisho, sasa kwenye suluhisho hapo maamuzi ndipo hutofautiana kwa wengine huona ni mwisho wa dunia na wengine huona mwanga mwisho wa safari.

Nini kifanyike katika hali kama hii? Nitaeleza kwa uchache japo suluhisho linaweza kuwa la aina mbalimbali, ila kitaalamu ningeshauri tufanye hili:

Ndoa ni taasisi kama ilivyo taasisi nyingine, inahitaji ujuzi, uvumilivu, utashi na uelewa. Misukosuko ya ndoa ni mikubwa kwa kuwa inahusisha hisia hivyo hata namna ya kuitatua inahitaji hisia imara hususani nafsi imara kuweza kuliendea tatizo kwa umakini.

Kitu kikubwa ambacho tunaweza kufanya kama wanandoa, tujenge tabia endapo matatizo yanakuwa makubwa tuende kuwaona wataalamu wa ushauri nasahi ama wanasaikolojia ambao wamefunzwa namna ya kufanya kazi na msongo wa hisia (Emotional Stress).

Wataalamu hawa hutoa maelekezo ambayo yanaweza kumjenga mtu na kufanya nafsi dhaifu kuwa imara.

Kwa wale ambao wanaona ni gharama kwenda kwa wataalamu wa saikolojia na ushauri nasahi waende kwa wanandoa wakongwe waliokaa kwenye ndoa kwa muda mrefu wanaweza kuzungumza na kuweza kumfanya mtu aone kuna mwanga mwisho wa safari badala ya kukata tamaa na kuchukua maamuzi magumu ya kumuua mwenzi wako.

Nihitimishe kwa kusema, saikolojia ya mwanadamu yeyote yule inahitaji matunzo na matibabu ya mara kwa mara kama vile mwili wa binadamu unavyokwenda kwa tabibu kupimwa na kupatiwa dawa. Wengi wetu hupuuza umuhimu huu na mwishowe tunatenda mambo mabaya bila kujua tu wagonjwa.

Continue Reading

Jamii

Jinsi ya kukabiliana na athari za kiafya za kukaa muda mrefu

Published

on

Imethibitishwa bila shaka kwamba kukaa muda mrefu kwenye magari, ofisini au kwenye viti kunasababisha matokeo hasi kwa afya.  Tabia hiyo ya kukaa muda mrefu inahusishwa na kupata uzito uliopitiliza, magonjwa ya moyo, kisukari na magonjwa mengine yasiyoambukiza.

Lakini utafiti mpya uliotolewa hivi karibuni, unatoa hamasa kwamba baadhi ya shughuli za mwili ikiwemo njia rahisi za kuimarisha misuli zinaweza kumsaidia mtu kukabiliana na athari za kiafya za kukaa muda mrefu.

Katika utafiti huo uliochapishwa kwenye jalida la BMC Medicine, watafiti wakiongozwa na Carlos Celis-Morales kutoka Chuo Kikuu cha Glasgow walichambua data za watu 400,000 wenye umri wa kati nchini Uingereza.

Watafiti hao walifanya ulinganifu wa ripoti za watu waliofanya  shughuli za mwili kama mazoezi na muda waliotumia kuangalia runinga au kompyuta. Ili kupata  vipimo halisi vya mazoezi waliyofanya watu hao, wanasayansi walifanya jaribio la uwezo wa kushika vitu ambapo watu walibana kifaa maalum kupima nguvu ya misuli.

Celis-Morales anasema jaribio la misuli ni rahisi kwasababu linasaidia kufahamu kwa kiasi gani mtu  yuko hai na nguvu ya misuli yake kuhimili mabadiliko ya mwili wakati amekaa.

Wamebaini kuwa watu ambao wana misuli dhaifu wana uwezekano wa asilimia 31 ya kufa mapema kama watatumia saa mbili mbele ya runinga, ukilinganisha na watu wenye misuli imara ambao wanatumia muda kama huo. Pia watu hao wana hatari kwa asilimia 21 kupata magonjwa ya moyo na 14% kupata kansa ukilinganisha na wale wenye misuli imara.

 Kukaa muda mrefu ni hatari kwa afya yako

Kwa muktadha huo, kwa kila masaa 2 ambayo watu wenye misuli dhaifu wanatumia mbele ya runinga au kompyuta, hatari ya kufa kwasababu yoyote inaongezeka mara mbili kuliko wale wenye misuli imara.

Habari njema ni kwamba nguvu ya misuli inaweza kuimarishwa kwa mafunzo ya kupunguza uzito na kufanya mazoezi ya mwili, amesema Celis-Morales. “Ujumbe wa jumla ni kwamba haijalishi kwa muda gani umekaa au kuangalia runinga hata kama uko imara na hai kimwili,” amesema. “Ikiwa utatembea, kusimama na kujinyoosha hautapata athari sawasawa na mtu ambaye amekaa muda wote bila kupasha misuli.”

Ni muhimu kufahamu kwamba kukaa muda mrefu sio jambo jema kiafya, amesema; ukilinganisha na watu ambao hawakaii muda mrefu. Watu ambao ni wavivu wana viwango vya juu kupata magonjwa na kufa mapema. Lakini kwa wale ambao wanakaa muda mrefu na kuwa hai wanaweza kupunguza athari za kiafya.

Hata hivyo, hilo sio kosa letu. Kadiri tunavyoondoka kwenye mtindo wa maisha ya zamani ya kilimo na kuingia kwenye shughuli za ofisini na usafiri wa kisasa hadi kwenye mfumo wa kila siku wa maisha, chakula, kazi na burudani tunajenga kipaombele kimoja kwenye akili; faraja. Wazee wetu walitumia muda wao mwingi kutembea, lakini maisha ya kisasa yanakulazimisha kukaa kukaa muda mrefu.

Lakini bado tuna wajibu wa kufanya kuhakikisha miili yetu inaendelea kuwa hai na kuepukana na magonjwa yasiyo ya lazima.

Continue Reading

Muhimu Kusoma

Copyright © 2018 FikraPevu.com