Utoaji mimba: Jinsi mtoto anavyouawa akiwa tumboni

PAMOJA na madhara na “dhambi” ya kuua inayowakabili wanawake wanaotoa mimba, bado hawakomi, FikraPevu imebaini.

Zipo njia nyingi wanazotumia “kuwaua” watoto waliomo tumboni, lakini uchunguzi wa FikraPevu umebaini njia tisa maarufu zaidi kutoa mimba, huku nyingine miongoni mwao zikiwa si salama kwa mujibu wa utafiti wa wataalamu mbalimbali.

Ukosefu wa taarifa sahihi na usiri kati ya mtoa mimba na mhudumu huchangia zaidi kuwapo vitendo hivi.

Utoaji mimba usiokuwa salama

Dk. Bahati Maxwell wa Kituo cha Afya cha Buguruni-Anglican Ilala na Dkt. Pasiens Mapunda wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU) – vyote vya Dar es Salaam, kwa nyakati tofauti wanasema, utoaji mimba usio salama ni ukatishaji wa uhai wa mtoto aliye tumboni mwa mama unachofanyika kinyume cha sheria katika mazingira na njia zisizo rasmi na salama.

Utoaji mimba salama

Kaimu Mkurugenzi wa Programu, Uzazi na Malezi Tanzania (UMATI), Dkt. Saili Mbukwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile, wanasema sababu pekee ya kutoa mimba kitaalamu ni kwa ruhusa za kitabibu. Na hufanyika kisheria katika mazingira salama kuokoa uhai wa mama.

Mratibu wa Mikoa na Kanda wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto Kitaifa katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Martha Shakinyau  anafafanua akisema, “Mwongozo wa serikali unataka mwanamke ambaye mimba imeharibika, ahudumiwe katika mazingira salama, penye mtaalamu, dawa na vifaa safi, sahihi na vya kutosha kwa kuangalia usalama wake.”

Uelewa wa wananchi

Imebainika kuwa, miongoni mwa taarifa muhimu zisizofahamika kwa wengi, ni usahihi wa lini mimba inatafsiriwa kuwa ni mtoto; na madhara yanayoweza kutokea kwa kutumia njia yoyote ya utoaji mimba.

Wilayani Ilala takriban wanawake 7 kati ya 10 (70%) wanaamini mimba kabla ya wiki 12, sio binadamu wala uhai kamili.

Wasemavyo waathirika wa kutoa mimba

“Nilipoelewa uhai huanza siku mimba inapotunga, iliniuma sana; hasa nilipojua nimeua mtoto wangu,” anasema Saida Said (sio jina halisi) mkazi wa Matembele Kivule, Ilala, Dar es Salaam.

Magdalena Athumani (28) anasema alitambua siku hiyo hiyo baada ya mhudumu wake kumlaumu. “Alisema sikumwambia ukweli kuhusu umri wa mimba aliposema, sio ya miezi mitatu maana mtoto ni mkubwa.”

Msimamo wa jamii

Grace Shayo wa Prolife Tanzania, inayohusika na masuala haki za kuishi, anasema, “kama ukweli ungesemwa wazi, hakuna mama; hata mgonjwa mmoja ambaye angekubali mtoto auawe eti ili yeye apone hakuna.”

Watetezi wa Uhai

Mkurugenzi wa Utume wa Familia Kupendana Tanzania (Fakuta), Padre Baptiste Mapunda anasema, “Uhai huanza pale tu mimba inapotungwa, hivyo mimba ni uhai; mimba ni mtoto tumboni haijalishi umri wa mimba.”

Uchunguzi umebaini kuwapo njia za kienyeji na za kisasa zinazotumika kutolea mimba.

Mratibu wa Shirika la Kimataifa la Human Life International (HLI) kwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini, Emil Hagamu anasema, “Njia hizi hutegemea mazingira na ukubwa wa mtoto tumboni. Hakuna iliyo salama kwa asilimia 100….”

Njia za kienyeji kutoa mimba

Njia hizi zimebainika kuwa ni pamoja na kujinunulia vidonge vikiwamo vya majira na kumeza kwa kiwango kikubwa.

