Humphrey Polepole aache dharau kwa Watanzania

Humphrey Polepole, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi, anawadharau Watanzania.

Anabeza uwezo wao wa kufikiri, anadhani yeye anajua zaidi pengine kuliko Watanzania wengi, na pengine anajiona kuwa ni msomi wa hali ya juu.

Kazi za Idara ya Itikadi na Uenezi, kwa mujibu wa Katiba ya CCM zipo sita, zimeainishwa, zinasomeka kwa Kiswahili na zinajulikana wazi.

Ya kwanza, kushughulikia masuala ya msingi ya Itikadi na Sera za CCM.

Ya pili, ni kueneza na kufafanua Itikadi na Sera za CCM.

Ya tatu, kupanga na kusimamia Mafunzo na Maandalizi ya Makada na Wanachama.

Ya nne, Kusimamia Vyombo vya Habari vya Chama, Mawasiliano na Uhamasishaji wa Umma kwa jumla.

Kazi ya Tano ni kuongoza na kusimamia maandalizi ya Sera, Programu na Ilani za Uchaguzi za CCM.

Ya Mwisho inayotajwa kwa mujibu wa katiba hiyo ni Kusimamia Utafiti, Maktaba na Nyaraka za Chama.

Tunafahamu kuwa Polepole anafahamu kusoma na kuandika, hivyo hizi kazi sita tu zilizoainishwa kwenye idara yake haziwezi kumchanganya akaanza kusema mengine yasiyomhusu.

Imeshangaza tangu Polepole achaguliwe kushika wadhifa huo ameanza kufanya majukumu ya idara zingine ambazo hata zipo nje ya CCM, kuna idara ambazo ni za serikali kabisa na zina upekee wa aina yake.

 Januari 17, 2017 waandishi wa habari waliitwa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba jijini Dar es Salaam kumsikiliza Polepole, walipofika alizungumzia hali ya chakula na utaratibu wa kutangaza njaa nchini.

Polepole, si Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Waziri mweye dhamana ndiye anaweza kuzungumzia suala la njaa.

Huyu Polepole hii kazi amejipachika kwa sababu ya nini? Anamdharau Waziri aliyepewa dhamana ya jambo hilo kwamba hawezi, yeye ndiye anaweza zaidi kwa hiyo amsemee?

Kazi ya kuzungumzia masuala ya chakula haijaainishwa kwenye kazi sita za Idara ya Itikadi na Uenezi iliyopo kwenye Katiba ya CCM. Polepole anadhani anawafurahisha Watanzania wanaojua wajibu wake anapowadanganya pia kwa kuzungumzia yale yasiyomhusu?

Cha kushangaza zaidi, kinachoonyesha pengine dharau kuzidi, Polepole amejitosa kuzungumzia suala la vyeti vya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Akizungumza katika kipindi cha Kinagaubaga, kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW) tarehe 14 Machi 2017, Polepole amenukuliwa akisema utaratibu utafuatwa wa kumwajibisha Makonda.

“Ninyi hamkujua kama tutawachukulia watu hatua, Serikali ina utaratibu wake, Bunge lina utaratibu wake na Chama kina utaratibu wake. Tunao utaratibu tunaufuata, wananchi wawe na subira.

"Wananchi wawe na subira, ninafahamu wananchi wana subira sana, wasubiri mamlaka za viongozi, hawa wote waliokosea, mchakato wa haki ufanyike na hatimaye tutaona matunda yake,” ndivyo alivyokaririwa akisema.

Tangu lini suala la vyeti bandia limekuwa kati ya masuala ya kushughulikiwa na Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM?

Polepole, hafanyi kazi Baraza la Mitihani, wala si Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, masuala ya kughushi vyeti ni jinai inayopaswa kuzungumzwa na polisi. Kwanini Polepole anadharau Watanzania na kuwaeleza masuala ambayo hayapo kwenye idara yake?

Hata Biblia inaonya, “Ukitumwa kadha, usitende kadha wa kadha”.

Polepole asidhani sababu anaweza kuita waandishi wa habari, au kuhojiwa na vyombo vya habari ndiyo sehemu ya kujipa mamlaka ya mambo yote hata yasiyomhusu, ambayo hayapo kwenye idara yake.

Aangalie kazi za Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM ni zipi. Masuala ya njaa, au kughushi vyeti na uwajibikaji wake aachie mamlaka husika, asionekane anawadharau Watanzania.

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Utamaduni wa Mtanzania: Kielelezo kilichobaki kuelekea uchumi wa viwanda

Tafsiri sahihi ya maendeleo inabaki kuwa gumzo katika jamii zetu. Wengi wetu hudhani tafsiri ...

Kasi ya wapinzani kuhamia CCM yawaibua wasomi nchini

Kutokana na kasi ya wanachama wa vyama vya upinzani kuhama vyama vyao na kukimbilia ...