Kesi namba 458 inayoikabili JamiiForums yapata Hakimu na Wakili mpya. Kusikilizwa tena Machi 26 mwaka huu

Kesi namba 458 ya mwaka 2016 imehamishiwa kwa Hakimu Huruma Shaidi baada ya Hakimu Victoria Nongwa ambaye alikuwa anasikiliza kesi hiyo kukabidhiwa majukumu mengine katika Idara mpya ya Usimamizi wa Mtiririko wa Kesi za mahakama.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Wakurugenzi wa mtandao huo ambao ni Maxence Melo na Micke William wanadaiwa kuendesha mtandao (JamiiForums.com)  bila kuwa na Kikoa cha .TZ (Tanzania Domain) kwa maana kwamba mtandao wa JamiiForums haujasajiliwa nchini .

Kesi hiyo ambayo imetajwa leo tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam ambapo mabadiliko hayo ya Mahakimu yamefanyika ili kuruhusu shauri hilo kuendelea kusikiliza na hatimaye kutolewa uamuzi. Kuanzia sasa kesi hiyo itasimamiwa na Hakimu Huruma Shaidi.

Hata hivyo, ilitegemewa kesi hiyo ingeendelea kusikilizwa leo kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri kutoa ushahidi lakini ilikuwa tofauti baada ya upande huo kumpendekeza Wakili Mpya, Clara Charwe  badala ya wakili Batilda Mushi ambaye amekuwa akiwakilisha Jamhuri hapo mwanzoni. 

Baada ya Wakili Clara Charwe kukabidhiwa jukumu hilo amesema hakuwa na ufahamu mzuri wa faili la shauri la mashataka na kuomba apatiwe muda wa kulipitia na kukumbushwa rekodi za mahakama juu ya shauri hilo ndipo aendelee kusimama upande wa Jamhuri.

                                                               Hati ya awali ya Mashtaka

Awali, shauri hilo wakati linaanza kusikilizwa mwaka 2016 lilikuwa chini ya Wakili Salum Mohammed ambaye baadaye alimkabidhi Wakili Mutalemwa Kishenyi. Kutokana na majukumu mengine ya kikazi shauri hilo lilienda mikononi mwa Wakili Batilda Mushi ambaye leo amejitoa na kumpisha wakili mwingine, Clara Charwe.

Kesi hiyo imeahirishwa mara kadhaa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mashaidi wa Jamhuri kutofika mahakamani na muingiliano wa ratiba za mahakama.

Ikumbukwe kuwa mara ya mwisho wakati wa ahirisho la shauri hilo Februari 20 mwaka huu, Hakimu Nongwa alisema lilikuwa ni ahirisho la mwisho na kuwataka Jamhuri kumaliza kuleta mashahidi wao ili hatua nyingine zifuate.

Pia alitoa angalizo kuwa inawezekana  upande wa Jamhuri wanataka  washtakiwa waendelee kuwa na kesi mahakamani kwa kuwa kila mara wanaahirisha kesi kwa kisingizio cha kukosa mashahidi na hata wakiwa na mashahidi wanaairisha kwa kisingizio cha kuwa ‘busy’ na kesi nyingi zinazoingiliana.

Kesi hiyo imeahirishwa na itasikilizwa tena Machi 5 mwaka huu chini ya Hakimu mpya Huruma Shaidi ambapo upande wa Jamhuri utawakilishwa na Wakili Clara Charwe na upande wa utetezi atakuwa Jeremiah Mtobesya.

Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Maxence Melo (katikati) akimsikiliza kwa makini Wakili Jeremiah Mtobesya (kushoto) akiwa na Micke William (kulia) muda mfupi kabla ya kusikilizwa kwa kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam leo

 

Kesi nyingine mbili dhidi ya JamiiForums nazo zatajwa

Wakati huo huo, kesi zingine mbili ambazo zinaikabili JamiiForums zimetajwa na kusikilizwa leo katika mahakama hiyo na kuahirishwa hadi wakati mwingine.

