Katavi: Zahanati nyingi zakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba, vitanda vya kujifungulia

WAKATI dunia ikiwa katika miaka ya mwanzo ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), huenda bado ipo haja ya kutazama upya utekelezwaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs).

Awamu zote za malengo hayo ziliandaliwa na Umoja wa Mataifa ili kuweka kipindi maalumu katika kupambana na matatizo mbalimbali yanayosababisha umasikini na vifo duniani.

FikraPevu inafahamu kwamba, utekelezaji wa MDGs ulikamilika mwaka 2015 huku ukitarajiwa kuwa umeboresha afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kila namna katika maeneo mbalimbali duniani, Afrika ikiwa ndiyo yenye mzigo mkubwa zaidi.

Mara baada ya kukamilika kwa muda wa utekelezwaji wa MDGs, malengo hayo yalirithiwa na SDGs huku Lengo Namba Tatu likiwa ni ‘kupatikana kwa huduma bora ya afya kwa kila mtu, popote alipo’.

Kitanda kinachotumika kwa ajili ya akina mama wajawazito kujifungulia katika Zahanati ya Kakese ambapo baadhi ya kina mama wanalazimika kwenda kujifungulia majumbani kutokana na Zahanati hiyo kuwa na kitanda kimoja tu.

 

Kwa bahati mbaya, FikraPevu imebaini kwamba, hali ya upatikanaji wa huduma ya afya, hasa ya mama na mtoto, mkoani Katavi bado si ya kuridhisha.

Takriban kilometa 15 tu kutoka Makao Makuu ya Mkoa wa Katavi yaliyopo mjini Mpanda, ipo Kata ya Kakese, ambayo ni maarufu kutokana na shughuli za kibiashara.

Pamoja na kipato cha kuridhisha walicho nacho wakazi wa Kakese, bado huduma ya afya si nzuri na FikraPevu imeshuhudia wajawazito kadhaa wakilazimika kujifungulia majumbani. Kisa? Zahanati ya eneo hilo ina kitanda kimoja tu maalum kwa uzazi.

Magdalena John ni mmoja wa akina mama wa eneo hilo aliyezungumza na FikraPevu na kuthibitisha kuwepo kwa tatizo hilo katika Kata ya Kakese.

“Ikitokea wazazi wawili wakaja kwa wakati mmoja, hakika atakayepata huduma stahiki ni yule mwenye bahati. Kitanda ni kimoja kwa ajili ya mama mmoja, hii ni aibu na majanga kwetu akina mama,” anasema Magdalena kwa uchungu.

FikraPevu imeelezwa kwamba, mara nyingi ushauri unaotolewa katika zahanati hiyo pale wajawazito zaidi ya mmoja wanapofika kutaka huduma ni kwenda mjini Mpanda kwenye Hospitali ya Manispaa ambayo pia ni Hospitali ya Mkoa, kunakoaminika kuwa na huduma bora kiasi kuliko Kakese.

“Kwenda Mpanda mjini ni safari. Unahitaji kuwa na ndugu huko ili kuwa na uhakika wa zile huduma za kawaida baada ya uzazi na kwa sababu hiyo, wapo wajawazito wengi tu ambao huamua kurudi makwao na kutafuta msaada kwa wakunga wa jadi au akina mama wazoefu,” anasema Magdalena.

Kwa mujibu wa Yusuph Ally ambaye ni muuguzi katika zahanati hiyo, vijiji vinne vyenye takriban wakazi 21,142 hutegemea huduma ya Zahanati ya Kakese. Wapo pia watu kutoka Kata ya Itenka iliyo karibu na Kakese wanaotegemea pia zahanati hiyo.

“Hata sehemu ya kupumzika wajawazito au wazazi nayo hakuna. Ni kweli kuwa tukipata wajawazito zaidi ya mmoja, ushauri wetu ni kuwaelekeza wengine waende kutafuta huduma mjini. Hapa ni mmoja tu kwa wakati mmoja, hakuna namna.

“Ni bahati mbaya kwamba akina mama wengi huwa na tatizo la kutokuwa na fedha za kuwafikisha mjini na hao ndio hurejea majumbani kwao na kujifungua kienyeji,” anasema Ally.

