Connect with us

Jukwaa la Maisha

GREENLAND: Ulevi, ukosefu wa usingizi unavyochochea watu kujiua

Published

on

Matukio ya watu kujiua yameendelea kushamiri katika maeneo mbalimbali nchini. Watu ambao wanaondoa uhai wao kwa kunywa sumu, kujinyonga au kujirusha kwenye majengo marefu, sio mambo mageni tena. Zipo sababu mbalimbali ambazo zinawasukuma watu kujiua ikiwemo mabadiliko ya mfumo wa maisha.

Lakini umewahi kujiuliza ni nchi gani inayoongoza kwa watu kujiua? Greenland inatajwa kuwa nchi ya kwanza yenye viwango vikubwa vya watu wanaojiua duniani.

Kimsingi Greenland sio nchi. Bado inachukuliwa kama sehemu ya Ufalme wa Denmark. Hata hivyo, katika siku za karibuni, Greenland imetambuliwa kama ‘nchi huru’, ikiwa na maana kuwa inafanya kazi kama Taifa huru katika maeneo mengi lakini sio katika mambo yote.

Greenland haitambuliki kama nchi rasmi, na huwezi kuiona kwenye orodha ya nchi zenye viwango vikubwa vya kujiua, lakini kiuhalisia inaongoza duniani kwa matukio hayo. Kwenye orodha hiyo, Guyana inatajwa kuwa katika nafasi ya kwanza, kwa wastani watu 44.2 kati ya 100,000. Ikiwa ina maana kuwa kati ya watu 100,000 wa nchi hiyo 44 hujiua kila mwaka.

Hata hivyo, nchini Greenland hali ni mbaya zaidi. Kulingana na ripoti za kuanzia mwaka 1985 hadi 2012, wastani wa  viwango vya kujiua katika nchi hiyo ulikuwa watu 83 kati ya 100,000, ambapo ni karibu mara mbili zaidi ya Guyana.

                                      Polisi wakibeba mwili wa mtu aliyejiua

Greenland imeziacha kwa mbali nchi zote duniani katika matukio makubwa ya watu wake kujiua, na matukio haya hayapungui badala yake yanaongezeka kila mwaka. Kwa kawaida, lazima kuna tatizo ambalo linasababisha hali hiyo kutokea.

Kwa haraka haraka utakuwa na maswali mengi ya kutaka kufahamu kwanini wakazi wa Greenland wanashawishika kuondoa uhai wa maisha yao kwa kiasi hicho. Watu wengi katika nchi hiyo wana kipato kizuri na uhakika wa kupata pensheni nzuri kabla na baada ya kustaafu.

Lakini bado asilimia 20 ya wakazi wa Greenland wamewahi kuthubutu kujiua angalau mara moja katika maisha yao. Hiyo ina maana kuwa watu 2 kati ya 10 wana uwezekano mkubwa wa kujiua.

Swali la kujiuliza ni kwamba nani alaumiwe kwa matukio ya kujiua nchini Greenland? Jibu ni wananchi wenyewe wa Greenland kutokana na sababu zifuatazo:

 Ulevi

Kwa tafsiri nyepesi neno ‘Greenland’ ni ardhi yenye uoto wa kijani. Lakini Greenland tunayoizungumzia hapa haina sifa hizo. Hali ya hewa ya nchi hiyo ni ya baridi nyingi. Sehemu kubwa imefunikwa na barafu na kuzuia mimea kuota.

Kulingana na historia ya nchi hiyo, alikuwepo mtu mmoja maarufu ajulikanaye kama Viking Erik ambaye alilipa jina eneo hilo ‘Greenland’ (ardhi ya kijani). Alifanya hivyo ili kumshawishi mwenzake kuungana naye ili waanzishe makazi katika nchi hiyo.

Ili kufanikisha hazima yake, alichagua jina la ‘Green’land, japokuwa kulikuwa hakuna kitu kama hicho katika nchi hiyo.