Wanawake wengine hutumia majani ya aloevera, kunywa chai ya rangi yenye majani mengi, au maji ya majivu na kuingiza dawa za kienyeji sehemu za siri kama kijiti kibichi/ cha jani la muhogo.

Kijiti cha muhogo

Dkt. Mbukwa anasema, “Utomvu wa kijiti kibichi cha muhogo una sumu iitwayo oxtoxin, kwa hiyo wakiweka ukeni, unafungua njia ya uzazi na utomvu unaua kiumbe; matokeo yake, mimba inaharibika na kutoka. Hii ni hatari.”

Kujipiga makonde tumbo

Wanawake wengine hujaribu kutoa mimba kwa kujipiga makonde tumboni. Vitendo hivi vinaweza kusababisha majeraha na damu nyingi kuvujia na kusababisha kifo.

Njia za kisasa

Chombo maalumu cha kunyonya mwili

Dkt. Maxwell anasema hufanywa kwa kutumia kifaa kiitwacho “suction aspiration.”

Imebainika kuwa, chombo hicho hutumika kumkatakata mtoto na kunyonya nyamanyama za mwili wake, damu na majimaji yanayozunguka tumbo la uzazi.

Kutumia mkasi kumkata mtoto

Imefahamika kuwa, mkasi hutumika kumkata mtoto na kumwondoa katika tumbo la uzazi. Kichwa huondolewa baada ya kukandamizwa na kuvunjwa kwa chombo maalumu.

Kumuunguza mtoto kwa chumvi kali

Hagamu anafahamisha kuwa, mwanamke huwekewa maji yenye chumvi kali inayomuunguza mtoto, kumbabua na kumharibu ngozi. Anasema, “Ndani ya siku tatu, mwanamke hupata uchungu na kumzaa mtoto aliyekufa akiwa ameharibika.”

Kutumia sindano ya methotrexate

Anasema, “mimba ya miezi mitatu mwanzoni, mwanamke anachomwa “methotrexate injection”. Sumu yake hushambulia seli zinazozunguka mimba. Mtoto hunyimwa chakula na hewa hatimaye kufa.

Siku saba baadaye, mama anadungwa sindano ya “misoprostol” ili kumwondoa mtoto tumboni.”

Kumtoa nje mtoto mzima na kumuua

Kwa kutumia mashine kumwona mtoto tumboni, mtoa mimba hukamata miguu ya mtoto kwa ‘koleo.’ Humvuta nje hadi kinapobaki kichwa.

Vyuma vikali huingizwa nyuma ya kichwa cha mtoto na kukipasua. Mrija wenye nguvu huingizwa na kuvuta ubongo wa mtoto.

Kisingizio

Ingawa umaskini umekuwa kisingizio kikubwa cha utoaji mimba, uchunguzi umebaini kuwa  wanawake wenye nyadhifa na hali nzuri kimaisha, wanaotoa mimba zaidi kuliko makundi mengine.

Mfano, ni nadra kumuona mwanamke mkuu wa wilaya au mkoa, mbunge au waziri akiwa mjamzito. Haijulikani ni kwanini.

Nini kifanyike?

Wadau washirikiane kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusu tafsiri ya mimba na utoaji mimba ili kuepusha madhara ya kiroho, kiuchumi, kiafya kimwili, ikiwamo vifo.

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Uhaba na uchafu wa vyoo shuleni unahatarisha afya za wanafunzi jijini Dar es Salaam

MAZINGIRA bora ya kufundishia na kujifunzia katika shule ni kichocheo kwa wanafunzi kufanya vizuri ...

Mwanza: Vifaa vya upasuaji vyakosa kazi, vyafungiwa stoo licha ya kuwepo kwa jengo na watendaji

WAKATI Serikali ikitumia fedha nyingi kuboresha na kusogeza karibu na wananchi huduma ya afya, ...

Pregnant women in Dakawa village go with delivery tools during birth giving

PREGNANT women in Dakawa village, Mvomero district Morogoro are asked to go with delivering ...