Aidha, FikraPevu imebaini kwamba, Zahanati ya Kakese ina tatizo la kutokuwa na kifaa au zana za kisasa za kuharibu takataka zinazoendana na huduma ya uzazi, badala yake, taka kama kondo la nyuma na nyinginezo hutupwa chooni.

“Huu si ustaarabu na ni hatari kwa afya za watumiaji wengine wa choo hicho cha umma,” anasema Domick Magulu, mkazi wa Kakese.

Diwani wa  Kata ya  Kakese, Maganga  Salangada, alisema kuwa wapo baadhi ya wajawazito ambao wamekuwa wakijifungulia njiani wakati wakielekea Hospitali ya Manispaa Mpanda baada ya kukosa huduma Kakese.

 

Mlele nako hali ni mbaya

Kama hali iko namna hiyo Kakese, umbali wa kilometa 15 kutoka mjini Mpanda, basi hali ni mbaya zaidi kwa maeneo yaliyo mbali na makao makuu ya mkoa na wilaya.

Kata ya Majimoto iliyoka Wilaya ya Mlele, iko umbali wa zaidi ya kilometa 130 kutoka Manispaa ya Mpanda. Wajawazito wa maeneo hayo nao wana changamoto chungu nzima.

FikraPevu ilishuhudia idadi kubwa ya wajawazito wakiwa juani kusubiri zamu zao za kuhudumiwa katika zahanati ya Kata kutokana na kuwepo kwa eneo dogo.

Akina mama wakisubiri kupata huduma ya tiba katika Zahanati ya Kakese ambayo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vitanda vya kujifungulia na chumba cha kupumzikia baada ya wajawazito kujifungua.

 

Salome Masanja na Magdalena Lubeleja ni miongoni mwa akina mama waliozungumza na FikraPevu wakiwa katika Zahanati ya Majimoto na kwa nyakati tofauti walikiri kuwa zahanati hiyo imezidiwa na kushauri halmashauri husika kujenga Kituo cha Afya.

“Majimoto, kwa mujibu wa takwimu zilizopo, ni miongoni mwa kata zenye wakazi wengi wilayani hapa. Ni vyema kikajengwa kituo cha afya na kuongeza miundombinu kusaidia kuboresha huduma za afya,” anasema Salome, hoja iliyoungwa mkono pia na muuguzi wa zahanati hiyo, Maria Leonard.

Maria anasema kila siku akina mama na watoto takriban 200 hufika katika zahanati hiyo ndogo. “Hapo ni bila kuwahesabu wagonjwa wa kawaida ambao hutibiwa na kurudi nyumbani.”

Maria ndiye muuguzi pekee aliyeajiriwa kituoni hapo akisaidiwa na wengine wawili wa kujitolea, na kwa hakika huzidiwa sana na kazi.

Mbunge wa Kavuu, Dk. Pudenciana Kikwembe, anakiri kuwepo kwa upungufu wa watumishi wa afya na kuwa hata jengo lenyewe la zahanati ni dogo ikilinganishwa na idadi ya wanaohitaji huduma.

“Tupo katika hatua nzuri za kumaliza kabisa tatizo hili. Ni ahadi yetu kwa wananchi kuwa serikali itatoa huduma bora za afya kwa watu wote,” anasema Dk. Pudenciana.

Katika harakati za kujaribu kupunguza tatizo hilo linalohitaji mikakati ya maana zaidi, aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hivi karibuni alitoa msaada wa vitanda 10 kwa Manispaa ya Mpanda.

Manispaa hiyo imeahidi kuvisambaza katika zahanati mbalimbali zilizopo na huenda Zahanati ya Kakese nayo ikabahatika.

Lakini swali litabaki kuwa, ni nani atajenga chumba kingine kwa ajili ya faragha?

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Waziri Ummy Mwalimu awaagiza wataalamu wa afya kuzigeukia tiba asili

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewaagiza wataalamu ...

Yabainika: Wanaume walaji nyama jijini Dar hatarini kufa mapema

JIJI la Dar es Salaam linalokadiriwa kuwa na idadi ya wakazi wanaokaribia milioni sita ...

Mwanza: Vifaa vya upasuaji vyakosa kazi, vyafungiwa stoo licha ya kuwepo kwa jengo na watendaji

WAKATI Serikali ikitumia fedha nyingi kuboresha na kusogeza karibu na wananchi huduma ya afya, ...