Kilimo cha kisasa cha kumkomboa mwanamke kiuchumi

   Nafasi ya mwanamke kukuza kilimo Tanzania

Serikali ya Tanzania katika sera na mipango yake mbalimbali inatambua kuwa usawa wa kijinsia na kumuwezesha mwanamke ni silaha muhimu ya kuondokana na umasikini na kuihakikishia jamii maendeleo endelevu. 

Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na Sera ya  Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000 zote kwa pamoja zinasisitiza umuhimu wa kumthamini na kumuwezesha mwanamke katika sekta zote za maendeleo.

Licha ya hatua kubwa iliyofikiwa na serikali na mashirika ya kimataifa katika kuendeleza usawa wa kijinsia katika shughuli za kimaendeleo bado idadi kubwa ya wanawake hawako katika sekta rasmi huku mashirika ya hifadhi ya jamii yakiongoza kuajiri wanawake wachache nchini Tanzania.

Wanaume wanaonekana kuendelea kushikilia nafasi nyingi katika sekta rasmi ikilinganishwa na wanawake ambao wengi wao wako katika sekta isiyo rasmi. Elimu imekuwa ni sababu kubwa inayopelekea utofauti mkubwa wa ajira, ambapo fursa kwa wanawake kupata elimu sawa na wanaume imekuwa changamoto jambo linalorudisha nyuma jitihada za kumkomboa mwanamke.

Ripoti ya Utafiti wa Nguvu Kazi Jumuishi (Integrated Labour Force Survey, 2014) inaeleza kuwa  mashirika ya hifadhi ya jamii yameajiri asilimia 18 tu ya wanawake, ambapo ni sawa na wanawake 2 kati ya 10 ambao wameajiriwa katika sekta nyingine.

Sekta hiyo ya hifadhi ya jamii inaajiri mara 5 zaidi wanaume kuliko wanawake. Kuna wanawake wachache katika sekta zinazoonekana kuwa ni rasmi, tofauti na hapo wanawake wengi wameajiriwa au kujiajiri katika sekta isiyo rasmi hasa biashara ndogo ndogo na kazi za nyumbani.

Sekta binafsi ikijumuisha mashirika yasiyo ya kiserikali imeajiri wanawake kwa 28% ikifuatiwa na serikali ambayo ina wanawake wanaofikia 42% ambapo kwa kila wafanyakazi 1000 waliopo serikalini kuna wanawake 261.

 

Serikali na mashirikali yasiyo ya kiserikali bado yana safari ndefu kuthamini uwezo wa wanawake na kuwapa nafasi kufanya maamuzi sahihi ya kazi. Sababu kubwa ya sekta rasmi kuwaacha wanawake ni dhana ya mfumo dume ambayo bado imetawala katika maeneo mbalimbali.

Baadhi ya mila na desturi zetu zinamchukulia mwanamke ni mtu wa kukaa nyumbani kulea watoto na kufanya shughuli ndogo ndogo. Na wazazi wengine hawawapeleki watoto wa kike shuleni na kuwalizimisha kuolewa ili familia ipate utajiri.

Licha ya sekta rasmi kutoajiri wanawake bado wanawake wanaongoza kuajiriwa katika sekta ya kilimo ikilinganishwa na wanaume. Kwa miaka mingi sasa wanawake wameendelea kuwa wazalishaji wakubwa wa mazao lakini wengi wao hawalimi kilimo cha kisasa ambacho kingeweza kuwapatia maslahi ya kutosha kuendesha familia zao.

Kwa mujibu wa ripoti ya ILFS, Kilimo kinaongoza kuajiri wanawake kwa 52% ambapo haitofautiani sana na wanaume kwa 48% na kuwafanya wanawake kuwa sehemu muhimu  ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara nchini.

Kilimo chao kimeegemea kuzalisha mazao ya chakula na kwa sehemu mazao ya biashara. Na fedha inayopatikana hutumika kulisha familia na kusomesha watoto.

Changamoto nyingine ni kukosa elimu ya kilimo na teknolojia ya kuzalisha mazao ya biashara ili kuweza kuingia kwenye ushindani wa soko la kimataifa. Na wakati mwingine wanaume huwa na maamuzi ya juu kuhusu mapato yatokanayo na kilimo na kuwaacha wanawake katika hali duni.

Kulingana na takwimu za Umoja wa nchi Afrika (AU-2017) zinaeleza kuwa wanawake katika nchi zinazoendelea wanachangia 43% ya nguvu kazi yote katika sekta ya kilimo. Ushahidi unaonyesha kuwa kama wanawake wakipata vitendea kazi vya uzalishaji kama wanaume, wanaweza kuongeza mavuno kwa asilimia 20 hadi 30, ambapo wataweza kupunguza idadi ya watu wenye njaa duniani kwa 12% hadi 17%.

 

 

Ili sekta ya kilimo iendelee na kustawi inategemea uwepo wa viwanda vyenye uwezo wa kutumia malighafi za kilimo kuzalisha bidhaa mbalimbali. Viwanda vingi nchini havifanyi kazi na hata vilivyopo havina mchango mkubwa katika kuendeleza kilimo ambacho hutegemewa na wanawake kama eneo muhimu kwa wao kujikomboa kimaisha.

Kutokana na kuwepo kwa pengo kubwa katika ya mwanaume na mwanamke katika ajira (gender disparity) imepelekea kuwepo kwa tofauti ya kipato, ambapo wanaume hupata kipato kikubwa kuliko wanawake.

Serikali inakiri kuwa bado viwanda havifanyi vizuri kuinua kilimo na jitihada mbalimbali zinafanyika ili kuinua sekta hiyo. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage akizungumza na vyombo vya habari mwezi Agosti 2016, alisema nia ya serikali ni kufufua viwanda vya ndani ili kutengeneza ajira nyingi, ambapo kwa sasa Tanzania ina viwanda zaidi ya 52,000 vinavyofanya kazi na 197 vimetelekezwa baada ya wenye viwanda kushindwa kuviendeleza.

Juhudi za kumuwezesha mwanamke

Akizungumza kwenye semina ya wajasiriamali hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Namaingo Business Agency, Biubwa Ibrahim, anasema wanawake wasikate tama bali waendelee na juhudi za uzalishaji mali na kupigania haki zao.

“Lazima muwe wabunifu, halafu ni dhambi kubwa kukata tamaa bali mnatakiwa kuongeza jitihada katika miradi yenu,” amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Jinsia Chuo Kikuu Cha Dar es salaam, Dkt. Eugenia J. Kafanabo anasema mila na desturi zetu pamoja na wanawake kukosa nguvu ya maamuzi katika jamii ndio sababu kuu ya wao kuachwa nyuma katika sekta rasmi.

Anasisitiza kuwa ni vyema kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili ibadilike na kuthamini mchango wa mwanamke katika maendeleo. Pia kuwaelimisha wanawake wengi zaidi kuchukua hatua kujikwamua katika mfumo dume ambao umekuwa ukiwakandamiza.

 “Unyanyasaji wa wanawake unaendelea chini kwa chini na umekita mizizi katika jamii yetu, kwa hiyo elimu iendelee kutolewa kwa watu ili mtu mmoja mmoja abadilike”

Hata hivyo serikali imeshauriwa kufanya mabadiliko ya kisera na sheria ili kumuwezesha mwanamke kushiriki kikamilifu katika maendeleo na kuwa na maamuzi juu ya rasilimali za nchi.  ikiwemo kufaidika na kilimo.

 

 

 

 

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Polisi kuwalinda wanaoshambuliwa na wananchi ili kupunguza vifo vinavyotokana na uhalifu

 Ili kupungu za vifo vinavyotokana na uhalifu nchini, Jeshi la Polisi limesema litawalinda wahalifu ...

Ruvuma: Samaki, dagaa wa Ziwa Nyasa sasa hawakamatiki sokoni

SAMAKI na dagaa kutoka Ziwa Nyasa wameadimika. Kuwala imekua kama anasa, kwani, licha kutopatikana ...