Katika kesi  456 inayoikabili JamiiForums kuhusu kampuni ya Oilcom inayodaiwa kukwepa kodi na uchakachuaji wa mafuta katika bandari ya Dar es Saalam  imetajwa tena leo mbele ya Hakimu Thomas Simba.

Hata hivyo, shauri hilo limehirishwa mpaka  Aprili 09, 2018 baada ya Hakimu Simba kusema kuwa hajamaliza kuandika uamuzi mdogo (ruling) kutokana na kupata safari ya ghafla ambapo siku hiyo kesi itasikilizwa kuanzia saa 4:00 asubuhi na amewataka mawakili wa Jamhuri kuwapeleka mashahidi wao wote waliobaki ili watoe ushahidi wao.

Katika kesi nyingine namba 457 ya mwaka 2016 kuhusu kampuni za CUSNA Investment na Oceanic Link ambazo zilidaiwa kufoji nyaraka bandarini, kukwepa kodi na kuwatesa wafanyakazi wazalendo na kupendelea wageni toka nje ya nchi imesikilizwa tena leo katika Mahakama ya Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Godfrey Mwambapa.

Wakati kesi hiyo ikianza Wakili wa Jamhuri, Batilda Mushi ameiomba mahakama impatie muda wa kulipitia upya jalada la kesi na ushahidi uliotolewa na kuwa atakamiilisha mapitio hayo Machi 26, 2018.

Hakimu Godfrey alitoa nafasi kwa wakili wa utetezi, Jeremiah Mtobesya ambapo aliiambia mahakama kuwa wameafiki ombi la upande wa Jamhuri kufanya mapitio ya shauri lakini ameiomba mahakama kukamilisha kesi hiyo kwa wakati kwasababu imekaa muda mrefu bila kufikia hitimisho la kutolewa hukumu.

Kwa upande wake, Hakimu Mwambapa baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili alikubali maombi ya Jamhuri na kuahirisha kesi hiyo mpaka Machi 26 mwaka huu ambapo itasikilizwa tena.

Ikumbukwe kuwa mahakama hiyo ilitoa angalizo kwa Jamhuri kukamilisha ushahidi wao na kwamba aihirisho la mwisho lilikuwa Machi 1, 2018 ambapo kesi hiyo ilitakiwa kusikilizwa lakini ilisogezwa mbele hadi leo.

Mnamo Disemba 9, 2016 Maxence Melo alikamatwa na polisi katika ofisi za JamiiForums zilizopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam na kufikishwa katika Mahakama Mkazi Kisutu Disemba 13, 2016 na mwenzake Micke William wakikabiliwa na mashtaka ya kukataa kutoa ushirikiano kwa Polisi ili wasaidie kupatikana kwa taaarifa za watumiaji wa mtandao wa JamiiForums, katika upepelezi wa majalada 2 ya uchunguzi yaliyofunguliwa na kampuni ya Oilcom na CUSNA Investment na Oceanic Link yakidai yamechafuliwa.

Shtaka la 3 ni kuendesha mtandao wa JamiiForums bila kutumia kikoa cha .TZ ambacho kina usajili wa Tanzania.

Hata hivyo, kesi zote tatu zinaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa nyakati tofauti. Kufuatilia mwenendo wa kesi hizo tangu zilivyoanza, ingia hapa

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Mwangosi Killing: Commander Kamuhanda acted illegally says Commission

The brutal killing of a Tanzanian journalist Daud Mwangosi earlier in September this year ...

Walimu wapya wa sekondari Mwanza wazua kizaazaa ofisi za Jiji

WALIMU wapya wa Shule za Sekondari Jijini Mwanza, wamelazimika kuacha kufundisha wanafunzi darasani kwa ...

Nadharia kinzani za mfumo wa chama kimoja, vyama vingi na Tanzania tuitakayo

Mwaka 1964, Serikali iliyokuwa ikiongozwa na chama cha TANU iliamua kupiga marufuku mfumo wa ...