Wakati wa majira ya joto, wastani wa jotoridi katika nchi hiyo huwa kati ya juzi joto 0 hadi 10 (10C). Wakati wa majira ya baridi (winter), jotoridi hushuka hadi juzi joto sifuri (0C). Nachelea kusema, Greenland ni kama kisiwa kilichofunikwa kwa barafu.

                       Barafu imefunika sehemu kubwa ya nchi ya Greenland

Ukweli ni kwamba, watu wanaoishi kwenye miji yenye baridi wanaowezekano mkubwa wa kuathirika na ulevi.  Watafiti wanaeleza kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya idadi ya watu wanaojiua na matumizi ya pombe.

Matumizi ya pombe ni tatizo kubwa la kijamii nchini Greenland. Pombe inasimama kama chanzo kikubwa cha ugomvi wa kifamilia, udhalilishaji wa kingono, ukosefu wa ajira, jambo linalochangia janga kubwa la kujiua katika nchi hiyo.

Ukosefu wa usingizi

Sehemu kubwa ya Greenland iko kwenye eneo la juu kabisa la nchi za Kaskazini, ambazo zinapata kipindi kimoja cha baridi. Pia inapata kipindi kimoja cha joto ambapo jua halipotei (sunset).

Katika eneo hilo la juu kabisa la Kaskazini mwa dunia, nchi zake nyingine zinatawaliwa na vipindi vingi vya baridi na giza hata wakati wa mchana na wakati wa majira ya joto, jua haliondoki angani.

Katika eneo hilo, kuna siku 120 katika mwaka ambapo jua halitui (sun never set), siku 108 katika mwaka jua halichomozi, na siku 137 tu ndiyo hupata mwanga na giza.

Unaweza kufikiri kwamba watu wanaweza kujiua kwasababu hakuna ishara ya jua wakati wa mchana hasa majira ya baridi, lakini la kushangaza ni kwamba tafiti zinaeleza kuwa matukio mengi ya kujiua yanatokea wakati wa majira ya joto.

Wataalamu wanasema wakati wa joto, watu hawapati usingizi wa uhakika jambo linalowaletea msongo wa mawazo na mkazo. Zaidi ya hapo, ukosefu kabisa wa giza unaweza kuathiri mwili wa binadamu na kutengeneza homoni ya ‘serotonin’ ambayo ni mahususi kusawazisha hali na hisia.

Swali la kujiuliza ni rahisi kwa kiasi gani akili zetu zinaweza zikabadilisha mfumo wa kupata usingizi kulingana na hali ya hewa? Hata hivyo sababu zote mbili – ulevi na ukosefu wa usingizi hazichukuliwi kama sababu zenye nguvu.

Kujiua halikuwa tatizo la siku zote nchini Greenland. Matukio ya kujiua yalikuwa machache katika miaka ya 1950. Baada ya kuingia miaka ya 1960, idadi ya matukio ya kujiua iliongezeka maradufu. Sababu za asili kama hali ya hewa zisingeweza kusababisha ongezeko hilo. Lakini zipo sababu zingine…

Uhamiaji na utengano

Greenland haina wakazi wengi ukilinganisha na nchi nyingine duniani. Japokuwa ni miongoni mwa visiwa vikubwa duniani ina wakazi wapatao 56,400 na 16,000 kati ya hao wanaishi katika mji mkuu wa Nuuk. Wakazi wengine wanaishi pembezoni mwa jiji hilo na wengine kwenye vijiji vya mbali ambapo vijiji vingine vina wakazi wasiozidi 50.

                            Makazi ya watu wa mji wa Nuuk, Greenland

Mnamo 1960, Greenland iliamua kutoendelea kuvisaidia vijiji vya mbali. Vijiji hivyo vilikuwa mbali na makao makuu ya Serikali na ikawa vigumu kwa wakazi wake kupata huduma muhimu za kijamii. Watu waliokuwa tayari kuondoka kwenye vijiji hivyo walipelekwa mjini ili kupata makazi na huduma za kijamii.

