Jamii Forums yazindua rasmi mradi wa ‘Tushirikishane’ katika kumulika ahadi na uwajibikaji wa viongozi Majimboni

Posted By -

(278)

Views

Jamii Media, kampuni inayojihusisha na mitandao, pamoja na kuendesha tovuti mbili maarufu nchini ambazo ni Gazeti la mtandaoni la FikraPevu na Jamii Forums, imezindua rasmi mradi wa Tushirikishane unaowashirikisha viongozi wa kuchaguliwa wakiwemo wabunge, na madiwani katika majadiliano ya mikakati ya maendeleo majimboni mwao.

Lengo kuu la mradi huu, ni kuweka wazi utekelezaji wa majukumu ya maendeleo wanayoyafanya na waliyoyaahidi Wabunge wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu Octoba 2015, kwa wapiga kura wao.

Katika majadiliano hayo ambayo viongozi ndio walengwa wakuu, wananchi pia wanapata nafasi ya kushiriki katika kuwauliza maswali na kupata ufafanuzi wa shughuli mbalimbali za maendeleo kutoka kwa viongozi wao.

Mradi huu utatekelezwa katika majimbo sita (6), ambayo ni Bukoba, Kigoma, Sengerema, Nzega, Lindi na Kigamboni, Jimbo la Bukoba Mjini limekuwa Jimbo la kwanza katika kuanza utekelezaji wake ambapo jopo la Jamii Media litadumu jimboni humo kwa muda wa siku tano katika uendeshaji wa vikao vya majadiliano.

Vilevie mradi huu una mwakilishi mmoja mmoja kutoka JamiiForums, ambaye ni Afisa Mawasiliano katika kila jimbo atakayekusanya maoni na uchambuzi wa wananchi katika jimbo husika.

                                                                      

Mkurugenzi wa Jamii Media, Bwana Maxence Melo, akimkabidhi vitendea kazi Afisa Mawasiliano (kutoka Jamii Forums) wa Jimbo la Bukoba Mjini Bi.Happiness Essau  

Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Jamii Media na mtandao wa JamiiForums.com, Bwana Maxence Melo Mubyazi, wakati wa uzinduzi wa mradi jimboni Bukoba, amesema mradi huu utachukua miezi 9 kukamilika, na hivyo Wabunge wanaohusika kwenye mradi huu wanatakiwa kukubaliana na wananchi juu ya ahadi 4 za maendeleo kati ya zile zilizoahidiwa, ni kwa jinsi gani zitatekelezeka ndani ya majimbo yao.

Wakati wa mikutanao inayoendelea kwa kuongozwa na jopo la Jamii Media, wananchi wanapata wasaa kujulisha kero zao, kutoa maoni, kupendekeza pia nini kifanyike, na kipi kiweze kurekebishwa katika harakati za kuleta maendeleo katika halmashauri zao kupitia viongozi wenye dhamana waliowachagua.

Jopo la Jamii Media tayari wamekutana na viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Mjini ikiwemo  Baraza la Madiwani, na Mbunge wa jimbo hilo Mhe. Wilfred Lwakatare katika vikao vya majadiliano na wananchi, katika ukumbi wa Bukoba Hotel.

                                            

Baraza la Halmashauri ya Bukoba, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Pamoja na Timu ya Jamii Media

katika picha ya Pamoja

Bwana Maxence Melo Mkurugenzi wa Jamii Media, aliwapongeza viongozi wa Wilaya, watendaji wa Halmashauri, Madiwani na Mbunge kwa mwitikio mkubwa walioonyesha katika kuupokea mradi wa Tushirikishane kwani ni sehemu ya utekelezaji wa maendeleo.

Vile vile, Bwana Maxence aliwafahamisha kwamba Mradi huu utatekelezwa katika majimbo sita (6) kwa kuanzia na Bukoba Mjini limekuwa Jimbo la kwanza katika kuanza utekelezaji wake. Alifafanua kuwa mradi huu utachukua miezi 9 na hivyo Wabunge wanaohusika kwenye mradi huu wanatakiwa kukubaliana na wananchi juu ya ahadi zisizozidi 4 za kuweza kuwa sehemu ya mradi huu zinazoweza kutekelezeka kwa kiwango kikubwa wakati wa mradi huo.

Miongoni mwa Malengo ya Mradi huu ni pamoja na kutekeleza yafuatayo:

i. Kupanua wigo wa mawasiliano kati ya Wananchi na viongozi wao wa kuchaguliwa na serikali yao (kwa njia ya mitandao, magazeti, redio, televisheni na mikutano ya wazi)

ii. Kurahisisha upatikanaji wa habari na taarifa za umma zikiwa kwenye lugha rahisi.

iii. Kuchochea majadiliano ya wazi, yenye tija na staha kati ya wananchi na viongozi wao.

iv. Kusaidiana na viongozi wa kuchaguliwa katika kutengeneza nyenzo za muhimu katika kutekeleza ahadi.​

Matarajio ya Mradi

Shughuli za Mradi huu zinatarajia kuchangia katika mabadiliko ya muda mfupi na muda mrefu kwenye tasnia ya uongozi wa Uwakilishi wake nchini Tanzania.

i. Kujengeka kwa utamaduni wa majadiliano yenye staha kati ya viongozi na wananchi kwenye mitandao ya kijamii.

ii. Kuboreshwa kwa mfumo wa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi katika utekelezaji wa sera na ahadi za wakati wa Uchaguzi.

iii. Kuongezeka kwa ufanisi katika utekelezaji wa sera na ahadi zilizo ongelewa kipindi cha uchaguzi.​

Pamojana na malengo hayo ya mradi wa Tushirikishane, pia ni matumaini ya mradi kujenga mahusiano mazuri kati ya viongozi na wananchi wao kwani kupitia vipindi mbalimbali vya kuwa pamoja katika ufafanuzi wa nini kitafanyika na kwa jinsi gani utekelezwaji wake utakuwa, wananchi wataongeza uaminifu kwa viongozi wao, kwani hitimisho lake ni viongozi kuleta mrejesho kwa wa utendaji wao kwa wananchi.

SambazaTweet about this on TwitterShare on Facebook0Share on Google+0Share on LinkedIn0Email this to someonePrint this page
Fikra Pevu

JamiiForums' Editorial Website | Tanzania's Online News Portal | Dedicated for Public Interest Journalism | mhariri@fikrapevu.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *