Asilimia 80 ya ardhi ya umwagiliaji Tanzania inalimwa kwa njia za kienyeji, kilimo cha kisasa kumkomboa mkulima

Wakulima katika maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka wameshauriwa kuvuna na kuhifadhi maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili kuwahakikishia usalama wa chakula.

Maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka  ni Kanda ya Magharibi, Kati, Nyanda za Juu Kusini Magharibi, maeneo ya Kusini, Ukanda wa Pwani ya Kusini  pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro.

Mvua hizo zimeanza kunyesha katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba 2017 na zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2018. Mvua hizo zitatofautiana kutoka eneo moja hadi lingine lakini tahadhari ni muhimu ili kujizuia na madhara yasiyo ya lazima.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi amesema kiwango cha maji katika udongo kitaongezeka katika maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka  kutokana na mvua ambazo  zinanyesha katika maeneo yaliyotajwa.

“Hali ya unyevunyevu kwa ajili ya mazao na malisho ya mifugo na wanyamapori inatarajiwa kuwa ya kuridhisha. Wakulima wanashauriwa kuvuna maji kipindi cha mvua  kwa matumizi ya baadae”, anaeeleza Dkt. Kijazi.

Matumizi ya baadaye ni pamoja kilimo cha umwagiliaji ambacho hasa hufanyika katika kipindi ambacho mvua hazinyeshi. Ikiwa mfumo mzuri wa kuhifadhi maji kwenye mabwawa na matanki utaandaliwa, wakulima wana nafasi nzuri ya kuendelea na shughuli za kilimo kwa mwaka mzima.

Kilimo cha umwagiliaji humuhakikishia mkulima chakula kwasababu mazao yanayolimwa ni yale yanayokomaa kwa muda mfupi hasa mwezi 1 hadi 3. Mbogamboga ni sehemu ya mazao hayo ambayo yakiwekewe mikakati mizuri yanaweza kutengeneza kipato.

Kutokana na umuhimu wa kuhifadhi maji ya mvua, serikali imesema inaendelea na mikakati ya kuliweka suala hilo kivitendo ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameathiri mwenendo wa mvua.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa wakati huo, Mhandisi Geryson Lwenge wakati akizindua Mkutano wa Wathibiti wa Huduma za Maji Kusini na Mashariki ya Afrika (ESAWAS), alisema serikali imeanza mipango ya kujenga mabwawa maalumu ya kuhifadhi maji ya mvua ili kukabiliana na uhaba wa maji na kuwawezesha wakulima kuendelea na kilimo pasipo kutegemea mvua.

Mabomba yakimwaga maji kwenye mazao shambani

Kulingana na Benki ya Dunia (WB) katika ripoti yake ya Mapitio ya Uchumi wa Tanzania ya mwaka 2017, inaitaja Tanzania kutumia asilimia 80 ya maji yake yote katika shughuli za kilimo. Matumizi hayo ni makubwa ikilinganishwa na matumizi ya dunia ambayo yanafikia 70% katika kilimo.

Lakini ukuaji wa miji na viwanda unatishia kupungua kwa maji yanayotumika katika sekta ya kilimo. Ili kukabiliana na changamoto ya kupungua kwa maji, wakulima wanashauriwa kuitumia fursa ya mvua za msimu kuhifadhi maji ambayo watayatumia baadaye kuendeleza kilimo.

Hata hivyo, baadhi ya wakulima wanaendelea na kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia njia za kienyeji ambazo hazileti matokeo makubwa. Inaeleza kuwa Tanzania ina ardhi kubwa lakini ni asilimia 1.5 ya ardhi ya umwagiliaji ndio inatumika, huku 80% ya ardhi ya umwagiliaji inalimwa kwa njia za kienyeji na maji yanayotumika hayazidi 15% ya maji yote yanayopaswa kutumika katika kilimo hicho.

Kutokana na changamoto hiyo wakulima pamoja na wadau wa kilimo wanashauriwa kukibadilisha kilimo cha umwagiliaji kuwa cha kisasa na viundwe vyombo maalum vya kusimamia matumizi ya uzalishaji wa maji na njia sahihi za kilimo kulingana na maeneo waliyopo wakulima.

 

Mwelekeo wa mvua za Msimu

Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi ya mikoa ya Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Ruvuma, Lindi na Mtwara  na kusini mwa  mkoa wa Morogoro.

Mvua katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Lindi, Mtwara na kusini mwa mkoa wa Morogoro zinatarajiwa kuanza mwezi wiki ya kwanza ya mwezi Novemba, 2017 na kusambaa katika mikoa ya Dodoma na Singida katika wiki ya kwanza ya mwezi Desemba, 2017.

Mtawanyiko hafifu wa mvua unatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Lindi na Mtwara katika kipindi cha Januari hadi Februari, 2018 kipindi ambacho ukanda wa mvua unatarajiwa kuwa nje ya  eneo la kusini mwa Tanzania. Mvua zinatarajiwa kuisha katika wiki ya mwisho ya mwezi Aprili, 2018 katika maeneo mengi yanayopata msimu mmoja wa mvua.

 

Mifumo ya Hali ya Hewa

Mvua hizo ambazo zitakuwa za wastani na juu wastani zitatokana na kuongezeka kwa joto katika bahari Hindi ambayo upepo wake utakuwa ukivuma zaidi kuelekea katika mikoa inayopokea mvua za msimu na kulifanya eneo hilo kupata mvua nyingi.

“Uwepo wa vimbunga kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi unatarajiwa kusababisha upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Congo kuelekea nchini. Hali hii ya upepo kutoka katika misitu ya Congo inatarajiwa kuongeza unyevunyevu katika baadhi ya maeneo ya magharibi na kusini magharibi mwa nchi”, anaeleza Dkt. Kijazi na kuongeza kuwa,

“Hali ya joto la juu ya wastani iliyopo magharibi mwa Bahari ya Hindi inatarajiwa kuendelea kuwepo katika kipindi cha Novemba, 2017 –Aprili, 2018”.

Ikiwa wakulima watatumia fursa ya mvua za msimu na kuvuna maji wana nafasi nzuri ya kuongeza kipato na kuondokana na umaskini wa kutegemea mvua ambazo zinaathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi.

tushirikishane
  • Show Comments

Your email address will not be published. Required fields are marked *

comment *

  • name *

  • email *

  • website *

Sponsors

tushirikishane

You May Also Like

Mashangingi mawili yakwamisha ununuzi wa vifaa vya maabara ya benki ya vinasaba vya wanyama Mpwapwa

KAMA Serikali ingesitisha kununua ‘mashangingi’ mawili tu kwa mwaka na kuelekeza fedha za magari ...

Kilimo cha viazi lishe kukabiliana na baa la njaa wilayani Ukerewe

WANANCHI wilayani Ukerewe katika Mkoa wa Mwanza wamejikita katika kilimo cha viazi lishe (viazi ...