Lakini watu wengine walikataa kuondoka na kuamua kubaki katika vijiji hivyo. Walitaka kuendelea kulinda utambulisho na nyumba za waasisi wa kabila la Inuit. Kwa bahati mbaya, hawakuwa na chaguo tena zaidi ya kuondoka na kuungana na wenzao waliopo mjini.

Wakazi wa mjini hasa mji mkuu wa Nuuk wanawaona watu hao wanaohamia katika miji yao kama wakimbizi na wakati mwingine wanawatenga katika shughuli muhimu za kiuchumi na  kijamii. Kutokana na kadhia hiyo, wale wanatajwa kuwa ni wakimbizi hujiua kwasababu ya kutengwa na kunyimwa haki za msingi za kuishi.

Hata hivyo, Serikali ya Greenland imechukua hatua mbalimbali kupambana na janga hilo kwa kutengeneza miundombinu ya simu za mkononi kuongeza mawasiliano na kutoa ushauri kwa watu wenye hatari ya kujiua kuendelea na maisha.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Jamii

UTAFITI: Watu wanaochelewa kulala wako katika hatari ya kufa mapema

Published

on

Utafiti uliotolewa hivi karibuni umebaini kuwa watu wanaochelewa kulala wana uwezekano mkubwa wa kufa mapema kuliko wale wanaoamka mapema wakati wa usubuhi.

Msingi wa utafiti huo ni kwamba watu wanaolala muda mzuri na kuamka mapema wanaweza kuishi muda mrefu ukilinganisha na wale ambao wanachelewa kulala  ambao wakati mwingine wanaamka mapema wakiwa na uchovu mwingi.

Matokeo ya utafiti huo ambayo yamechapishwa kwenye Jalida la Chronobiology International, yamechambua  sampuli ya watu laki 5  wenye umri wa miaka 30 hadi 73 ambao walifuatiliwa tabia za ulalaji wao kwa zaidi ya miaka 6 na nusu.

Watafiti walibaini kuwa watu ambao  walikuwa wanachelewa kulala walikuwa na hatari kwa asilimia 10 kufa mapema katika kipindi cha utafiti kuliko wale ambao wanalala mapema na kuamka mapema.

Watafiti wengine kutoka Chuo Kikuu cha Surrey nchini Uingereza na wale wa Chuo Kikuu cha Northwestern kilichopo Chicago, Marekani walibaini kuwa watu wanaochelewa kulala au wanaokesha kama bundi (night owls) wana uwezekano mkubwa wa kupata matatizo ya kisukari, akili na mfumo wa upumuaji.

Hii siyo mara ya kwanza kwa utafiti ambao unahusianisha kati ya kuchelewa kulala na matatizo ya kiafya. Tafiti zingine zimehusianisha ukeshaji na hatari kubwa ya kupata msongo wa mawazo, matumizi ya madawa ya kulevya, mtindo wa tabia hasi kama kutokula mlo kamili, unene uliopitiza.

Sababu nyingine ambayo ni muhimu ni kwamba dunia imeundwa kwa watu wa asubuhi (wanaoamka mapema). “Afya dhoofu ya watu wanaochelewa kulala inni matokeo ya kushindwa kupanga muda wa kulala na muda wa shughuli za kijamii,” inaeleza sehemu ya utafiti huo.

Hata hivyo, Utafiti umeonyesha uhusiano pekee kati ya kuchelewa kulala na kufa mapema, lakini matokeo hayo bado  hayajakamilika. Haiwezekani kusema watu walioshiriki kwenye utafiti walikuwa wanachelewa  kulala au walikuwa wanaamka mapema wakati wote.

Ikiwa shughuli zinazomfanya mtu achelewe kulala zinaweza kusababisha kufa mapema, kuna nafasi ya kuingilia kati na kuchunguza zaidi. Japokuwa watafiti wanasema mfumo wa vinasaba vinaweza kuchangia  mtu  kuchelewa kulala au kuamka mapema, lakini hilo linaweza kudhibitiwa na baadhi ya watu.

Katika taarifa ya utafiti huo, Mwandishi kiongozi, Profesa Mshiriki katika Shule Kuu ya Feinberg ya Chuo  Kikuu cha Northwestern , Kristen Knutson amesema ikiwa watu wanataka kuwa na tabia ya kuamka mapema wanatakiwa kuzingatia muda wa kulala ili kujiepusha na hatari inayoweza kuwapata. Kukamilisha shughuli mapema ili kupata muda mzuri wa kupumzika, kuamka mapema na kupata jua la asubuhi  lenye vitamin D.

Continue Reading

Jamii

Asimilia 43 ya watanzania kukimbilia ughaibuni wakipata fursa

Published

on

Imebainika kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 6 za Afrika ambazo raia wake wanapenda kuhama na kwenda kuishi nchi zingine hasa Marekani na Ulaya ikiwa watapata fedha na fursa zitakazowawezesha kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa  Matokeo ya Utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew (2017) yanaonyesha kuwa asilimia 43 ya watanzania waliohojiwa walisema kuwa kama wangepata fedha na fursa wangependelea kuachana na nchi yao na kwenda kuishi zingine.

Hiyo ina maana kuwa, mtanzania 1 kati ya 4 kama atapata fedha au fursa anaweza kuondoka nchi na kuhamia nchi nyingine anayoipenda.

Nchi zingine ni Ghana ambayo ilishika nafasi ya kwanza kwa kupata asilimia 75, ikifuatiwa na Nigeria (74) na ya tatu ilikuwa Kenya (54). Nafasi ya nne ilishikwa na  Afrika Kusini (51), Senegal (46) na nafasi ya sita ilienda kwa Tanzania kwa asilimia 43.

Asilimia (%) ya Waafrika wanaotaka kwenda Ughaibuni

 

Maoni ya watu wa nchi ambazo wanasema wanataka kuishi nchi zingine yanafanana na tafiti zingine kama Afrobarameter  uliofanyika Nigeria na Ghana,  ambao uliuliza swali la uwezekano wa kuhama. Ukilinganisha na maeneo mengine duniani, utafiti wa  ‘Gallup polls’  ulibaini kuwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, zina idadi kubwa ya watu ambao wanapenda kuondoka katika nchi zao.

Watafiti hao waliuliza washiriki wa utafiti huo juu ya mipango ya miaka 5 ya kuhama nchi zao. Kutokana na  shauku ya kwenda kuishi nje ya nchi, asilimia 8 (sawa na kusema mtanzania 1 kati ya 8) ya watanzania walisema miaka 5 ijayo watakuwa wanaishi nje ya nchi. Huku raia wa Senegal kwa 44% ambayo ni kiwango cha juu Afrika wana mipango ya kuishi nje ya nchi yao.

Kundi ambalo linaonekana zaidi kuzikimbia nchi zao ni la vijana ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi. Kundi hili ni muhimu kwa nguvu kazi ya taifa, lakini halitulii likihaha huku na kule kutafuta fursa za kuboresha maisha.

Mipango yao itafanikiwa? Wengi wao hawatafanikiwa kuondoka katika nchi zao. Mfano, mwaka 2015, raia milioni 1.7 (sawa na 6% ya raia wote wa Ghana) walituma maombi ya Visa ya kwenda Marekani, huku idadi ya watu wanaotakiwa kupata Visa hiyo kila mwaka ni 50,000 tu duniani kote.

Kwasababu program hiyo ya Visa inawaruhusu watu wenye elimu ya juu ya Chuo, vijana wengi wanaotuma maombi wanakosa sifa hiyo. Kwa muktadha huo wanakosa sifa ya kuingia Marekani.

                      Wahamiaji wa Afrika wakiwa kwenye jahazi kuelekea Ulaya

 

Sababu zinazowasukuma kuziacha nchi zao?

Sababu zinazowasukuma watu kuziacha nchi zao za Afrika na kuamua kwenda kuishi ughaibuni zinatofautiana baina ya nchi moja na nyingine; pia kutoka mtu mmoja na mwingine.

Kwanza, wakati uchumi wa Afrika ukikua kwa kiwango cha kuridhisha, nchi nyingi za bara hilo zinakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa ajira na malipo madogo kwa walioajiriwa. Hata hivyo, soko la ajira halionyeshi kuimarika siku za karibuni, jambo linalozidisha ushindani katika sekta ya ajira. Tatizo hilo pia linachangiwa zaidi na kutokuwepo kwa mipango ya kudhibiti ongezeko la idadi ya watu.

Hali hiyo huwasukuma vijana kukimbilia nchi ambazo zina mazingira mazuri ya kufanyia kazi ili kujihakikishia usalama wa kipato na maisha.

Machafuko ya kisiasa ni sababu nyingine inayowasukuma Waafrika kukimbilia nchi zingine. Mathalani, watu ambao wamepoteza makazi na kuwa wakimbizi katika nchi zao imeongezeka mara dufu hadi kufikia milioni 9 katika kipindi cha mwaka 2010 na 2016, hii ni kwa mujibu wa Shirika la wakimbizi duniani (United Nations High Commissioner for Refugees (UNHCR) estimates.

Pia idadi ya wakimbizi wa Afrika wanaoishi kwenye nchi zingine za Afrika imeongezeka hadi kufikia watu milioni 2.3 katika kipindi hicho. Katika kipindi hicho, ripoti zinaonyesha kuwa watu hao kati ya 400,000 hadi milioni 1 wanapatikana Libya; baadhi yao wanauzwa kama watumwa na kuwekwa jela kama vifaa.

Sababu nyingine ambayo ina nguvu, ni kwamba watu wanaotaka kwenda nchi za nje hasa Marekani na Ulaya ni kwasababu wana ndugu au marafiki wanaoishi katika nchi hizo. Mathalani, asilimia 13 ya watanzania walisema wana ndugu katika nchi za Ulaya, huku 18% walisema wana ndugu au marafaiki nchini Marekani.

Wanapendelea kwenda nchi zipi?

Nchi ambazo watu hao wanapendelea kwenda ni zile za Ulaya na Marekani. Kwa nchi za Ulaya, wahamiaji ambao wamekimbia vita katika nchi zao hupendelea kwenda huko kwasababu ni rahisi kufikika kuliko Marekani.

Utafiti wa Pew umebaini kuwa asilimia kubwa ya wahamiaji hao wanapendelea kwenda Marekani kuliko Ulaya. Kwa mfano 42% ya raia wa Ghana ambao walisema wanapanga kwenda ughaibuni kwa miaka 5 ijayo, wanne kati ya 10 (41%) walichagua Marekani kama eneo la kufikia.

Inadaiwa kuwa hadi mwaka 2017, kulikuwa na watanzania wasiopungua 50,000 wanaoishi nchini Marekani. Kulingana na Idara ya Marekani ya Usalama, inaeleza kuwa kati ya mwaka 2010 hadi 2017, Waafrika 400,000 waliingia Marekani.  Kati ya hao 110,000 walikuwa wakimbizi, 190,000 walipata vibali vya kuishi kutokana na mafungamano ya kifamilia zinazoishi huko. Na 110,000 waliingia kupitia program ya  visa

Continue Reading

Jamii

Programu za jinsia shuleni kuvunja mnyororo wa ukatili kwa watoto Dar

Published

on

Imeelezwa kuwa watoto yatima wako katika hatari kubwa ya kukumbwa na ukatili wa kijinsia na kuathiri ustawi wa maisha yao kiuchumi na kielimu.

Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ni suala zito la haki za binadamu, jamii na afya ya jamii nchini Tanzania kama ilivyo katika nchi nyingi duniani. Vitendo hivi vinamomonyoa msingi imara ambao watoto wanahitaji ili wawe na afya bora na maisha yenye tija, na vinasigana na haki ya msingi ya watoto ya kuishi salama utotoni.

Kwa mujibu wa Ripoti ya utafiti wa  Ukatili Dhidi ya Watoto Tanzania ya mwaka 2009 iliyotolewa na shirika la Watoto Duniani (UNICEF), yatima wako katika hatari zaidi ya kukumbwa na ukatili kuliko wasio yatima kutokana na kukosa malezi ya familia ambayo ndiyo msingi wa ukuaji wa mtoto.

“Ukatili wa kijinsia uliowakumba watoto kabla ya miaka 18 ni asilimia 36 ya wasichana waliokuwa yatima ukilinganisha na asilimia 25 ya wasichana ambao hawakuwa yatima, na ukatili wa kiakilia utotoni uliwakumba wasichana yatima asilimia 31 ukilinganisha na asilimia 21 ya wasichana wasio yatima,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inaelezwa kuwa ukatili unawakumba zaidi watoto yatima ni ule wa kiakili na kimwili ambapo asilimia 9 ya wasichana na asilimia 14 ya wavulana nchini Tanzania wamewahi kufanyiwa ukatili wa kiakili na kimwili kama kupigwa na kutukanwa.

Kulingana na Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, mtoto anahesabika kuwa ni yatima endapo atafiwa na mzazi mmoja au wote wawili. Kimsingi anakosa matunzo au upendo wa mzazi mmoja au wote wawili ambapo inaweza kuwa ni changamoto katika ukuaji wake hasa katika upatikanaji wa elimu.

              Watoto bado wako kwenye hatari kubwa ya kufanyiwa ukatili

 

UNICEF katika ripoti hiyo, inaeleza kuwa umaskini, mmonyoko wa maadili na ongezeko la magonjwa ni baadhi ya sababu zinazoshamirisha watoto yatima katika jamii.

“Yatima wako katika hali hatarishi zaidi. Umasikini, kupanuka kwa miji, kumomonyoka kwa maadili na desturi za familia, na athari za janga la UKIMWI/VVU vinaashiria kwamba watoto ambao hawako katika utamaduni wa kuishi kifamilia na kijamii wako katika hali hatarishi ya kukumbwa na ukatili,” inafafanua ripoti hiyo.

Wavulana waliopoteza mzazi mmoja hasa mama, ndiyo wako katika hatari ya kufanyiwa ukatili na mama zao wa kambo kwa hufanyishwa kazi ngumu na wakati mwingine hunyimwa chakula na sehemu ya kulala.

Ripoti ya UNICEF inafafanua zaidi kuwa, “Wavulana waliopoteza mama zao kabla ya kufika umri wa miaka 18 walikumbwa zaidi na ukatili wa kiakili kuliko wale wasio kuwa yatima (asilimia 44 ya wavulana yatima ukilinganisha na asilimia 26 wasiokuwa yatima)”.

Matokeo ya utafiti huo ni kielelezo tosha cha hali halisi ya ukatili dhidi ya watoto yatima  iliyopo katika jamii hasa katika jiji la Dar es Salaam, ambapo katika mitaa na barabara kuu hutaacha kuwaona watoto wadogo wakizurula na kuomba fedha kwaajili ya kujikimu.

Ili kupambana na ukatili dhidi ya watoto yatima serikali imeshauriwa kujumuisha ujumbe wa kuzuia ukatili wa kijinsia na sehemu salama kwenye programu za shule kuzungumzia jinsia, afya ya uzazi, na maendeleo ya jamii.

Hata hivyo,  ili mapambano yafanikiwe imetakiwa  kupanua ulinzi stahili wa kisheria kwa watoto na adhabu za kisheria kwa wakosaji; kuendeleza jitihada zilizopo kwenye Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi kitaifa

Continue Reading

Must Read

Copyright © 2018 FikraPevu.com